Tafuta

Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2023 inayoadhimishwa Jumamosi tarehe 11 Februari 2023 sanjari na Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes. Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2023 inayoadhimishwa Jumamosi tarehe 11 Februari 2023 sanjari na Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes. 

Bikira Maria wa Lourdes: Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani, Ndanda, Mtwara, Tanzania

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuanza kujiandaa kiroho katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes sanjari na Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2023 inayoadhimishwa Jumamosi tarehe 11 Februari 2023 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Mtunze”: Huruma kama zoezi la Sinodi ya Uponyaji.”

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Wagonjwa Duniani, ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 13 Mei 1992 na kuadhimishwa kwa mara ya kwanza kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes nchini Ufaransa kunako tarehe 11 Februari 1993. Hii ni siku maalum ambayo Mama Kanisa anapenda kutoa kipaumbele cha pekee kwa wagonjwa wa kimwili na kiroho bila kuwasahau wale wote wanaoteseka kutokana na sababu mbalimbali. Siku ya Wagonjwa Duniani ni nafasi ya kutafakari kanuni maadili na utu wema; sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya wagonjwa na wazee, tayari kusoma alama za nyakati kwa kusikiliza na kujibu kilio cha wagonjwa na wale wanaoteseka. Siku ya Wagonjwa Duniani kwa Kanisa Katoliki ni siku maalum kwa ajili ya kukoleza uragibishaji na maadhimisho yanayokusudia kuwasaidia waamini kusali na kushiriki mateso ya wagonjwa; na kwa wagonjwa wenyewe kutolea mateso na mahangaiko yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo Yesu na hatimaye, kuwaonjesha wagonjwa kuwa ni sura na ufunuo wa Kristo Yesu, anayeteseka kati pamoja nao. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 8 Februari, 2023 mintarafu Hija yake ya 40 ya Kitume Barani Afrika, hususan nchini DRC na Sudan ya Kusini kuanzia tarehe 31 Januari hadi 5 Februari 2023 amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuanza kujiandaa kiroho katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes sanjari na Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2023 inayoadhimishwa Jumamosi tarehe 11 Februari 2023 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Mtunze”: Huruma kama zoezi la Sinodi ya Uponyaji.”

Tiba shufaa imeanzishwa kwenye Hospitali ya Ndanda, Mtwara, Tanzania.
Tiba shufaa imeanzishwa kwenye Hospitali ya Ndanda, Mtwara, Tanzania.

Baba Mtakatifu kwa maombezi ya Bikira Maria Afya ya Wagonjwa anapenda kuwakabidhi na kuwazamisha wagonjwa wote, familia zao na wale wanaoendelea kujisadaka usiku na mchana kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa, kwa kujenga na kudumisha mshikamano na kifungo cha maisha binafsi, kikanisa na udugu wa kibinadamu. Iwe ni siku ya sala kwa ajili ya wagonjwa ili waweze kuhakikishiwa huduma na matibabu bora; wasaidiwe na kusindikizwa na huduma za maisha ya kiroho na wahudumu wa afya waweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao kwa jamii. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwapatia wote hawa baraka zake, ili waweze kuwa kweli ni Wasamaria wema tayari kuganga kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini wale wote waliovunjika na kupondeka moyo kutokana na magonjwa ya kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuyaelekeza mawazo yao kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes katika Maadhimisho ya Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2023, ili kujifunza somo la kinabii ambalo Mama Kanisa amekabidhiwa katika nyakati hizi za kisasa. Si watu wazima na wale wanaofanya shughuli zao barabara ndio wanaopaswa kupewa kipaumbele. Kinyume chake na kwa hakika wagonjwa wako katikati ya watu wa Mungu na Mama Kanisa anasonga mbele pamoja nao kama ishara ya ubinadamu ambamo kila mtu anathamini kubwa mbele ya Mungu na wala hakuna anayepaswa kutelekezwa au kuachwa nyuma. Bikira Maria Mwenye Moyo Safi, awasaidie kuwaombea furaha na ujasiri katika hija ya maisha yao huku bondeni kwenye machozi.

Wagonjwa wapate huduma za kimwili na kiroho.
Wagonjwa wapate huduma za kimwili na kiroho.

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC limeatangaza kwamba, Maadhimisho ya Siku ya 31 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2023, yanaadhimishwa kitaifa kwenye Hospitali ya Mtakatifu Benedikto Ndanda, Jimbo Katoliki la Mtwara kutokana na maboresho makubwa yaliyofanyika Hospitalini hapo kiasi cha kuiwezesha kuanza kutoa huduma ya tiba shufaa. Ongezeko la magonjwa sugu kama saratani, kiharusi, figo na UKIMWI huambatana na gharama kubwa za matibabu ambazo mgonjwa anatakiwa kulipa ili kumrejesha katika hali ya kawaida.  Hata hivyo, siyo wagonjwa wote wana uwezo wa kwenda hospitali kutokana na hali ngumu ya hali na kiuchumi au kuugua muda mrefu na hivyo kulazimika kukaa nyumbani akisubiri kifo. Hapo ndipo inaibuka tiba shufaa kuokoa: utu na maisha ya mgonjwa.  Tiba Shufaa ni tiba ni mahususi kwa watu wenye magonjwa sugu ambao wameumwa kwa muda mrefu bila kupata uponyaji. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, WHO huduma za tiba shufaa ni utaratibu wa matibabu unaoboresha ubora wa maisha ya mgonjwa na familia iliyo katika matatizo yatokanayo na kuuguliwa kwa kuzuia na kupunguza matatizo katika maana ya kutambua mapema dalili za tatizo na namna ya kuhakiki tatizo na kutuliza maumivu na matatizo mengine ya kimwili, kijamii, kiakili na kiroho kwa wagonjwa wenye magonjwa sugu. Kutokana na umuhimu wa tiba hiyo, Hospitali ya Ndanda imeanzisha huduma hii, (Palliative Care Services). Wafanyakazi katika sekta ya afya wanahamasishwa kushiriki kikamilifu ikiwa ni pamoja na kutuma wawakilishi katika maadhimisho haya Kitaifa.

Siku ya Wagonjwa 2023
08 February 2023, 18:05