Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 12 Aprili 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Mfuko wa Papa waliofika mjini Vatican kumtembelea na kuwasilisha mchango wao wa maendeleo. Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 12 Aprili 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Mfuko wa Papa waliofika mjini Vatican kumtembelea na kuwasilisha mchango wao wa maendeleo.  (Vatican Media)

Boresheni Maisha Yenu ya Kiroho: Kwa Sala, Neno, Ibada na Ushiriki Mkamilifu katika Utume

Papa Francisko tarehe 12 Aprili 2024 amekutana na wajumbe wa Mfuko wa Papa waliofika kumtembelea pamoja na kuwasilisha mchango wao kwa ajili ya shughuli za maendeleo zinazosimamiwa na kuendeshwa na Papa Francisko katika kipindi cha mwaka 2024. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake ameushukuru na kuupongeza Mfuko wa Papa kwa kuwa ni kielelezo cha ukaribu, huruma na upole wa Kristo Yesu kwa wahitaji sehemu mbalimbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Mfuko wa Papa: “Papal Foundation” ni Shirika pekee la hisani kutoka nchini Marekani ambalo limejizatiti kwa ajili ya kusaidia juhudi za Khalifa wa Mtakatifu Petro kugharimia mahitaji ya Kanisa la Kristo! Mfuko huu ulianzishwa kunako mwaka 1988 na tangu wakati huo, zaidi ya dola za Kimarekani milioni 200 zimetolewa kama msaada au ruzuku pamoja na kugharimia miradi 2, 000 chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko, Benedikto XVI pamoja na Mtakatifu Yohane Paulo II. Fedha hii imetumika kwa ajili ya kugharimia ujenzi wa Makanisa 358; ufadhili wa masomo, malezi na majiundo kwa Majandokasisi 170; Ujenzi wa nyumba za Mapadre, Konventi za watawa na Monasteri 404. Mfuko pia umegharimia ujenzi wa Shule 273 pamoja na Hospitali 104. Huu ni ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 12 Aprili 2024 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Mfuko wa Papa waliofika mjini Vatican kumtembelea pamoja na kuwasilisha mchango wao kwa ajili ya shughuli za maendeleo zinazosimamiwa na kuendeshwa na Papa Francisko katika kipindi cha mwaka 2024. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake ameushukuru na kuupongeza Mfuko wa Papa kwa kuwa ni kielelezo cha ukaribu, huruma na upole wa Kristo Yesu kwa wahitaji sehemu mbalimbali za dunia. Huu ni ushiriki mkamilifu katika maisha na utume wa Kanisa sanjari na maadhimisho ya Mwaka wa Sala. Ufufuko wa Kristo Yesu ni kilele cha ukweli wa imani ya Kikristo, ambayo jamii ya kwanza ya wakristo iliusadiki na kuuishi kama kiini cha ukweli; waliiendeleza kama msingi kwa njia ya Mapokeo; waliithibitisha kwa njia ya Maandiko ya Agano Jipya; na wakaihubiri kama sehemu muhimu sana ya Fumbo la Pasaka yaani: mateso na kifo cha Kristo Msalabani.

Waamini waboreshe maisha yao ya kiroho kwa sala na ibada
Waamini waboreshe maisha yao ya kiroho kwa sala na ibada

