Papa Leo,Makatekista:Tukumbuke hakuna atoaye asichokuwa nacho!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Hatimaye Jubilei ya Makatekista kutoka sehemu mbalimbali dunia ambao wamefika kufanya Jubilie yo kuanzia tarehe 26 imepata kilele chake cha kushiriki Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Leo XIV katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican katika Dominika ya 26 ya Mwaka C, tarehe 28 Septemba 2025. Makatekesia zaidi elfu ishirini kutoka nchi 115 ni kutoka: Italia, Hispania, Ureno, Ufaransa, Poland, Ukraine, Marekani, Argentina, Brazili, Paraguai, Mexico, Peru, Colombia, Ufilipino, India, na Australia na kwingineko. Hawa wanawakilisha ofisi za kijimbo na kitaifa za katekesi na Mabaraza ya Maaskofu ya nchi zao. Baada ya Masomo na Injili ilifuatiwa kuwakaribisha makatekesi 39 kwa kutajwa majina yao, yaliyosomwa na Shemasi, George Francis wa Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi, Tanzania, na kabla ya Mahubiri ya Papa Leo, VI aliwaweka wakfu na kuwatuma kuwa wamisionari kwa kukabidhiwa misalaba.
Baba Mtakatifu alianza mahubiri yake akisema kuwa Maneno ya Yesu yanatuambia jinsi Mungu anavyoutazama Ulimwengu, katika kila wakati na mahali. Katika Injili tuliyokwisha kuisikia hivi punde (Lk 16:19-31), macho yake yanaona mtu maskini na tajiri, wale wanaokufa kwa njaa na wale wanaojisongesha mbele yake; anaona nguo za kifahari za mmoja na majeraha ya mwingine yanayolambwa na mbwa (rej. Lk 16:19-21). Lakini si hivyo tu: Bwana hutazama ndani ya mioyo ya wanadamu, na kupitia macho yake, tunatambua mtu maskini na mtu asiyejali. Lazaro anasahauliwa na wale wanaosimama mbele yake, nje ya mlango wa nyumba yake, lakini Mungu yuko karibu naye na analikumbuka jina lake.
Papa aliendelea kusema kuwa Mtu anayeishi na wingi, hata hivyo, hana jina, kwa sababu anapoteza mwenyewe utambulisho wake, akimsahau jirani yake. Amepotea katika mawazo ya moyo wake, amejaa mambo na upendo mtupu. Mali zake hazimfanyi kuwa mzuri. Historia ambayo Kristo anatuambia, kwa bahati mbaya, inafaa sana. Leo hii kwenye malango ya utajiri kuna taabu ya watu wote, wanaosumbuliwa na vita na unyonyaji. Kwa karne nyingi, hakuna kinachoonekana kuwa kimebadilika: Ni akina Lazaro wangapi wanakufa kabla ya uchoyo unaopuuza haki, faida inayokanyaga upendo, mali hupofusha uchungu wa maskini! Hata hivyo Injili inatuhakikishia kwamba mateso ya Lazaro yana mwisho. Maumivu yake yanaisha wakati karamu ya tajiri inaisha, na Mungu analeta haki kwa wote wawili: "Yule maskini akafa na akachukuliwa na Malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Tajiri naye akafa, akazikwa" (Lk 16, 22). Kanisa linatangaza neno hili la Bwana bila kuchoka, ili liweze kugeuza mioyo yetu.
Papa alieleza kwamba kwa bahati nzuri na ya kipekee kifungu hiki hiki cha Injili kilitangazwa hata wakati wa Jubilei ya Makatekista katika Mwaka Mtakatifu wa Huruma. Akiwahutubia mahujaji waliofika Roma kwa ajili ya hafla hiyo, Papa Francisko alisisitiza kwamba Mungu anaukomboa ulimwengu na uovu wote, akitoa maisha yake kwa ajili ya wokovu wetu. Hatua yake ni mwanzo wa utume wetu, kwa sababu inatualika kujitoa kwa manufaa ya wote. Papa aliwaambia makatekista kuwa: “Kituo hiki ambacho kila kitu kinazungukia, moyo huu unaodunda unaotoa uhai kwa kila kitu, ni tangazo la Pasaka, tangazo la kwanza: Bwana Yesu amefufuka, Bwana Yesu anakupenda, alitoa maisha yake kwa ajili yako; aliyefufuka na kuwa hai, yuko kando yako na anakungoja kila siku” (Mahubiri Septemba 25, 2016). Papa Leo aliongeza kusema kuwa maneno haya yanatufanya tutafakari juu ya mazungumzo kati ya tajiri na Ibrahimu, tuliyoyasikia katika Injili: ni ombi ambalo tajiri anatoa ili kuokoa ndugu zake na ambayo inakuwa changamoto kwetu.
