Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 75 ya Jimbo Kuu la Cape Coast!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Neno la Mungu linasema: “Bwana, kazi zako zote zitakushukuru, na wacha Mungu wako watakuhimidi. Wataunena utukufu wa ufalme wako, na kuuhadithia uweza wako. Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu, na utukufu wa fahari ya ufalme wake. Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote, na mamlaka yako ni ya vizazi vyote.” Zab 145:10-11. Jimbo kuu Katoliki la Cape Coast, nchini Ghana, lilianzishwa kunako mwaka 1879 na hatimaye, kutangazwa kuwa ni Jimbo kuu kunako mwaka 1950 na kwa sasa linaongozwa na Askofu mkuu Charles Gabriel Palmer-Buckle. Jimbo hili katika maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 75 tangu liundwe kuwa ni Jimbo kuu na Papa Pio XII. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 75 tangu kuundwa kwake, Baba Mtakatifu Leo XIV amemteuwa Kardinali Wilfrid Fox Napier, O.F.M., Askofu mkuu Mstaafu wa Jimbo kuu la Durban, Afrika ya Kusini kuwa Mwakilishi wake, katika kilele cha Jubilei hii kinachoadhimishwa tarehe 25 Oktoba 2025.
Kardinali Wilfrid Fox Napier, O.F.M., anaongoza ujumbe wa Mapadre wawili. Katika orodha hii yamo Majimbo ya Accra, Keta, Kumasi na Tamale ambayo kwa pamoja yanammwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa furaha na shukrani kwa kazi kubwa ya uinjilishaji wa kina iliyofanyika katika maeneo haya Barani Afrika. Hii ni kazi ya kuchosha, lakini imekuwa ni kielelezo cha ushujaa wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, utume ambao umetekelezwa kwa ari na moyo mkuu, sanjari na kuendeleza mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi unaofumbatwa katika majadiliano ya kidini na kiuekumene; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mfao ya wengi. Ombi la kuwa na mgeni rasmi liliungwa mkono na Askofu mkuu Mathayo Kwasi Gyamfi ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana pamoja na Majimbo yanayo sherehekea Kumbukizi ya Miaka 75 tangu kuanzishwa kwayo.
Kardinali Wilfrid Fox Napier, O.F.M., ni mchungaji mwenye bidii, uchaji wa Mungu na mwenye mafundisho ya kina, ndiye aliyeteuliwa kumwakislisha Baba Mtakatifu Leo XIV katika ibada takatifu inayo adhimishwa Jumamosi tarehe 25 Oktoba 2023 katika Jimbo Kuu la Gold Coast. Washiriki wote wa tukio hili wanatiwa moyo kuonesha upendo wa pekee kwa Kristo Yesu na Injili yake na kuwa na bidii kwa ajili ya imani katika maisha yao ya kila siku, kwa nguvu na bidii inayopyaishwa katika: Sala, tafakari, na kwa kuzingatia pia mahitaji msingi ya shughuli za kichungaji. Baba Mtakatifu Leo XIV anamtaka Kardinali Napier kuwafikishia salam na matashi mema, watu wa Mungu kutoka Ghana watakao shiriki katika tukio hili na kwamba, anamsindikiza kwa sala zake na kwa maombezi ya Bikira Maria na ya Mtakatifu Yosefu anampatia baraka zake za kitume, Ishara ya ukarimu wake kwake, na kama kielelezo cha zawadi za mbinguni, anazo tamani kuwashirikisha kikamilifu watu wa Mungu kutoka ndani na nje ya Ghana, wanaoshiriki kikamilifu Jubilei Miaka 75 tangu kuundwa kwa majimbo haya.
