Tafuta

Mkesha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Tasaufi ya Bikira Maria, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican tarehe 11 Oktoba 2025. Mkesha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Tasaufi ya Bikira Maria, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican tarehe 11 Oktoba 2025.  (@Vatican Media)

Maadhimisho ya Jubilei ya Tasaufi ya Bikira Maria 2025

Jubilei ya Tasaufi ya Bikira Maria: Ibada ya Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi; .Sanamu ya Bikira wa Fatima, imepamba Ibada na fursa ya kuombea amani sehemu mbalimbali za dunia, kwa kuongozwa na Baba Mtakatifu Leo XIV, ambaye pia ameongoza Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na kumbukizi ya miaka 63 tangu Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipozindua Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani “Mahujaji wa matumaini” ni kwa ajili ya kutafakari kuhusu: Imani, matumaini, mapendo, huruma ya Mungu, na wongofu wa ndani. Katika kipindi hiki, waamini wanahimizwa kusoma na kutafakari Neno la Mungu, kufanya matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja, na kupitia "Lango la Imani" ambalo linatambulisha upendo na msamaha kutoka kwa Kristo Yesu. Maadhimisho haya yanafanyika kote duniani, yakilenga kuwapatia matumaini wale wanaosumbuka, waliovunjika na kupondeka moyo, ili kujenga tena: umoja, haki na amani. Jubilei ya Tasaufi ya Bikira Maria, imeadhimishwa kuanzia Jumamosi tarehe 11 Oktoba na kuhitimishwa Dominika tarehe 12 Oktoba 2025 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Jubilei hii imezinduliwa kwa Ibada ya Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi; maisha na utume wa Kristo Yesu. Bikira Maria alipowatokea Watoto watatu wa Fatima yaani Francis, Yacinta na Lucia aliwaagiza kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya toba, wongofu wa ndani na amani duniani. Ibada hii imehudhuria na wajumbe kutoka katika nchi 100, wengi wao wakiwa ni wale wanaotoka Italia, Poland, Ufaransa, Marekani na Canada. Sanamu ya Bikira wa Fatima, imepamba Ibada ya Jubilei ya Mahujaji wa Tasaufi ya Bikira Maria. Sanamu hii imepitishwa kwenye njia ile ya jaribio la kutaka kumuua Mtakatifu Yohane Paulo ll. Hii imekuwa ni fursa ya kuombea amani sehemu mbalimbali za dunia, kwa kuongozwa na Baba Mtakatifu Leo XIV, ambaye pia ameongoza Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, kwa ajili ya kuombea amani. Itakumbukwa kwamba, hii pia ilikuwa ni sehemu ya kumbukizi ya miaka 63 tangu Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipozindua Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, hapo tarehe 11Oktoba 1962 sanjari na kumbukumbu ya Mtakatifu Yohane XXIII.

Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na Kuombea Amani Duniani
Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na Kuombea Amani Duniani   (@Vatican Media)

Madhabahu ni mahali muafaka pa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni mahali pa toba na wongofu wa ndani, unaomwezesha mwamini kuchuchumilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha, kama chachu ya utimilifu na utakatifu wa maisha. Hapa ni mahali pa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani kwa kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu kama alivyofanya Baba mwenye huruma kwa Mwana mpotevu! Waamini wanakumbushwa kwamba, wao ni sehemu ya familia kubwa ya watu wa Mungu, daima wako chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Wakristo ni sehemu ya viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kumbe, kama sehemu ya Kanisa wanao wajibu na dhamana ya kuliombea Kanisa zima; kuwaombea watu wanaoteseka kutokana na sababu mbalimbali; watu wanaoogelea katika dimbwi la huzuni na machungu ya maisha; wagonjwa na wale wote walioko kufani; wakimbizi na wahamiaji bila kuwasahau watu wanaoteseka kutokana na athari za majanga asilia.  Haya ni maeneo yanayodhihirisha ufunuo wa: Upendo, ukuu, wema na huruma ya Mungu kwa waja wake. Ibada kwa Bikira Maria inapata chimbuko lake chini ya Msalaba wa Kristo Yesu. Bikira Maria ni daraja inayowawezesha waamini kumwendea Kristo Yesu kwa imani, matumaini na mapendo kamili. Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba Mwenyezi Mungu anapewa nafasi ya kwanza katika maisha ya waamini kwa kushika kikamilifu Amri Kumi za Mungu, dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu.  Ni changamoto ya kutangaza na kushuhudia upyaisho wa maisha ya Kikristo, ili kujenga na kudumisha: ukarimu, umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, daima wakijielekeza kuangalia leo na kesho ya binadamu. Wakristo waoneshe uaminifu kwa dhamana na maisha yao ya Kikristo. Waamini wasisite kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, kwani Kristo Yesu akiwa Msalabani aliwakabidhi wafuasi wake wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Kristo Yesu akiwa juu Msalabani alimkabidhi Bikira Maria kwa Mtakatifu Yohane na hivyo Bikira Maria akawa Mama wa maisha ya kiroho, tayari kuwaombea msaada wale wote wanaokimbilia ulinzi na tunza yake.

