Tafuta

Papa esorta seminaristi, preghiera, studio, fraternit�, missione

Mambo Msingi Katika Malezi na Majiundo ya Kipadre: Sala, Masomo, Udugu na Utume

Katika hotuba yake amekazia: Maisha ya sala, masomo, utume na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu amempongeza Askofu mkuu Josep wa Jimbo kuu la Siviglia kwa kufika mjini Roma ili kutembelea makaburi ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani. Ni muda wa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya imani iliyotangazwa na kushuhudiwa na Mitume wa Kristo Yesu. Padre Chesco Peter Msaga, ametia neno kuhusu miito, ukuaji wa Kanisa la Tanzania na umisionari

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Mwongozo wa Malezi ya Kipadre unaojulikana kama “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre” ni muhtasari wa mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika malezi na majiundo ya kipadre ambayo yanapaswa kupyaishwa, kuendelezwa na kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Mama Kanisa kwa kusoma alama za nyakati. Mwongozo wa sasa unazingatia na kukidhi mahitaji msingi ya malezi na majiundo ya Kipadre ili kuweza kukabiliana na changamoto za ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ni mwongozo unaotoa mwelekeo na uwiano sahihi wa malezi: kiutu, kiroho, kiakili na kichungaji kwa njia ya safari ya malezi na majiundo makini ya Kipadre, taratibu, lakini kila jandokasisi akiangaliwa kwa jicho la pekee. Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo anakabiliana na changamoto nyingi kati yake ni: Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano. Kutokana na changamoto zote hizi, Kanisa limeona kwamba, kuna busara ya kuanzisha, kupyaisha na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi na majiundo ya Kipadre katika maisha na utume wa Kanisa.Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, amekuwa ni changamoto kubwa ya kuangalia tena mchakato wa malezi na majiundo ya maisha, wito na utume wa Kipadre ndani ya Kanisa kwa kuendelea kusoma alama za nyakati, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Hii inatokana na ukweli kwamba, Mapadre si watu wa mshahara, bali ni wachungaji wa familia ya Mungu, wanaopaswa kwa namna ya pekee, kuwa ni watu wasikivu, wenye huruma na upendo kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Aliwaonea watu huruma, akawasikiliza kwa makini, akawaganga na kuwaponya, akawasamehe dhambi zao na kuwapatia tena furaha ya kuendelea kuishi kwa imani na matumaini, kwani walikuwa wameonja na kukutana na Uso wa huruma ya Mungu katika safari ya maisha yao!

Muhimu: Malezi na majiundo ya Kipadre
Muhimu: Malezi na majiundo ya Kipadre

Kumbe, majiundo na malezi makini ya Kipadre ni kiini cha maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu, ili kweli Kanisa liweze kuwapata Mapadre wema, watakatifu na wachapakazi wanaoweza kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Maaskofu wanawajibika sana katika malezi na majiundo ya Majandokasisi pamoja na wakleri wao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo! Hapa mkazo ni kuwa na muungano kamili na endelevu wa majiundo na malezi ya Kipadre: kiutu, kiroho, kiakili na katika shughuli za kichungaji. Malezi ya kiutu yanamtaka Jandokasisi kuwa na ukomavu na uwiano mzuri kati ya maisha ya kiroho na kiutu; mahusiano kati ya watu yanayojikita katika heshima na nidhamu. Bila ya kuwa na jicho la kichungaji, matatizo na changamoto zinazoweza kujitokeza katika maisha ya majandokasisi, yanaweza kuwa ni mzigo mkubwa kwa siku za baadaye kwa Padre mwenyewe na kwa ajili ya familia ya Mungu inayomzunguka. Hapa hakuna njia ya mkato, kila hatua inapaswa kushughuliwa kikamilifu pasi na haraka wala upendeleo, ili kuhakikisha ukomavu wa jandokasisi. Lazima kuwepo na malezi endelevu yanayomsaidia mseminari kupata mambo msingi katika maisha na utume wake wa Kipadre hapo baadaye. Kumbe, majiundo ya falsafa, taalimungu na shughuli za kichungaji yameboreshwa kwa kuongezewa tena majiundo ya kitume, utambulisho wa wito na utume wa Kipadre, ili kuweza kuwa na mwelekeo mkamilifu wa Kristo Yesu mchungaji mwema. Padre mwema, mtakatifu na mchapakazi hapatikani kwa kufaulu vyema masomo na mitihani yake, bali anahitaji kuwa na ukomavu wa kiutu, maisha ya kiroho na shughuli za kichungaji. Awe makini na lugha anayoitumia katika maisha na utume wake bila kusahau mbinu msingi za malezi na majiundo. Mambo makuu mawili yamepewa kipaumbele cha kwanza: “Utu”, yaani, waseminari wanapaswa kusindikizwa ili waweze kuwa na ukomavu katika utu wa binadamu, ili kweli waweze kupenda na kupendwa katika hali ya ukomavu; watu huru kutoka katika sakafu ya maisha yao; watu wanaoweza kujenga na kudumisha mahusiano ya kijamii; watu wenye amani na utulivu wa ndani; wanaoweza kutoa, kupokea na kumwilisha Mashauri ya Kiinjili katika maisha yao bila shuruti, unafiki wala kutafuta njia ya mkato.

