Tafuta

Jumuiya ya Kikatoliki ya Shalom; Comunita' cattolica Shalom mwaka 2022 inaadhimisha miaka 40 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1982 huko Brazil. Jumuiya ya Kikatoliki ya Shalom; Comunita' cattolica Shalom mwaka 2022 inaadhimisha miaka 40 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1982 huko Brazil.  (Vatican Media)

Kumbukizi la Miaka 40 ya Jumuiya ya Kikatoliki ya Shalom: Ekaristi Takatifu

Maisha na utume wa Kanisa unaopata chimbuko na hatima yake katika Ekaristi Takatifu. Wajitahidi kushikamana na Yesu katika: Neno, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, Rozari, lakini zaidi katika Sakramenti na huduma Huduma kwa maskini iwe ni chimbuko la furaha, amana na utajiri wao wa ndani. Ili kutekeleza yote haya, wanapaswa kuwa na: ujasiri mbunifu pamoja na ukarimu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Moysés Louro de Azevedo Filho tarehe 9 Julai 1980 wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa mjini Fortaleza, Brazil alikutana na kuzungumza na Mtakatifu Yohane Paulo II akimwelezea nia yake ya kutaka kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, hususan miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, pamoja na kuwasaidia watu waliojisikia kuwa nje ya maisha na utume wa Kanisa kwa sababu mbalimbali.  Moysés Louro de Azevedo Filho, Maria Emmir Nogueira, pamoja na vijana wenzao tarehe 9 Julai 1982, wakaanzisha Jumuiya ya Kikatoliki ya Shalom “La Comunità Cattolica Shalom” huko mjini Fortaleza, nchini Brazili. Ni Jumuiya ambayo imezaliwa katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili kunogesha ari, moyo na utamaduni wa sala miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu sera na mbinu mkakati wa uinjilishaji mpya unaosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; kwa kukazia malezi na makuzi ya maisha ya: kiroho na kiutu. Mwaka 1998 Jumuiya ya Kikatoliki ya Shalom ikatambuliwa rasmi kisheria na Kardinali Claudio Hummes, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Fortaleza. Tarehe 22 Februari 2007, Baraza la Kipapa la Walei, likaitambua Jumuiya hii, inayowamasisha wanajumuiya wake kuwa ni vyombo na mashuhuda wa amani; umoja, upendo na mshikamano wa dhati, ili kuwainjilisha watu wa Mataifa, daima wakijiweka chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu; kwa kusoma, kutafakari na hatimaye kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha yao.

Jumuiya ya Kikatoliki ya Shalom inaadhimisha Miaka 40 ya utume wake 2022.
Jumuiya ya Kikatoliki ya Shalom inaadhimisha Miaka 40 ya utume wake 2022.

Jumuiya hii, daima inataka kujiweka chini ya Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium”; Ushiriki mkamilifu katika maisha ya sala, Liturujia na Sakramenti za Kanisa, huku wakijitahidi kujenga na kudumisha maisha ya kidugu na kimisionari, chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Jumuiya hii, iko chini ya ulinzi na maombezi ya Mtakatifu Francisko wa Assisi na Theresa wa Avila. Ni katika muktadha wa kumbukizi la Miaka 40 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Kikatoliki ya Shalom, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 26 Septemba 2022 amekutana na kuzungumza na wanajumuiya hawa. Imekuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu kusikiliza maisha na utume wao wa kimisionari; mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya vijana pamoja na changamoto mbalimbali wanazoendelea kukumbana nazo katika maisha na utume wao. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia umuhimu wa maisha na utume wa Kanisa unaopata chimbuko na hatima yake katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Wajitahidi kubaki wakiwa wameshikamana na kufungamana na Kristo Yesu katika: Neno la Mungu, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, Rozari Takatifu, lakini zaidi katika maisha ya Kisakramenti. Huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, iwe ni chimbuko la furaha, amana na utajiri wao wa ndani. Ili kutekeleza yote haya, wanapaswa kuwa na: ujasiri mbunifu, ukarimu, ari na mwamko wa kimisionari.

