Tafuta

Papa Leo XIV:tunachopewa ni zawadi ya Mungu,tujenge Ulimwengu wa haki,usawa na udugu zaidi!

Ni lazima tusimamie zawadi tulizopokea kutoka kwa Baba,maisha yetu yenyewe,kwa uangalifu na wajibu,tukijua kwamba sisi si mabwana wake na kwamba kulimbikiza sio thamani kuu zaidi.Utajiri wa kweli ni urafiki na Bwana na pamoja na kaka na dada zetu.Ni katika tafakari ya Papa Leo XIV kabla ya sala ya Malaika wa Bwana,Dominika tarehe 21 Septemba,kwa waamini waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro,Vatican.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV, Dominika tarehe 21 Septemba 2025, kama kawaida ameongeza tafakari yake akiwa katika Dirisha la Jumba la Kitume mjini Vatican kwa waamini na mahujaji wapatoa 15,000 waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican. Akiwageukia wote kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana, Papa aliwatakia Dominika njema na kuendelea kusema kuwa, mfano tunaousikia leo  hii kutoka katika Injili (Lk 16:1-13) unatufanya tutafakari juu ya matumizi ya mali na, kwa ujumla zaidi, jinsi tunavyosimamia mali ya thamani kuliko zote yaani: maisha yetu. Katika historia, tunaona msimamizi aliyeitwa na bwana wake "kutoa hesabu." Picha hii inawasilisha jambo muhimu kuwa: sisi si mabwana wa maisha yetu au wa bidhaa tunazofurahia; kila kitu kimetolewa kwetu kama zawadi na Bwana, na amekabidhi urithi huu kwa utunzaji wetu, uhuru wetu, na wajibu wetu.”

Waamini katika Uwanja wa Mtakatifu Petro
Waamini katika Uwanja wa Mtakatifu Petro   (@VATICAN MEDIA)

Papa Leo XIV, aliongeza: “Siku moja, tutaitwa kuwajibika kwa jinsi tulivyojisimamia sisi wenyewe, mali zetu, na rasilimali za dunia, mbele ya Mungu na mbele ya wengine, jamii, na zaidi ya yote, wale wanaokuja baada yetu.” Kadhalika, Papa Leo alidadavua kifungu hiki cha Injili kwamba “Wakili katika mfano huo alitafuta faida yake mwenyewe tu, na siku ikafika ambapo lazima atoe hesabu na uwakili wake kuondolewa kwake, lazima afikirie nini cha kufanya kwa ajili ya wakati wake ujao.” Katika hali hii ngumu, anatambua kwamba mrundikano wa mali si jambo la maana zaidi, kwa sababu utajiri wa dunia hii ni wa kupita. Kwa hivyo anakuja na wazo zuri: Anawaita wadeni wake na "kukata" madeni yao, na hivyo kukataa sehemu ambayo ingekuwa yake. Kwa njia hiyo, anapoteza mali yake ya kimwili,  lakini anapata marafiki, ambao watakuwa tayari kumsaidia na kumtegemeza.

Makundi ya waamini wanahija katika Uwanja wa Mtakatifu Petro
Makundi ya waamini wanahija katika Uwanja wa Mtakatifu Petro   (@VATICAN MEDIA)

Tukiwa na msukumo kutoka katika historia hiyo, Yesu anatuhimiza hivi: “Jifanyieni marafiki kwa mali isiyo ya haki, ili itakaposhindikana wawakaribishe katika nyumba za milele” (Lk 16,9). Kiukweli, msimamizi katika mfano huo, hata anaposimamia mali isiyo ya haki ya ulimwengu huu, anafaulu kutafuta njia ya kupata marafiki, akiibuka kutoka katika upweke wa ubinafsi wake mwenyewe.” Papa Leo XIV aliongeza “zaidi ya hayo, sisi, tulio wanafunzi na tunaoishi katika nuru ya Injili, lazima tutumie mali ya Ulimwengu na maisha yetu tukiwa na mali ya kweli akilini, ambayo ni urafiki na Bwana na kaka na dada zetu.”

Papa Leo akiwapungia mkono
Papa Leo akiwapungia mkono   (@VATICAN MEDIA)

Papa alikazia kusema kwamba “mfano huo unatualika kujiuliza: je, tunasimamiaje mali, mali ya dunia, na maisha yetu ambayo Mungu ametukabidhi? Tunaweza kufuata kigezo cha ubinafsi, kutanguliza mali na kujifikiria sisi wenyewe tu; lakini hii inatutenga na wengine na kueneza sumu ya ushindani ambayo mara nyingi huzalisha migogoro.  Au tunaweza kutambua kila kitu tulicho nacho kama zawadi kutoka kwa Mungu ya kusimamiwa, na kuitumia kama chombo cha kushirikiana, kuunda mitandao ya urafiki na mshikamano, kujenga wema, kujenga ulimwengu wa haki zaidi, usawa zaidi, na wa kidugu zaidi.” Kwa kuhitimisha Baba Mtakatifu alisema Tuombe kwa Bikira Mtakatifu ili atuombee sisi na kutusaidia kusimamia vema kile ambacho Bwana anatukabidhi, kwa haki na uwajibikaji.

Papa kabla ya Sala ya Malaika,Septemba 21
21 Septemba 2025, 14:30