Tafuta

Baba Mtakatifu Leo XIV amekutana na kuzungumza na Watawa wa Shule za Kikristo, mjini Vatican. Baba Mtakatifu Leo XIV amekutana na kuzungumza na Watawa wa Shule za Kikristo, mjini Vatican.   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV Umuhimu wa Shule za Kikristo: Malezi na Majiundo Makini

Papa Leo XIV amekazia, umuhimu wa kuzingatia matukio ya sasa na mwelekeo wa huduma na kimisionari katika muktadha wa kufundisha katika jumuiya. Mwamini mlei Adriano Nyel alikuwa ni msaada mkubwa sana kwa Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle na hivyo akawa ni chachu ya kuanzishwa kwa Shule za Kikristo, zilizokuwa zinatoa elimu ya bure na zilikuwa ni wazi kwa wote Ni shule zilizowafundisha vijana kufanya kazi hata wakati wa likizo; ushirikishwaji wa familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Watawa wa Shule za Kikristo: Kwa Lugha ya Kilatini: Institutum Fratrum Scholarum Christianarum; kwa Kifaransa: Frères Des écoles Chrétiennes; kwa kifupi: F.S.C. ni Shirika lililoanzishwa kwa tabu nyingi na Mtakatifu Yohane Baptista de La Salle (1651-1719) kwa ajili ya malezi ya kiutu na ya kikristo ya vijana, hasa maskini, huko Reims nchini Ufaransa kunako mwaka 1680 na kuidhinishwa rasmi na Papa Benedikto XIII tarehe 26 Januari 1725. Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle, kunako mwaka 1950, akatangazwa na Papa Pio wa XII kuwa ni mwombezi na msimamizi wa waalimu kutokana na mchango wake mkubwa katika sekta ya elimu, kwani kwa mfano na ushuhuda wake, ameisaidia jamii kuzingatia mambo makuu matatu: Dhana ya shule; Uelewa wa mwalimu pamoja na Mbinu za kufundishia. Huu ni mwaliko wa kujenga utamaduni wa watu kukutana, ili kuwashirikisha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, amana na utajiri wa Habari Njema ya Wokovu! Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 300 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Watawa wa Shule za Kikristo ni fursa ya kumwangalia tena na tena Kristo Yesu kama dira ya maisha, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini, kwa kutangaza Habari Njema kwa njia ya elimu inayomwambata mtu mzima: kiroho na kimwili.

Shirika la Watawa wa Shule za Kikristo: Huduma kwa vijana
Shirika la Watawa wa Shule za Kikristo: Huduma kwa vijana   (@Vatican Media)

Kwa mfano wa maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle pamoja na maongozi ya Roho Mtakatifu, wamefanikiwa kupyaisha ari yao kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu kwa kugundua pia njia mpya za maisha na utume wao!Katika utekelezaji wa huduma hii kwa watu wa Mungu, watawa hawa wanaendelea kushirikiana na watu mbalimbali wanaojisadaka kwa ukarimu na weledi ili kutekeleza utume huu katika sekta ya elimu. Ni watu wanaoshiriki pia amana na utajiri wa maisha ya kiroho, daima Kristo Yesu akipewa kipaumbele cha kwanza. Kwa njia hii, wanaendelea kuandika ukurasa mpya wa simulizi ya Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle. Wanaitwa na Kanisa pamoja na kusukumwa na tunu msingi za Kiinjili kugusa akili na nyoyo za watu, ili kuwaonjesha upendo hai wa Kristo Yesu kwa kuimarisha mafungamano kati ya mwalimu na mwanafunzi, ili kweli darasa liweze kuwa ni mahali pa ukombozi wa watu wa Mungu. Hii ni tasaufi inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu; huduma makini kwa jirani na mshikamano na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, bila kuwasahau vijana wa kizazi kipya wanaohitaji msaada wao.

Huduma ya elimu kwa vijana ni muhimu sana kwa maisha yao
Huduma ya elimu kwa vijana ni muhimu sana kwa maisha yao   (@Vatican Media)

Lengo ni kutangaza na kushuhudia uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Uwepo wao katika sekta ya elimu ni kama Sakramenti ya ufunuo wa Mungu, mahali pa kukutana na Kristo Yesu Mfufuka kwa kuendelea kusoma alama za nyakati. Watawa hawa wanasukumwa kujibu kilio cha watu ambao utu, heshima na haki zao msingi zinasiginwa. Lengo ni kuhakikisha kwamba, kwa njia ya elimu wanaweza kuinuka na kusonga mbele kama watoto wa Mungu. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Miaka 75 tangu Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle, atangazwe na Papa Pio wa XII kuwa ni mwombezi na msimamizi wa waalimu sanjari na Jubilei ya Miaka 300 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Watawa wa Shule za Kikristo: “Institutum Fratrum Scholarum Christianarum”, Baba Mtakatifu Leo XIV Alhamisi tarehe 15 Mei 2025 amekutana na kuzungumza na Watawa wa Shule za Kikristo, mjini Vatican.

