Mama Vincenza Poloni alipenda Kristo katika Watu wa Kawaida
Na Sr. Christine Masivo, CPS – Vatican.
Wakristo kutoka pembe tofauti za Ulimwengu walikusanyika mjini Vatican ili kushuhudia sherehe kuu ya Kutangazwa kwa Watakatifu saba katika Kanisa katoliki, Dominika tarehe 19 Oktoba 2025, sambamba na Dominika ya 99 ya Kimisionari Ulimwenguni. Misa hiyo iliongozwa na Baba Mtakatifu Leo XIV kwa ushiriki wa Makardinali, Maaskofu wakuu, Maaskofu, Mapadre, Watawa, Mamlaka za Kiraia na waamini wengine wengi. Miongoni mwa Watakatifu hao alikuwa ni Mtawa mmoja ambaye ndiye Mwanzilishi wa Shirika la Kimisionari la (Misericordia)- Huruma Sr Vincenza Maria Poloni.
Katika fursa hiyo, Masista kutoka Verona na kwingineko duniani mahali walipo walishiriki Misa Takatifu. Baadhi ya watawa hawa wa Shirika hilo hawakuficha hisia yao ya furaha walipopata fursa ya kushuhudia tukio hili Takatifu wakizungumza na vyombo vya habari. Katika mahojiano na Radio Vatican, masista wa Shirika hilo kutoka Tanzania walizungumzia kwa kina kuhusu mama yao, mwanzilishi wa Shirika ambaye kwa sasa ni Mtakatifu wakisema kwamba alikuwa Mama wa wote.
Ushuhuda
Mtawa mmoja, Sr Christina alisema, “nimefurai sana, basi na shirika zima tunafuraha kubwa mno kwa kushiriki adhimisho kubwa la kumtangaza mwenye heri wetu mtawa Vicenza Maria Poloni kuwa mtakatifu. Ni mama ambaye aliishi maisha ya kawaida. Alitoa huduma kwa wagonjwa, kuwasaidia maskini wenye mahitaji mbalimbali. “Aliishi maisha ya kawaida, kama mwanadamu wa kawaida. Tunajisikia fahari sana kwa kuwa na Mtakatifu katika shirika letu. Anatukimbusha kwamba tunawajibu wa kuishi fadhila zake, basi kuziishi zaidi na zaidi. Anatufunza na sisi basi kuishi utakatifu, sio kutafuta mambo ya hali ya juu. Utakatifu ni kuishi katika mambo madogo madogo ya kila siku. Kumpenda huyu Kristo katika watu wa kawaida,” alisisitiza Sr. Christina.
Sr Hongera Adam Manga yeye alionesha furaha yake na kusema, “Ninamshukuru Mungu kwa zawadi ya mama yetu, Sr Vicenza Maria Poloni alitangazwa kuwa Mtakatifu, tulisubiri kwa hamu kwa muda mrefu. Sisi kama wanashirika, mama yetu aliishi kama sisi, kama sista wamisericordia lakini alijitaidi kuishi wito wake kwa kumtumikia Mungu kwa njia ya maskini. Tunamwita shujaa wa upendo kwa sababu alifanya mambo madogo ambayo kwa kibinadamu yanaonekana ni mambo yasiyo eleweka au ya kipuuzi. Lakini yeye aliyafanya kwa imani kubwa na upendo mkubwa. Na sisi anatufundisha tuweze kufanya kama vile. Aliwaita maskini ni mabwana zetu, na sisi katika maskini wa nyakati zetu, tunawaita maskini ndiyo mabwana zetu ambao kupitia kwao wanatusaidia, tuweze kumfikia Mungu.” alisistiza Sr. Hongera.
Ni furaha kubwa kwa sababu ni tukio ambalo limeingia kwenye historia yetu kama wanashirika na hata pia Kanisa kwa ujumla, tumeweza kushuhudia sisi wenyewe kwa macho yetu, tunandelea kumuomba Mama yetu aendelee kutuombea huko aliko. Na sisi tuendelea kwa kwa kuishi hii karama ya huruma ya Mungu kila siku katika maisha yetu. Mama Sr Vincenza Maria Poloni alisukumwa na upendo mkuu kwa Mungu baada ya kuona mahitaji ya watu ambao wanahangaikia kwa sababu alitoka kwenye familia iliyokuwa na Imani. Ni kutoka kwenye familia yake alijifunza kuwahudumia watu wa tabaka la chini. Alijitolea kuwasaidia watu waliokuwa wanateseka hasa pia kwenye vitu vya wazazi hata kabla ya kuanzisha Shirika la Masisitiza wa huruma wa Verona, na aliwahudumia wote.
Baadaaye kusindikizwa na kiongozi wake wa kiroho Padre Carlo Steeb alimuomba ili waweze kuanzisha Shirika la Masista wa Huruma. Kwa sababu alijiona yeye ni kiumbe dhaifu lakini Bwana kwa wakati mwingine hukitumia kiumbe dhaifu ilikuifanya kazi yake. Na basi baadaye alikubali na kuanzisha shirika letu hili lama sista Misericordia,” alisisitiza Sr. Hongera. “Ndio maana sisi pia bado tupo hadi wakati huu tunaendelea kumtumikia Mungu kwa njia maskini na wale watu wanaohitaji msaada wetu.” Sr Julia Pia Zakaria Joseph Kusena alisema kuwa: “mimi binafsi nina furaha kubwa sana hasa kama mwana Shirika, kwa mama yetu Sr Vincenza Maria Poloni Kutangazwa pamoja na Watakatifu wengine kuwa Mtakatifu. Ni mama aliyeishi maisha yake ya kawaida na kama wanashirika, tunapaswa kuiga mfano wake hasa kuishi upendo kati yetu, na kuwahudumia wale wote wanaohitaji msaada katika maisha ya kawaida.
“Nimeguswa katika maisha yangu kwa ujumla sana na sherehe ya mama Vincenza Maria Poloni kutangazwa kwa Mtakatifu. Nijisikia mwenye furaha na raha ya kuwa kwenye kikundi hiki na nashukuru sana vile masista wanavyotembea na sisi katika malezi yao. Mama Vincenza ametenda mambo mengi katika maisha yangu, amekuwa faraja na kimbiliola langu wakati wa sala. Namshukuru Mungu sana, ninaendelea kuiombea Shirika na ninawaombea watawa wawe wengi na pia walei wajitokeze kwa wingi ilituweze kumuenzi mama yetu vizuri, na nimefuatana na masista wangu,” alisema hayo Esther Madah, Mlei wa Chama cha Shirika la Masista wa Huruma kutoka Dodoma, nchini Tanzania.
