Tagle:Leo XIV, mchungaji mmisionari atakayeongoza kwa kusikiliza
Na Alessandro Gisotti.
Katika kikanisa cha Sistine, wakati wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi(Conclave,) walikuwa wameketi pamoja karibu. Ijumaa tarehe 16 Mei 2025, Kardinali Luis Antonio Tagle na Robert Francis Prevost walikutana kwa mara nyingine tena, katika mkutano wa pamoja kwenye Jumba la kitume mjini Vatican, Juma moja baada ya tangazo lile la: “Habemus Papam” yaani Tunaye Papa iliyotangulia baraka ya kwanza ya "Urbi et Orbi," yaani ya 'Mji na Ulimwengu mzima' ya Papa Leo XIV. Kardinali wa Marekani na Peru ambaye amekuja kuwa Papa na Kardinali wa Ufilipino wamefahamiana kwa miaka mingi na katika miaka miwili iliyopita wameshirikiana bega kwa bega kwa karibu sana kama wakuu wa mabaraza ya kipapa: ya Maaskofu (Prevost) na ile ya Uinjilishaji(Tagle). Katika mahojiano na vyombo vya habari vya Vatican, Kardinali Tagle ametoa taswira binafsi ya Papa mpya, huku akisimulia uzoefu wa kiroho alioishi katika Mkutano mkuu wa uchaguzi na alimkumbuka Baba Mtakatifu Francisko kwa hisia kuu. Tunachapisha mahojiano kamili.
Kardinali Tagle, Papa Leo XIV anachukua hatua za kwanza za Upapa baada ya Mkutano Mkuu wa Uchaguzo uliomalizika haraka. Ni nini kinakugusa kuhusu Papa huyu, ambaye sote tuko tunajifunza kumfahamu?
Nilikutana na Papa Leo XIV kwa mara ya kwanza huko Manila (Ufilippino) na Roma alipokuwa bado Mkuu wa Shirila la Mtakatifu Agostino. Tumekuwa pamoja katika Curia Romana tangu 2023. Ana uwezo wa kina na wa subira wa kusikiliza. Kabla ya kufanya uamuzi, anajitolea kusoma kwa uangalifu na kutafakari. Anaonesha hisia na matakwa yake bila kutaka kulazimisha. Ameandaliwa kiakili na kiutamaduni bila kujipigia debe. Katika mahusiano, yeye anatoa joto la utulivu, lililosafishwa na sala na uzoefu wa kimisionari.
Katika mkesha wa Mkutano Mkuu wa uchaguzi, wengi walizungumza juu ya Kanisa lililogawanyika, la makardinali wenye mawazo yasiyoeleweka kuhusu uchaguzi wa Papa mpya. Badala yake, uchaguzi ulitatuliwa siku ya pili. Je, uzoefu wa Mkutano huu ulikuwaje kwako, wa pili baada ya ule wa 2013?
Kabla ya matukio makubwa yenye matokeo makuu ya kimataifa, husikika makisio mbalimbali, chambuzi na tabiri. Mkutano Mkuu wa uchaguzi huu hauachwi nje kutoka kwao. Ni kweli kwamba nilishiriki katika mikutano mikuu miwili ya uchaguzi, ambayo nimeona kuwa ni neema ya kweli. Katika Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa mwaka 2013, Papa Benedikto XVI alikuwa bado hai, wakati katika Mkutano mkuu wa uchaguzi wa 2025, Papa Francisko alikuwa tayari amepita kwenda kwenye uzima wa milele. Lazima tuzingatie tofauti ya miktadha na mazingira. Ningeongeza pia kwamba wakati kila moja ya mikutano mikuu miwili ya uchaguzi ilikuwa uzoefu wa kipekee na usioweza kurudiwa, pia kulikuwa na vipengele fulani. Mnamo 2013, nilishangaa kwa nini tulilazimika kuvaa mavazi ya kwaya wakati wa Mkutano mkuu wa uchaguzi. Kisha nikajifunza na kujionea kwamba Mkutano Mkuu wa uchaguzi ni tukio la kiliturujia, kwa kuwa linaongozwa nafasi ya maombi, na kwa ajili ya kusikiliza Neno la Mungu, kwa misukumo ya Roho Mtakatifu, kwa kuomboleza kwa Kanisa, kwa wanadamu na kwa Uumbaji, kwa ajili ya utakaso wa kibinafsi na wa kawaida wa motisha na kwa ajili ya ibada na kumwabudu Mungu, ambaye mapenzi yake makuu lazima yatawale. Kwa wote yaani Papa Francisko na Papa Leo walichaguliwa siku ya pili. Mkutano Mkuu wa uchaguzi unatufundisha sisi, pamoja na familia, parokia, majimbo na mataifa, kwamba ushirika wa mioyo na akili unawezekana ikiwa tutamwabudu Mungu wa kweli.
