Tafuta

Mkutano wa Ulimwengu wa Udugu wa Kibinadamu, kuhusu Udugu wa kibinadamu kwa mwaka 2024 unaonogeshwa na kauli mbiu “Be Human." Mkutano wa Ulimwengu wa Udugu wa Kibinadamu, kuhusu Udugu wa kibinadamu kwa mwaka 2024 unaonogeshwa na kauli mbiu “Be Human."  (Vatican Media)

Majadiliano Katika Ukweli Na Uwazi Ni Muhimu Katika Kudumisha Amani Duniani

Papa amekazia kuhusu: huruma, utu, heshima, na haki msingi za binadamu kama Katiba ya Binadamu; huu ni mwaliko kwa wajumbe kujikita katika majadiliano. Baba Mtakatifu amewapongeza wajumbe kwa kuendelea kujizatiti kusimamia haki, amani, ustawi na maendeleo ya binadamu, kwa kuishi pamoja kama ndugu wamoja. Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa huruma kama inavyofafanuliwa kwa Mfano wa Msamaria mwema, maarufu kama Injili ya Msamaria mwema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko wa: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ni kitovu cha Mamlaka Matakatifu ya Ufundishaji katika Kanisa, mintarafu masuala ya kijamii kadiri ya Baba Mtakatifu Francisko. Huu ni muhtasari wa mafundisho, hotuba na mawazo yake tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kunako mwaka 2013. Waraka huu wa kijamii unachota amana na utajiri mkubwa kutoka katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu uliotiwa mkwaju kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Baba Mtakatifu anawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha utamaduni wa amani unaosimikwa katika majadiliano ya kidini; huruma, mshikamano, maendeleo endelevu na fungamani. Mkutano wa Ulimwengu wa Udugu wa Kibinadamu, kuhusu Udugu wa kibinadamu unaonogeshwa na kauli mbiu “Be Human” kuanzia tarehe 10 hadi 11 Mei 2024 umeandaliwa na Mfuko wa Udugu wa Kibinadamu unaopania pamoja na mambo mengine kumwilisha mawazo msingi yaliyobainishwa kwenye Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko wa: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” ili kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu; sanaa; majiundo pamoja na kukoleza majadiliano na walimwengu. Mkutano huu wa Kimataifa unawashirikisha watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia wakiwa ni: Washindi wa Tuzo ya Nobel, wanasayansi, wasanii, maprofesa, mameya, madaktari, mameneja, wafanyakazi pamoja na mabingwa wa michezo, wamekusanyika kwa pamoja ili kujadiliana jinsi ya kukuza na kudumisha thamani ya udugu wa kibinadamu miongoni mwa watu wa Mataifa, wakati ambapo vita, hofu na misigano ya kijamii inaendelea kuwaka moto sehemu mbalimbali za dunia.

Wajumbe wa Mkutano wa Ulimwengu wa Udugu wa Kibinadamu
Wajumbe wa Mkutano wa Ulimwengu wa Udugu wa Kibinadamu

Wajumbe wa Mkutano wa Ulimwengu wa Udugu wa Kibinadamu,  kuhusu Udugu wa kibinadamu, Jumamosi tarehe 11 Mei 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia kuhusu: huruma, utu, heshima, na haki msingi za binadamu kama Katiba ya Binadamu; huu ni mwaliko kwa wajumbe kujikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli na uwazi. Baba Mtakatifu amewapongeza wajumbe kwa kuendelea kujizatiti kusimamia haki, amani, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu, kwa kuishi pamoja kama ndugu wamoja. Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa huruma kama inavyofafanuliwa kwa Mfano wa Msamaria mwema, maarufu kama Injili ya Msamaria mwema. “Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu, Na jirani yangu ni nani? Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang’anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa. Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipita kando. Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapita kando. Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa. Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi? Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.” Lk 10: 25-37. Wito kwa kila mwamini ni kuwa na huruma kwa maskini na wale wote wanaoteseka na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Majadiliano katika makundi yasaidie kuibua Katiba ya Ubinadamu inayobainisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu amewataka kuendeleza majadiliano katika ukweli na uwazi na kwamba, vita ni dalili za kushindwa kwa binadamu. Maisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu ni kati ya mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, yote haya yafanyike kwa kuzingatia unyenyekevu.

