Papa,Katekesi:Nicholas alijua hakujua&hivyo alizidi kuelewa ukweli.Ni zawadi kubwa kwa Kanisa!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV aliendelea na Katekesi yake ya Jubilei ya Matumaini, kwa mahujaji na waamini waliofika kutoka Ulimwenguni kote katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, mara baada ya kuzungukia Uwanja huo, akiwa katika kigari chake akiwabariki watoto na waamini. Mada ya 7 ya Katekesi hii, Jumamosi tarehe 25 Oktoba 2025 ilikuwa ni “Sperare è non sapere,” yaani “kutumaini pia ni kutojua – Nicola Cusanus,” ambapo lilisomwa Somo kutoka Rm 8,24-25: “Kwa maana kwa tumaini tuliokolewa. Sasa tumaini la kile kinachoonekana si tumaini; kwa maana ni nani anayetumainia kile anachokiona? Lakini tukitumainia kile ambacho hatukioni, tunakingojea kwa uvumilivu.”
Papa alianza kusema kuwa “Kaka na dada wapendwa, habari za asubuhi na karibu! Mmefikia lengo la hija yenu, lakini, kama wanafunzi wa Yesu, sasa lazima tujifunze kuishi katika ulimwengu mpya. Jubilei imetufanya kuwa mahujaji wa matumaini kwa sababu hii hasa: kila kitu lazima sasa kionekane katika nuru ya ufufuko wa Aliyesulubiwa. Ni katika tumaini hili ndipo tunaokolewa! Hata hivyo, macho yetu hayajazoea. Hivyo, kabla ya kupaa mbinguni, Aliyefufuka alianza kutuelimisha mtazamo wetu wa macho. Na anaendelea kufanya hivyo leo hii! Hakika, mambo si kama yanavyoonekana: upendo umeshinda, ingawa mbele ya macho yetu tuna migogoro mingi na tunaona mgongano wa wapinzani wengi. Katika enzi yenye matatizo sawa na haya, katika karne ya 15, Kanisa lilikuwa na Kardinali ambaye bado hajulikani sana leo.
Alikuwa mtafakuri mkubwa na mtumishi wa umoja. Jina lake lilikuwa Nicholas. Alitoka Kues, nchini Ujerumani: Nicholas Cusanus, ambaye anaweza kutufundisha kwamba kutumaini pia ni "kutojua." Kama Mtakatifu Paulo anavyoandika, "mtu anawezaje kutumaini kile ambacho tayari anakiona?" (Rm 8:24). Nicholas Cusanus hakuweza kuvumilia kuona umoja wa Kanisa, ukitikiswa na mikondo inayopingana na kugawanywa kati ya Mashariki na Magharibi. Hakuweza kuvumilia kuona amani duniani na miongoni mwa dini, katika enzi ambapo Ukristo ulihisi kutishiwa kutoka nje. Hata hivyo, alipokuwa akisafiri kama mwanadiplomasia wa Papa, aliomba na kufikiria. Hii ndiyo sababu maandishi yake yamejaa nuru.
Papa Leo aliendelea kudadavua kuwa “Wengi wa watu wa wakati wake waliishi kwa hofu; wengine walijihami, wakiandaa njia za vita vipya. Hata hivyo, Nicholas, alichagua tangu akiwa na umri mdogo kushirikiana na wale waliokuwa na tumaini, wale waliozama katika taaluma mpya, wale waliosoma tena vitabu vya kale na kurudi kwenye vyanzo. Aliamini katika ubinadamu. Alielewa kwamba kinyume chake lazima kishikamane pamoja, kwamba Mungu ni fumbo ambalo, kile kilicho katika mvutano hupata umoja. Nicholas alijua hakujua, na kwa hivyo alizidi kuelewa ukweli. Ni zawadi kubwa kwa Kanisa! Ni wito gani wa kupyaishwa kwa moyo! Haya ndiyo mafundisho yake: tengeneza nafasi, shikamaneni pamoja, na tumaini kwa kile ambacho hakijaonekana bado.
Cusanus alizungumzia juu "msomi ujinga," ishara ya akili. Mhusika mkuu wa baadhi ya maandishi yake ni mhusika mdadisi: mjinga. Ni mtu rahisi, asiye na elimu, na anauliza maswali ya msingi kwa wasomi, ambayo yanapinga uhakika wao. Ni vivyo hivyo katika Kanisa la leo. Maswali mangapi yanapinga mafundisho yetu! Maswali kutoka kwa vijana, maswali kutoka kwa maskini, maswali kutoka kwa wanawake, maswali kutoka kwa wale walionyamazishwa au kulaaniwa kwa sababu wanatofautiana na walio wengi. Tunaishi katika wakati uliobarikiwa: maswali mangapi! Kanisa linakuwa mtaalamu wa ubinadamu ikiwa linatembea na ubinadamu na kurudisha maswali yake moyoni mwake.
