Papa Leo XIV:damu ya wafia imani ni mbegu ya Wakristo wapya
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika Siku kuu ya Kutukuka kwa Msalaba Mtakatifu, Baba Mtakatifu Leo XIV aliongoza tafakari ya kina na ya dhati katika Kumbukumbu ya mashahidi wapya na mashahidi wa imani wa karne ya 21, pamoja na wawakilishi wa Makanisa na jumuiya mbali mbali za Kikristo, katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo, Nje ya Kuta, Roma mbele ya takriban waamini 4,000. Kwa kuanza na kifungu cha Mtume Paulo kwa Wagalatia “ kisemacho “la hasha, mimi sitajisifu, ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo”(Gal 6:14), Papa alibainisha kuwa maneno ya Mtume Paulo, ambaye walikusanyika karibu na kaburi lake, yamewaletea ukumbusho wa mashahidi na mashuhuda wa imani ya karne ya 21, katika sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba Mtakatifu. Chini ya Msalaba wa Kristo, wokovu wetu, unaoelezewa kuwa "tumaini la Wakristo" na "utukufu wa mashahidi.”
Kwa njia hiyo Papa katika utangulizi alipenda kuwasalimu wawakilishi wa Makanisa ya Kiorthodox, Makanisa ya Kale ya Mashariki, Umoja wa Kikristo, na mashirika ya kiekumene kwa kukubali mwaliko huo na kwa wote waliokuwapo aliwapa kumbatio lake la amani. “Tunasadikishwa kwamba kifo cha kishahidi hadi kifo, ni ushirika wa kweli kabisa uliopo pamoja na Kristo, ambaye humwaga damu yake na, katika sadaka hii, huwaleta karibu wale ambao hapo awali walikuwa mbali (taz. Efe 2:13)” (Ut Unum Sint, 84).
Papa Leo XIV akiendelea alibainisha "leo hii tunaweza kuthibitisha pamoja na Yohane Paulo wa Pili kwamba, pale ambapo chuki ilionekana kupenya katika kila nyanja ya maisha, watumishi hawa wajasiri wa Injili na wafia imani walionesha wazi kwamba “upendo una nguvu zaidi kuliko mauti” (Ukumbusho wa Mashahidi wa Imani katika Karne ya Ishirini, Mei 7, 2000). Tuwakumbuke hawa ndugu zetu na mtazamo wetu ukiwa umeelekezwa kwenye Msalaba. Kwa Msalaba wake, Yesu alitufunulia uso wa kweli wa Mungu, huruma yake isiyo na kikomo kwa wanadamu; alijitwika mwenyewe chuki na jeuri ya Ulimwengu, ili kushiriki hatima ya wale wote waliofedheheshwa na kuonewa: “Yeye ameuchukua udhaifu wetu, amejitwika huzuni zetu” (Isa 53:4).
Papa alisisisitiza kuwa “Kaka na dada wengi sana, hata leo, kwa sababu ya ushuhuda wao wa imani katika hali ngumu na mazingira ya uhasama, wanabeba msalaba sawa na Bwana: kama yeye, wanateswa, wanahukumiwa, na kuuawa. Yesu alisema hivi juu yao: “Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki, kwa maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo kwa ajili yangu.” (Mt 5:10-11). Wao ni wanawake na wanaume, watawa wa kike na kiume, walei na makuhani, ambao hulipa maisha yao kwa ajili ya uaminifu wao kwa Injili, kujitolea kwao kwa haki, kupambania kwao kwa uhuru wa kidini ambapo bado unavunjwa na uthabiti wao duni. Kwa viwango vya kidunia, "walishindwa." Kiukweli, kama vile Kitabu cha Hekima kinavyotuambia: "Ingawa wanaadhibiwa machoni pa watu, tumaini lao linabaki bila kufa" (Hekima 3:4).
Baba Mtakatifu Leo XIV aliendelea na tafakari kuwa, katika Mwaka huu wa Jubilei, tunasherehekea matumaini ya mashahidi hawa wajasiri wa imani. Ni tumaini lililojaa hali ya kutokufa, kwa sababu kuuawa kwao kwa imani kunaendelea kueneza Injili katika Ulimwengu wenye chuki, jeuri, na vita; ni tumaini lililojaa kutokufa, kwa sababu, ingawa waliuawa katika mwili, hakuna mtu anayeweza kunyamazisha sauti yao au kufuta upendo waliotoa; ni tumaini lililojaa kutokufa, kwa sababu ushuhuda wao hudumu kama unabii wa ushindi wa mema dhidi ya uovu. Ndiyo, tumaini lao ni kunyang'anywa silaha. Walishuhudia imani yao bila hata kutumia silaha za nguvu na jeuri, lakini kwa kukumbatia nguvu dhaifu na ya upole ya Injili, kulingana na maneno ya mtume Paulo: “Nitajivunia udhaifu wangu kwa furaha zaidi ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. […] Kwa maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu” (2Kor 12:9-10).