Akizungumza na Ibrahamu, anapaza sauti: “Kama mtu kutoka kwa wafu akiwaendea, watatubu” ( Lk 16:30 ). Ibrahimu anajibu: “Ikiwa hawasikii Musa na Manabii, hawatasadiki hata kama mtu atafufuka kutoka kwa wafu” (Lk 16, 31).Vema, mmoja amefufuka kutoka kwa wafu: Yesu Kristo. Basi, maneno ya Maandiko hayakusudiwi kutuvunja moyo au kutukatisha tamaa, bali kuamsha dhamiri zetu. Kumsikiliza Musa na Manabii kunamaanisha kukumbuka amri na ahadi za Mungu, ambaye usimamizi wake haumwachi mtu yeyote. Injili inatuambia kwamba maisha ya kila mtu yanaweza kubadilika, kwa sababu Kristo amefufuka kutoka kwa wafu. Tukio hili ni ukweli unaotuokoa: kwa hiyo, ni lazima ijulikane na kutangazwa, lakini haitoshi. Inapaswa kupendwa: ni upendo huu unaotuongoza kuelewa Injili, kwa sababu inatubadilisha kwa kufungua mioyo yetu kwa neno la Mungu na kwa uso wa jirani.
Papa aliwageukia Makatekista kwamba “Katika suala hili, ninyi makatekista ni wale wanafunzi wa Yesu ambao wanakuwa mashahidi kwake: jina la huduma mnayofanya linatokana na kitenzi cha Kigiriki katēchein, ambacho kinamaanisha kufundisha kwa neno la kinywa, kufanya isikike sauti.”Hii inataka kutuambia kwamba katekista ni mtu wa neno lake, neno analotamka kwa maisha yake. Kwa hiyo, makatekista wa kwanza ni wazazi wetu, wale ambao kwanza walizungumza nasi na kutufundisha kuzungumza. Kama vile tulivyojifunza lugha yetu ya asili, utangazaji wa imani hauwezi kukabidhiwa kwa wengine, lakini hufanyika mahali tunapoishi. Kwanza kabisa, katika nyumba zetu, karibu na meza: wakati kuna sauti, ishara, uso unaoongoza kwa Kristo, familia hupata uzuri wa Injili. Sote tulifundishwa kuamini kupitia ushuhuda wa wale walioamini kabla yetu.
Ushauri wa Papa kwa makatekesita kwamba “Kama watoto na vijana, kama vijana, basi kama watu wazima na hata kama wazee, makatekista husindikizana nasi kwa imani, mkishiriki safari ya kudumu, kama mlivyofanya siku hizi zilizopita kwenye hija ya Jubilei. Nguvu hii inahusisha Kanisa zima: kwa hakika, watu wa Mungu wanapowazalisha wanaume na wanawake kwenye imani, “ufahamu hukua, wa mambo na maneno yanayopitishwa, iwe kwa kuyatafakari na kuyachunguza waamini wanaoyatafakari mioyoni mwao (rej. Lk 2:19, 51), au kupitia ufahamu unaotolewa na uzoefu wa ndani zaidi wa mambo ya kiroho, au kwa njia ya mahubiri ya wale ambao kupitia urithi wa kiaskofu wamepokea karama ya hakika ya ukweli”(Dei Verbum, 8).
Katika muungano huo Katekisimu ni “chombo cha kusafiria” kinachotulinda dhidi ya ubinafsi na mifarakano, kwa sababu inathibitisha imani ya Kanisa Katoliki zima. Kila mwamini hushirikiana katika kazi yake ya kichungaji kwa kusikiliza maswali, kushiriki majaribu, kutumikia hamu ya haki na ukweli inayokaa ndani ya dhamiri ya mwanadamu. Hivi ndivyo makatekista wanavyofundisha, yaani, wanaacha alama ya ndani: tunapoelimisha katika imani, hatutoi somo, bali tunaweka neno la uzima mioyoni mwao, ili liweze kuzaa matunda ya wema.
Kwa shemasi Deogratias, ambaye alimuuliza jinsi ya kuwa katekista mzuri, Mtakatifu Agostino alijibu: "Eleza kila kitu kwa njia ambayo wale wanaokusikiliza wapate kuamini, wakiamini wawe na matumaini, na wakitumaini wanaweza kupenda"(De catechizandis rudibus, 4, 8). Kwa maana hiyo Papa leo XIV alitoa ushauri kwamba, “hebu tufanye mwaliko huo kuwa wetu! Tukumbuke hakuna atoaye asichonacho. Ikiwa tajiri katika Injili angeonesha upendo kwa Lazaro, angemnufaisha sio maskini tu bali pia yeye mwenyewe. Ikiwa mtu huyo asiye na jina angekuwa na imani, Mungu angalimwokoa kutoka katika kila mateso: ni kushikamana kwake na utajiri wa kilimwengu ndiko kulikompokonya tumaini la wema wa kweli na wa milele. Sisi pia tunapojaribiwa na ulafi na kutojali, Lazaro wengi wa siku hizi wanatukumbusha maneno ya Yesu, yanakuwa kwetu katekesi yenye ufanisi zaidi katika Jubilei hii, ambayo kwa wote ni wakati wa wongofu na msamaha, wa kujitolea kwa haki na kutafuta kwa dhati amani.”
