Papa Leo,Utume wa Kichungaji kwa wazee:kutambua kuwa kuzeeka ni sehemu ya maajabu ya uumbaji
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV alikutana mjini Vatican tarehe 3 Oktoba 2025 na washiriki wa Kongamano la II la Kimataifa la Malezi ya Kichungaji kwa Wazee, likiongozwa na kauli mbiu: “Wazee Wenu Wataota Ndoto,” lililoandaliwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, ambalo litahitimishwa Oktoba 4, katika Ukumbi Mkuu wa Shirika la Kijesuit, mjini Roma. Akianza hotuba yake, Papa aliwakaribisha wote na kuonesha furaha kukutana nao katika maadhimisho ya Kongamano hilo la Pili la Kimataifa la Malezi ya Wazee. Papa alibainisha juu ya mada yao ya, "Wazee wako wataota ndoto!" (taz. Yoeli 2:28) na kwamba inakumbuka maneno ya nabii Yoeli aliyependwa sana na Papa Francisko, ambaye mara nyingi alizungumza juu ya hitaji la muungano kati ya vijana na wazee, uliochochewa na “ndoto” za wale ambao wameishi maisha marefu na waliotajirishwa na “maono” ya wale wanaoanza safari kuu ya maisha.
Askofu wa Roma aliendelea kukazia kuwa katika kifungu hiki, nabii anatangaza kumiminiwa kwa Roho Mtakatifu ulimwenguni pote, ambaye anaunda umoja kati ya vizazi na kusambaza karama tofauti kwa kila mtu. Katika wakati wetu, kwa bahati mbaya, mahusiano kati ya vizazi mara nyingi yanajulikana na mgawanyiko na migogoro ambayo inawashindanisha. Wazee, kwa mfano, wanalaumiwa kwa kutowaachia nafasi vijana kazini, au kutumia rasilimali nyingi za kiuchumi na kijamii kwa madhara ya vizazi vingine, kana kwamba maisha marefu ni makosa. Hizi ni njia za kufikiri zinazofichua mitazamo isiyo na matumaini na migongano ya maisha. Wazee ni zawadi, baraka ya kukaribishwa, na maisha marefu ni kitu chanya; hakika, ni mojawapo ya ishara za matumaini katika wakati wetu, kila mahali ulimwenguni.
Kuhusiana na suala hili la Kichungaji, Papa Leo XIV aidha alisisitiza kwamba bila shaka, pia ni changamoto, kwa sababu idadi inayoongezeka ya wazee ni jambo la kihistoria ambalo halijawahi kutokea ambalo linatuita kutambua na kuelewa ukweli kwa njia mpya. Uzee juu ya yote ni ukumbusho wa manufaa wa nguvu ya ulimwengu ya maisha. Mawazo yaliyopo leo hii huelekea kuthamini kuwepo ikiwa huzalisha mali au mafanikio, ikiwa hutumia nguvu au mamlaka, kusahau kwamba mwanadamu daima ni kiumbe mdogo na mahitaji. Udhaifu unaoonekana kwa wazee unatukumbusha ukweli huu wa kawaida; kwa hiyo wamefichwa au kuondolewa na wale wanaokuza ndoto za kidunia, ili wasiwe na mbele ya macho yao picha ya kile ambacho tukikuwa hakiwezi kuepukika. Badala yake, inafaa kutambua kwamba kuzeeka “ni sehemu ya maajabu ya uumbaji.” Udhaifu huu, “ikiwa tuna ujasiri wa kuukubali,” kuukumbatia na kuutunza, “ni daraja la kuelekea mbinguni.” Badala ya kuaibishwa na udhaifu wa kibinadamu, kiukweli tutaongozwa kuomba msaada kutoka kwa kaka na dada zetu na kutoka kwa Mungu, ambaye hutazama viumbe vyake vyote akiwa Baba.
