Papa akutana na Washiriki wa Mikutano Mikuu:Tambueni alama za nyakati na hudumieni wahitaji!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Alhamisi tarehe 18 Septemba 2025 akikutana na watawa wa kike na kiume wa Mashirika na Taasisi mbali mbali za Roma wakiwa ni washiriki wa Mikutano Mikuu ya Mashirika yao, katika Ukumbi wa Clementine katika Jumba la Kitume mjini Vatican, alisisitiza wazingatie mambo muhimu hasa ishara za nyakati, kuwahudumia wengine katika mahitaji yao, kuishi utii kama tendo la upendo katika Ulimwengu wa leo na umuhimu wa maisha ya kawaida hasa ya kuishi pamoja kama ndugu. Mashirika haya yalikuwa ni Wamisionari wa Damu Azizi, Shirika la Maria (Marist), Ndugu Wafransiskani wa Imakulata na Wa Ursulines wa Maria Imakulata.
Akianza hotuba yake Papa alionesha furaha ya kukutana nao katika fursa hiyo ya Mikuano Mikuu. Aliwasalimia Wakuu wa Mashirika hayo waliokuwapo na wote ambao wanajikita katika siku hizi za kazi ya kusikiliza na kufanya mang’amuzi. Baadhi ya Mashirika yao ni ya kiteule. Papa aliongeza kuwa hata hiyo ni zawadi kubwa kwa Kanisa na kwa uwajibikaji ambao wanamkabidhi pamoja Bwana. Baba Mtakatifu Leo alisema kuwa: “Taasisi zao ni ushuhuda angavu na tofauti, mahali ambapo wanajumuika kwa wingi wa zawadi zilizotolewa na Mungu kwa waanzilishi wa kike na kiume ambao kwa ufunguzi wa matendo ya Roho Mtakatifu, walitambua kutafsiri ishara za nyakati na kujibu kwa namna iliyoakisiwa na mahitaji ya taratibu za dharura(Mt.Yohane Paulo: Waraka wa Maisha ya Kitawa,9).
Papa alielezea juu ya waanzilishi wa Mashirika haya ambapo Papa alisema, kama Brigida wa Yesu Morello, tayari kwenye karne ya 17, kwa njia malezi ya vijana, katika nyakati ambazo Jamii haikuwa ikitambua kikamilifu, thamani, alizindua kazi ya kuhamasisha mwanamke ambaye baadye aliweza kutoa matunda mengi ya wakati ujao. Na kwa namna hiyo Mtakatifu Gaspare del Bufaro, karne mbili baadaye, katika jijini Roma, kwa utume wa watu na kwa kusambaza ibada ya Damu Azizi ya Kristo, alijibidisha kupambana na roho iliyokuwa imeenea ya "ukana Mungu na uasi" iliyokuwa inatesa kwa wakati wake. Hii ni sawa na shughuli iliyokabiliwa huko Ufaransa na Padre Jean- Claude Coli, kwa kuhuishwa, katika utume wake, kwa roho ya unyenyekevu na kujificha kwa Maria wa Nazareth. Na hatimaye, katika miaka ya 90, katika karne ya 21, katika nyayo za Mtakatifu Francis na Mtakatifu Maximilian Kolbe, walizaliwa Ndugu Wafransiskani wa Imakulata.
Kwa njia hiyo Papa aliongeza kwamba hiyo ni pembe bapa ya urithi ambao wameupeleka siku hiyo na ambayo Papa alipenda kusisitiza baadhi ya mantiki zinazojenga. Kwa njia hiyo Papa Leo XIV alidadavua ya kuwa, kwanza ni muhimu, kutambua katika wito wa mtawa ambapo wanashirikishana, maisha ya pamoja, kama mahali pa kutakatifuza na kisima cha kuhuisha, shuhuda na nguvu ya kitume. Ndani yake “nguvu ya Roho ambayo ni moja, inapitia wakati na huo kwa wote, na si tu kumimina zawadi yake binafsi, lakini kuiongeza katika kufanya kuwa sehemu ya wengine na kufurahia tunda la zawadi kama binafsi. Na si kitu, Roho Mtakatifu alihuisha kwa yule aliyewatangulia kuungana na kaka na dada ambao kwa mapenzi ya Mungu aliwaweka katika safari yake, kwa sababu katika muungano wa mazuri, mema yanaongezeka na kukua. Na ndivyo ilianza mwanzo wa mashirika yao na kupitia karne na kuendelea kuwa hivi hata leo hii.