Jubilei ya Miaka 300 tangu kuanzishwa kwa Shirika la F.S.C.
Jubilei ya Miaka 300 tangu kuanzishwa kwa Shirika la F.S.C.   (@Vatican Media)

Katika hotuba yake, Papa Leo XIV amekazia, umuhimu wa kuzingatia matukio ya sasa na mwelekeo wa huduma na kimisionari katika muktadha wa kufundisha katika jumuiya. Mwamini mlei Adriano Nyel alikuwa ni msaada mkubwa sana kwa Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle na hivyo akawa ni chachu ya kuanzishwa kwa Shule za Kikristo, zilizokuwa zinatoa elimu ya bure na zilikuwa ni wazi kwa watu wote bila upendeleo. Ni shule zilizowafundisha vijana kufanya kazi hata wakati wa likizo; ushirikishwaji wa familia katika masuala ya masomo, hali ambayo imesaidia kukuza na kudumisha kipaji cha ugunduzi. Baba Mtakatifu Leo XIV anauliza swali la msingi, Je, ni changamoto ipi ambayo vijana wa kizazi kipya wanakabiliana nayo katika ulimwengu mamboleo? Je, ni tunu zipi ambazo Jamii inapaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya? Na kwa kutumia rasilimali gani? Vijana wana uwezo wa kufanya mambo mengi katika medani mbalimbali za maisha, jambo la msingi wanalohitaji ni kuwasaidia ili waweze kukua katika hali ya amani na utulivu, ili waendelee kukua na kukomaa, ili kukoleza maendeleo endelevu.

Miaka 75 Mt. Yohane Baptisti wa Salle: Atangazwe kuwa Mwombezi wa Waalimu
Miaka 75 Mt. Yohane Baptisti wa Salle: Atangazwe kuwa Mwombezi wa Waalimu   (@Vatican Media)

Changamoto kwa vijana wa kizazi kipya ni kukabiliana na: mahusiano tenge, tabia ya uchoyo na ubinafsi, lakini vijana hawa wanakosa fursa ya kusikilizwa, kutafakari na kujadiliana, shule, tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, bila kusahau upweke hasi miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Hizi ni changamoto zinazohitaji nguvu, lakini zinahitaji kutumiwa kama vichocheo vya kuchunguza njia, kukuza zana na kupitisha lugha mpya, ambazo kwazo jamii itaendelea kugusa mioyo ya wanafunzi, kuwasaidia na kuwatia moyo kukabiliana kwa ujasiri na kila changamoto na vikwazo ili kuendelea kujisadaka zaidi maishani mintarafu mipango ya Mungu katika maisha. Kumbe, watawa hawa wamekuwa makini katika shule zao kutokana na mafunzo ya walimu wanayowapatia sanjari na uundwaji wa Jumuiya za kielimu na maboresho ya mchakato wa ufundishaji; mambo ambayo kimsingi ni ya kupongezwa sana. Hii ndiyo njia muafaka ambayo wanapaswa kuifuata.

Uwepo wao katika sekta ya elimu ni Sakramenti ya ufunuo wa Mungu
Uwepo wao katika sekta ya elimu ni Sakramenti ya ufunuo wa Mungu   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, ualimu unapaswa kuchukuliwa kama ni wito na utume na kama njia ya kujiweka wakfu ndani ya Kanisa na ndiyo maana Mtakatifu Yohane Baptisti wa Salle, alipenda utume wake wa Shule za Kikristo kuwakabidhi Mabruda, ili waweze kujituma na kujisadaka kwa ajili ya kukoleza elimu kwa vijana wa kizazi kipya na kwamba, shule kwao ilikuwa ni Altare, mahali ambapo Mabruda na Makatekista wangeweza kujizatiti katika mchakato wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, mintarafu kanuni ya kuinjilisha kwa kuelimisha, ili kuelimisha kwa kuinjilisha. Kumbe, shule inakuwa ni nadhiri ya nne na hivyo inakuwa ni Karama muhimu sana ya Shirika la Watawa wa Shule za Kikristo: “Institutum Fratrum Scholarum Christianarum,” kielelezo makini cha huduma ya upendo, ambayo hadi leo hii ina umuhimu wa pekee sana kwani inashiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu, kama wanavyokaza kusema Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kwamba, waamini walei kama viungo hai vya Fumbo la mwili wa Kristo yaani Kanisa wanaitwa na kutumwa kulikuza Kanisa na kulitakatifuza daima, kwa ajili ya wokovu wa walimwengu. Rej. LG 44, 33. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV anaendelea kuombea ustawi na maendeleo ya miito ya kitawa katika shule zao, ili zisaidie kuamsha miito miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, ili watembee kwa furaha katika njia ya utakatifu wa maisha. Mwishoni amewapongeza kwa kazi zao njema!

Papa XIV Shule za Kikristo
15 Mei 2025, 15:31