Tafuta

Shule ya Pango hifadhi ilianzishwa na Papa Leo XIII na huo ukawa mwanzo wa Pango hifadhi ya Vatican. Shule ya Sayansi ya Maktaba ilianzishwa na Papa Pio XI, kama kituo maalum cha taifiti za kivita. Shule ya Pango hifadhi ilianzishwa na Papa Leo XIII na huo ukawa mwanzo wa Pango hifadhi ya Vatican. Shule ya Sayansi ya Maktaba ilianzishwa na Papa Pio XI, kama kituo maalum cha taifiti za kivita.  (Vatican Media)

Mchango wa Shule za Vatican Katika Kuhifadhi Nyaraka Mbalimbali

Baba Mtakatifu amegusia mchango mkubwa unaotolewa na shule hizi; wawe tayari kukabiliana na changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza katika medani za utamaduni; ujasiri wa kufikiri na kutenda mintarafu changamoto za kitamaduni na kitaaluma na kwamba, vijana hawa wanayo bahati ya kufundwa moja kwa moja kutoka katika Maktaba ya kitume. Baba Mtakatifu amezipongeza shule hizi kwa mchango wake katika kuwaandaa wakutubi na majaalimu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shule ya Vatican kuhusu Maandishi ya zamani, “Paleografia” Diplomasia “Diplomatica,” Pango hifadhi pamoja na Sayansi ya Maktaba “Biblioteconomia” ni shule zinazosimamiwa na kuendeshwa na Vatican na kwamba, kwa mwaka 2024 zinaadhimisha kumbukizi maalum: Shule ya Sayansi ya Maktaba “Biblioteconomia” inaadhimisha miaka 90 tangu kuanzishwa kwake sanjari na miaka 140 ya Shue ya Pango hifadhi. Hizi zimekuwa ni shule za mafunzo na majiundo maalum, ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa kuwaandaa walimu mahiri, watafiti na viongozi ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo katika muktadha wa kusimamia na kuratibu masuala ya kitamaduni, pango hifadhi na maktaba. Huu ni mwanzo wa ushirikiano na mafungamano katika msingi wa haki na amani dhidi ya vita, kinzani na mipasuko ya kijamii hasa katika karne ya ishirini iliyopita.

Mchango wa Shule za Vatican katika kuhifadhi nyaraka mbalimbali
Mchango wa Shule za Vatican katika kuhifadhi nyaraka mbalimbali

Mama Kanisa katika maisha na utume wake amekuwa akitoa kipaumbele cha pekee katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, hii ikiwa ni pamoja na kujikita katika sekta ya elimu. Shule ya Pango hifadhi ilianzishwa na Papa Leo XIII na huo ukawa mwanzo wa Pango hifadhi ya Vatican. Shule ya Sayansi ya Maktaba ilianzishwa na Papa Pio XI, kama kituo maalum cha taifiti za kivita, majadiliano kati ya Mataifa kwa kuzingatia ustawi, maendeleo na mafao ya nchi husika. Sekretarieri kuu ya Vatican imekuwa mstari wa mbele kulinda maisha ya majaalimu na watafiti dhidi ya vitisho, sanjari na kulinda amana na urithi mkubwa ulioko kwenye vitabu na nyaraka hizo. Shule hizi zimekuwa zikitoa mafunzo maalum kwa ajili ya kulinda, kuhifadhi pamoja na kuwaandaa vijana wa kizazi kipya kuwa wabobezi kama wakutubi na wakufunzi kwa vizazi vijavyo katika muktadha wa kufunda, kuelimisha, kuhifadhi na kuthaminisha nyaraka hizi, kwa kuzingatia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano.

Shule hizi ziwe tayari kukabiliana na changamoto mamboleo.
Shule hizi ziwe tayari kukabiliana na changamoto mamboleo.