Majiundo ya Kipadre: Sala, masomo, utume na udugu wa kibinadamu
Majiundo ya Kipadre: Sala, masomo, utume na udugu wa kibinadamu

Pili ni “Tasaufi” neno lililopewa kipaumbele cha pekee katika malezi na majiundo ya kipadre kwa kufunda dhamiri nyofu mintarafu maisha na wito wa Kipadre. Ikumbukwe kwamba, Padre si mfanyakazi wa mshahara wala mfanyabiashara anayelitumia Kanisa kwa ajili ya mafao yake binafsi. Padre ni mfuasi wa Kristo Yesu anayejisadaka kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake, kwa kujenga na kudumisha mahusiano ya pekee na Kristo Yesu kwa njia ya Neno, Sakramenti, Matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na sadaka binafsi, kielelezo cha Kristo Yesu mchungaji mwema. Mapadre wanapaswa kuboresha maisha yao ya kiroho yanayofumbatwa katika tunu msingi za Kiinjili kwa kujisikia kuwa na Kanisa kwa ajili ya Kanisa kama alivyokuwa kwa Kristo Yesu. nMapadre wanapaswa kuwa ni watu wa “Huduma” yaani “Wasamaria wema”, watu wenye huruma, upendo na msamaha. Hawa ni watu wanaopaswa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini, kwani katika maisha na utume wao, watakutana na watu wenye kiu ya kusikilizwa; watu wanaweza kuanzisha na kudumisha mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi pasi ya kuwa na jazba au kutaka kulipiza kisasi. Ikumbukwe kwamba, ndani ya familia ya Mungu kuna watu ambao wamejeruhiwa vibaya wanapaswa kugangwa na kuponywa na huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, ushauri makini na ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Majandokasisi wanapaswa kuondokana na tabia ya kujifungia katika uchoyo na ubinafsi wao, tayari kujielekeza katika mwono mpana utakaowapatia mang’amuzi ya kina katika maisha na utume wao kwa siku za baadaye, kama Mapadre! Baadhi yao wanaishi na kufanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi, kumbe, wanahitaji kusindikizwa kwa njia ya sala na sadaka, ili kamwe wasikate tamaa, hata pale wanapoteleza na kuanguka katika udhaifu wa kibinadamu wawe na ujasiri wa kusimama na kusonga mbele kwa imani na matumaini. Padre ni ufunguo wa malango ya huruma, msamaha na upendo wa Mungu kwa binadamu! Ikumbukwe kwamba, wito na maisha ya Upadre ni neema na zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kumwilishwa katika fadhila ya huruma na mapendo kwa Mungu na jirani.

Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema, Siku ya 61 ya Kuombea Miito
Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema, Siku ya 61 ya Kuombea Miito

Ni katika muktadha wa malezi, majiundo na makuzi ya wito, maisha na utume wa Mapadre, Majandokasisi kutoka Seminari kuu ya “Redemptoris Mater” Jimbo kuu la Siviglia, nchini Hispania, Jumamosi tarehe 20 April 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Katika hotuba yake amekazia zaidi kuhusu: Maisha ya sala, masomo, utume na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu amempongeza Askofu mkuu Josep Angel Saiz Meneses wa Jimbo kuu la Siviglia kwa kufika mjini Roma ili kutembelea makaburi ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani. Ni muda muafaka wa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya imani iliyotangazwa na kushuhudiwa na Mitume wa Kristo Yesu. Huu ni mkutano ambao umefanyika katika mkesha wa Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji mwema. Baba Mtakatifu amewakumbusha kwamba, wao wako katika malezi na makuzi yao mintarafu Moyo Mtakatifu wa Yesu. Amewataka Majandokasisi kujikita zaidi na zaidi katika: Maisha ya sala, masomo, utume na udugu wa kibinadamu kwa kutambua kwamba, Upadre ni zawadi kubwa kwa Mungu na jirani zao. Mtumishi wa Mungu Kardinali Marcello Spignola Maestre “Marcello Spinola y Maestre”; Baba na mlezi wa Mapadre ambaye katika maisha na utume wake alikazia fadhila na sayansi katika malezi, maisha na utume wa Mapadre kimsingi yanafumbata: Maisha ya sala, masomo, utume na udugu wa kibinadamu. Kumbe kipindi cha malezi na makuzi ya wito, maisha na utume wa Mapadre iwe ni fursa ya kujisadaka bila ya kujibakiza katika majiundo kadiri ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, huku wakiwa wamepanua mikono yao kwa tabasamu la “kukata na soka” waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya furaha kwa wale wote watakaokutana nao katika safari ya maisha yao!

Kwa sasa kuna baraka na neema ya miito mingi ya Kipadre na Kitawa Tanzania
Kwa sasa kuna baraka na neema ya miito mingi ya Kipadre na Kitawa Tanzania

Padre Chesco Peter Msaga, C.PP.S., Naibu Katibu mkuu, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, katika mahojiano maalum na Radio Vatican anaelezea kuhusu kukua na kuendelea kushamiri kwa Kanisa Katoliki nchini Tanzania, kwa idadi ya Majimbo, Parokia na Vigango baraka na neema ya ongezeko la miito pamoja na changamoto zake na kwamba, kuna idadi kubwa ya wamisionari kutoka Tanzania wanaotekeleza dhamana na wajibu wao ughaibuni.  

Malezi ya Kipadre
21 April 2024, 15:22