Tafuta

2025.09.19 Papa katika Basilika ya Mtakatifu Yohane huko Laterano - Mkutano wa Jimbo Kuu. 2025.09.19 Papa katika Basilika ya Mtakatifu Yohane huko Laterano - Mkutano wa Jimbo Kuu.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV kwa Kanisa la Roma:kufanya kazi ya Kanisa kuwa maabara ya sinodi!

Papa Leo XIV amekutana na zizi lake la Jimbo Kuu la Roma katika Kanisa lake Kuu la Mtakatifu Yohane huko Laterano.Katika hotuba yake amefafanua umuhimu wa kuanzisha huduma ya kichungaji inayounga mkono,isiyohukumu na inayokaribisha wote:kuimarisha makatekista,vijana na familia,wenye maono ya pamoja ili kuleta matokeo,katika kuwahudumia maskini na walio katika mazingira magumu zaidi.Kwa upande wa Makamu wa Papa ameonesha huzuni wa dunia inayomwaga damu.

Na Angella Rwezaula- Vatican.

Kwa mara nyingine tena, Baba Mtakatifu amerudia katika Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, ambalo ni kanisa la kale, kwa ajili ya ufunguzi wa Mwaka wa kichungaji Ijumaa jioni tarehe 19 Septemba 2025. Katika Kanisa lilojaa waamini wapatao elfu mbili wawakilishi kutoka maparokia yote ya Jiji la Roma, ambao walikuwa ni wanaume na wanawake watawa, makatekista, na mapadre ambao wanajitahidi kila siku katika utume wa Kanisa la Roma kila siku. Kabla ya hotuba ya Papa lilisomwa Neno la Mungu kutoka Barua ya Mtakatifu Paulo kwa Waefeso, Zaburi 34, na Injili ya Yohane, ambayo inasimulia tukio la mwanamke Msamaria ambaye alikutana na Yesu.

Furaha ya Papa kama Askofu wa Roma

Kwa njia hiyo Papa alianza kusema kuwa Wapendwa kaka na dada zangu, ni furaha kwangu kuwa pamoja nanyi katika Kanisa Kuu la Roma: Papa ni kama Askofu wa Roma, na mimi niko pamoja nanyi kama Mkristo, na kwa ajili yenu. Ninamshukuru Kardinali kwa maneno yake ya kutambulisha mkutano huu, ambao ninauona kama mkumbatio mkubwa kati ya Askofu na watu wake. Nawasalimu wajumbe wa Baraza la Maaskofu, mapadre wa parokia, mapadre wote, mashemasi, wanaume na wanawake watawa, na ninyi nyote mliopo hapa mnawakilisha parokia. Ninakushukuru kwa furaha ya uanafunzi wenu  kwa kazi yenu  ya uchungaji, kwa mizigo mnayobeba na kwa wale mnaowainua kutoka kwenye mabega ya wengi wanaobisha hodi kwenye milango ya jumuiya zenu.”

Kipaji cha Roho Mtakatifu hukata kiu yetu

Baba Mtakatifu kwa kutazama Neno la Mungu alisema, maneno yaliyoelekezwa kwa mwanamke Msamaria na Yesu, ambayo tumesikia hivi punde katika Injili, katika wakati huu mgumu wa kihistoria, sasa yanaelekezwa kwetu sisi, Kanisa la Roma: "Kama ungeijua karama ya Mungu!" (Yh 4:10 ). Kwa yule mwanamke mchovu aliyekuja kwenye kisima katika saa yenye joto kali zaidi ya siku, Yesu alifunua kwamba kuna maji yaliyo hai ambayo huzimika milele, chemchemi inayobubujika isiyokauka kamwe: ni uhai wenyewe wa Mungu uliotolewa kwa wanadamu. Kipaji hiki ni Roho Mtakatifu, ambaye hukata kiu yetu na kumwagilia ukame wetu, akitoa nuru kwenye njia yetu. Mtakatifu Luka, katika Matendo ya Mitume, pia anatumia neno “karama” kuashiria Roho Mtakatifu, Roho muumba anayeweza kufanya vitu vyo upya. Kwa njia ya mchakato wa sinodi, Roho ametia moyo tumaini la upyaisho wa kikanisa wenye uwezo wa kuzihuisha jumuiya, ili zikue katika njia ya Kiinjili, katika ukaribu na Mungu, na mbele ya huduma na ushuhuda ulimwenguni.