Kristo amefufuka kwa wafu, kwa kifo chake alishinda dhambi na mauti na amewakirimia wafu uzima wa milele. Ufufuko kwa wafu ni ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Lile jiwe lililoonekana kuwa kizingiti, lilikuwa limeondolewa kaburini, mwaliko na changamoto kwa waamini kuyainua macho yao, tayari kumpokea katika maisha yao kwa kumwambia “Ndiyo.” Uwepo angavu wa Kristo Mfufuka ni chemchemi ya furaha na hakuna awaondoleaye. Rej. Yn 16:22. Mara nyingi wajumbe wa Mfuko wa Papa: “Papal Foundation” hufanya hija zao wakati wa kipindi cha Sherehe ya Pasaka ya Bwana. Huu mfuko umekuwa ni chombo na kielelezo cha ukaribu, huruma na upole wa Kristo Yesu kwa wahitaji sehemu mbalimbali za dunia. Wamekuwa ni wafadhili katika miradi ya elimu, huduma ya upendo na shughuli za kitume kwa ajili ya kukoleza maendeleo fungamani ya binadamu, bila kusahau huduma makini kwa maskini, wakimbizi na wahamiaji pamoja na waathirika wa majanga asilia pamoja na vita. Baba Mtakatifu amewashukuru wajumbe kwa kugharimia majiundo ya waamini walei, watawa, majandokasisi na mapadre kutoka sehemu mbalimbali za dunia, ili kuendelea na masomo yao katika vyuo vikuu vya Kipapa vilivyoko mjini Roma. Huu ni ushuhuda makini wa Injili, kwa watu wanaofaidika na mchango wao katika malezi na majiundo hata katika nchi zao asilia. Kwa njia ya huduma hii ya upendo, Mfuko wa Papa unaendelea kumwezesha Khalifa wa Mtakatifu Petro kusaidia ujenzi wa Makanisa na kutoa huduma kwa maskini na wale wote ambao Kristo Yesu amemkabidhi Mtakatifu Petro ili kuwaimarisha na kuwalisha. Rej. Lk 22:32; Yn 21:17. Baba Mtakatifu amewashukuru kwa moyo wao wa ukarimu na mapendo kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Mfuko wa Papa Umejizatiti kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa
Mfuko wa Papa Umejizatiti kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa

Baba Mtakatifu amewakumbusha kwamba, kazi yao inapata chimbuko lake katika imani ya Kanisa Katoliki, ambayo inapaswa kurutubishwa kila wakati, kwa ushiriki mkamilifu katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kupokea Sakramenti za Kanisa; Kwa kukuza na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na katika maisha ya Sala. Wajumbe wa Mfuko wa Papa wanafanya hija hii, wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka wa Sala, kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025. Mwaka wa Sala unapania pamoja na mambo mengine: Kugundua na kupyaisha umuhimu wa maisha ya sala katika maisha ya mtu binafsi, ndani ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025, yatazinduliwa rasmi kwa kufungua Lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican tarehe 24 Desemba 2024. Mwaka wa Sala Kuelelea Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 unapania pamoja na mambo mengine anasema Baba Mtakatifu Francisko ni: Kupyaisha matumaini baada ya watu wengi kukata na kujikatia tamaa ya maisha kutokana na hali ngumu ya maisha, vita na mipasuko ya kijamii bila kusahau athari za mabadiliko ya tabianchi.

Papa amewapongeza wajumbe wa Mfuko wa Papa.
Papa amewapongeza wajumbe wa Mfuko wa Papa.

Huu ni mkakati wa shughuli za kichungaji unaopania kuwarejeshea tena watu wa Mungu matumaini. Huu ni mwaliko kwa kila jimbo, baada ya kusoma alama za nyakati kwa watu wake, liandae katekesi kuanzia wakati huu, hadi wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Jubilei ya mwaka 2025 hapo tarehe 24 Desemba 2024. Katekesi hii ilenge kuwasaidia waamini kujiandaa kikamilifu kuingia katika lango la Jubilei, ambalo ni Kristo Yesu, Mwanakondoo Mungu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwa wadumifu katika sala, ili hatimaye waweze kuwa moyo mmoja na roho moja; Rej. Mdo. 4:32 katika Kristo Yesu pamoja na jirani zao, kielelezo cha mshikamano na ushirikiano katika kuumega mkate wa kila siku. Tunu hizi msingi ni muhimu sana kwa maboresho ya maisha ya kiroho ili kujenga na kudumisha muungano wa maisha ya kiroho na udugu kwa watu wenye tamaduni, lugha na dini mbalimbali wanaopokea pamoja na kunufaika na misaada inayotolewa na Mfuko huu wa Papa. Hii ni huduma muhimu sana katika ulimwengu mamboleo ambao umegubikwa na ubinafsi, uchoyo pamoja na ile hali ya kutoguswa na mahitaji ya watu wengine. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewatakia heri na baraka katika shughuli zao na hija yao mjini Roma. Amewaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa na mwishowe akawabariki wote.

Mfuko wa Papa
12 April 2024, 14:59