Papa amekazia kuhusu: Huruma, utu na heshima ya binadamu
Papa amekazia kuhusu: Huruma, utu na heshima ya binadamu

Kwa upande wake, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika hotuba yake ya ufunguzi, amekazia umuhimu wa majadiliano katika ukweli kama njia ya ujenzi wa misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo endelevu. Mwenyezi Mungu amewaumba binadamu ili waweze kuishi kwa amani, walinde na kutunza mazingira nyumba ya wote; kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kardinali Parolin anaendelea kufafanua kwamba, ujenzi wa amani ni wito wa kweli wa binadamu na wala hakuna vita halali duniani! “Dhana ya vita halali imepitwa na wakati” huu ni muda muafaka wa kujenga kanuni maadili zinazolenga kukuza na kudumisha misingi ya haki na amani, ili kupambana na vita pamoja na mauaji ya kimbari.  Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma ni chemchemi ya furaha, amani na utulivu wa ndani, unaopaswa kukita mizizi yake katika sakafu ya moyo wa mwanadamu; kwa mwelekeo huu, amani inakuwa ni chachu ya upatanisho kati ya watu wa Mataifa. Amani ni changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo unaoendelea kuogelea katika vita, kinzani na mipasuko mbalimbali ya kijamii! Vita ni chanzo kikuu cha umaskini, magonjwa na majanga katika maisha ya mwanadamu; lakini amani ni utamaduni unaodumisha Injili ya uhai, ustawi na maendeleo ya wengi. Silaha za vita na maangamizi ni kielelezo cha matumizi mabaya ya rasilimali fedha ambayo ingeweza kutumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na badala yake zinakuwa ni chanzo cha maafa. Amani ni amana na wajibu kwa watu wote wenye mapenzi mema kwani vita haina macho wala pazia! Hakuna kinachoweza kupotea kwa njia ya amani, lakini vita ni chanzo cha uharibifu mkubwa wa maisha ya binadamu! Amani ya kweli inapata chimbuko lake kutoka katika sakafu ya maisha ya mwanadamu. Kumbe kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika ujenzi wa haki jami.

Huruma kama inavyofafanuliwa kwenye Injili ya Msamaria mwema
Huruma kama inavyofafanuliwa kwenye Injili ya Msamaria mwema

TAMKO KUHUSU UDUGU WA KIBINADAMU, ROMA, lililotiwa mkwaju kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro Mjini Vatican Juni 10, 2023 "Sisi ni watu mbalimbali, sisi ni tofauti, tuna tamaduni na dini tofauti, lakini sisi ni ndugu na dada na tunataka kuishi kwa amani" (Papa Francisko). Kila mwanaume ni kaka yetu, kila mwanamke ni dada yetu, siku zote. Tunataka wote tuishi pamoja, kama kaka na dada katika bustani ambayo ni Dunia. Bustani ya udugu ni hali ya maisha yote. Sisi ni mashuhuda wa jinsi, katika kila kona ya dunia, maelewano yaliyopotea yanachanua tena wakati utu unaheshimiwa, machozi yanafutwa, kazi inalipwa kwa haki, elimu ni uhakika, afya inatunzwa, utofauti unathaminiwa, asili inarudishwa, haki inaheshimiwa, na jamii zinakabiliana na upweke wao na hofu zao. Kwa pamoja, tunachagua kuishi mahusiano yetu kwa msingi wa udugu, unaochochewa na mazungumzo na msamaha ambao "haimaanishi kusahau" (FT, n. 250), lakini tunakataa na "hautoi kwa nguvu ile ile ya uharibifu" (FT, n. . 251) ambayo matokeo yake sote tunateseka nayo, Tukiungana na Papa Francisko, tunataka kuthibitisha kwamba "upatanisho wa kweli hauepukiki kutokana na mzozo, lakini unapatikana katika mzozo, na kuutatua kwa njia ya mazungumzo na mazungumzo ya wazi, ya uaminifu na yenye subira." , n. 244) Haya yote ni katika muktadha wa mfumo wa haki msingi za binadamu woga, hapana kwa unyanyasaji wa kingono na majumbani lazima ufikie hatima yake.