Katika kikanisa cha Sistine ulikuwa umeketi karibu na Kardinali Prevost. Je! Papa wa baadaye alikuwaje wakati alipofikia theluthi mbili za kura?
Mwitikio wake ulikuwa wa kubadilishana tabasamu na kupumua kwa kina. Ilikuwa ni moja ya kukubalika kitakatifu na hofu takatifu kwa wakati mmoja. Nilimwombea kimya kimya. Mara tu alipopata idadi muhimu ya kura, makofi ya kishindo yalianza, sawa sawa na uchaguzi wa Papa Francisko. Makardinali hao walionesha furaha na shukrani kwa kaka yao Kardinali Prevost. Lakini pia ilikuwa ni wakati wa ukaribu sana kati ya Yesu na yeye, mahali ambamo hatungeweza kuingia na ambamo hatungepaswa kusumbua. Nilijiambia mwenyewe: “Tuache ukimya mtakatifu wa Yesu na Petro umfunike.”
Baada ya mtoto wa Mtakatifu Ignatius, ni mtoto wa Mtakatifu Agostino. Ina maana gani, kwa maoni yako, kwamba katika Kanisa Mapapa wawili wanatoka katika mashirika muhimu ya kitawa, yaani baada ya Mjesuit, anaanza Muagostino?
Mtakatifu Agostino na Mtakatifu Ignatius walikuwa na mambo mengi yanayofanana. Wote wawili walipitia njia ya kidunia na walikuwa wameishi hali ya kutotulia ambayo iliwasukuma kwenye utafutaji wa ajabu. Kisha, katika wakati wa maamuzi ya Mungu, walipata ndani ya Yesu kile ambacho mioyo yao ilitamani. "Uzuri daima wa zamani na daima mpya," "Bwana wa Milele wa vitu vyote." "Shule" za Agostiniani na Ignatius zinazaliwa kutokana na msingi wa kawaida wa pamoja yaani wa neema na huruma ya Mungu, ambayo inafungua moyo wa kupenda, kutumikia na kwenda kwenye utume. Kwa kuzingatia tasaufi ya Kiagostino, Papa Leo XIV ataunga mkono Tasaufi ya Mtakatifu Ignatius ya Papa Francisko. Nafikiri Kanisa zima na hata wanadamu wote watafaidika na karama zao. Baada ya yote, Mtakatifu Agostino na Mtakatifu Ignatius (na watakatifu wote) ni hazina ya Kanisa zima.
Prevost alikuwa Askofu mmisionari, aliyezaliwa na kukulia nchini Marekani, lakini alifundwa nchini Peru kama Padre na mchungaji. Mtu fulani alisema kwamba yeye ni "Papa wa dunia mbili." Huko Asia, unakotoka wewe, watu wanamwonaje Papa wa namna hiyo?
