Tafuta

Katekesi Kuhusu Fadhila Na Mizizi ya Dhambi: Fadhila Kuu: Busara

Kuna fadhila kuu nne zinazotenda kazi kama bawaba ndiyo maana zinaitwa “Kuu.” Fadhila nyingine zote zajikusanya kuzizunguka nazo ni: Busara, haki, nguvu na kiasi. Kama mtu anapenda haki, basi fadhila ni matunda ya juhudi yake; kwani hufundisha kiasi na ufahamu, na haki na ushujaa. Fadhila hizi zasifiwa katika matini mbalimbali za Maandiko Matakatifu kwa majina mengine. Rej. KKK 1805. Fadhila ya busara inapaswa kupewa kipaumbele cha pekee kwa wakati huu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Mizizi ya dhambi, vilema vikuu vya dhambi au vichwa vya dhambi ni orodha ya maovu ambayo tangu zamani za Mababa wa Kanisa katika kanuni maadili ya Ukristo yanahesabiwa kumuelekeza binadamu kutenda dhambi nyingine, hata kubwa zaidi. Mizizi ya dhambi iko saba nayo ni: Majivuno, uzembe, kijicho, hasira, uroho, utovu wa kiasi na uzinzi, si dhambi kuu kuliko zote; lakini ndivyo vilema tunavyovielekea kwanza na ndivyo vinavyomsogeza mwanadamu mbali zaidi na Mwenyezi Mungu na hivyo kumtumbukiza katika makosa makubwa zaidi kama vile: uzushi, uasi wa dini, kukata tamaa na hatimaye, kumchukia Mungu. Mtu hafikii uovu mkubwa mara moja, bali polepole na hatua kwa hatua.  “Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.” Flp 4:8. Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, fadhila ni tabia ya kawaida na imara ya kutenda mema. Yamruhusu mtu si kutenda mema tu bali kutoa kilicho chema kabisa cha nafsi yake. Mtu wa fadhila huelekea mema kwa hisi zake zote pamoja na nguvu za kiroho. Hutafuta mema na kuyachagua kwa matendo halisi. Kuna fadhila za kibinadamu ambayo ni hali thabiti, maelekeo imara, ukamilifu wa kawaida wa akili na utashi zinazotawala matendo ya binadamu, zinazoratibu harara na kuongoza mwenendo kufuata akili na imani. Zinawezesha raha, kujitawala na furaha katika kuishi maisha mema kimaadili. Fadhila adili hupatikana kwa juhudi za kibinadamu kuungana na upendo wa Mungu. Shabaha ya mtu mwenye fadhila ni kuwa kama Mungu. Kuna fadhila kuu ambazo hutenda kazi kama bawaba nazo ni: Busara, haki, nguvu, na kiasi. Rej. KKK 1803-1803. Kuna fadhila tatu za Kimungu: imani, matumaini na mapendo.

Fadhila za Kimungu: Imani, Matumaini na Mapendo
Fadhila za Kimungu: Imani, Matumaini na Mapendo

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 27 Desemba 2023 alianza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu fadhila na mizizi ya dhambi mambo msingi katika kuulinda moyo. Baba Mtakatifu amekwisha kuchambua mizizi hii ya dhambi hatua kwa hatua na kwamba, tiba ya uvivu ni uvumilivu wa kiimani. Amezungumzia pia kuhusu wivu, utepetevu, uchoyo, majivuno na sasa ameanza kutafakari kuhusu fadhila. Kuna fadhila kuu nne zinazotenda kazi kama bawaba ndiyo maana zinaitwa “Kuu.” Fadhila nyingine zote zajikusanya kuzizunguka nazo ni: Busara, haki, nguvu na kiasi. Kama mtu anapenda haki, basi fadhila ni matunda ya juhudi yake; kwani hufundisha kiasi na ufahamu, na haki na ushujaa. Fadhila hizi zasifiwa katika matini mbalimbali za Maandiko Matakatifu kwa majina mengine. Rej. KKK 1805. Mababa wa Kanisa wanasema, Busara ni fadhila inayoiandaa akili ya kawaida kupambanua katika mazingira yote mema yetu ya kweli na kuchagua njia zitakiwazo kuyapata. “Mtu mwenye busara huangalia sana aendavyo. Iweni na akili, mkeshe katika sala. Busara ni sheria sahihi ya utendaji ameandika Mtakatifu Thoma wa Akwino, akimfuata Aristotle. Busara isichanganwe na hofu au woga, wala hila au udanganyifu. Hekima huitwa “Auriga virtutum” yaani “Mwendesha fadhila; huongoza fadhila nyingine kwa kuweka sheria na kipimo. Ni busara inayoongoza mara moja hukumu ya dhamiri. Mtu mwenye busara huamua na kuongoza mwenendo wake kulingana na hukumu hiyo. Kwa msaada wa fadhila hii tunatumia misingi ya maadili katika masuala ya pekee bila kosa na kushinda mashaka ya mema ya kupata, na mabaya ya kuepuka. Rej. KKK. 1806.