Baba Mtakatifu Leo kwa washirika hao alisisitiza kuwa, mtazamo wa pili aliotaka kusisitiza ni thamani msingi, kwa wawekwa wakfu wa kitawa, kwa kutii kama tendo la upendo. Yesu yupo na alitoa mfano katika uhusiano wake na Baba: “Sitafuti mapenzi yangu, bali mapenzi ya yule aliyenituma (Yh 5,30). Katika mkutadha huo, Mtakatifu Agostino alisisitiza kwa nguvu juu ya uhusiano wa kina ambao upo, katika maisha ya kikristo, kati ya utii na upendo wa kweli kwamba: “kilicho moyoni mwenu ni upendo, alisema katika hotuba; sasa utii ni binti yake(…),mzizi uko chini ya ardhi, ni matunda ya kugundua. Siamini kile kinachong'ang'ania chini ikiwa sioni kinachoning'inia kwenye tawi. Je! una upendo? Nioneshe matunda yake! Acha nione utii […]. Naomba nimshike binti yangu mikononi mwangu ili kutambua [matunda ya] mama” (Sermo 359 B, 12).
Papa Leo XIV aliongeza kusema kuwa: “Leo, kuzungumza juu ya utii si jambo la mtindo sana: linachukuliwa kuwa kukataa uhuru wa mtu. Lakini si hivyo. Utii, katika maana yake ya ndani kabisa ya kuwasikiliza wengine kwa bidii na kwa ukarimu, ni tendo kubwa la upendo ambalo kwalo mtu hukubali kufa mwenyewe ili kaka na dada yake wakue na kuishi. Kwa kutia nadhiri na kuishi kwa imani, inafuatilia njia ing’aayo ya kujitolea, ambayo inaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa Ulimwengu tunamoishi kugundua tena thamani ya sadaka, uwezo wa mahusiano ya kudumu, na ukomavu wa kuwa pamoja ambao unapita zaidi ya “hisia” ya wakati wa kuunganishwa katika uaminifu. Utii ni shule ya uhuru katika upendo.
Hatimaye, kipengele cha tatu ambacho alipenda kuzingatia ni mtazamo wa alama za nyakati. Hapo Papa alisisitiza kuwa “Bila mtazamo huo wa wazi na wa makini katika mahitaji halisi ya kaka na dada zetu, hakuna Mashirika hata moja ambalo lingezaliwa. Kwa njia hiyo waanzilishi wao wa kike na kiume walikuwa watu wenye uwezo wa kutazama, kutathmini, kupenda, na kisha kujiweka, hata katika hatari ya mateso makubwa, hata kwa gharama ya wao wenyewe, kuwahudumia ndugu zao katika mahitaji yao halisi, wakiitambua sauti ya Mungu katika umaskini wa jirani zao.
Ndio maana ni muhimu kwao kufanya kazi katika kumbukumbu hai ya mwanzo huu wa ujasiri, sio kwa maana ya "kujihusisha na akiolojia au kukuza ndoto isiyo na maana, lakini badala ya kurudisha njia ya vizazi vilivyopita ili kushika ndani yake cheche zenye msukumo, maadili, mipango, na maadili yaliyowasukuma" (Papa Francisko, Barua ya Kitume kwa Watu Wote Waliowekwa Wakfu Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Maisha ya Kuwekwa wakfu, 21 Novemba 2014, I, 1), nikibainisha uwezo ambao huenda bado haujachunguzwa, ili kuutumia vyema katika huduma ya "hapa na sasa." Papa Leo kwa kuhitimisha alisema anavyojua ni kiasi gani kizuri wanachofanya kila siku, katika sehemu nyingi za dunia, wema ambao mara nyingi haujulikani kwa macho ya wanadamu, lakini si kwa yale wa Mungu! Ameshukuru na kuwabariki kutoka moyoni mwake, akiwatia moyo kuendeleza utume wao kwa imani na ukarimu.
