Tafuta

Waandamanaji wa Madagascar warejea mitaani licha ya hatua ya kuvunja serikali. Waandamanaji wa Madagascar warejea mitaani licha ya hatua ya kuvunja serikali. 

Kuhuzunishwa kwa Papa Leo XIV kufuatia na mapigano nchini Madagascar:ghasia zote zisitishwe

Mwishoni mwa Katekesi katika Uwanja wa Mtakatifu Petro,Papa Leo XIV alizindua wito kwa Madagascar,ambayo imetikiswa kwa siku hizi na maandamano ya vijana kupinga hali mbaya ya kiuchumi na kijamii.Mapigano makali na Polisi yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 20 na mamia kujeruhiwa.Papa aliwaombea wahanga na kuomba mtangamano wa kijamii uimarishwe kwa kukuza haki na manufaa ya wote.

Na Angella Rwezaula - Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV, alielezea hisia zake za huzuni kutokana na habari za  Madagascar, kisiwa kikubwa cha  Afrika ya Mashariki iliyotikiswa kwa siku kadhaa na ghasia kufuatia maandamano yaliyoongozwa na makundi ya vijana kuhusu kukatwa kwa maji na umeme. Alionesha huzuni hiyo na kutoa wito wake mwishoni kwa Katekesi yake, Jumatano tarehe 1 Oktoba 2025 kwa waamini na mahujaji waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, mjini Vatican. kwa njia hiyo Papa alizungumzia   juu ya "mapigano makali kati ya watekelezaji sheria na waandamanaji ambayo yalisababisha vifo vya baadhi na karibu mia kujeruhiwa. Kulingana na takwimu za hivi punde zilizotolewa na Umoja wa Mataifa, watu 22 wamefariki na zaidi ya 100 wamejeruhiwa. Papa alisema kuwa "Tuombe kwa Mungu ili kila aina ya unyanyasaji iepukwe na kwamba ufuatiliaji wa mara kwa mara wa maelewano ya kijamii uimarishwe kupitia uendelezaji wa haki na manufaa ya wote."

Maandamano

Kwa kuchochewa na maandamano ya "Gen Z" ya  kizazi cha vijana nchini Kenya na Nepal, maandamano nchini Madagascar, ni miongoni mwa maandamano makubwa zaidi kuwahi kutokea nchini humo, yalitokana na msisimko wa kiuchumi na kijamii wa mamilioni ya watu wa Madagascar. Huduma duni za kimsingi, kuporomoka kwa miundombinu, kukatika kwa umeme mara kwa mara, na ufisadi katika serikali ya ngazi ya juu kuwa sehemu  ya  chanzo cha kutoridhika huku katika nchi. Vikundi vya vijana, kwa kutumia mitandao ya kijamii, kisha vilianzisha uhamasishaji ambao uliishia kwenye maandamano yaliyopelekea Rais Andry Rajoelina-ambaye aliingia madarakani kwa mara ya kwanza kupitia mapinduzi mwaka 2009-kuifuta serikali yake mnamo  Septemba 29.

Miji mingine pia iliyoathiriwa na maandamano hayo

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, waathirika hao ni pamoja na sio tu waandamanaji bali pia watu waliokuwa karibu waliouawa katika makabiliano na vikosi vya usalama, waliofyatua mabomu ya machozi, na wengine kuuawa katika ghasia zilizotekelezwa na magenge ya wahalifu baadaye. Wizara ya Mambo ya Nje ya Masakota ilikataa idadi hiyo ya vifo, ikiona kuwa ilitokana na "uvumi au habari potofu." Wakati huo huo, mwito mpya wa uhamasishaji wa kitaifa umezinduliwa  na kuwataka wafanyakazi wa umma kujiunga na mgomo mkuu. Maandamano mapya yaliitishwa katika kitongoji cha Ambohijatovo katika mji mkuu, Antananarivo, kitovu cha mfano cha maisha ya kisiasa ya Madagascar, ambapo waandamanaji waliingia Septemba 30. Maandamano hayo yalienea katika miji mingine, ikiwa ni pamoja na Diego Suarez, kaskazini mwa kisiwa hicho.

Salamu mbali mbali:Tusali Rozari kila siku kwa ajili ya amani

Papa aliendelea na salamu kwamba "Ninawasalimu kwa moyo mkunjufu watu wa Poland, hasa mahujaji kutoka Jimbo la Włocławek, pamoja na Askofu wa Jimbo hilo na Askofu Msaidizi Mstaafu. Ninawaalika kusali Rozari ya kila siku kwa ajili ya amani mwezi huu. Ulinzi wa Malaika Walinzi Watakatifu wawasindikize! Ninawabariki kwa moyo wote!"

Papa akiwageukia waamini wanaozungumza kwa lugha ya kiitaliano alisema "Ninawakaribisha kwa moyo mkunjufu mahujaji wanaozungumza Kiitaliano. Hasa, ninawasalimu Parokia za Maglie, Capodrise, Melito di Napoli, na Campocavallo di Osimo, pamoja na Askofu Mkuu Angelo Spina. Ninawakaribisha kwa upendo Chama cha Kitaifa cha Polisi cha Jimbo la Enna, Chama cha AICCOS cha Molfetta, na wanafunzi na walimu wa shule za Maestre Pie Filippini huko Aquila. Hatimaye, mawazo yangu yanageukia vijana, wagonjwa, na wenye ndoa wapya".

Kumbukizi ya Mtakatifu Teresa wa mtoto Yesu

 

Kwa kumbukizi ya Mtakatifu wa Siku alisema " Leo tunamkumbuka Mtakatifu Therese wa Mtoto Yesu, Mwalimu wa  Kanisa na Msimamizi wa utume wa Kimisionari. Mfano wake utie moyo kila mmoja kumfuata Yesu katika njia ya uzima, kwa kutoa ushuhuda wa Injili kwa furaha kila mahali."

Wito wa Papa kwa ajili ya Madagascar
01 Oktoba 2025, 12:40