Papa atuma ujumbe kwa wagonjwa wa ALS:ubora wa maisha unategemea upendo
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika ujumbe wake wa video kwa lugha ya Kiingereza uliotumwa katika tukio la kila mwaka "liitwalo Walk of Life," yaani matembezi yaliyohamasishwa huko Chicago na Mfuko wa Les Turner ALS, Baba Mtakatifu Leo XIV Jumamosi tarehe 20 Septemba anakuwa karibu na wale ambao wanaathirika na ALS (Amyotrophic Lateral Sclerosis) ambao ni ugonjwa wa mfumo wa neva. Katika hotuba yake kwa washiriki wa Tukio hilo Papa alianza kutoa “amani iwe nanyi. Salamu kutoka Roma! Nina furaha sana kujiunga nanyi huko Chicago katika mfuko wa Les Turner ALS unaotukusanya kwa ajili ya Matembezi ya Maisha ya kila mwaka ya ALS.
Pongezi na shukrani kwa watafiti na wanasayansi
Mkusanyiko huo ni wa watu wengi. Acha niseme, kwanza kabisa, kwamba nimejawa na pongezi na shukrani kwa watafiti na wanasayansi waliokusanyika hapo. Kaka na dada zetu Wayahudi wanatuambia kwamba mojawapo ya mipango mikubwa ambayo familia ya kibinadamu imepewa na Mungu ni kutimiza na kukamilisha uumbaji mzuri sana tuliopewa—tikkun olam. Mtangulizi wangu, Papa Yohane Paulo wa Pili, aliandika: “Ikiwa msanii hawezi kuzuiwa kutumia ubunifu wake, wale walio na vipawa hususani vya kuendeleza sayansi na teknolojia hawapaswi kuzuiwa kutumia talanta zao walizopewa na Mungu kwa ajili ya huduma ya wengine.”
Katika miaka 10 iliyopita - kwa kutumia ujuzi wenu wote na huruma kuelewa magonjwa ya mfumo wa neva na kupunguza mateso ambayo magonjwa hayo husababisha, mmepata maendeleo ya ajabu. Mimi, kama ilivyo kwa kila mtu hapo, ninawashukuru sana. Kwa saa nyingi mnazotumia peke yenu kujaribu kutafuta njia ya kusonga mbele katika maswali yenu au kutafuta nyenzo za kuendeleza kazi zenu muhimu, kwa wanaume na wanawake wanaofanya utafiti wa kisayansi katika Kituo cha Les Turner ALS katika Tiba ya Kaskazini-Magharibi na kwingineko, tafadhali mpokee shukrani zangu na za kutia moyo. Ninashukuru pia kuwa mbele ya walezi wengi sana: madaktari na wauguzi, wasaidizi wa kiafya, wa kimwili, na wa usemi, wafanyakazi wa kijamii, na, hasa, marafiki na familia.
Utunzaji wa huruma kwa wanaoishi na ALS
Utunzaji wenu na huruma kwa wale wanaoishi na ALS na magonjwa mengine ya mfumo wa neva ni msukumo kwangu na kwa watu wote. Kama marafiki zetu Waislamu wanashiriki, katika Historia, tunaambiwa kwamba Malaika 70,000 wapo wakati waangalizi wanapofika asubuhi. Malaika wengine 70,000 wanawasili jioni. Ninaamini kwamba ninyi pia ni Malaika. Kwa kujitolea, maarifa na ustadi, unawajali dada na kaka zetu walio na ALS - familia, marafiki, na watu ambao walikuwa wageni. Mara nyingi utunzaji wenu hutolewa kwa sadaka kubwa ya kibinafsi. Kama wanafamilia na marafiki wanaohusika katika utunzaji wa kila siku wa wale walio na ALS, unatuonesha ubinadamu bora zaidi. Ninyi ni Wasamaria wema ambao Yesu alisema juu yao. Acha niseme jambo kwenu ninyi mnaoishi na ALS: Mna nafasi ya pekee katika mawazo na maombi yangu.
Mzigo mzito wa kuubeba
Mmepewa mzigo mzito sana kuubeba. Ninatamani vinginevyo. Mateso yenu, hata hivyo, yanawapa fursa ya kugundua na kuthibitisha ukweli wa kina: Ubora wa maisha ya binadamu hautegemei mafanikio. Ubora wa maisha yetu unategemea upendo. Katika mateso yenu, mnaweza kupata kina cha upendo wa kibinadamu ambao haukujulikana hapo awali. Mnaweza kukua katika shukrani kwa yote ambayo mmepewa na kwa watu wote wanaowajali sasa. Mnaweza kukuza hisia ya kina ya uzuri wa uumbaji, wa maisha katika ulimwengu huu na siri ya upendo.
Jisalimisheni katika fumbo la uwepo wa mwanadamu
Ninawaombea. Ninaomba kwamba badala ya kuchanganyikiwa au kukata tamaa mjisalimishe wenyewe kwa fumbo la kuwepo kwa mwanadamu, kwa upendo wa walezi wenu na kukumbatiana na Mungu Mmoja. Na hatimaye, neno kwa wale wanaoomboleza. Baada ya muda wa kuwatunza wapendwa wenu kwa ALS, sasa mnaomboleza kifo chao. Hamjawasahau. Na, kiuweli, upendo wenu umetakaswa na huduma yenu na kisha kwa maombolezo yenu. Mmmejifunza na kila siku mnaingia kwa undani zaidi katika mafumbo mazito zaidi kuwa - kifo sio neno la mwisho. Upendo hushinda kifo. Upendo hushinda kifo. Upendo hushinda kifo.
Pongezi kwa Bonnie na Gaffen
Ninaomba nitoe neno maalum la salamu kwa Harvey na Bonnie Gaffen. Kwa karibu miaka 50, Bwana na Bibi Gaffen, mmedumisha kumbukumbu, ya maisha ya Les Turner. Upendo wenu kwa Bwana Turner, na kujitolea kwenu na nguvu, kumeboresha maisha ya watu wengi. Tazameni karibu nanyi leo hii. Watu hawa wote wako hapo kwa sababu yenu, ukuu wa moyo wenu. Asante, Harvey na Bonnie. Kwa mara nyingine tena, kwenu nyote, asante kwa kuwa hapo. Asante kwa kunialika. Asante kwa Mfuko wa Les Turner ALS, kwa kutukusanya leo hii. Mkusanyiko wetu uwe chanzo cha baraka kwetu sote. Asante!
