Tafuta

Papa Francisko amepyaisha Waraka mpya wa kitume katika mfumo wa “Motu proprio” ujulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”. Papa Francisko amepyaisha Waraka mpya wa kitume katika mfumo wa “Motu proprio” ujulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”.  (Vatican Media)

Waraka wa Papa Francisko Uliopyaishwa: "Ninyi Ni Nuru ya Ulimwengu" Waanza Kutumika

Papa Francisko amepyaisha Waraka wa kitume katika mfumo wa “Motu proprio” ujulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Toleo hili jipya linaonesha nia thabiti ya Kanisa Katoliki kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Maaskofu mahalia, wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume pamoja na waamini wote wanawajibishwa kisheria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Barua binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko “Motu proprio” ijulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia.  Katika barua hii, Baba Mtakatifu anabainisha sheria, kanuni na taratibu mpya zinazopaswa kutekelezwa pale kunapojitokeza shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Maaskofu mahalia pamoja na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume wanapaswa kuwajibika barabara. Sheria hizi zinawalazimisha wakleri na watawa kutoa taarifa pale kunapokuwepo na shutuma kama hizi. Kila Jimbo linapaswa kuwa na mfumo maalum utakaoiwezesha jamii kutoa taarifa za shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha wakleri na watawa kwamba, wao ni nuru ya ulimwengu na kwamba, Kristo Yesu anawaita na kuwataka kuwa waaminifu na mfano mahiri wa tunu msingi za maisha, uadilifu na utakatifu. Hii ni sehemu ya mafundisho mazito yaliyomo kwenye barua binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia zinazoweza kutendwa na wakleri pamoja na watawa. Nyanyaso za kijinsia ni uhalifu unaosababisha madhara makubwa ya kimwili, kisaokolojia na kiroho si tu kwa waathirika bali hata kwa Jumuiya ya waamini. Viongozi wa Kanisa wanapaswa kuwa mstari wa mbele kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Huu ni wajibu wao wa kimaadili. Hati hii ni matunda ya mkutano wa ulinzi wa watoto wadogo uliofanyika mjini Vatican, mwezi Februari 2019.

Maaskofu na wakuu wa mashirika wanao wajibu wa kwanza kabisa
Maaskofu na wakuu wa mashirika wanao wajibu wa kwanza kabisa

Hizi ni sheria kwa ajili ya Kanisa Katoliki katika ujumla wake. Hadi kufikia Juni 2020, Majimbo yote ya Kanisa Katoliki sehemu mbalimbali za dunia, yalipaswa kuwa na mfumo maalum utakaoiwezesha jamii kutoa taarifa za shutuma za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Sheria hii inahusu pia matumizi ya picha za ngono pamoja na viongozi wa Kanisa kuficha kashfa ya nyanyaso za kijinsia. Kumbe, Sheria inatoa mwanya kwa kila jimbo kuhakikisha kwamba linatenda kadiri ya tamaduni na mazingira ya Kanisa mahalia. Jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa, waathirika wa nyanyaso za kijinsia wanapokelewa na kusikilizwa, hata kama kunaweza kutokea pia shutuma za uongo, lakini shutuma hizi zitapaswa kushughulikiwa kikamilifu. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Machi 2023, Sherehe ya Bikira Maria Kupashwa Habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu, “Theotokos” amepyaisha Waraka wake wa kitume katika mfumo wa “Motu proprio” ujulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Toleo hili jipya linaonesha nia thabiti ya Kanisa Katoliki kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Linakazia mabadiliko ya Sheria za Kanisa yaliyofanywa na Baba Mtakatifu Francisko kuanzia mwaka 2019, Motu proprio wa “Sacramentorum sanctitatis tutela ya mwaka 2021, Kitabu cha VI cha Sheria za Kanisa, Mabadiliko ya Mwaka 2021. Ni katika muktadha huu, Kanisa linapaswa kujikita katika wongofu wa kimisionari, kwa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Kanisa lijitambulishe na kueleweka kuwa ni Fumbo la Ushirika unaomwilishwa katika dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.

