Tafuta

Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde wa Jimbo kuu la Mombasa, Kenya katika mahojiano maalum na Radio Vatican anagusia kuhusu: Mshikamano wa udugu toka AMECEA. Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde wa Jimbo kuu la Mombasa, Kenya katika mahojiano maalum na Radio Vatican anagusia kuhusu: Mshikamano wa udugu toka AMECEA.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Sudan ya Kusini: Mchango wa AMECEA: Haki na Amani

Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde wa Jimbo kuu la Mombasa, Kenya katika mahojiano maalum na Radio Vatican anagusia kuhusu: Mshikamano wa udugu katika ya Nchi za AMECEA, changamoto ya amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mchango wa Papa Francisko kwa ajili ya amani Sudan ya Kusini pamoja na mchamngo wa Shirikisho la Mabaraza ya Watawa wa Kike Afrika Mashariki, ACWECA na kwamba, kuna haja ya kuweka nia na kuitekeleza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Sudan ya Kusini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 31 Januari 2023 hadi tarehe 5 Februari 2023 amefanya Hija ya 40 ya Kitume nchini DRC na Sudan ya Kusini. Lengo likiwa ni kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo; amani na majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika nchi hizi mbili ambazo kimsingi zimepekenywa sana na vita, magonjwa, njaa na majanga asilia. Baba Mtakatifu alikuwa ameambatana na Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani na Mheshimiwa Dr Iain Greenshields Mkuu wa Kanisa la “Presbyterian” la Scotland kama kielelezo cha ushuhuda wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika huduma kwa watu wa Mungu, maisha ya kiroho, ushuhuda wa damu na sala. Huu ni shuhuda wa hija ya uekumene wa amani na watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini. Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde wa Jimbo kuu la Mombasa, Kenya katika mahojiano maalum na Radio Vatican anagusia kuhusu: Mshikamano wa udugu katika ya Nchi za AMECEA, changamoto ya amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mchango wa Papa Francisko kwa ajili ya amani Sudan ya Kusini pamoja na mchango wa Shirikisho la Mabaraza ya Watawa wa Kike Afrika Mashariki, ACWECA na kwamba, kuna haja ya kuweka nia na kuitekeleza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Sudan ya Kusini.

Mshikamano wa AMECEA na Watu wa Sudan ya Kusini: Amani
Mshikamano wa AMECEA na Watu wa Sudan ya Kusini: Amani

Nchini Sudan ya Kusini hija hii imenogeshwa na kauli mbiu “Wote wawe na umoja” Yn 17:21, hiki ni kielelezo cha ushuhuda wa kiekumene, mshikamano na udugu wa kibinadamu, mwaliko na changamoto ya kujizatiti katika mchakato wa upatanisho na ujenzi wa umoja wa Kitaifa. Tukio hili limehudhuriwa pia wawakilishi kutoka katika nchi za AMECEA yaani: Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati AMECEA, linaundwa na Nchi 8 ambazo ni: Zambia, Malawi, Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan, Ethiopia na Eritrea. Miongozo ya Mababa waanzilishi wa AMECEA ilikuwa kuimarisha imani Katoliki na maendeleo endelevu na fungamani ya jamii kwa kuwa na mpango mkakati wa muda mrefu uliowekwa katika Mkutano Mkuu wa AMECEA uliofanyika Julai 1961, kwenye Ukumbi wa Msimbazi Center, Jimbo kuu la Dar es Salaam, ukiongozwa na dhamira kuu: “Kesho ya Kanisa la Bara la Afrika.” Tangu wakati huo, AMECEA kimekuwa ni chombo madhubuti za shughuli za kichungaji katika mchakato wa ujenzi wa umoja, udugu wa kibinadamu, ushirikiano na mshikamano sanjari na maboresho ya huduma za kichungaji kwa watu wa Mungu Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Kumekuwepo na mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwa AMECEA.

ACWECA liko mstari wa mbele katika elimu, afya na ustawi wa jamii
ACWECA liko mstari wa mbele katika elimu, afya na ustawi wa jamii

Kati ya matunda haya ni pamoja na uundwaji wa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo. Kusimama kidete katika mchakato wa kutetea haki, amani, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kulea dhamiri nyofu ili watu watende kadiri ya mapenzi ya Mungu pamoja na utekelezaji wa dhamana na wajibu wa waamini katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu Afrika Mashariki na Kati. Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde wa Jimbo kuu la Mombasa, Kenya, katika mahojiano maalum na Radio Vatican wakati wa hija ya Kitume ya 40 ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Sudan ya Kusini anasema, Sudan ya Kusini ni sehemu muhimu sana ya AMECEA, lakini inakabiliwa na changamoto nyingi katika maisha na utume wake, na kubwa zaidi ni changamoto ya haki, amani na maridhiano, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake Kusini mwa Sudan, alikwenda kama hujaji wa amani na matumaini yanayofumbatwa katika Fumbo la Msalaba. Amewakumbusha waamini kwamba wao ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu, mwaliko kwa waamini kuwa ni mashuhuda wa tunu hizi katika maisha na utume nchini Sudan ya Kusini, ili watu waweze kuangaziwa na: amani, wema na upendo wa Mungu, matumaini na hivyo kuendelea kujikita katika mchakato wa haki, amani na upatanisho; Ushuhuda wa Mungu ambaye ni chemchemi ya amani na faraja. 

