Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 11 Mei 2024 amekutana na kuzungumza na watoto na vijana zaidi ya elfu moja kutoka Jimbo kuu la Genova, Kaskazini mwa Italia. Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 11 Mei 2024 amekutana na kuzungumza na watoto na vijana zaidi ya elfu moja kutoka Jimbo kuu la Genova, Kaskazini mwa Italia.  (Vatican Media)

Sakramenti ya Kipaimara Iwawezeshe Waamini Kuwa ni Mashuhuda wa Imani

Waamini wanapopakwa mafuta ya Krisma wanapokea mhuri wa Paji la Roho Mtakatifu kutoka kwa Askofu mahalia: Huyu ni Roho wa hekima na akili; Roho wa shauri na nguvu; Roho wa elimu na ibada na ni Roho wa Uchaji Mtakatifu. Mapaji yote haya yanapaswa kukua na kuzaa matunda kwa ajili ya jirani zao. Kwa njia ya Kipaimara waamini wanakamilishwa na hivyo kufanana zaidi na Kristo Yesu; Ni Sakramenti inayowaunganisha na Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara muungano wa wabatizwa na Kanisa hufanywa kuwa mkamilifu zaidi, kwani wanatajirishwa kwa nguvu ya pekee ya Roho Mtakatifu na hivi hulazimika kwa nguvu zaidi kuineza na kuitetea imani kwa maneno na matendo, kama mashuhuda wa kweli wa Kristo Yesu. Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara waamini wanampokea Roho Mtakatifu anayewawezeshwa kufanywa wana wa Mungu; kwa kuunganishwa zaidi na nguvu za Kristo Yesu pamoja na kupata mapaji ya Roho Mtakatifu na hivyo kuwasaidia kukamilika zaidi kama viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Kwa njia hii, waamini wanajitoa sadaka na kuwa ni zawadi kwa ajili ya jirani zao! Waamini wanapopakwa mafuta ya Krisma wanapokea mhuri wa Paji la Roho Mtakatifu kutoka kwa Askofu mahalia: Huyu ni Roho wa hekima na akili; Roho wa shauri na nguvu; Roho wa elimu na ibada na ni Roho wa Uchaji Mtakatifu. Mapaji yote haya yanapaswa kukua na kuzaa matunda kwa ajili ya jirani zao. Haya ndiyo maisha ya Kristo Yesu anayewawezesha waamini kujisadaka kwa ajili ya jirani zao kwa kuondokana na uchoyo na ubinafsi; ili hatimaye, kufungua njia katika maisha ya jumuiya inayopokea na kutoa. Waamini wakumbuke kwamba, wao ni vyombo vya Roho Mtakatifu kwa ajili ya jirani zao. Kwa njia ya Sakramenti hii, wabatizwa wanakamilishwa na hivyo kufanana na Kristo Yesu. Ni Sakramenti inayowaunganisha waamini kuwa viungo hai zaidi vya Fumbo la Mwili wake yaani Kanisa. Utume wa Kanisa unapata asili na chimbuko lake kwa wale wote wanaofanyika kuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Hakuna mtu awaye yote ndani ya Kanisa anayeweza kujigamba kwamba, Kanisa ni mali yake!

Watoto na vijana kutoka Jimbo kuu la Genova Italia, 2024
Watoto na vijana kutoka Jimbo kuu la Genova Italia, 2024

Kila mwamini anao wajibu wa kusaidiana na waamini wenzake katika mchakato wa kutakatifuzana, kusaidiana na kutaabikiana. Kila mwamini anayo dhamana na wajibu wake ndani ya Kanisa, lakini wote kwa pamoja wanaunda Kanisa la Kristo linatoka kifua mbele ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo kwa kutambua kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara wote wamefungwa pamoja katika kifungo cha upendo kati ya waamini, Askofu mahalia pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara waamini wanapokea zawadi ya amani, wanayopaswa kuwashirikisha pia majirani zao; kwa kuendeleza Injili ya upendo na mshikamano, kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu katika Kristo Yesu, huku wakitakiana mema! Wakristo wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya amani, umoja, mshikamano katika udugu wa kibinadamu. Sakramenti ya Kipaimara hutolewa mara moja tu na huchapa katika roho alama ya kiroho isiyofutika ambayo ni ishara kwamba, Kristo Yesu amemtia Mkristo alama ya mhuri wa Roho wake, kwa kumvika nguvu itokayo juu, ili aweze kuwa shuhuda wake kwa kutoa harufu nzuri ya utakatifu wa maisha unaobubujika kutoka katika tunu msingi za Kiinjili.

Vijana wajifunze wajibu wa kusali daima
Vijana wajifunze wajibu wa kusali daima

Waamini walioimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara wanapaswa kutambua kwamba, wanawajibika kuwasaidia jirani zao kukua na kukomaa katika maisha ya kiroho. Waamini wawe na ujasiri wa kutoka katika uchoyo na ubinafsi wao, tayari kukutana na jirani zao, ili kwa pamoja, waweze kukua na kusaidiana katika kuziishi karama mbalimbali walizokirimiwa na Roho Mtakatifu, ili kuzaa matunda kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Wakristo wote walioimarishwa kwa Roho Mtakatifu, kamwe wasimfungie Roho Mtakatifu katika ubinafsi wao; wasizime moto wa upendo uliowasha na Roho Mtakatifu, wala kuzuia upepo wa mageuzi unaovumishwa na Roho Mtakatifu.

Sakramenti ya Kipaimara iwawezeshe kuwa ni mashuhuda wa Kristo na Kanisa
Sakramenti ya Kipaimara iwawezeshe kuwa ni mashuhuda wa Kristo na Kanisa

Ni katika muktadha wa Sakramenti ya Kipaimara, Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 11 Mei 2024 amekutana na kuzungumza na watoto na vijana zaidi ya elfu moja kutoka Jimbo kuu la Genova, Kaskazini mwa Italia wanaojiandaa kuimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara, huku wakiwa wameongozana na Askofu mkuu Marco Angelo Tasca wa Jimbo kuu la Genova. Baba Mtakatifu amewazawadia vijana hawa kila mmoja wao Rozari Takatifu kwa kuwapatia agizo la kusali daima, bila kuchoka. Wanaporejea nyumbani, wawasalimie wazazi pamoja na babu na bibi zao, kwani hawa ni watu muhimu sana katika malezi na makuzi yao. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwahimiza wale wote wanaojisadaka kwa ajili ya malezi na majiundo ya watoto hawa, watekeleze dhamana na wajibu wao kwa ari na moyo mkuu. Watoto na vijana hawa walionesha moyo wa furaha kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu, kiasi kwamba, ule uchovu wa masaa nane ya safari kutoka Genova, ulionekana kutoweka. Mwishoni, walisali pamoja Salam Maria na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume.

Kipaimara

 

12 May 2024, 14:55