Ni katika muktadha huu, Vatican na Serikali ya Italia, zinaendelea kufanya maboresho katika Mkataba wa Mwaka 1984, ili kutoa elimu ya juu, tayari kukabiliana na changamoto mamboleo. Wanafunzi pamoja na majaalimu wa shule hizi mbili, Jumatatu tarehe 13 Mei 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amegusia mchango mkubwa unaotolewa na shule hizi; wawe tayari kukabiliana na changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza katika medani za utamaduni; ujasiri wa kufikiri na kutenda mintarafu changamoto za kitamaduni na kitaaluma na kwamba, vijana hawa wanayo bahati ya kufundwa moja kwa moja kutoka katika Maktaba ya kitume. Baba Mtakatifu amezipongeza shule hizi kwa mchango wake katika kuwaandaa wakutubi na majaalimu katika Kanisa na jamii katika ujumla wake na kwamba, hii ni huduma makini katika nyakati hizi ambamo taarifa zinatolewa bila ya kuhakikiwa wala kufanyiwa tafiti. Haya ni majiundo yanayohitaji kupyaishwa kila wakati kwa kusoma alama za nyakati.

Wanafunzi na Majaalimu wamekutana na Papa Francisko
Wanafunzi na Majaalimu wamekutana na Papa Francisko

Baba Mtakatifu anawataka wadau katika shule hizi kutobweteka kwa mafanikio yaliyokwisha kupatikana, kwa sababu mbele yao kuna changamoto pevu za kitamaduni kwa mfano: Utandawazi, hatari ya kutothamini tena kazi hizi kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia na hivyo mapokeo na tamaduni za kale kuonekana kana kwamba, zimepitwa na wakati kutokana na maendeleo makubwa ya teknolojia na mitandao ya kijamii. Jambo la msingi ni kukubali na kupokea mabadiliko haya kwa moyo wa unyenyekevu unaofumbatwa na wanafunzi pamoja na majaalimu wenyewe. Baba Mtakatifu amewaonya kutojitafuta wenyewe katika mchakato wa kuendelea kuwa wazi, kwa kuwa na moyo wa shukrani kwa wale waliojitaabisha kulinda na kuhifadhi haya yote wanayoyaona mbele yao; wawe na ujasiri wa kuyaangalia ya mbeleni kwa ujasiri ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utamaduni na taaluma. Hizi ni shule ambazo zimejipambanua kwa kukabiliana na hali halisi kuliko itikadi mbalimbali zilizokuwa zinajitokeza. Baba Mtakatifu amewakumbusha wanafunzi hawa kwamba, wanao upendeleo wa pekee kabisa kufundwa moja kwa moja kutoka katika Maktaba ya Kitume, tayari kujiweka wazi kiakili na kiutu, mihimili mikuu kwa ajili ya majiundo na upyaisho kwa siku za usoni.

Walimu wakisalimiana na Papa Francisko
Walimu wakisalimiana na Papa Francisko

Kwa upande wake, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika hotuba ya ufunguzi wa maadhimisho haya amekazia: Umuhimu wa sadaka na majitoleo yao katika kurithisha utaalam wao kwa vijana wa kizazi kipya, kwa kuendelea kuwa makini, waaminifu na wataalam wema, tayari kumwilisha ujuzi na maarifa haya katika ukomavu wa vijana kitaaluma. Waendeleze na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi na taasisi nyingine zenye mwelekeo kama wao, ili wajifunze, kupokea na kutekeleza yale mambo msingi wanayojifunza kutoka kwa wengine. Wajenge na kudumisha utamaduni wa kupenda kusoma vitabu, nyaraka mbalimbali na kusikiliza shuhuda za watu, ili kujichotea matumaini yatakayosaidia kujenga na kuimarisha kesho iliyo bora zaidi; kesho ambayo iko wazi kwa ajili ya kuenzi amani. Katika ari na moyo wa upyaisho, kwa kufahamu mapokeo na tamaduni za watu mahalia, wataweza kuwafunda vijana kitaaluma na kiutu na kwamba, Vatican iko tayari kuwekeza katika taasisi hizi: kiutu na kikristo.

Maktaba
14 May 2024, 14:25