Papa Leo amefikiria juu ya nguvu ya kiinjili ya Sr Dorothy Stang, ambaye alifanya kazi kwa wasio na ardhi huko Amazonia: kwa wale ambao walikuwa karibu kumuua na kuomba silaha, alionesha Biblia yake na kujibu, "Hii ndiyo silaha yangu pekee." Papa alimfikiria Padre Ragheed Ganni, Padre Mkaldayo kutoka Mosul, Iraq, ambaye aliacha kupigana ili kutoa ushahidi wa mwenendo wa Mkristo wa kweli. Alimfikiria Ndugu Francis Tofi, Mwanglikani na mshiriki wa Udugu wa Melanesia, ambaye alitoa maisha yake kwa ajili ya amani katika Visiwa vya Solomon. Mifano ni nyingi sana, kwa sababu cha kusikitisha ni kwamba, licha ya mwisho wa udikteta mkubwa wa karne ya ishirini, mateso ya Wakristo bado hayajatatuliwa; kiukweli, katika sehemu fulani za ulimwengu, imeongezeka. Watumishi hawa wajasiri wa Injili na mashahidi wa imani "huunda picha kubwa ya pamoja ya ubinadamu wa Kikristo [...]. Mchoro wa Injili ya Heri za Mlimani waliziishi hadi kumwaga damu" (Papa Yohane Paulo II,Ukumbusho wa Mashahidi wa Imani katika Karne ya Ishirini, 7 Mei 2000).
Papa alisisitiza kwa kaka na dada “, hatuwezi, hatutaki, kusahau. Tunataka kukumbuka. Tunafanya hivyo, tukiwa na hakika kwamba, kama ilivyokuwa katika karne za kwanza, vivyo hivyo katika milenia ya tatu, “damu ya wafia imani ni mbegu ya Wakristo wapya” (Tertullian). Tunataka kuhifadhi kumbukumbu pamoja na kaka na dada zetu wa Makanisa mengine ya Kikristo na Umoja. Kwa hiyo Papa alipenda kusisitiza dhamira ya Kanisa Katoliki katika kuhifadhi kumbukumbu za mashahidi wa imani ya mapokeo yote ya Kikristo. Tume ya Wafia imani Wapya, imo ndani ya Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Kikristo.
Kama tulivyotambua wakati wa Sinodi ya hivi karibuni, uekumene wa damu unawaunganisha “Wakristo wa imani mbalimbali ambao kwa pamoja wanatoa maisha yao kwa ajili ya imani katika Yesu Kristo. Ushuhuda wa kifo chao cha imani ni fasaha zaidi kuliko neno lolote: umoja hutoka kwa Msalaba wa Bwana” (Mkutano wa XVI wa Sinodi, Hati ya Mwisho, n. 23). Damu ya mashahidi wengi sana ilete karibu siku yenye baraka tutakapokunywa kikombe kimoja cha wokovu! Kwa kuhitimisha Papa alisema mtoto wa kiume wa kipakstani Aish Masih, aliyeuawa katika shambulio dhidi ya Kanisa Katoliki, alikuwa ameandika katika daftari yake kuwa: "Kuifanya dunia kuwa mahali pazuri." Ndoto ya mtoto huyu ituchochee kushuhudia kwa ujasiri imani yetu, ili kwa pamoja tuwe chachu ya ubinadamu wa amani na udugu.
Siku ya Kuzaliwa kwa Papa yaadhimishwa
Mwishoni mwa Maadhimisho ya Wafiadini na Mashuhuda wa Imani ya Karne ya 21 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo, Baba Mtakatifu Leo XIV, kwa mujibu wa Ofisi ya Vyombo vya habari aliwasalimia wawakilishi wa Makanisa mengine na Jumuiya za Kikristo katika Kanisa hilo. Kisha akakutana na makardinali na viongozi wengine katika Ukumbi wa Pinacoteca, ambapo Dekano wa Makardinali, Kardinali Giovanni Battista Re, alimtolea maneno machache ya pongezi kwa siku yake ya kuzaliwa. Papa alimshukuru, akibainisha sifa ya Siku kuu ya Kutukuka kwa Msalaba: "Tangu mwanzo wa wito wangu, siku zote nimejibu 'si mapenzi yangu, bali yako, Bwana."
Akielezea matumaini yake kwamba, hamasa ya waamini katika Mwaka huu wa Jubilei itazaa matunda kwa ajili ya utume wa kutangaza Injili, Papa alionesha furaha yake kwa kuadhimisha siku hii kwa maadhimisho ya kiekumene na kuwaalika watu wote kuendelea kwa pamoja, kuwa mashahidi wa umoja, upendo na matumaini.
Baada ya tafrija fupi, kukata kwa keki na wimbo wa siku ya kuzaliwa ulioimbwa na waliohudhuria, Papa Leo XIV aliondoka kwenye Basilika na kusimama ili kusalimiana na umati wa watu waliokuwa nje kabla ya kurejea Vatican.