Baba Mtakatifu Leo alisema kwamba Wazee hutufundisha kwamba “wokovu haupatikani katika kujitawala, bali kwa kutambua kwa unyenyekevu hitaji la mtu mwenyewe na katika kuweza kulieleza kwa uhuru,” ili “kipimo cha ubinadamu wetu hakitolewi na kile tunachoweza kufikia, bali kwa uwezo wetu wa kujiruhusu kupendwa na, inapohitajika, hata kusaidiwa.” Ingawa inaweza kuonekana kuwa ya ajabu, uzee kwa huzuni unazidi kuwa kitu ambacho huja ghafla na kutupata bila kujiandaa. Kwa kutumia Maandiko Matakatifu, hekima ya Mababa na uzoefu wa watakatifu, Kanisa linaitwa kutoa nyakati na zana za kuelewa uzee, ili tuweze kuuishi kwa njia ya Kikristo, bila kujifanya kuwa bado vijana milele na bila kujiruhusu kushindwa na kukatishwa tamaa. Kwa maana hiyo, katekesi ambayo Baba Mtakatifu Francisko alijitolea kwa mada hiyo kunako mwaka 2022 ni ya thamani sana, inakuza hali ya kiroho ya kweli ya wazee: na tunaweza kuichukua ili kuanzisha kazi muhimu ya kichungaji.
Papa kadhalika alisema kwamba leo hii, watu wengi, baada ya kuhitimisha miaka yao ya kazi, wana fursa ya kufurahia kipindi kirefu cha afya njema, ustawi wa kiuchumi na wakati zaidi wa bure. Wanaitwa “vijana wazee”: mara nyingi wao ndio wanaohudhuria Misa kwa bidii na kuongoza shughuli za parokia, kama vile katekesi na huduma mbalimbali za kichungaji. Ni muhimu kuwatafutia lugha na fursa zinazofaa, zikiwahusisha si kama wapokeaji wa uinjilishaji tu, bali kama somo tendaji, na kujibu pamoja nao, na si katika nafasi zao, kwa masuala ambayo maisha na Injili yanatuletea. Kuna hali mbalimbali zinazoweza kutokea: baadhi ya watu hupokea tangazo lao la kwanza la imani katika uzee; wengine wamempitia Mungu na Kanisa katika ujana wao lakini baadaye wamekengeuka; bado wengine wamedumu katika maisha ya Kikristo. Kwa wote hao, huduma ya kichungaji kwa wazee inapaswa kuwa ni uinjilishaji na umisionari, kwani Kanisa daima linaitwa kumtangaza Yesu Kristo Mwokozi kwa kila mwanamume na mwanamke, katika kila umri na hatua ya maisha.
Papa alitoa ushauri kuwa, mahali ambapo wazee na babu wako peke yao na wametupwa, hilo litamaanisha kuwapelekea habari njema ya upole wa Bwana, kushinda, pamoja nao, giza la upweke, adui mkuu wa maisha ya wazee na mababu. Mtu yeyote asiachwe! Mtu asijisikie hana maana! Hata sala rahisi, iliyosaliwa kwa imani nyumbani, inachangia wema wa Watu wa Mungu na inatuunganisha katika ushirika wa kiroho. Kazi hii ya umisionari inatupatia changamoto sisi sote, parokia zetu na, kwa namna fulani, vijana, ambao wanaweza kuwa mashuhuda wa ukaribu na kusikilizana kwa wale ambao wanaendelea zaidi katika maisha yao. Katika hali nyingine, uinjilishaji wa kimisionari utawasaidia wazee kukutana na Bwana na neno lake. Pamoja na uzee, watu wengi huanza kutilia shaka maana ya kuwepo, wakitengeneza fursa ya kutafuta uhusiano wa kweli na Mungu na kuimarisha wito wao wa utakatifu.
Kwa kuhitimisha Papa Leo aliomba kukumbuka daima kwamba kutangaza Injili ndiyo kazi kuu ya huduma yetu ya kichungaji: kwa kuwashirikisha wazee katika mienendo hii ya kimisionari, wao pia watakuwa mashuhuda wa matumaini, hasa kwa hekima, ibada na mang’amuzi. Hakika, Papa anaomba hilo, na juu yao kwa maombezi ya uzazi ya Bikira Maria, na anawasndikiza kwa baraka yake.
Asante sana kusoma makala hii, ikiwa unakata kubaki na masasisho zaidi, tunakualika kujiandikisha hapa: Just click here
