Papa Leo XIV: Ibada ya Misa ya Ufunguzi wa Utume Wake: Pallio Takatifu na Pete ya Mvuvi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 21 Januari anaadhimisha kumbukumbu ya Mtakatifu Agnes, Bikira na Shahidi, aliyeuwawa kunako karne ya tatu; akaonesha upendo wa pekee sana kwa Kristo Yesu mchumba wake wa daima kiasi cha kuyasadaka maisha yake, ili asiuchafue ubikira wake. Yesu mwenyewe alitambulishwa na Yohane Mbatizaji kama Mwana Kondoo wa Mungu anayebeba na kuondoa dhambi za ulimwengu. Ni Mapokeo ya Kanisa kwamba, Siku kuu ya Mtakatifu Agnes, wanabarikiwa kondoo ambao manyoya yao yatatumika kutengenezea Pallio Takatifu, wanazovishwa: Papa, Maaskofu wakuu na Mapatriaki katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Petro na Paulo Mitume, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni na katika muktadha huu, Mwadhama Kardinali Robert Francis Prevost, wa Shirika la Mtakatifu Augustino, O.S.A. ndiye Baba Mtakatifu wa 267 aliyechaguliwa na Baraza la Makardinali katika mkutano wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Askofu mkuu wa Roma, na kama alivyotangazwa na Kardinali Shemasi Dominique Mamberti, Alhamisi tarehe 8 Mei 2025 na kuchagua jina la Leo wa XIV.
Pallio Takatifu ni kitambaa cha sufi safi kinachovaliwa na Baba Mtakatifu, Maaskofu wakuu wa majimbo ya Kanisa Katoliki pamoja na Mapatriaki. Hii ni alama ya Kristo mchungaji mwema aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, Mchungaji mwema, hata kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, Maaskofu wakuu na Mapatriaki wanahamasishwa kuwabeba kondoo wao kama kielelezo cha wachungaji wema; wakumbuke kwamba, wameteuliwa si kwa ajili ya mafao yao binafsi, bali kwa ajili ya kondoo wa Kristo Yesu. Papa mpya na Maaskofu wakuu wanapaswa pia kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Pallio takatifu ni alama ya umoja na mshikamano kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, Maaskofu wakuu na Mapatriaki.
Kwa hiyo Baba Mtakatifu Leo XIV anapouanza utume wake wa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Dominika tarehe 18 Mei 2025 avavishwa Pallio Takatifu. Kabla ya mahubiri, Baba Mtakatifu Leo XIV atavishwa pia “Pete ya Mvuvi”, Pete ambayo inamwakilisha Mtakatifu Petro aliyekuwa ni Mvuvi kutoka Galilaya. Pete hii inatumika kama muhuri binafsi wa Baba Mtakatifu; Imani na hivyo kuthibitisha uhalisia wake. Asili yake haijulikani lakini ilitumika kama muhuri wa kibinafsi wa Papa kutoka wakati wa Clement IV, mnamo mwaka 1265. Muhuri wa zamani zaidi uliobaki, wa nta nyekundu, ni wa Papa Nicolas III (1277-1280). Hadi Papa Nicolas V (1447-1455) pete hiyo inamwakilisha Mtume Petro, akiwa kwenye mashua, akivua samaki. Hadi karne ya kumi na saba, muhuri uliwekwa kwenye sehemu ya chini ya hati; kutoka karne ya 17 hata hivyo iliwekwa kwenye nyaraka kutoka kwa Baba Mtakatifu. Kutoka kwa Papa Leo XIII hadi Mtakatifu Yohane Paul II waliacha desturi ya kutumia Pete. Papa Benedikto XVI aliweka sheria za matumizi yake. Baada ya kifo cha Papa, pete hiyo inabatilishwa na “Kardinali Camerlengo” mwanzoni mwa mikutano elekezi ya Baraza la Makardinali. Katika nyakati hizi pete hii inaparuzwa tu.