Mateso na mahangaiko ya watu wasio na hatia
Mateso na mahangaiko ya watu wasio na hatia

Hakuna tena uhamaji wa kulazimishwa, utakaso wa kikabila, udikteta, ufisadi na utumwa. Tuache upotoshaji wa teknolojia na Akili Mnemba, AI, tuweke udugu mbele ya maendeleo ya kiteknolojia, ili iweze kupenyeza ndani yake. Tunahimiza nchi kukuza juhudi za pamoja ili kuunda jamii ya amani, kwa mfano kwa kuanzisha Wizara za Amani. Tunajitolea kuponya ardhi iliyotiwa doa na damu ya vurugu na chuki, na ukosefu wa usawa wa kijamii na ufisadi wa moyo. Tupinge chuki kwa upendo. Huruma, kushiriki, ukarimu, kiasi, na wajibu ni kwetu sisi chaguo zinazokuza udugu wa kibinafsi, udugu wa moyo. Kukuza mbegu ya udugu wa kiroho huanza na sisi wenyewe. Inatosha kupanda mbegu ndogo kila siku katika mahusiano yetu: nyumba zetu, vitongoji, shule, mahali pa kazi, viwanja vya umma, na ndani ya taasisi za kufanya maamuzi. Pia tunaamini katika udugu wa kijamii ambao unatambua utu sawa kwa wote, unakuza urafiki na mali, unakuza elimu, fursa sawa, kazi yenye staha na haki ya kijamii, ukarimu, mshikamano na ushirikiano, uchumi wa mshikamano wa kijamii na mabadiliko ya haki ya kiikolojia, kilimo endelevu ambacho kinahakikisha usalama wa chakula na upatikanaji wa chakula kwa wote, na hivyo kupendelea uhusiano wenye usawa unaotegemea kuheshimiana na kujali ustawi na mafao ya wote. Katika mtazamo huu, inawezekana kuendeleza vitendo vya ukaribu na sheria za kibinadamu, kwa sababu "udugu lazima unahitaji kitu kikubwa zaidi, ambacho kinaongeza uhuru na usawa" (FT, n. 103).

Raais Sergio Mattarella wa Italia
Raais Sergio Mattarella wa Italia

Kwa pamoja, tunataka kujenga udugu wa mazingira, kufanya amani na maumbile, tukijua kwamba "kila kitu kinahusiana na kila kitu kingine": hatima ya ulimwengu, utunzaji wa kazi ya uumbaji, maelewano ya asili na maisha endelevu. Tunataka kujenga siku zijazo juu ya maelezo ya Utenzi wa Viumbe kama ulivyotungwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi, wimbo wa Uzima wa Milele. Njama ya udugu wa ulimwengu wote hufunga nyuzi za aya za Utenzi huu: kila kitu kiko katika uhusiano, na kwa uhusiano na kila kitu na kila mtu ni uzima. Kwa hivyo, sisi, tuliokusanyika katika hafla ya Mkutano wa Kwanza wa Ulimwengu wa Udugu wa Kibinadamu, tunatoa wito kwa wanawake na wanaume wote wenye mapenzi mema kukumbatia ombi letu kwa udugu. Watoto wetu, mustakabali wetu unaweza kustawi tu katika ulimwengu wa amani, haki na usawa, kwa manufaa ya familia moja ya binadamu: udugu pekee unaweza kuzalisha ubinadamu. Ni juu ya uhuru wetu kutaka udugu na kuujenga pamoja, kwa umoja. Ungana nasi katika kutia saini ombi hili la kukumbatia ndoto hii na kuibadilisha kuwa mazoea ya kila siku, ili iweze kufikia akili na mioyo ya viongozi wote na wale ambao, katika kila ngazi, wana jukumu ndogo au kubwa la kiraia.

Udugu wa Kibinadamu
11 May 2024, 14:35