Papa Francisko: Chombo na shuhuda wa Amani
Papa Francisko: Chombo na shuhuda wa Amani

Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde anasema, Baba Mtakatifu ametembelea Sudan ya Kusini ili kunogesha uekumene wa amani na matumaini, ili kukoleza mchakato wa: upatanisho, haki na amani kwa kutambua madhara ya vita kwa maisha ya watu wa Mungu, Sudan ya Kusini. Baba Mtakatifu Francisko amesema moyoni mwake kuna chapa ya matukio muhimu katika maisha na utume wake kwa watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini: Sala kwa ajili ya kuombea amani Sudan ya Kusini iliyoadhimishwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kunako mwaka 2017, Mafungo ya kiroho kwa ajili ya viongozi wa Sudan ya Kusini yaliyofanyika mwaka 2019 kama sehemu ya mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kutafuta na hatimaye, kuambata mchakato wa amani na udugu wa kibinadamu nchini Sudan ya Kusini kwa kumpokea Kristo Yesu amani na matumaini ya waja wake. Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde anasema, Baba Mtakatifu ameyatenda yote haya kwa moyo wa unyenyekevu, kwa kutambua kwamba, haki, amani na maridhiano ni kilio cha watu wengi wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Kwa hakika anataka kuwa ni chombo cha amani, kama ilivyo sala ya Mtakatifu Francisko wa Assisi; chombo cha matumaini kwa wale waliokata tamaa na kuvunjika moyo. Huu ni mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene, kisiasa na kitamaduni, ili wote waweze kuwa wamoja, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Bila amani ya kudumu, hakuna maendeleo ya kweli. Hizi ni juhudi pia katika mchakato wa uinjilishaji wa kina; ujenzi wa familia ya Mungu inayowajibikiana na kutumikiana kwa kutambua kwamba vita ina madhara makubwa kwa watu na mali zao.

Mchakato wa majadiliano ya amani umepyaishwa.
Mchakato wa majadiliano ya amani umepyaishwa.

Ni kutokana na msukumo huu mpya, Rais Salva Kiir Mayardit wa Sudan ya Kusini katika hotuba yake aligusia umuhimu wa hija ya uekumene wa amani utakaosaidia kupyaisha mchakato wa haki, amani na upatanisho wa Kitaifa kwa kutekeleza Mkataba wa Amani wa Mwaka 2018. Licha ya matatizo na changamoto zilizopo, lakini wadau wakuu wa Mkataba wa Amani wa mwaka 2018 “Revitalised Agreement on the Resolution of Conflict in South Sudan” (R-ARCSS) wanaendelea kushirikiana, kujadiliana na kushikamana ili kuhakikisha kwamba, Mkataba huu unatekelezwa kwa vitendo, kwa kujenga miundo mbinu itakayoweza kusikiliza sauti za wananchi wa Sudan ya Kusini. Mwezi Septemba 2022 Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Mkataba wa Amani ulisogezwa mbele kwa muda wa miaka miwili, ili kuhakikisha kwamba uchaguzi unafanyika kwa kuzingatia misingi ya ukweli, uwazi, haki na amani. Shirikisho la Mabaraza ya Watawa wa Kike Afrika Mashariki, ACWECA. “The Regional Association of Consecrated Women in Eastern and Central Africa) lilianzishwa kunako mwaka 1974 na kwa sasa linawajumuisha Watawa wa kike wapatao 30, 000 kutoka katika Nchi za Afrika Mashariki na Kati. Kwa hakika, hawa ni Watawa wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA. ACWECA pamoja na mambo mengine, linapania: Kukuza na kuendeleza majiundo makini ya watawa; kuwajengea uwezo watawa ili waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upatanisho pamoja na kujitegemea.

AMECEA: Mshikamano na Sudan ya Kusini
AMECEA: Mshikamano na Sudan ya Kusini

Ni Shirikisho linalotoa msaada wa kiufundi kwa Mashirika ya kitawa, ili kweli watawa waweze kuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu kati ya watu wanaowahudumia katika sekta mbalimbali za maisha, kama sehemu ya uinjilishaji wa kina. Wanaunga mkono jitihada za Baba Mtakatifu Francisko katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama anavyobainisha katika Waraka wake wa Kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote. Shirikisho linajielekeza zaidi katika nyanja kuu nne yaani: Malezi na utume, Familia na Utume wa Vijana, Haki, Amani na Uumbaji fungamani sanjari na ustawi, maendeleo na mafao ya Mashirika ya Kitawa. Askofu mkuu Martin Kivuva Musonde anasema Umoja wa Afrika, unawataka watu wa Mungu Barani Afrika kushikamana ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano. Jambo la msingi kwa watu wa Mungu nchini Sudan, ni kutokubali kufa moyo na kukata tamaa. Waendelee kujikita katika mapambano dhidi ya ukoloni mambo leo. Kanisa litaendelea kuwa ni shuhuda wa imani na mwanga wa Mataifa. Jambo la msingi ni kuweka ni na kuanza kutekeleza kwa vitendo. Huu ni wakati wa kuweka tofauti zao kando na kuanza kujielekeza zaidi ujenzi wa amani; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini wanapaswa kujenga umoja na mafungamano ya kijamii na kisiasa, ili hatimaye, waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano nchini Sudan ya Kusini.

Amani Sudan ya Kusini
15 February 2023, 14:20