Tafuta

Ni katika muktadha wa kumbukizi ya miaka mia mbili tangu alipofariki dunia, Mtumishi wa Mungu Papa Pio VII, watu wa Mungu kutoka Majimbo ya Cesena-Sarsina, Savona, Imola na Tivoli Jumamosi tarehe 20 Aprili 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Ni katika muktadha wa kumbukizi ya miaka mia mbili tangu alipofariki dunia, Mtumishi wa Mungu Papa Pio VII, watu wa Mungu kutoka Majimbo ya Cesena-Sarsina, Savona, Imola na Tivoli Jumamosi tarehe 20 Aprili 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.   (Vatican Media)

Mtumishi wa Mungu Papa Pio VII: Shuhuda wa Ushirika, Uinjilishaji, Huruma na Upendo

Mtumishi wa Mungu Papa Pio VII alikuwa ni shuhuda wa: Ushirika wa Kanisa; utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu kwa ujasiri na mfano bora wa kuigwa na shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini. Anakumbukwa kwa kusimamia upendo katika ukweli, umoja, majadiliano, msamaha pamoja na kujikita kutafuta na kudumisha amani na utulivu wa ndani. Mtumishi wa Mungu Papa Pio VII alikazia ushirika wa Kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Mtumishi wa Mungu Papa Pio VII aliyejulikana kama Barnaba (Gregorio) Chiaramonti, O.S.B. alizaliwa huko Cesena, Italia tarehe 14 Agosti 1742. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa na kipadre tarehe 21 Septemba 1765 akapewa daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 16 Desemba 1782 akateuliwa kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Tivoli, Italia na kuwekwa wakfu tarehe 21 Desemba 1782. Tarehe 14 Februari 1785 akateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Imola na huko anakumbukwa sana kutokana na upendo wake kwa utamaduni. Tarehe 14 Februari 1785 Papa Pio VI akamteuwa kuwa ni Kardinali. Mkutano wa Baraza la Makardinali ukamchagua kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro tarehe 14 Machi 1800 na kusimikwa rasmi tarehe 21 Machi 1800. Alipowasili mjini Vatican alikumbana na hali ngumu sana ya kifedha na uchumi. Hiki kilikuwa ni kipindi cha uvamizi wa Mfalme Napoleon wa Ufaransa na hivyo majimbo mengi yalikuwa wazi, bila kuwa na Maaskofu katika azma ya kuwaongoza, kuwafundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu.

Mtumishi wa Mungu Papa Pio VII: Ushirika, Uinjilishaji na Huruma
Mtumishi wa Mungu Papa Pio VII: Ushirika, Uinjilishaji na Huruma

Katika "patashika shika hii nguo kuchanika," alikamatwa na kupelekwa kizuizini nchini Ufaransa. Tarehe 8 Machi 1816 akang’atuka kutoka madarakani, Jimbo Katoliki la Imola. Tarehe 20 Agosti 1823 akafariki dunia na kuzikwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Mama Kanisa mwaka 2024 anaadhimisha kumbukizi ya Miaka 200 tangu Mtumishi wa Mungu Papa Pio VII alipofariki dunia. Kwa hakika katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ameacha alama za kudumu kama Mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya Kondoo wake. Alikuwa ni msomi aliyebobea na mwenye ibada na uchaji wa Mungu kama: Mmonaki, Abate, Askofu na hatimaye, kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hata baada ya kukamatwa kwake, kuna baadhi ya watu walitaka kumtorosha kutoka kizuizini, lakini majibu yake yalikuwa “Non debemus, non possumus, non volumus” yaani “Hatupaswi, hatuwezi, hatutafanya” huku akijizatiti katika kukuza na kudumisha uhuru wake wa ndani, kama alivyokuwa ameapa wakati wa kusimikwa kwake kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kadiri ya neema na baraka za Mungu.

Alikuwa na upendo usiokuwa na kifani kwa watu wa Mungu
Alikuwa na upendo usiokuwa na kifani kwa watu wa Mungu

Ni katika muktadha wa kumbukizi ya miaka mia mbili tangu alipofariki dunia, Mtumishi wa Mungu Papa Pio VII, watu wa Mungu kutoka Majimbo ya Cesena-Sarsina, Savona, Imola na Tivoli nchini Italia, Jumamosi tarehe 20 Aprili 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amesema, Mtumishi wa Mungu Papa Pio VII alikuwa ni shuhuda wa: Ushirika wa Kanisa, Shuhuda wa utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu kwa ujasiri na mfano bora wa kuigwa na shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini. Anakumbukwa kwa kusimamia upendo katika ukweli, umoja, majadiliano, msamaha pamoja na kujikita katika kutafuta na kudumisha amani na utulivu wa ndani. Mtumishi wa Mungu Papa Pio VII alikazia ushirika wa Kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wao hasa kutokana na madhulumu na ukatili, mmong’onyoko wa kimaadili na tunu msingi za kiutu. Akatumia kikamilifu fursa hii iliyotaka kumnyanyasa na kumdhalilisha kwa kumtupa uhamishoni kama nguvu ya kujikita katika upendo kwa Kanisa, hali ambayo watu wa Mungu waliiona na kuishuhudia. Aliishi katika Jumuiya iliyokuwa imesiginwa na umaskini wa hali na kipato, lakini akaibuka kidedea, kama chombo na shuhuda wa ushirika wa Kanisa la kiulimwengu, na katika Majimbo, Parokia hadi kwenye kitovu cha familia. Ni kiongozi aliyejizatiti katika mchakato wa upatanisho, ujenzi wa haki na amani; uaminifu katika ukweli na upendo. Ni kiongozi ambaye hakushabikia mambo ya “umbea na majungu” na kama haya yote yangekuwa ni mtaji, wangetajirika wengi. Papa Pio VII alikazia ushirika na umoja wa Kanisa la Kristo Yesu.

Kumbukizi ya Miaka 200 tangu afariki dunia Papa Pio VII
Kumbukizi ya Miaka 200 tangu afariki dunia Papa Pio VII

Alikuwa ni shuhuda na chombo maarufu cha kutangaza na kushuhudia kwa ujasiri tunu msingi za Kiinjili kwa njia ya maneno, lakini zaidi kwa ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko. Akajizatiti katika kushuhudia unyenyekevu, uvumilivu, kiasi na upendo wa dhati, daima akasimama kidedea kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; mambo yaliyopelekea kukinzana na viongozi wakuu wa dunia kwa wakati wake. Papa Pio VII licha ya hali ngumu aliyokabiliana nayo kutokana na utawala wa Mfalme Napoleon, lakini alifanikiwa kuleta mageuzi katika maisha na utume wa Kanisa; akaonesha upendeleo wa pekee kwa maskini na wale wote waliokuwa wakisukumizwa pembezoni mwa jamii; akasimama kidete kupinga ukatili na kuanza kuboresha huduma za afya na tafiti za kisayansi  Mtumishi wa Mungu Papa Pio VII aliliongoza Kanisa kwa akili sana na busara, akaonesha huruma, upendo na msamaha kwa watesi wake; akawaonesha ukarimu. Kimsingi Mtumishi wa Mungu Papa Pio VII anakumbukwa kwa kusimamia upendo katika ukweli, umoja, majadiliano, msamaha pamoja na kujikita katika kutafuta na kudumisha amani na utulivu wa ndani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni amana na utajiri mkubwa kutoka kwa Mtumishi wa Mungu Papa Pio VII, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuutafakari kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jumuiya za Kikristo. Alikuwa ni mpole kama njia, lakini mwerevu kama nyoka!

Papa Pio VII

 

20 April 2024, 14:22