Papa Francisko waraka huu umepyaisha sasa unaanza kutumika
Papa Francisko waraka huu umepyaisha sasa unaanza kutumika

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Machi 2022, Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria, akaridhia kuchapishwa kwa Katiba mpya ya Kitume inayojulikana kama “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Katiba imeanza kutumika rasmi tarehe 5 Juni 2022, Sherehe ya Pentekoste na hivyo kuchukua nafasi ya Katiba ya Kitume “Pastor bonus” ya tarehe 28 Juni 1988 iliyoanza kutumika rasmi 1 Machi 1989. Katiba hii mpya ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Baraza la Makardinali katika mikutano yake elekezi kabla ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro uliofanyika mwaka 2013. Haya ni matunda ya kazi kubwa iliyotekelezwa na Baraza la Makardinali Washauri kuanzia mwezi Oktoba 2013 hadi Februari 2022 na hatimaye, kuchapishwa tarehe 19 Machi 2022 chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko bila kusahau mchango uliotolewa na Makanisa mahalia kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Katiba hii kwa sasa inatekeleza mabadiliko makubwa yanayoendelea kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Askofu mkuu Charles Jude Scicluna wa Jimbo kuu la Malta, ambaye pia ni Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kwa upande wake anakaza kusema, baada ya Barua binafsi ya Baba Mtakatifu Francisko katika mfumo wa “Motu proprio” ijulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia kufanyiwa majaribio kwa muda wa miaka minne, tangu tarehe 25 Machi 2023 imeanza kufanya kazi rasmi kwa Kanisa Katoliki.

Watu wote wa Mungu wasimame kidete kulinda watoto
Watu wote wa Mungu wasimame kidete kulinda watoto

Wakleri na watawa wote wanawajibika sasa kisheria kutoa taarifa kuhusu nyanyaso za kijinsia wanazozifahamu, haraka iwezekanvyo kwa uongozi wa Jimbo! Watapaswa pia kutoa taarifa pale ambapo kiongozi wa Kanisa hakutimiza wajibu wake au amefumbia macho uwepo wa nyanyaso za kijinsia katika eneo lake. Hadi wakati huu, wajibu wa kutoa taarifa kuhusu nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa lilibaki ni jambo la dhamiri ya mtu binafsi, lakini kuanzia sasa na kuendelea huu ni wajibu wa kisheria kwa wakleri, watawa pamoja na waamini walei! Familia ya Mungu katika ujumla wake inapaswa kusimama kidete kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia kwa kutoa taarifa. Hati hii inaendelea kuwabana hata wakleri wanapowakosea haki watawa au nyanyaso dhidi ya waseminari na wanovisi. Kuficha kashfa ya nyanyaso za kijinsia ni kesi ambayo imepewa uzito wa pekee kabisa. Haya ni matukio yanayoweza kufanyika moja kwa moja au kwa kutotimiza wajibu; kwa kuingilia au kuvuruga uchunguzi unaofanywa na vyombo vya kiraia au kadiri ya Sheria za Kanisa na uongozi dhidi ya mkleri au mtawa aliyemdhalilisha mtu kijinsia. Wahusika wakuu ni wale waliopewa dhamana na wajibu ndani ya Kanisa, badala ya kufuatilia kashfa ya nyanyaso za kijinsia zilizotendwa na watu wengine, wao wamezificha na kujenga ngome ya kuwalinda watuhumiwa badala ya kuwalinda waathirika.

Sheria, Taratibu na Kanuni hizi zisaidie kulitakasa Kanisa dhidi ya maovu
Sheria, Taratibu na Kanuni hizi zisaidie kulitakasa Kanisa dhidi ya maovu

Baba Mtakatiifu katika barua yake binafsi: “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia anapenda kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ulinzi wa watoto wadogo wenye umri chini ya miaka 18 pamoja na watu wanyonge ndani ya jamii. Hili ni kundi ambalo linawaunganisha watu wote ambao licha ya kufikiri na kutenda kwa ufasaha, wanaweza kujikuta wametumbukia katika nyanyaso za kijinsia. Sehemu hii ya barua binafsi ya Baba Mtakatifu inafanya rejea kwenye Sheria za Vatican: Namba CCXCVII. Baba Mtakatifu anakaza kusema, wajibu wa kutoa taarifa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa, kwa namna yoyote ile haiwezi kuingiliana na sheria za nchi husika. Kumbe, hapa kinachotakiwa ni kuhakikisha kwamba, sheria na wajibu wa wale wote wanaohusika zinatekelezwa kikamilifu. Wale wote wanaofikisha tuhuma za nyanyaso za kijinsia dhidi ya wakleri na watawa wanapaswa kulindwa na kamwe wasibezwe, kutengwa wala kudhalilishwa. Baba Mtakatifu anapenda kuona kwamba, waathirika wanasikilizwa kwa umakini mkubwa kuliko ilivyokuwa huko nyuma kwa kunyamazishwa. Lakini, ikumbukwe kwamba, siri ya maungamo inabaki kuwa ni siri ya maungamo na kamwe haiwezi kubatilishwa na Barua hii binafsi anasema Baba Mtakatifu Francisko. Waathirika pamoja na familia zao wanapaswa kusaidiwa: kiroho, kisaikolojia pamoja na kupewa huduma ya afya wanayohitaji.

