Tafuta

Papa Francisko Tangazeni na Kushuhudia Injili ya Furaha Kwa Watu wa Mataifa

Baba Mtakatifu Francisko anasema uinjilishaji unapata chimbuko lake kutoka katika kisima cha Injili ya furaha kama ilivyokuwa kule kondeni wakati Malaika wanatangaza habari ya kuzaliwa kwa Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. Huu ni mwaliko kwa kila mwamini, mahali popote pale alipo kupyaisha mkutano wake na Kristo Yesu katika Neno, Sakramenti za kanisa na matendo ya huruma kwa sababu Kristo Yesu ni chanzo cha uinjilishaji na kiini cha furaha timilifu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waraka wa Kitume wa Furaha ya Injili, “Evangelii gaudium” uliochapishwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 24 Novemba 2013, miaka kumi iliyopita unatoa kipaumbele cha kwanza kwa furaha ya Injili, kwa kuwaalika waamini kushirikisha furaha yao inayopata chimbuko kutoka katika huruma na upendo wa Mungu kwa wanadamu. Katika mwono huu, Kristo ni kiini cha Injili na kwamba, Kanisa linaalikwa kufanya mageuzi makubwa kama sehemu ya Uinjilishaji Mpya. Waraka huu ni ramani inayotoa dira na mwongozo thabiti wa shughuli za kichungaji unaopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa siku za usoni kwa kuwa na mwono wa kinabii na mwelekeo chanya, licha ya vikwazo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa, ili Kristo Mfufuka aendelee kupeperusha bendera ya ushindi. Waraka huu wa kitume unachota utajiri wake katika mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi juu ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza na kushuhudia imani ya Kikristo. Baba Mtakatifu Francisko, akayasoma na kuyafanyia tafakari ya kina na hatimaye kuyaweka kuwa ni sehemu ya ujumbe wake kwa Familia ya Mungu wakati huu inapojielekeza katika hija ya Uinjilishaji Mpya, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ndiye kiini cha Uinjilishaji na ndiye Mwinjilishaji Mkuu. Wakristo wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo Yesu mwenyewe katika mazingira mapya ya uinjilishaji. Baba Mtakatifu katika mwono huu wa kimisionari ambao ndio msingi wa waraka huu wa kitume anaugawa sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza ni mwaliko kwa Makanisa mahalia kuangalia changamoto na fursa zilizopo mintarafu tamaduni na hali halisi ya nchi husika. Baba Mtakatifu anatoa kigezo kwa ajili ya Kanisa la Kiulimwengu na kwa kila mdau wa uinjilishaji, ili kwa pamoja waweze kuibua mbinu shirikishi katika mchakato wa uinjilishaji pasi na kujitenga kama kisiwa!

Waamini wanahamasishwa kuwa ni watangazaji wa Injili ya furaha
Waamini wanahamasishwa kuwa ni watangazaji wa Injili ya furaha

Baba Mtakatifu Francisko anabainisha nguzo kuu saba za uinjilishaji zinazopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika mwono wa Uinjilishaji Mpya: Mageuzi ndani ya Kanisa kwa kutambua kwamba, Kanisa kimsingi ni la Kimisionari; vishawishi vya Wainjilishaji, Kanisa kama Familia ya Mungu inayotumwa Kuinjilisha; Mahubiri na matayarisho yake; Ushiriki wa kijamii wa maskini katika maisha na utume wa Kanisa; Amani na majadiliano ya kijamii na kiini cha kazi ya Uinjilishaji inayofanywa na Mama Kanisa. Yote haya yanafumbatwa kwa umakini mkubwa katika huruma na upendo mfunuliwa wa Mungu unaogusa moyo wa kila mtu kwa kukutana na Kristo Yesu, chemchemi ya furaha inayomsukuma mwamini kushirikisha upendo huu kwa wengine. Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume. Rej. Mt 9:9-13. Hii ndiyo tema iliyokuwa inaongoza mzunguko wa Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 11 Januari 2023 na sasa umefikia ukomo. Hii ni tema ya dharura na madhubuti kwa maisha ya Kikristo. Baba Mtakatifu anasema, Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume ni mambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuwa, jumuiya ya waamini inazaliwa kwa sababu ya utume na umisionari, huku ikisukumwa na Roho Mtakatifu, waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Huu ndio mwelekeo na dira ya utume na maisha ya Kikristo, vinginevyo, Wakristo wanaweza kujikuta wakijitafuta wao wenyewe katika ubinafsi wao. Bila ya kuwa na shauku ya uinjilishaji, imani itadhohofu na hatimaye, kunyauka na utume ndicho kiini cha maisha ya mwamini.