Baba Mtakatifu alisisitiza kwamba, “kutumaini si kujua.” Tayari hatuna majibu ya maswali yote. Lakini tunaye Yesu. Tumfuate Yesu. Na kwa hivyo tutumainie kile ambacho hatujaona bado. Tuwe watu ambao ni wapinzani wameunganishwa katika umoja. Tunaingia kama wachunguzi katika ulimwengu mpya wa Mfufuka. Yesu anatutangulia. Tunajifunza, tukisonga hatua moja baada ya nyingine. Ni safari, lakini si ya Kanisa tu, bali ya wanadamu wote. Safari ya matumaini,” Papa alihitimisha.
Baada ya Katekesi
Baba Mtatifu Leo XIV mara baada ya katekesi yake alitoa salamu mbali mbali na kwa hiyo alitoa salamu za dhati kwa waamini wanaozungumza Kifaransa, hasa waamini wa Majimbo ya Grenoble-Vienne na Mtakatifu Etienne, pamoja na mahujaji kutoka Uswiss, Ugiriki, Canada, na Madagascar. “Kwa kufuata mfano wa Maria, aliyelinda mambo yote, akiyatafakari moyoni mwake, tujifunze katika Mwezi huu wa Rozari kwamba tumaini la kweli ni lile ambalo halitafuti kujua au kuelewa kila kitu, bali hujiruhusu kuongozwa na imani.” Papa pia aliwasalimu kwa uchangamfu Wapoland.
“Siku hizi zinaadhimisha miaka mia moja ya Hati ya kihistoria ya Papa Pio XI, anbaye zamani alikuwa Balozi shujaa wa Kitume huko Warsaw na hati ambayo ililipanga upya utawala wa Kanisa huko Poland na, baada ya kipindi cha kusikitisha cha mgawanyiko na vita, ikaunda majimbo kadhaa mapya. Hazina ya imani, iliyolindwa kwa karne nyingi, iwaimarishe mapadre na waamini kwa matumaini ya kujitolea kwa bidii wa kitume. “Ninawabariki kwa moyo wote!”
Papa kadhalika alitoa salamu kwa mahujaji wote wanaozungumza Kireno, hasa wale kutoka Parokia ya Mkombozi Mtakatifu sana huko Luanda, nchini Angola. “Kaka na dada wapendwa, Yesu Kristo ndiye jibu la msingi kwa maswali ya ndani kabisa ya mioyo yetu. Hebu tujikabidhi Kwake kusafiri safari hii ya Jubilei pamoja kama wahamasishaji wa kweli wa amani, maelewano na umoja, kwa msaada wa Bikira Maria.”
Papa akizungumza kwa wanaozungumza Kijerumani, kama mahujaji wa matumaini aliwaeleza: “tumeitwa kuwa mashahidi wa Yesu Kristo aliyefufuka. Na atupe zawadi zilizoahidiwa za umoja na amani.”
Hatimaye aliwakaribisha waamini wa lugha ya kiitaliano hasa wale wanatoka majimbo ya Aversa, wakiwa na Askofu wao Angelo Spinillo; Pozzuoli na Ischia Askofu wao Carlo Villano; AndriaAskofu Mons. Luigi Mansi; Catanzaro-Squillace, na Askofu Mkuu Claudio Maniago; Rossano-Cariato, na Askofu Mkuu Maurizio Aloise. Ni matumaini yake kwamba kwa kuhamasishwa na bidii ya kitume na wataeneza ujumbe wa kiinjili kwa mfano wao wenyewe. Papa Leo aliwatia moyo kupata ndani ya sala, hasa katika maadhimisho ya Misa, nguvu ya kushiriki kikamilifu katika maisha ya jumuiya zao. Kisha aliwasalimu waamini wa Saluzzo na Novara, pamoja na Hospitali ya Yohane wa Mateso, Roma na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Campus ya amadawa, Roma: Ninawakumbusha kila mtu kwamba kila mfuasi wa Bwana ameitwa kuchukua jukumu lake katika kujenga Kanisa. Hatimaye, mawazo yake yaliwageukia vijana, wagonjwa, na wenye ndoa mpya: “uzoefu wa Jubilei ya leo uwe kichocheo chenye ufanisi cha upendo, haki, na amani, hivyo kuchangia katika upya katika Kristo wa kila nyanja ya maisha. Baraka yangu kwa wote!”