Safari ya Sinodi

Matunda ya safari ya Sinodi, baada ya muda mrefu wa kusikiliza na majadiliano, kwanza kabisa ilikuwa ni msukumo wa kuimarisha huduma na karama, kuvuta wito wa ubatizo, kuweka uhusiano na Kristo na ukaribisho wa kaka na dada zetu kwenye kituo, kuanzia na maskini zaidi, kushiriki furaha na huzuni zao, matumaini na shida zao. Kwa njia hiyo, tabia ya kisakramenti ya Kanisa inaakisiwa. Kama ishara ya upendo wa Mungu kwa wanadamu, wameitwa kuwa njia ya upendeleo kwa maji ya uzima ya Roho kuwafikia wote. Hili linahitaji hali ya kielelezo ya watu watakatifu wa Mungu. Papa alisisitiza kuwa kama tujuavyo, sakramenti na kielelezo ni dhana mbili muhimu katika kanisa la Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na katika kufikiri na kuishi Kanisa katika zama za kisasa  na kwa maneno ya Papa Francisko. Mtakumbuka jinsi ambavyo Mwezi ni  fumbo, ambalo ni, Kanisa linaloonekana katika kuakisi mwanga wa Kristo, katika uhusiano wake na Yeye, jua la haki na mwanga wa watu lilivyokuwa muhimu kwake.

Kuongoza utambuzi wa jamii hadi maamuzi ya kichungaji

Baba Mtakatifu Francisko, katika hati inayoambatana na Hati ya Mwisho wa Mkutano Mkuu wa XVI wa Sinodi (24 Novemba 2024), aliandika kwamba "ina viashiria ambavyo, kwa kuzingatia mwelekeo wake wa kimsingi, vinaweza kukubaliwa na Makanisa mahalia na vikundi vya Makanisa, kwa kuzingatia miktadha tofauti, kile ambacho tayari kimefanywa na kile kinachobaki kufanywa ili kujifunza na mtindo maalum wa umisionari wa Kanisa." Kwa hiyo mienendo ya Sinodi lazima iendelezwe katika miktadha halisi ya kila Kanisa la mahalia. Hii ina maana gani katika maneno madhubuti? Papa alifafanua kuwa, kwanza kabisa ni suala la kufanya kazi kwa ajili ya ushiriki hai wa wote katika maisha ya Kanisa. Katika suala hili, chombo kimoja cha kuimarisha maono ya Sinodi na Kanisa la kimisionari ni kile cha mihimili fungamani. Inasaidia Watu wa Mungu kutumia kikamilifu utambulisho wao wa ubatizo, kuimarisha kifungo kati ya wahudumu waliowekwa rasmi na jumuiya, na kuongoza mchakato kutoka katika utambuzi wa jamii hadi maamuzi ya kichungaji. Kwa sababu hiyo Papa Leo ametoa mwaliko wa kuimarisha uundaji wa vyombo shirikishi na, katika ngazi ya parokia, kupitia upya hatua zilizochukuliwa hadi sasa au, pale ambapo vyombo hivyo vinakosekana, kuelewa upinzani ili kushinda.

Onyo kuhusu Jimbo na viunganishi vya maeneo ya kichungaji

Papa alipenda pia kusema neno moja kuhusu majimbo na vyombo vingine vinavyounganisha maeneo mbalimbali ya maisha ya kichungaji, pamoja na sekta za kijimbo zenyewe, zilizoundwa ili kuunganisha vyema parokia za jirani katika eneo fulani na kituo cha Jimbo. Hatari ni kwamba vikundi hivi vitapoteza kazi yao kama vyombo vya ushirika na kupunguzwa kwa mikutano michache, ambapo tunajadili mada chache pamoja na kisha tunarudi kwenye kufikiria na kufanya mazoezi ya uchungaji kwa kutengwa, ndani ya parokia yetu au ndani ya mifumo yetu wenyewe. Papa Leo alisema kuwa, kama tunavyojua, katika ulimwengu mgumu zaidi na katika jiji linalokwenda kasi ambapo watu wanaishi katika uhamaji wa kila wakati, tunahitaji kufikiria na kupanga pamoja, tukiachana na mipaka iliyowekwa na kujaribu mipango ya pamoja ya kichungaji. Kwa hiyo, Papa aliwasihi wafanye ushirika huo kuwa maeneo ya kweli ya maisha ya jumuiya ambapo ushirika unaweza kutekelezwa, mahali pa  kuwa na majadiliano ambapo utambuzi wa jumuiya na wajibu wa pamoja wa ubatizo na wa kichungaji unaweza kutekelezwa.

Kuanzishwa kwa Uinjilishaji

Na leo tunaitwa kupambanua nini? Papa aliuliza na kujibu kuwa Yale ambayo yamefanywa katika miaka ya hivi karibuni ni ya thamani, lakini kuna baadhi ya malengo ya kutekelezwa kwa njia ya sinodi ambayo ningependa kuzingatia. Jambo la kwanza ninalopendekeza ni kukuza uhusiano kati ya uanzishwaji wa Kikristo na uinjilishaji, tukikumbuka kwamba ombi la Sakramenti linazidi kuwa chaguo lisilo la kawaida. Kuanzishwa katika maisha ya Kikristo ni mchakato ambao lazima uunganishe uwepo katika nyanja zake mbalimbali, kuwatayarisha watu hatua kwa hatua kwa ajili ya uhusiano na Bwana Yesu, kuwafanya wawe na ujasiri katika kusikiliza Neno, kuwa na shauku ya kufanya maombi, na kufanya kazi katika upendo. Tunahitaji kufanya majaribio, ikiwa ni lazima, kwa zana na lugha mpya, zinazohusisha familia katika mchakato na kutafuta kusonga mbele zaidi ya mbinu ya kielimu ya katekesi. Kwa mtazamo huu, ni lazima tuwatendee kwa usikivu na kuwajali wale wanaoonesha hamu ya Ubatizo wakiwa vijana na watu wazima. Ofisi za Vicariate zinazohusika na hili lazima zishirikiane na parokia, zikizingatia hasa malezi yanayoendelea ya makatekista.