Bila kukataa ukuu wa neema katika huduma ya Papa Leo, ninaamini kwamba malezi yake ya kibinadamu, kiutamaduni, kitawa na kimisionari yanaweza kutoa sura ya kipekee kwa huduma yake. Lakini hii ni kweli kwa Mapapa wote. Huduma ya Mfuasi wa Petro ya kuwathibitisha kaka na dada katika imani katika Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai, inabaki thabiti, lakini inaishi na kutekelezwa na kila Papa katika ubinadamu wake wa pekee. Uzoefu wa Papa Leo wa mabara na tamaduni nyingi hakika utamsaidia katika huduma yake na kunufaisha Kanisa. Watu wa Asia wanampenda Papa kama Papa, haijalishi anatoka nchi gani. Anapendwa sio tu na Wakatoliki, bali pia na Wakristo wengine na wafuasi wa dini zisizo za Kikristo.
Wengi "walikuunga mkono," wakitumaini kwamba ungekuwa Papa. Ulikumbanaje na hili? Je! ulikuwa unajua kuwa, kama isemavyo kwa Kiitaliano, ulikuwa mmoja wa (papabili)anayewezekana kuwa Papa?
Kwa kuwa mimi si mmoja wa kuwa katika uangalizi, nilipata tahadhari iliyoelekezwa kwangu badala ya kutatanisha. Nilijaribu kukusanya nguvu zangu za kiroho na za kibinadamu ili kuepuka kujihusisha. Nilitafakari sana maneno ya katiba ya kitume Universi Dominici Gregis, kuhusu “kazi nzito sana iliyo juu yao (makardinali) na, kwa hiyo, juu ya hitaji la kutenda kwa nia ifaayo kwa manufaa ya Kanisa la ulimwengu wote, solum Deum prae oculis habentes.” Kila Kardinali anapopiga kura, yeye anasema hivi: “Ninamwita Kristo Bwana, ambaye atanihukumu, ashuhudie kwamba kura yangu imetolewa kwa yule ambaye, mbele ya macho ya Mungu, ninaamini kwamba anapaswa kuchaguliwa.” Ni wazi kwamba hakuna wagombea katika "maana ya kidunia" ya chaguzi za kisiasa, ambapo kura yako kwa mgombea mmoja ni kura dhidi ya mgombea mwingine, hapana. Unapotafuta mema ya Kanisa la ulimwengu wote, hutafuti washindi na walioshindwa. Kanuni hii elekezi husafisha akili na kutoa utulivu.
Tunakaribia mwezi mmoja tangu kifo cha Papa Francisko. Je, kwa maoni yako, ni urithi gani wa kina na wa kudumu ulioachwa na Papa huyu kwa Kanisa na kwa wanadamu?
Moyo wangu unafurahia ushuhuda mwingi unaotolewa na waamini wa Kikatoliki, jumuiya za Wakristo wasio Wakatoliki, na washiriki wa dini zisizo za Kikristo kuhusu mafundisho na urithi wa Papa Francisko. Ninatumaini kwamba shuhuda hizi zitaongezeka na "kukusanywa" kama sehemu ya ufahamu wetu sio tu wa Papa Francisko, lakini pia kwa huduma ya Mfuasi wa Petro. Kwa upande wangu, ninapenda kukazia zawadi ya hadhi ya kuwa binadamu kwa ajili ya wengine, ambayo imedhihirisha sifa ya Upapa wa Baba Mtakatifu Francisko. Ikiwa una historia ya kibinafsi ya kusimulia juu yake, fanya hivyo. Ulimwengu wetu unahitaji kugundua tena na kuhamasisha uzuri na thamani ya kuwa binadamu halisi. Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya ubinadamu wake kamili na hata udhaifu, ametoa mchango mkubwa katika utafiti huu, si kwa ajili ya utukufu wake, bali kwa ajili ya utukufu mkuu wa Mungu, ambaye katika Yesu alifanyika kuwa mwanadamu kikamilifu.