Ni jukumu la viongozi wa Kanisa sasa kutekeleza kwa vitendo kanuni hizi
Ni jukumu la viongozi wa Kanisa sasa kutekeleza kwa vitendo kanuni hizi

Baba Mtakatifu anafafanua sheria, taratibu na kanuni zinazopaswa kuzingatiwa pale ambapo watuhumiwa ni kati ya: maaskofu, makardinali au wakuu wa mashirika ya kitawa, au wale wenye dhamana ya kuongoza jimbo hata ikiwa ni kwa kipindi kifupi. Viongozi hawa watawajibishwa kwa kesi za nyanyaso za kijinsia zilizofanywa moja kwa moja au zile ambazo, walizinyamazia, bila kuzishughulikia, ingawa walikuwa na habari kuhusu nyanyaso hizi! Itakuwa ni jukumu lao kuweza kujitetea. Askofu mkuu wa kanda husika atapewa dhamana na Vatican ya kufanya uchunguzi ikiwa kama mtuhumiwa ni Askofu. Dhamana na wajibu wake kadiri ya Mapokeo ya Kanisa yanaendelea kuimarishwa sanjari na kuendelea kutumia rasilimali na utajiri wa Kanisa mahalia mintarafu uchunguzi dhidi ya askofu anayetuhumiwa. Askofu mkuu anayepewa dhamana ya kufanya uchunguzi, atapaswa katika muda wa siku 30 kutoa taarifa Vatican kuhusu uchunguzi uliofanywa na uchunguzi huu utapaswa kuwa umekamilika katika kipindi cha siku 90. Muda huu unaweza kuongezwa, ikiwa kama kutakuwepo na sababu msingi. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Mabaraza ya Kipapa yanayohusika, yaweze kufanya maamuzi kwa haraka zaidi. Baba Mtakatifu Francisko katika Barua hii binafsi, anagusia pia nafasi ya waamini walei wenye uwezo na sifa, wanaweza kushirikiana na Askofu mkuu kufanya uchunguzi.

Vitendo hivi viovu vinelifedhehesha Kanisa
Vitendo hivi viovu vinelifedhehesha Kanisa

Waamini walei ni amana na utajiri mkubwa kwa Kanisa. Sheria hizi mpya zinayataka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki pamoja na Majimbo yote kuwaandaa watalaam watakaoweza kusimamia uchunguzi, lakini wajibu msingi unabaki kuwa chini ya Askofu mkuu. Baba Mtakatifu tangu mwanzo anasema, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, kanuni ya kutokuwa na hatia inaheshimiwa hadi pale Baraza lenye dhamana litakapokuwa limetoa taarifa. Mtuhumiwa hana budi kufahamishwa, ikiwa kama uchunguzi utaanza kufanyika kama sehemu ya utekelezaji wa taratibu za kawaida na kama itaonekana inafaa, ili kulinda uadilifu katika mchakato wa uchunguzi, vidhibiti au hatua hii inaweza kurukwa katika hatua za mwanzo! Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake binafsi “Motu proprio” ijulikanayo kama “Vos estis lux mundi” yaani “Ninyi ni nuru ya ulimwengu”: Sheria mpya kwa ajili ya Kanisa Katoliki dhidi ya nyanyaso za kijinsia anahitimisha kwa kukazia mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa kufanya upelelezi wa kesi husika. Baada ya upelelezi kukamilika, Askofu mkuu, au Askofu mahalia mwenye umri mkubwa zaidi, anawasilisha uchunguzi wa tuhuma hizi kwenye Baraza linalohusika na huu ndio unakuwa ni mwisho wa dhamana yake. Baraza linalohusika litaendelea kushughulikia kesi kadiri ya Sheria, Taratibu na Kanuni zilizopo. Baada ya uchunguzi na upelelezi kufanyika na matokeo yake kutumwa panapohusika, Vatican inaweza kuchukua hatua ili kujihami dhidi ya mtuhumiwa! Sheria hizi ni nyenzo muhimu sana kwa Kanisa Katoliki kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia, kwa kukazia mambo msingi yanayopaswa kutekelezwa. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linasimama kidete kuhakikisha kwamba, kashfa kama hizi, hazijirudii tena. Hapa kuna haja ya kuwa na wongofu endelevu kutoka katika undani wa waamini. Familia yote ya Mungu inahusishwa kikamilifu katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa.

Papa Motu Proprio

 

 

25 March 2023, 14:35