Waraka wa Kitume Furaha ya Injili Unaadhimisha Miaka 10 tangu uchapishwe
Waraka wa Kitume Furaha ya Injili Unaadhimisha Miaka 10 tangu uchapishwe

Kumbe, mzunguko wa katekesi hii ulipania kupyaisha shauku ya uinjilishaji kwa kuzama zaidi katika: Maandiko Matakatifu sanjari na Mafundisho Tanzu ya Mama Kanisa ili kuchota amana na utajiri wa ari, mwamko na bidii ya kitume. Katika mzunguko huu, Baba Mtakatifu amejitahidi kuweka mbele ya waamini mifano hai na baadhi ya mashuhuda wa imani, walioamsha shauku ya Habari Njema ya Wokovu, ili wawasaidie waamini kuwasha tena ule moto wa Roho Mtakatifu, ili hatimaye, uweze kuzijaza nyoyo za waamini wote mapendo. Ni katika muktadha huu, wakristo wanapaswa kujitahidi katika maisha yao ya kila siku kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili; huruma na upendo wa Kristo Yesu unaoganga, kuponya na kuwaokoa watu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. “Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku. Malaika wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang’aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu. Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.” Lk 2: 8-11. Hii ni sehemu ya Injili iliyonogesha Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 15 Novemba 2023 kwamba, uinjilishaji unapata chimbuko lake kutoka katika kisima cha Injili ya furaha kama ilivyokuwa kule kondeni wakati Malaika wanatangaza habari ya kuzaliwa kwa Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.

Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya waami: Wito wa Utume
Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya waami: Wito wa Utume

Wakristo wanapaswa kuratibu hisia zao hasa katika nchi zile ambazo Kanisa linakabiliana na changamoto pamoja na kinzani za kijamii, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya furaha inayosimikwa katika hali ya unyenyekevu na utu wema mambo msingi yanayo shuhudiwa na mwamini baada ya kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yake. Kumbe, kuzaliwa kwa Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha inayopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Hii ndiyo furaha waliyokuwa nayo wafuasi wa Emau kama anavyosimulia Mwinjili Luka sura ya 24: 1-53, kwa hakika Injili ya Luka ni Injili ya furaha na faraja kama wanavyo shuhudia wafuasi wa Emau. Hii ni furaha ya Pasaka changamoto na mwaliko kwa Wakristo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya furaha hasa katika maeneo ambamo kuna changamoto ya imani na hali ya kukatisha tamaa kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Emau waliokuwa na huzuni pamoja na hali ya kukata tamaa, wafungwa wa matumaini yao yaliyoyeyuka kama ndoto ya mchana kutokana na kashfa ya Msalaba, lakini kwa kukutana mubashara na Kristo Mfufuka, hapo furaha inachanua upya kama maua ya kondeni. Wahusika wakuu wa uinjilishaji ni Mitume wanaohamasishwa kumtafuta, ili hatimaye, waweze kumgundua Kristo Yesu anayeambatana nao, huku akiwafafanulia Maandiko Matakatifu, inakuwa ni fursa ya kukuza na kuimarisha imani na hivyo kuondokana na mawazo yaliyowapelekea kumezwa na malimwengu. Kukutana na Kristo Yesu mubashara na kwa njia ya Neno lake kunapyaisha uwepo na upendo wa Kristo Yesu katika kuumega Mkate. Na katika tukio hili wafuasi wanafunguliwa macho na kumtambua, kiasi cha kuondoka kwa haraka ili kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha ambayo kimsingi ni zawadi ya Roho ya Kristo Mfufuka.

Wito ni kutangaza na kushuhudia Injili ya Furaha kwa watu wote
Wito ni kutangaza na kushuhudia Injili ya Furaha kwa watu wote

Katika Ulimwengu mamboleo, Wakristo ndio wadau wa mchakato wa uinjilishaji wanaoitwa na kutumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka, bila ya kutumbukia kwenye kishawishi kwamba, kazi ya uinjilishaji inaweza kutekelezwa na watu wengine. Kuhubiri upya kunaweza kuwapa waamini, pamoja na wale waliolegea na wasioiishi imani yao, furaha mpya katika imani na uaminifu katika kazi ya uinjilishaji. Wakristo wanapojitahidi kurudi katika chanzo na kuupata tena ule upya wa asili wa Injili, mwelekeo mpya huonekana, njia mpya za ubunifu hufunguka na uinjilishaji unapyaishwa. Daima wema hutaka kusambaa. Kila mara ukweli halisi na wa uhakika unapotambulika, kwa asili yake unatafuta namna ya kukua ndani mwa waamini na mtu yeyote aliyewahi kupata ukombozi wa ndani huwa mwepesi zaidi kutambua mahitaji ya wengine. Rej. Evangelii gaudium No, 9 & 11. Kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Emau kurejea tena katika uhalisia wa maisha yao baada ya kukutana na amana na utajiri wa imani, Wakristo pia wanapaswa kutambua kwamba, kuna watu wanaosubiri neno la matumaini na kwamba, watu wa kila nyakati wana kiu ya Neno la Mungu hata katika walimwengu mamboleo kwa sababu kuna utupu wa maisha ya kiroho unaoachwa wazi. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume Furaha ya Injili, “Evangelii gaudium” anaendelea kusema, furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Kristo Yesu. Wale wanaoikubali zawadi yake ya ukombozi wanawekwa huru kuondokana na dhambi, uchungu, utupu wa ndani na upweke. Pamoja na Kristo Yesu, daima furaha inazaliwa upya.” Evangelii gaudium, 1. Huu ni mwaliko kwa kila mwamini, mahali popote pale alipo kupyaisha mkutano wake na Kristo Yesu kwa sababu Kristo Yesu ni chanzo cha uinjilishaji na kiini cha furaha.

Papa Injili ya Furaha
15 November 2023, 14:27

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >