Bikira Maria Malkia wa Rozari Takatifu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Rozari Takatifu ni muhtasari wa huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Ni njia muafaka ya kutafakari maisha na utume wa Kristo Yesu, ili kumfahamu, kumpenda, kumfuasa na kumtumikia kwa njia ya upendo kwa jirani wenye shida. Waamini wanahamasishwa kuendelea kusali Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi; maisha na utume wa Kristo Yesu! Itakumbukwa kwamba, Tarehe 7 Oktoba ya kila Mwaka, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Bikira Maria Malkia wa Rozari Takatifu. Huu ni mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema katika Kipindi hiki cha Mwezi wa Oktoba, kujibidiisha kusali Rozari Takatifu, huku wakimwachia nafasi Bikira Maria, ili aweze kuwasindikiza kwenda kwa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu! Tarehe 7 Oktoba 2025, Jumuiya ya Kimataifa, inafanya kumbukumbu ya miaka mitatu tangu Jeshi la Hamasi lilipoivamia na kuishambulia Israeli. Tangu wakati huo, kuna zaidi ya watu 66, 055 wamefariki dunia na majeruhi ni zaidi ya watu 168, 346. Hizi ni takwimu hadi kufikia tarehe 29 Septemba 2025.
Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” anamwangalia Bikira Maria aliyemwilisha Heri za Mlimani kuliko mtakatifu yoyote yule. Ni mwanamke wa imani aliyefurahia uwepo wa Mungu katika maisha yake na kuhifadhi yote katika sakafu ya moyo wake! Bikira Maria ni Mtakatifu kuliko watakatifu wote. Bikira Maria ni kimbilio la waamini katika ulinzi na tunza yake ya kimama. Anawafundisha na kuwasindikiza waamini katika unyofu na utakatifu wa maisha; anawalinda bila kuwahukumu; anawafariji, kuwaombea na kuwatakatifuza kwa uwepo wake mwanana, changamoto na mwaliko kwa waamini kumkimbilia katika sala, lakini zaidi kwa njia ya tafakari ya Rozari Takatifu. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, Rozari Takatifu ni muhtasari wa huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Ni njia muafaka kabisa ya kutafakari maisha na utume wa Kristo Yesu, ili kumfahamu, kumpenda, kumfuasa na kumtumikia kwa njia ya upendo kwa Mungu na kwa jirani wenye shida na mahangaiko mbalimbali wanaokumbukwa katika Sala ya Rozari Takatifu. Waamini wanahamasishwa kuendelea kusali Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi; maisha na utume wa Kristo Yesu.
Bikira Maria alipowatokea Watoto watatu wa Fatima yaani: Francis, Yacinta na Lucia aliwaagiza kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya toba, wongofu wa ndani na amani duniani. Kila mwezi Oktoba waamini Wakatoliki wanaalikwa kusali Rozari kwa mwezi mzima. Lengo kubwa ni kumheshimu na kumshukuru Mama Bikira Maria kwa maombezi yake ya kimama. Mwezi Oktoba ni fursa nyingine tena ya kumwendea Mama Bikira Maria na kumshirikisha furaha, shukrani, taabu, changamoto na matarajio ya waamini kwa njia ya Rozari Takatifu ambayo hutoa nafasi ya kutafakari mafumbo ya maisha ya Kristo Yesu na Bikira Maria katika safari ya wokovu. Mwaka 1930 Kanisa lilitamka wazi kuwa Sala ya Fatima itumiwe na Wakristo wote wa Kanisa zima wasalipo Rozari Takatifu. Sala hii ilifanya rozari kuwa na jumla ya sala 6. Kuanzia karne ya 16 hadi mwanzoni mwa Karne ya 21 kulikuwa na makundi matatu ya mafumbo ya Rozari: Mafumbo ya Furaha, Utukufu na Mafumbo ya Uchungu. Mwaka 2001 Mtakatifu Yohane Paulo II aliongeza Mafumbo ya Mwanga. Katika Maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Safi wa Bikira Maria, tarehe 20 Juni 2020, Hayati Baba Mtakatifu Francisko aliridhia kwamba, katika Litania ya Bikira Maria wa Loreto inayojulikana na kupendwa na wengi, viongezwe vifungu vitatu. Yaani: “Mater Misericordiæ”, yaani “Mama wa huruma; “Mater Spei,” yaani “Mama wa Matumaini na hatimaye “Solacium Migrantium” yaani “Mfariji wa wakimbizi” sehemu hii inaweza pia kutafsiriwa kuwa ni “Msaada wa Wakimbizi.” Nia kubwa ni kuwafanya waamini watafakari maisha ya Kristo Yesu kati ya kuzaliwa kwake, Mateso na Ufufuko wake uletao uzima wa milele.
Itakumbukwa kwamba, Mama Kanisa ametenga mwezi Mei na Oktoba kuwa miezi ya kumweshimu Mama Bikira Maria. Wengi wetu hufahamu tu mwezi Oktoba. Mwezi Mei ni mwezi wa Bikira Maria kwa kuwa Bikira Maria aliwatokea Lucia, Francis na Yacinta huko Fatima Ureno kwa mara ya kwanza tarehe 13, Mei, 1917 ujumbe mkuu ukiwa kuhangaikia wokovu wa roho za binadamu kwa njia ya kusali rozari na ibada kwa Moyo Safi wa Bikira Maria. Mwezi Oktoba ni mwezi wa kusali Rozari Takatifu. Kuchanguliwa kwa mwezi wa Oktoba kuna msingi wake katika historia ya Kanisa. Waislam wa Kituruki miaka ya 1500 waliamua kutumia mwanya wa vuguvugu la kujitenga kwa Waprotestanti kutoka Kanisa Katoliki. Hivyo waliamua kuvamia nchi za Ulaya ili kueneza dini yao kwa nguvu ya upanga na vita kwa kuwalazimisha Wakristo kuongokea dini ya Kiislamu. Tarehe 7 Oktoba 1571 Waislamu wa Kituruki waliamua kuivamia Italia kwa kuanzisha vita ya baharini iliyojulikana kama Vita vya Lepanto (Ugiriki). Baba Mtakatifu Pio V (7 Januari 1566 hadi 1 Mei 1572). Baba Mtakatifu Pio V alifahamu wazi kuwa Waislamu walikuwa ni wengi kwa idadi kuliko Wakristo na ya kuwa Waislamu walikuwa na meli nyingi za kivita kuliko Wakristo. Hata hivyo Baba Mtakatifu Pio V aliamuru jeshi lake likisaidiwa na wanajeshi kutoka Hispania kwenda baharini kupambana na Waislamu. Baba Mtakatifu aliamuru kila askari abebe Rozari na kuisali wanapokuwa vitani; pia aliamuru wananchi wa Italia waliobaki majumbani mwao wafanye maandamo makubwa huku wakisali Rozari kuomba msaada, ulinzi na tunza ya Bikira Maria ili Wakristo washinde vita. Yeye mwenyewe alisali Rozari siku hiyo ya tarehe 7 Oktoba. Muda si mrefu habari zilimfikia Baba Mtakatifu kuwa Wakristo wameshinda vita na kati ya meli 242 za Waislamu zimesalia meli 12 tu huku jumla ya Waislamu 30,000 wakiwa wameuwa, takribani 8,000 wamejeruhiwa au kutekwa. Kwa upande wa Wakristo ni watu 7,500 tu waliokuwa ama wameuawa au wamejeruhiwa au kutekwa ambao baadaye wengi wao walifanikiwa kutoroka. Baba Mtakatifu Pio V alitamka kuwa ushindi huo haujatokana na weledi wa askari wala ubora wa vifaa vya kivita bali ni ushindi uliotokana na maombezi ya Bikira Maria Malkia wa Rozari.
Kutokana na ushindi huo dhidi ya Waislamu Baba Mtakatifu Pio V alianzisha rasmi Sikukuu ya Mama Yetu wa Ushindi mwaka 1572. Baba Mtakatifu Pius V ndiye pia aliyeongeza maneno “Msaada wa Wakristo” kwenye Litania ya Bikira Maria kama moja ya sifa za Bikira Maria. Mwaka 1573 Baba Mtakatifu Gregori XIII aliibadilisha jina la Sikuu hiyo na kuipa jina la Sikukuu ya Bikira Maria Mama wa Rozari Takatifu. Mwaka 1884 Baba Mtakatifu Leo XIII alitangaza rasmi kuwa mwezi wote wa Oktoba utakuwa mwezi wa kusali Rozari Takatifu akiwa na kumbukumbu ya ushindi ambao Wakristo waliupata dhidi ya Waislamu katika vita vya Lepanto tarehe 7 Oktoba 1571. Lengo kubwa la kutangaza mwezi wa Oktoba kuwa mwezi wa Rozari Takatifu lilikuwa kumheshimu na kumshukuru Bikira Maria ambaye kwa maombezi yake Wakristo walipata ushindi tarehe 7 Oktoba 1571. Rozari inatuwezesha kuwa na ufahamu kamili kuhusu Yesu siku kwa siku. Rozari Takatifu inatakasa roho zetu. Rozari inatupatia ushindi dhidi ya adui zetu. Rozari inatuwezesha kuishi maisha ya fadhila. Rozari inawasha ndani yetu moyo wa mapendo kwa Bwana Wetu Yesu Kristo. Rozari inatutajirisha kwa neema na mastahili. Rozari inatuwezesha kupata yale tunayohitaji kutoka kwa Mungu. Rozari inawezesha kufunguliwa kwa roho zilizopo toharani. Rozari inatutia nguvu tuwapo katika madhaifu na changamoto za kimwili na kiroho. Matokeo ya Kusali Rozari: Kwa hakika Rozari ni sala yenye nguvu sana. Ukijiwekea mazoea ya kuisali utaona uzuri wa Rozari na kamwe hutaiacha. Kuna watu wanadhani kwamba kusali Rozari ni mzigo, ni kupoteza muda na kama kero tupu. Lakini kila siku nazidi kuonja uzuri na nguvu ya Sala ya Rozari. Muda mzuri wa kusali Rozari ya binafsi, kwa kadiri ya uzoefu wangu binafsi, ni alfajiri kwani akili huwa imetulia sana. Hata hivyo, kila mtu anaweza kutenga muda wake atakaoona unafaa kwake. Kwa njia ya kusali Rozari: Wadhambi wanasamehewa. Roho zenye kiu zinaburudishwa. Magumu yanafanywa kuwa mepesi. Wanaopitia majaribu wanapata amani na utulivu wa ndani. Maskini na wenye mahangaiko wanapata faraja na matumaini. Roho za marehemu toharani zinapunguziwa mateso na zingine kufunguliwa. Ee Mama Mpendelevu sana, utujalie nguvu ya kuweza kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya wokovu wetu na wa dunia nzima. Amina.
ITANIA YA BIKIRA MARIA
Baba wa mbinguni Mungu Utuhurumie.
Mwana, Mkombozi wa dunia, Mungu, Utuhurumie.
Roho Mtakatifu, Mungu, Utuhurumie.
Utatu Mtakatifu, Mungu mmoja, Utuhurumie.
Maria Mtakatifu, Utuombee.
Mzazi Mtakatifu wa Mungu, Utuombee.
Bikira Mtakatifu, mkuu wa Mabikira, Utuombee.
Mama wa Kristo, Utuombee.
Mama wa neema ya Mungu, Utuombee.
Mama wa matumaini Utuombee.
Mama wa Kanisa utuombee Utuombee.
Mama wa huruma Utuombee
Mama mtakatifu sana, Utuombee.
Mama mwenye moyo safi, Utuombee.
Mama mwenye ubikira, Utuombee.
Mama usiye na dhambi Utuombee.
Mama mpendelevu, Utuombee.
Mama mstaajabivu, Utuombee.
Mama wa shauri jema, Utuombee.
Mama wa Mwumba, Utuombee.
Mama wa Mkombozi, Utuombee.
Bikira mwenye utaratibu, Utuombee.
Bikira mwenye heshima, Utuombee.
Bikira mwenye sifa, Utuombee.
Bikira mwenye huruma, Utuombee.
Bikira mwaminifu, Utuombee.
Kioo cha haki, Utuombee.
Kikao cha hekima, Utuombee.
Sababu ya furaha yetu, Utuombee.
Chombo cha neema, Utuombee.
Chombo cha heshima, Utuombee.
Chombo bora cha ibada, Utuombee.
Waridi lenye fumbo, Utuombee.
Mnara wa Daudi, Utuombee.
Mnara wa pembe, Utuombee.
Nyumba ya dhahabu, Utuombee.
Sanduku la Agano, Utuombee.
Mlango wa mbingu, Utuombee.
Nyota ya asubuhi, Utuombee.
Afya ya wagonjwa, Utuombee.
Kimbilio la wakosefu, Utuombee.
Mfariji wa wakimbizi Utuombee.
Mfariji wa wenye uchungu, Utuombee.
Msaada wa Wakristo, Utuombee.
Malkia wa Malaika, Utuombee.
Malkia wa Mababu, Utuombee.
Malkia wa Manabii, Utuombee.
Malkia wa Mitume, Utuombee.
Malkia wa Mashahidi, Utuombee.
Malkia wa Waungama, Utuombee.
Malkia wa Mabikira, Utuombee.
Malkia wa Watakatifu wote, Utuombee.
Malkia uliyeumbwa pasipo dhambi ya asili, Utuombee.
Malkia uliyepalizwa mbinguni, Utuombee.
Malkia wa Rozari Takatifu, Utuombee.
Malkia wa Amani, Utuombee.
Malkia wa Familia, Utuombee.
Mwana kondoo wa Mungu, uondoaye dhambi za Ulimwengu, UtusameheEe Bwana.
Mwana kondoo wa Mungu, uondoaye dhambi za Ulimwengu, Utusikilize Ee Bwana.
Mwana kondoo wa Mungu, uondoaye dhambi za Ulimwengu, Utuhurumie Ee Bwana.