Fadhila za Kibinadamu: Busara, haki, nguvu na kiasi
Fadhila za Kibinadamu: Busara, haki, nguvu na kiasi

Hii ni sehemu ya Katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 20 Machi 2024 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kusomwa kwa niaba yake na Monsinyo Pierluigi Giroli kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican na kusema kwamba, busara ni kati ya tema zilizokuwa na mvuto mkubwa kwa wanafalsafa wa Kigiriki katika mchakato wa utamadunisho kiasi kwamba, wanataalimungu wa Kikristo wakataja fadhila za Kimungu zinazowaandaa waamini kuishi katika uhusiano na Fumbo la Utatu Mtakatifu. Nazo zina Mungu mmoja, na Mwenye Nafsi Tatu, kama chanzo chao, sababu yao na lengo lao. Fadhila hizi ni: Imani, Matumaini na Mapendo. Kuna fadhila za kibinadamu nazo ni: Busara, haki, nguvu na kiasi. Fadhila za kibinadamu ni maelekeo imara ya akili na utashi yanayotawala matendo ya binadamu, yanayorekebisha harara na kuongoza tabia ya mwanadamu kwa kufuata akili na imani. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, mtu mwenye busara ni mbunifu, anayefikiri kwanza kabla ya kutenda, anajitahidi kufahamu hali na mazingira halisi na kamwe si mtu anayetawaliwa na hisia, uvivu na msongo wa mambo ya kufikirika. Katika ulimwengu unaoelemewa na mambo ya kufikirika katika wema na ubaya, kuna haja kwa fadhila ya busara kupewa kipaumbele cha pekee. Hekima huitwa na Mtakatifu Thoma wa Akwino na akina Aristotle “Auriga virtutum” yaani “Mwendesha fadhila; huongoza fadhila nyingine kwa kuweka sheria na kipimo. Maisha yakibaki tu vitabuni yanavutia sana, lakini msukosuko na mawimbi makubwa ya bahari katika maisha yanahitaji busara. Hata wenye busara kuna wakati wanaweza kukosea, lakini busara humwongoza mtu kutenda kwa haki, ustawi na maendeleo ya wengi.

Busara humwongoza mtu kutenda kwa haki
Busara humwongoza mtu kutenda kwa haki

Busara inamfundisha mtu kuwatofautisha maadui. Mtu mwenye busara anafahamu kutunza kumbukumbu ya mambo yaliyopita na kuyatumia kama amana na busara katika kutatua matatizo na changamano za maisha. Mtu mwenye busara akibainisha njia za kupitia, atatafuta kila njia ili aweze kufikia lengo lake. Sehemu nyingi za Maandiko Matakatifu zinaweza kuwasaidia waamini kujifunza kuhusu busara katika maisha: umuhimu wa ujenzi wa nyumba juu ya mwamba. Rej Mt 7: 24-27. Mfano wa wanawali kumi: watano wao walikuwa wapumbavu na watano wenye busara. Rej Mt 25: 1-3. Itakumbukwa kwamba, maisha ya Kikristo ni mchanganyiko wa urahisi na busara. Kristo Yesu aliwaandaa Mitume wake kwa ajili ya kushiriki Utume wake akisema, “Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa-mwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua.” Mt. 10:16. Mwenyezi Mungu anawataka watu wote kuwa watakatifu wenye akili na busara, kwa sababu bila busara ni rahisi kutembea katika njia mbaya. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii, kuwatakia heri na baraka waamini wote katika maandali ya Maadhimisho ya Juma kuu yaani kumbukumbu ya: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu, kiini cha imani na matumaini ya Kikristo. Kumbe, hija hii ya Kipindi cha Kwaresima iwajalie kushiriki furaha ya Pasaka, huku nyoyo zao zikiwa zimetakaswa na kupyaishwa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Waamini wahakikishe kwamba, wanaongozwa na busara katika kufikiri, kuamua na kutenda.

Fadhila ya Busara
20 March 2024, 15:02

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >