Papa Leo XIV Hotuba Kwa Viongozi wa Italia Wakati wa Ziara Yake Ikulu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, akiwa ameambatana na Kardinali Pietro Parolin Katibu mkuu wa Vatican, Kardinali Matteo Maria Zuppi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI; Kardinali Baldassare Reina, Makamu Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma, pamoja na viongozi wengine wa ngazi ya juu kutoka Vatican, Jumanne tarehe 14 Oktoba 2025 wamekutana na kuzungumza na Rais Sergio Mattarella wa Italia pamoja na ujumbe wake. Baba Mtakatifu Leo XIV pamoja na ujumbe wake, walipofika mpakani mwa Italia na Vatican, walikaribishwa kwa msafara wa Farasi na Magari, nyimbo za nchi ya Vatican na Italia, zikaimbwa na hatimaye, Baba Mtakatifu Leo XIV akakagua gwaride lililoandaliwa kwa heshima yake. Rais Sergio Mattarella na Baba Mtakatifu wamepata nafasi ya kufanya mazungumzo ya faragha; wakabadilishana zawadi na kati ya zawadi hizi ni Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Leo XIV “Dilexi te” Yaani “Nimekupenda” Kuhusu Upendo kwa Maskini. Ufu 3:9 uliotiwa mkwaju, tarehe 4 Oktoba 2025 katika kumbukumbu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi.
Baba Mtakatifu Leo XIV amepata nafasi ya kusali kwa kitambo kidogo katika Kikanisa cha “Annunziata” yaani “Kikanisa cha Kupashwa Habari Bikira Maria kwamba atakuwa Mama wa Mungu.” Amepata nafasi ya kusalimiana na viongozi wakuu wa Serikali ya Italia na hatimaye, Rais Sergio Mattarella akatoa hotuba ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Leo XIV pamoja na ujumbe wake. Baba Mtakatifu katika hotuba yake ameishukuru Serikali ya Italia kwa kudumisha uhusiano mwema unaopata chimbuko lake katika historia ya Kanisa pamoja na viongozi wakuu wa Kanisa, ambao umewezesha ushirikiano mwema kati ya Italia na Vatican. Ameishukuru Italia kwa ushuhuda wake katika kuwapokea na kuwakirimia wageni na mahujaji katika maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini,” Mkataba wa Lateran maarufu kama “Patti Lateranensi” na kwamba, kipaumbele chake cha kwanza ni amani; tarehe 3 Oktoba 1226, Mtakatifu Francisko wa Assis aliaga dunia, Kanisa linajiandaa kuadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 800 tangu alipofariki; Umuhimu wa kusimama kidete kuenzi tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kwa kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; huduma kwa wakimbizi na wahamiaji; sanjari na umuhimu wa kulinda na kudumisha mapokeo.
Baba Mtakatifu katika hotuba yake ameishukuru Serikali ya Italia kwa kudumisha uhusiano mwema unaopata chimbuko lake katika historia ya Kanisa pamoja na viongozi wakuu wa Kanisa, ambao umewezesha ushirikiano mwema kati ya Italia na Vatican na hivyo kuyasimika mahusiano haya katika urafiki wa kweli na ushirikiano wa kidugu na hivyo kuendelea kujikita katika mapokeo ya kidini na kitamaduni yaliyoko nchini Italia: Makanisa, sanaa na utamaduni, Ibada mambo ambayo ni ushuhuda wa imani, kanuni maadili na utu wema. Ameishukuru Italia kwa ushuhuda wake katika kuwapokea na kuwakirimia wageni na mahujaji katika maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini,” ushirikiano na mshikamano huu unajidhihirisha mjini Roma na hata katika sehemu mbalimbali za dunia. Hayati Baba Mtakatifu Francisko alikuwa na upendo mkubwa kwa Italia na watu wake, hali ambayo ilichangia pia mafanikio makubwa kwa Kanisa kuweza kuchagua Khalifa mpya wa Mtakatifu Petro. Italia imeonesha ushuhuda mkubwa wa ukarimu kwa wageni na mahujaji waliofika mjini Roma kuhudhuria Maadhimisho ya Jubilei ya matumaini. Kumekuwepo na ulinzi wa kutosha, miundo mbinu na huduma za hali ya juu kabisa. Mama Kanisa anaendelea kuadhimisha Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo, kwa amani na utulivu, alama ya matumaini kwa waamini wote wanaofika mjini Roma kupitia katika Lango la huruma ya Mungu sanjari na kusali kwenye Makaburi ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume.
Itakumbukwa kwamba, Vatican ni kati ya nchi ndogo kabisa duniani, tarehe 11 Februari, 2025 imeadhimisha kumbukizi ya miaka 96 tangu Kanisa Katoliki lilipotiliana saini Mkataba na Serikali ya Italia “Inter Sanctam Sedem e Italiae Regnum Conventiones” kwa kifupi “Patti Lateranensi” yaani “Mkataba wa Lateran” unaoratibiwa na kusimamiwa na Sheria za Kimataifa na hivyo kuhitimisha kile kilichojulikana “Masuala ya Roma, Questione Roman.” Hii ni Italia iliyokuwa inaibuka baada ya kutenganisha shughuli za Kanisa na Serikali ya Italia. Mkataba huu ukapyaishwa kunako mwaka 1984. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kumekuwepo na ushirikiano mwema kati ya Vatican na Italia, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu; huduma kwa binadamu; kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu. Pamoja na mafanikio yote haya lakini bado kuna hali zinazoonesha shida, mateso na mahangaiko ya binadamu sehemu mbalimbali za dunia, mambo yanayohitaji sera na mbinu mkakati wa muda mfupi na muda mrefu.
Mtakatifu Yohane XXIII katika Wosia wake wa Kitume, “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” anasema, amani inasimikwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha utamaduni wa kuheshimu: utu, heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu sanjari na haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu anapaswa kuwajibika, ili kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii na mahusiano pamoja na Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, vita, maafa na majanga yanaendelea kusikika sehemu mbalimbali za dunia, changamoto na mwaliko wa kusikiliza na kujibu kilio cha wale wote wanaoteseka kutokana na madhara ya vita. Mtakatifu Yohane XXIII anasema: “kila mtu ni binadamu, yaani, nafsi iliyo na akili na utashi huru; na kila mtu ana haki na wajibu ambavyo vyote vinatokana moja kwa moja na asili yake hiyo.Kwa hiyo haki na wajibu hivyo ni vya watu wote, visivyovunjika na visivyobatilika.” Pacem in terris, 5.
Baba Mtakatifu Leo XIV anakazia misingi ya haki, usawa, ushirikiano na mshikamano kati ya watu wa Mataifa. Anaipongeza Serikali ya Italia kwa kuendelea kuwajibika katika mchakato wa kutafuta na kudumisha amani kwa kuwasaidia watoto walioathirika na vita Ukanda wa Gaza, huduma inayotolewa kwa ushirikiano na Hospitali ya Bambino Gesù inayosimamiwa na kuendeshwa na Vatican. Serikali ya Italia imechangia ujenzi wa amani na utulivu; maridhiano, ustawi na maendeleo ya familia kubwa ya binadamu. Lengo hili hakika linaendelezwa na dhamira ya pamoja kati ya Vatican na Italia kwa kukazia umoja, suluhu ya changamoto na kinzani zinazoendelea kujitokeza sanjari na kukuza maendeleo fungamani ya binadamu. Tarehe 3 Oktoba 1226, Mtakatifu Francisko wa Assis aliaga dunia, Kanisa linajiandaa kuadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 800 tangu alipofariki dunia. Huu ni muda muafaka wa kukazia utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa nchini Italia ni janga la kitaifa na kimataifa linalosigana na mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Sera zinazopania kukuza na kudumisha tunu msingi za familia ni sehemu ya mchakato wa uwekezaji. Leo hii vijana wengi nchini Italia hawana mpango wa kupata watoto na wale waliotia nia hii, inaonekana kana kwamba, ni jambo linaloleta karaha kwenye familia na wala si jambo la kujivunia na watoto si tena amana na utajiri wa familia kama ilivyokuwa hapo awali.
Ikumbukwe kwamba, watoto ni amana na utajiri wa jamii husika kwani hawa ndio watakaoendeleza uchumi wa kijani na maendeleo fungamani ya binadamu na wala hakuna mageuzi katika sekta mbalimbali za maisha bila ya uwepo wa vijana wa kizazi kipya. Italia inakabiliwa na idadi kubwa ya wafanyakazi wanaokula pensheni, ikilinganishwa na vijana wanaozalisha na kutoa huduma. Watoto ni matumaini ya jamii kwa leo na kesho iliyo bora zaidi, kumbe, inalipa kuwekeza kwa watoto. Umefika wakati kwa Italia kuwekeza katika sera bora za familia, ili kupata watoto zaidi. Jambo la msingi kwa wakati huu ni kufanya mabadiliko makubwa katika: miundombinu ya familia, kwa kuwekeza katika uzazi na kupandikiza mbegu ya matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kuna haja ya kusimama kidete kulinda, kudumisha na kuendeleza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa kukazia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, tangu mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi kifo kinapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Kumbe, kuna haja ya kuboresha huduma ya afya kwa mahitaji ya kila umri.
Italia imekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji, Baba Mtakatifu Leo XIV anaitaka Italia kuendelea kufungua malango yake kwa upendo na ukarimu na mshikamano kwa wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaoteseka kutokana na biashara haramu ya binadamu pamoja na viungo vyake. Hii ni changamoto ya kuendeleza mchakato wa mwingiliano huu, unaowatajirisha watu wa Mungu nchini Italia, wakimbizi na wahamiaji. Sera ya Kanisa Katoliki kwa wakimbizi na wahamiaji inatokana na misingi minne mikuu: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha. Mbinu hizi zinahusu kutoa hifadhi, kuhakikisha usalama, kukuza maendeleo yao na kuwaunganisha katika jamii inayowapatia hifadhi, bila ya kuogopa wala kuwa na maamuzi mbele. Baba Mtakatifu anaitaka Italia kukuza na kudumisha kumbukumbu hai ya wale waliowatangulia, ili kuangalia yaliyopo na yale yajayo kwa kuwa na ufahamu, utulivu, uwajibikaji na maendeleo. Baba Mtakatifu Leo XIV amehitimisha hotuba yake, kwa kuwatakia watu wa Mungu nchini Italia: Ustawi, maendeleo na mafanikio katika maisha. Italia ni nchi yenye utajiri mkubwa unaofumbatwa katika unyenyekevu; unaohitaji wakati mwingine kugunduliwa tena na tena. Haya ni matukio mazuri na himizo kwa Waitalia wote kuanza kupata matumaini kutoka kwayo na hivyo kukabiliana na changamoto mamboleo na zile zijazo kwa ujasiri.