Jaribio la kutaka kumuua Yohane Paulo II, 1981
Jaribio la kutaka kumuua Yohane Paulo II, 1981   (ANSA)

Zawadi kubwa ambazo Kristo Yesu ameliachia Kanisa lake ni Bikira Maria kama Mama wa Kanisa na Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Bikira Maria anachukua nafasi ya pekee katika Fumbo la Umwilisho linalopata hitimisho lake katika Fumbo la Pasaka. Bikira Maria ni shule maalum ya kuweza kumjifunza Kristo Yesu na njia inayowapeleka waamini kwa Kristo Yesu. Waamini wajenge na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, huku wakimtukuza Kristo Yesu, Mwana wa Baba wa milele, daima wakijitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Kwa njia ya Kristo Yesu na kwa maombezi ya Bikira Maria, waamini wajitahidi kuwa ni mashuhuda waaminifu wa tunu msingi za Kikristo katika maisha yao ya kila siku. Bikira Maria ni shule ya imani kwa Mwenyezi Mungu; upendo kwa Mungu na jirani. Kristo Yesu ni mwingi wa huruma na mapendo, kwa wale waamini wanaokimbilia chini ya mbawa zake kama alivyofanya kwa Mtakatifu Petro alipomkana mara tatu na alipokutana mubashara na Mtakatifu Paulo Mtume akiwa njiani kuelekea Dameski. Ni furaha kwa Bikira Maria kuwaona watoto wake wakikimbilia kwenye Mahakama ya huruma ya Mungu ili kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuambata utakatifu wa maisha. Bikira Maria, Mama wa huruma, awaombee mwanga angavu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili kuweza kubadili yale ambayo yamo katika uwezo wao. Wawe na moyo wa utulivu, kupokea yale wasiyoweza kubadili. Awakirimie hekima na busara ya kuweza kung’amua mema yakufuata katika maisha!

Kumbukizi la Miaka 63 tangu kuzinduliwa kwa Mtaguso Mkuu II Vatican
Kumbukizi la Miaka 63 tangu kuzinduliwa kwa Mtaguso Mkuu II Vatican   (@Vatican Media)

Hayati Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema kwamba, Kanisa katika ulimwengu mamboleo ni Kanisa la mashuhuda ambalo linaendelea kujengwa kutokana na damu ya watoto wake inayomwagika sehemu mbalimbali za dunia. Kuna watu wanauwawa, wanayanyaswa na kudhulumiwa kutokana na chuki za kidini na kiimani. Huu ndio ukweli uliokuwa umefumbatwa katika ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima, yaani Francis, Lucia na Yacinta. Ni Siri inayogusa matukio ya kihistoria, maisha na utume wa Kanisa. Hata leo hii, Kanisa linaendelea kujaribiwa, kwa baadhi ya watu kutaka kujenga hisia za chuki na uhasama dhidi ya Kanisa pamoja na kupandikiza mbegu ya kifo. Bikira Maria alipowatokea watoto wa Fatima, aliwapatia Siri kuu tatu ambazo zote zimekwisha fafanuliwa na viongozi wa Kanisa kwa wakati wake. Ni siri ambazo zimejikita katika mwono wa vita, majanga, kinzani na migawanyiko kati ya watu. Siri zote hizi ziliandikwa na Sr. Lucia. Siri ya tatu hakikuweza kufunuliwa kutokana na amri iliyotolewa na Askofu mahalia. Mtakatifu Yohane Paulo II baada ya jaribio la kutaka kumuua kushindikana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, Mjini Vatican hapo tarehe 13 Mei 1981 aliamuru kwamba, siri ya tatu ifunuliwe na kuwekwa hadharani. Tafsiri ya siri hii ilitolewa na Kardinali Joseph Ratzinger, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la mafundisho tanzu ya Kanisa, na alisema kwamba, siri ya tatu ya Fatima ilikuwa ni mwaliko kwa Wakristo kusoma alama za nyakati na kutoa majibu muafaka kwa njia ya ushuhuda wa imani. Mtakatifu Yohane Paulo II anakiri kwamba, ni mkono na kinga ya Bikira Maria iliyomwezesha kusalimika katika jaribio la kutaka kumuua hapo tarehe 13 Mei 1981. Sala ni nguzo muhimu sana katika maisha dhidi ya wasi wasi wa kifo anasema Mtakatifu Yohane Paulo II. Huu ni ufafanuzi ambao ulitolewa na Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu wakati alipokuwa anatoa mhadhara kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha Antonianum kuhusu: Ujumbe wa Fatima kati ya Karama na Unabii.

Jubilei Tasaufi B. Maria Ok

 

12 Oktoba 2025, 14:15