Jumuiya ya Shalom imezaliwa katika Ekaristi Takatifu
Jumuiya ya Shalom imezaliwa katika Ekaristi Takatifu

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Jumuiya ya Kikatoliki ya Shalom “La Comunità Cattolica Shalom” ilizaliwa katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kazi ya Roho Mtakatifu anayeliwezesha Kanisa kusonga mbele. Roho Mtakatifu anatenda kazi zake katika Liturujia, kumbe, wanapaswa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusali vizuri zaidi na kwamba, sala inogeshe maisha yao ya kila siku. Ikiwa kama wanapenda kubaki wakiwa wameungana na kushikamana na Mwenyezi Mungu katika maisha na utume wao hawana budi kujenga na kudumisha: urafiki na mahusiano na Mungu kwa njia ya: Sala, Neno, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, Rozari Takatifu muhtasari wa historia nzima ya ukombozi na kwa njia hii, wataweza kuzaa sana kwani Kristo Yesu ni Mzabibu wa kweli. Rej Yn 15:1-11. Matunda yanayokusudiwa ni upendo kwa Mungu na jirani, dhamana na wajibu unaotekelezwa kwa ufanisi zaidi na Roho Mtakatifu katika maisha ya vijana wa kizazi kipya. Wajitahidi kujenga maisha yao katika toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha, huku wakiwaiga vijana wakatifu, kama akina Carlo Acutis na wengineo. Wote hawa wamejitahidi kujenga Fumbo la Mwili wa kristo yaani Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa maisha na utume wao.

Watakatifu vijana wawe ni mifano na waombezi wao
Watakatifu vijana wawe ni mifano na waombezi wao

Viongozi wa Kanisa wanaojihusisha na utume na shughuli za kichungaji miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, wajitahidi kuwa ni walezi wasikivu na wala si wamiliki wa vijana, daima wajitahidi kuwashirikisha vijana katika maisha na utume wa Kanisa. Vijana wajitahidi kujenga na kudumisha urafiki na mafungamano na jirani zao na hasa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama alivyojitahidi kutenda Mama Theresa wa Calcutta. Aliutambua Uso wa Kristo Mfufuka miongoni mwa maskini na wale wote waliokuwa kufani; akawasaidia kutambua na kuthamini utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Washiriki pia katika huduma ya upendo kwa maskini. Baba Mtakatifu anawataka vijana wa Jumuiya ya Kikatoliki ya Shalom “La Comunità Cattolica Shalom” kupyaisha ndani mwao ujasiri wenye ubunifu wakijitahidi daima kujenga na kudumisha amani na utulivu wa ndani. Watambue kwamba, wanabeba mwilini wao Msalaba wa Kristo Yesu Mfufuka, kumbe, wanaitwa na kutumwa kuwa ni wamisionari Mitume wa Kristo Yesu.

Neno la Mungu, Sakramenti na huduma ya upendo ni muhimu sana kwa vijana
Neno la Mungu, Sakramenti na huduma ya upendo ni muhimu sana kwa vijana

Hii ni Jumuiya ya Kikatoliki, kumbe, wanapaswa kukita maisha na kutoa kipaumbele cha kwanza katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na kupokea mara kwa mara Sakramenti ya Upatanisho. Wajitahidi kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa: Mahubiri, Sala na Muziki, bila kusahau amana na utajiri unaobubujika kutoka katika Kanisa Katoliki. Wajitahidi kujenga na kudumisha umoja na ushirikiano na viongozi wao wa Kanisa, kwa kuwaonesha utii. Wawe wanyenyekevu kwa kazi ya Roho Mtakatifu, ili waweze kuwa na mang’amuzi bora zaidi katika maisha na utume wao. Waendelee kuwajibika na kuwa na busara; wakiheshimu uhuru wao binafsi sanjari na kusikiliza kwa makini mafundisho ya Mama Kanisa. Watambue na kuheshimu karama na miito mbalimbali inayofumbatwa katika Jumuiya ya Kikatoliki ya Shalom. Kwa hakika karama na utume wa Jumuiya hii ni kazi ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Jumuiya imekuwa ni chachu ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha katika medani mbalimbali za utume wa Kanisa.

Jumuiya ya Shalom

 

 

26 September 2022, 16:26