Papa Leo XIV:Gaza,hakuna wakati ujao wenye vurugu,uhamisho wa kulazimishwa na kulipiza kisasi
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Picha za Wapalestina wanaoukimbia mji wa Gaza wakiwa na magari, malori, mikokoteni ya kubahatisha, na hata kwa miguu, kufuatia agizo la jeshi la Israel la kuwahamisha, ndizo zilikuwa karibu ndani ya moyo maneno Papa Leo XIV, mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 21 Septemba 2025, akiwaelekea wawakilishi wa vyama kadhaa vya Kikatoliki vilivyojitolea kuwa na mshikamano na watu wa Ukanda wa Gaza na wote waliokuwa katika Uwanja wa Mtakatifu Petro ambapo Papa alisisitiza uthamini wake kwa ajili ya mpango wao na kwa wengine wengi katika Kanisa wanaoonesha ukaribu kwa kaka na dada zetu wanaoteseka katika nchi hiyo inayoteswa.
Baba Mtakatifu Leo alisema: “Ninawasalimu nyote, mliopo katika Uwanja wa Mtakatifu Petro na kuunganishwa kupitia vyombo vya habari. Kwanza kabisa ninawahutubia wawakilishi wa vyama mbalimbali vya Kikatoliki vilivyojitolea kwa mshikamano na watu wa Ukanda wa Gaza. Wapendwa marafiki, ninashukuru kwa mpango wenu na wengine wengi katika Kanisa wote ambao wanaonesha ukaribu kwa kaka na dada zetu wanaoteseka katika nchi hiyo inayoteswa.”
Papa Leo XIV aliongeza “Pamoja na nanyi na Wachungaji wa Makanisa katika Nchi Takatifu, ninarudia kusema: hakuna wakati ujao unaotegemea vurugu, uhamisho wa kulazimishwa, au kulipiza kisasi. Watu wanahitaji amani: wale wanaowapenda kweli hufanya kazi kwa amani.”
Babab Mtakatifu aliwageukia hata mahujaji na waamini waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro : “Nawasalimu mahujaji wa majimbo ya Mindelo, Cape Verde, na wale wa Jimbo la Como; pamoja na makundi kutoka Angola, Poland, hasa kutoka Bliżyn, Ciudad Real ya Hispania, Porto ya Ureno, na Mwanza nchini Tanzania.”
Papa Leo, hakuishia hapo bali alisema “Ninayofuraha kuwakaribisha Kwaya ya Chama cha Wanasheria wa Verona; kwaya ya Wanawake ya Malo huko Vicenza; Mfuko wa Oasi Nazareth ya Corato; Chama cha Mikono na Moyo cha H-Earth; na heshima maalum kwa wale wanaosumbuliwa na ugonjwa wa Alzheimers na ataxia. Asanteni nyote, na ninawatakia Dominika."