Vijana na familia uwanja wa changamoto

Lengo la pili ni ushiriki wa vijana na familia, uwanja ambao tunakumbana na changamoto mbalimbali leo. Ninaamini kwamba ni muhimu kuanzisha huduma ya kichungaji ambayo ni ya kuunga mkono, yenye huruma, ya busara, na isiyohukumu, inayokaribisha watu wote, na ambayo inatoa njia za kibinafsi zaidi iwezekanavyo, zilizochukuliwa kwa hali mbalimbali za maisha za wale wanaoipokea. Kwa kuwa familia zinatatizika kusambaza imani na zinaweza kujaribiwa kukwepa kazi hii, ni lazima tujitahidi kuziunga mkono bila kuzibadilisha, tukiwa wenzi njiani na kutoa zana za kumtafuta Mungu. Ni—lazima tuwe waaminifu—huduma ya kichungaji ambayo hairudii mambo yale yale ya zamani, bali inatoa wajenzi wapya; huduma ya kichungaji ambayo inakuwa kama shule yenye uwezo wa kuwatambulisha watu katika maisha ya Kikristo, ya kuwasindikiza katika hatua za maisha, kujenga mahusiano ya kibinadamu yenye maana, na hivyo kuathiri mfumo wa kijamii, hasa katika kuwahudumia maskini zaidi na walio hatarini zaidi.

Dharura ya kielimu

Hatimaye, lengo la tatu, ambalo Papa alikazia kusema ni kwamba: ningependa kupendekeza uundaji katika viwango vyote. Tunakumbwa na dharura ya kielimu, na hatupaswi kujidanganya kwamba kuendelea tu na shughuli chache za kiutamaduni kutafanya jumuiya zetu za Kikristo ziendelee kuwa hai. Ni lazima ziwe za kuzaa: tumbo la uzazi ambalo huanzisha watu katika imani na moyo unaowatafuta wale ambao wameiacha. Parokia zinahitaji malezi, na pale ambapo hayapo, itakuwa muhimu kujumuisha kozi za kibiblia na kiliturujia, bila kupuuza masuala ambayo yanahusiana na shauku ya vizazi vichanga lakini yanatuhusu sisi sote: haki ya kijamii, amani, hali ngumu ya uhamiaji, utunzaji wa  kazi ya uumbaji, utumiaji sahihi wa uraia, heshima kwa wanandoa, mateso ya kiakili na ulevi, na changamoto zingine nyingi. Hakika hatuwezi kuwa wataalam katika kila kitu, lakini lazima tutafakari juu ya masuala haya, labda kwa kusikiliza ujuzi mwingi ambao jiji letu linaweza kutoa. Yote haya, ninapendekeza, yatungwe na kukamilishwa kwa pamoja, kwa njia ya sinodi, kama watu wa Mungu ambao, chini ya uongozi wa wachungaji wao, daima wanangoja na kutumaini kwamba siku moja, wote wataweza kweli kuketi kwenye karamu iliyoandaliwa na Bwana, kulingana na maono ya nabii Isaya (taz. 25:6-10).

kuwa wamisionari kama Msamaria aliyekwenda kutangaza kilichompata

Kifungu cha Injili cha mwanamke Msamaria kinahitimisha na umisionari, kwani  mwanamke Msamaria anakwenda kwa raia wenzake, anasimulia yaliyompata, na wanamwendea Yesu na kufikia ungamo la imani. Nina hakika kwamba katika jimbo letu pia, safari iliyoanza na kusindikizwa katika miaka ya hivi karibuni itatupeleka kukomaa katika sinodi, ushirika, uwajibikaji pamoja na utume. Tutajipyaish ndani yetu hamu ya kutangaza Injili kwa kila mwanamume na mwanamke wa wakati wetu; tutakimbia kuelekea kwao kama yule mwanamke Msamaria, tukiacha mtungi wetu na badala yake kubeba maji yanayozima kiu ya milele. Na tutakuwa na shangwe ya kusikia akina dada na kaka wengi ambao, kama Wasamaria, watatuambia: “Hatuamini tena kwa sababu ya hayo mliyosema, kwa maana tumesikia wenyewe, na twajua ya kuwa huyu ndiye kweli Mwokozi wa ulimwengu” ( Yh. 4:42 ). Bikira wa imani na matumaini, Salus Populi Romani, atusindikize na atulinde katika safari yetu.

 

19 Septemba 2025, 19:22