Tafuta

Injili ni Chemchemi ya Furaha Kwa Watu Wa Nyakati Zote

Utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu ni chemchemi ya furaha na ni kwa ajili ya watu wote na hasa leo hii. Kutokana na changamoto za afya, Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko imesomwa kwa niaba yake na Monsinyo Filippo Ciampanelli, kwa kukazia: Habari Njema ya Wokovu na changamoto katika Ulimwengu mamboleo; Ushuhuda wa Injili pamoja na wongofu wa kichungaji na kimisionari kwa kujikita katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume. Rej. Mt 9:9-13. Hii ndiyo tema inayoongoza Mzunguko wa Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 11 Januari 2023. Hii ni tema ya dharura na madhubuti kwa maisha ya Kikristo. Baba Mtakatifu anasema, Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume ni mambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuwa, Jumuiya ya waamini inazaliwa kwa sababu ya utume na umisionari, huku ikisukumwa na Roho Mtakatifu, waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Huu ndio mwelekeo na dira ya utume na maisha ya Kikristo, vinginevyo, Wakristo wanaweza kujikuta wakijitafuta wao wenyewe katika ubinafsi wao. Bila ya kuwa na shauku ya uinjilishaji, imani itadhohofu na hatimaye, kunyauka na utume ndicho kiini cha maisha ya mwamini. Kumbe, mzunguko huu wa katekesi unalenga kupyaisha shauku ya uinjilishaji kwa kuzama zaidi katika Maandiko Matakatifu sanjari na Mafundisho Tanzu ya Mama Kanisa ili kuchota amana na utajiri wa ari, mwamko na bidii ya kitume kwa kuweka mbele ya waamini mifano hai na baadhi ya mashuhuda wa imani, walioamsha shauku ya Injili ili wawasaidie waamini kuwasha tena ule moto wa Roho Mtakatifu, ili hatimaye, uweze kuzijaza nyoyo za waamini wote mapendo. “Bali mtakaseni Kristo kuwa Bwana mioyoni mwenu. Siku zote mwe tayari kumjibu mtu yeyote atakayewauliza kuhusu sababu ya tumaini lililomo ndani yenu. Lakini fanyeni hivyo kwa upole na kwa hofu. Nanyi mwe na dhamiri njema, ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo wenu mwema katika Kristo.” 1Pt 3:15-16. Hii ni sehemu ya Maandiko Matakatifu iliyonogesha Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 29 Novemba 2023.

Ushuhuda wa Injili unamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku
Ushuhuda wa Injili unamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku

Utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu ni chemchemi ya furaha na ni kwa ajili ya watu wote na hasa leo hii. Kutokana na changamoto za afya, Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko imesomwa kwa niaba yake na Monsinyo Filippo Ciampanelli, Afisa kutoka Sektretarieti kuu ya Vatican kwa kukazia: Habari Njema ya Wokovu na changamoto katika Ulimwengu mamboleo; Ushuhuda wa Injili pamoja na wongofu wa shughuli za kichungaji na kimisionari kwa kujikita katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, leo hii habari kuu inayosikika masikioni mwa walimwengu ni: vita, athari za mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa haki msingi za binadamu, changamoto za kifamilia sanjari na ukosefu wa matumaini. Leo hii kuna hatari ya kuwapatia baadhi ya watu kipaumbele cha pekee, maendeleo makubwa ya teknolojia, mambo ambayo yana kasoro zake kwani yanampatia binadamu matumaini makubwa ya kiuchumi lakini yenye mwelekeo tenge wa maisha, maendeleo makubwa pasi ya uwepo wa Mungu. Baba Mtakatifu amezungumzia kuhusu mnara wa Babeli ambapo watu wote walikuwa wakizungumza lugha moja na usemi mmoja na wakataka kujijengea mji, na mnara na kilele chake kifike mbinguni ili kujifanyia “jina” na hivyo kuchukua nafasi ya Mungu, lakini Mwenyezi Mungu akawachafulia usemi wao ili wasisikilizane wao kwa wao. Haya ndiyo yanayotendeka hata katika ulimwengu mamboleo. Badala ya watu kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu; haki na amani wao wanazama zaidi katika: utaifa, ufanisi mkubwa wa miundo ya kiufundi-kiuchumi ambayo haitoi maana na umuhimu wowote wa uwepo wa Mungu kwa kujitafutia nguvu kubwa zaidi ya kutawala. Haya ni majaribu yanayokumbana na changamoto kubwa ya ulimwengu mamboleo.

Ushuhuda wa Injili, Wongofu wa Kichungaji na Kimisionari ni muhimu
Ushuhuda wa Injili, Wongofu wa Kichungaji na Kimisionari ni muhimu

Waraka wa Kitume wa Furaha ya Injili, “Evangelii gaudium” uliochapishwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 24 Novemba 2013, miaka kumi iliyopita, unatoa kipaumbele cha kwanza kwa furaha ya Injili, kwa kuwaalika waamini kushirikisha furaha yao inayopata chimbuko kutoka katika huruma na upendo wa Mungu kwa wanadamu. Katika mwono huu, Kristo Yesu ni kiini cha Injili na kwamba, Kanisa linaalikwa kufanya mageuzi makubwa kama sehemu ya uinjilishaji mpya kwa kukataa uchumi unaobagua, tabia ya kuabudu pesa; kukataa mfumo wa fedha unaotawala badala ya kutumikia; waamini wawe mstari wa mbele kudumisha usawa ili kujenga amani na kuitamadunisha imani; kwa kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia. Huu ni mwaliko wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili ili mchakato wa Uinjilishaji uweze kutoa mwanga kwa changamoto mamboleo kuhusiana na Mungu, wengine pamoja na tunu msingi. “Ni lazima uinjilishaji huo ufike kule ambako maelezo na mielekeo mipya vinaundwa, ili kufikisha neno la Yesu kwenye roho ndani kabisa ya miji yetu.” Evangelii gaudium, 74. Hapa kuna umuhimu wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili. “Tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa.” 2Kor 6:2. Baba Mtakatifu anakazia ushuhuda unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini. Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume ni mambo yanayosimikwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa kutambua kwamba, tamaduni mbalimbali ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, ushuhuda wa imani unapaswa kumwilishwa katika medani mbalimbali za maisha; mambo yanayokita mizizi yake katika majadiliano, tabia ya watu kukutana sanjari na ujenzi wa umoja. Waamini wajenge utamaduni wa majadiliano ili kuleta mageuzi yanayohitajika katika mang’amuzi ya imani yanayopyaisha tumaini. Ili kuweza kuleta wongofu katika ulimwengu mamboleo kuna haja ya kujikita katika wongofu wa shughuli za kichungaji na kimisionari ili kuliwezesha Kanisa kuwa katika mchakato wa umissionari, kwa kupyaisha ari na mwamko wa imani kwa wandani wa safari ya maisha ya kiroho ili kupyaisha ile hamu ya uwepo wa Mungu kwa kumfungulia malango ya maisha yao, ili aweze kuwakirimia watu wa Mungu amani na furaha.

Furaha ya Injili
29 November 2023, 15:45

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >