Papa Leo XIV,Maaskofu:Wawe na uhuru wa ndani,umaskini wa roho na utayari wa kutumikia
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV tarehe 11 Septemba 2025 alikutana katika Ukumbi wa Sinodi, na maaskofu waliowekwa wakfu katika mwaka uliopita na wale wanaohudumu katika nchi za Kimisionari. Papa Leo alizungumza kwa Kiingereza na Kiitaliano, na kutania kuhusu sauti yake kabla ya kuimba wimbo wa Uje Roho Mtakatifu na pia aliakisi hali ya mshangao ambayo bado ilionekana miezi minne baada ya kuchaguliwa kwake. "Nilifikiri, ningefika kwa kozi hii nikiwa nimevaa nguo nyeusi, pia." Kwa njia hiyo alihutubia maaskofu 192 kutoka mabara matano ambao tangu tarehe 3 Septemba, wamekuwa wakijishughulisha na mafunzo ya malezi yanayohamasishwa na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji na Baraza la kipapa la Maaskofu. Maneno ya Papa yalihusu utambulisho wa askofu. Papa alionyesha mawazo yake mwenyewe na ya wale waliochaguliwa na kwamba labda baadhi yenu bado mnasema: 'Imekuwaje nilichaguliwa?' na Mimi, najiuliza."
Kwa njia hiyo Maaskofu waliowekwa wakfu wa uaskofu katika kipindi hiki cha mwaka mmoja uliopita walihudhuria Kozi ya Malezi jijini Roma, iliyohitimishwa siku ya Alhamisi tarehe 11 Septemba 2025 kwa kwa Mkutano katika Ukumbi wa Sinodi mjini Vatican alitoa hotuba yake, huku akiwaomba Maaskofu wapya kukumbuka kwamba wamechaguliwa, wameitwa na kutumwa kuwa watumishi wa imani. "Ningependa kukumbuka jambo rahisi kama si la kuchukuliwa kuwa la kawaida: zawadi mliyopokea si kwa ajili yenu wenyewe, bali kutumikia kazi ya Injili.”
Baba Mtakatifu Leo XIV alijikita katika utume wa huduma waliokabidhiwa kwa Maaskofu, akisema unagusa utambulisho wao wenyewe. Utumishi, alisema, si tabia ya nje au seti ya matendo, bali ni mwito wa uhuru wa ndani, umaskini wa roho, na utayari wa utumishi unaotokana na upendo, ili kumwilisha chaguo la Yesu mwenyewe, ambaye alikuja kuwa maskini ili kututajirisha. Mungu alikuja kwetu si kwa nguvu bali kwa upendo wa Baba, aliongeza Papa, akibainisha kwamba “Mungu anatuita katika ushirika na Yeye mwenyewe.” Mtakatifu Agostino alisema kwamba Maaskofu, wanaosimamia wengine, ni lazima wajue kwamba wao ni “mtumishi wa wengi,” akielekeza kwenye onyo la Yesu kwa wanafunzi Wake ambao walikuwa wameanza kujitafutia ukuu.
Kwa hiyo “ninawaomba ninyi siku zote mkeshe na kutembea kwa unyenyekevu na sala, ili kujifanya watumishi wa watu ambao Bwana anawatuma ninyi kwao.” Papa Leo XIV alikumbuka maneno ya mtangulizi wake, Papa Francisko, aliyewaalika Maaskofu kukaribia kundi lao, kwani ukaribu wao unadhihirisha utunzaji wa Mungu kwa watu wake. Kama watumishi wa wote, Maaskofu wanapaswa kufahamu kwamba huduma yao inapaswa kumwilisha sura ya Kristo na huduma yake. Lakini, alibainisha Papa, lazima pia waunde utume wao ili kuakisi huduma ya Kristo, ikijumuisha katika njia yao ya uchungaji, kutangaza, na utawala.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba yake alisisitiza kusema kuwa “Mgogoro wa imani na uenezaji wake, pamoja na ugumu wa kumiliki na utendaji wa kikanisa, unatualika kugundua tena shauku na ujasiri wa kutangaza Injili mpya.” Maaskofu aliongeza: “wanapaswa kuwakaribisha wale wanaobisha hodi kwenye milango ya Kanisa, bila kusahau changamoto nyingine ambazo ni za kitamaduni na kijamii zaidi, zikiwemo vita, ghasia, mateso ya maskini, changamoto za kimaadili, na tamaa ya dunia inayojikita katika misingi ya udugu na mshikamano.
Papa Leo alisema kuwa “Kanisa, linawatuma ninyi kama wachungaji wanaojali, wasikivu wanaojua jinsi ya kushiriki safari, maswali, mahangaiko, na matumaini ya watu; wachungaji wanaotamani kuwa viongozi, baba, na kaka kwa mapadre na kwa dada na kaka zetu katika imani.” Kwa kuhitimisha Baba Mtakatifu Leo XIV aliomba kwamba Maaskofu wapya wasikose kamwe upepo wa Roho, na kwamba furaha ya kuwekwa wao kwa, kama harufu nzuri, ipate pia kuenea juu ya wale unaoenda kuwatumikia.”
