Tafuta

Maadhimisho ya Jubilei ya Tasaufi ya Bikira Maria inayorutubisha imani, matumaini na mapendo kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Maadhimisho ya Jubilei ya Tasaufi ya Bikira Maria inayorutubisha imani, matumaini na mapendo kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV: Jubilei ya Tasaufi ya Bikira Maria Inarutubisha Imani Kwa Kristo Yesu

Papa Leo XIV: Tasaufi ya B. Maria inarutubisha imani kwa Fumbo la Pasaka; Neno la Mungu ni hai, tena lina nguvu, na lina ukali kuliko upanga! Tasaufi hii ni kwa ajili ya huduma ya Injili, amana na utajiri unaobubujika kutoka katika furaha ya utenzi wa Magnificat; ni tasaufi inayofuata nyayo za Yesu; Ulimwengu una kiu ya haki na amani na Yesu ni kiini cha wokovu wa watu wote. Jubilei ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, upyaisho wa maisha ya kiroho sanjari na ukombozi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jubilei ya Tasaufi ya Bikira Maria, inayorutubisha imani ya waamini inatoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu imezinduliwa Jumamosi tarehe 11 Oktoba 2025 kwa Ibada ya Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi; maisha na utume wa Kristo Yesu. Hii imekuwa ni fursa ya kuombea amani sehemu mbalimbali za dunia, kwa kuongozwa na Baba Mtakatifu Leo XIV, ambaye pia ameongoza Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, kwa ajili ya kuombea amani duniani. Itakumbukwa kwamba, hii pia ilikuwa ni sehemu ya kumbukizi ya miaka 63 tangu Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipozindua Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, hapo tarehe 11Oktoba 1962 sanjari na kumbukumbu ya Mtakatifu Yohane XXIII, Muasisi wa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Baba Mtakatifu Leo XIV, Dominika tarehe 12 Oktoba 2025 katika mahubiri yake kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amekazia kwamba, Tasaufi ya Bikira Maria inarutubisha imani ya Wakristo kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; Neno la Mungu ni hai, tena lina nguvu, na lina ukali kuliko upanga! Tasaufi ya Bikira Maria ni kwa ajili ya huduma ya Injili, amana na utajiri unaobubujika kutoka katika furaha ya utenzi wa Magnificat; ni tasaufi inayofuata nyayo za Yesu; Ulimwengu una kiu ya haki na amani na kwamba, Yesu ni kiini cha wokovu wa watu wote. Jubilei ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, upyaisho wa maisha ya kiroho sanjari na ukombozi.

Tasaufi ya Bikira Maria inarutubisha imani ya Fumbo la Pasaka
Tasaufi ya Bikira Maria inarutubisha imani ya Fumbo la Pasaka   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Tasaufi ya Bikira Maria inarutubisha imani ya Wakristo kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu, Historia ya Jina lake Takatifu na Msalaba wake Mtakatifu na kwamba, Kristo Yesu ni mwaminifu kwa Baba yake wa milele; kwa hakika Mungu ni mwaminifu. Kumbe, maadhimisho ya Siku ya Bwana, Dominika, iwasaidie waamini kujisikia na kufikiri, ili hatimaye, kuboresha maisha yao ya pamoja hapa duniani. Kila tasaufi ya Kikristo inajikita katika moto huu unaoipyaisha na kuwa hai zaidi. Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa inaonesha: Upendo, wema na huruma ya Mungu iliyomwokoa, ikamponya na kumtakasa Naamani, Jemedari wa jeshi la Mfalme wa Shamu ingawa Israeli ilikuwa na wakoma wengi. Wakati wa Kristo Yesu, tukio hili liliwajaza ghadhabu wote waliokuwa kwenye Sinagogi, wakamkamata na kumtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake, wapate kumtupa chini. Mwinjili Luka, ataji uwepo wa Bikira Maria katika tukio hili, ili utimie ule utabiri wa Mzee Simeoni: “Nawe mwenyewe upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi.” Ll 2: 34-35.

Tasaufi ya Bikira Maria inatoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu
Tasaufi ya Bikira Maria inatoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu   (@Vatican Media)

Naamani, Jemedari wa jeshi la Mfalme wa Shamu licha ya umaarufu wake, anasema Hayati Baba Mtakatifu Francisko, alikuwa ni dhaifu na mgonjwa, aliyejifungia katika undani wake, akatengwa kutokana na ugonjwa wa ukoma. Kristo Yesu katika Injili anawakirimia wakoma zawadi ya uponywaji na utakaso, wala hawalazimishi wakoma kutambua uweza na nguvu zake za kuokoa, lakini Msamaria anatambua mwilini mwake, kwamba ameponywa na kutakasika, na kwamba, alionja zawadi ya upendo wa Mungu. Kwa hakika Tasaufi ya Bikira Maria ni kwa ajili ya huduma ya Injili na kwamba, upendo kwa Bikira Maria, unawakirimia waamini fursa ya kuwa ni wafuasi wa Kristo Yesu, anawafundisha kumrudia, kumtafakari ili hatimaye kuweza kuunganisha matukio mbalimbali ya maisha na Kristo Mfufuka anayewatembelea na kuwaalika waja wake, wakite maisha yao katika Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho yake makuu, kielelezo cha nguvu na huruma yake isiyokuwa na kifani. Wakoma kumi waliponywa bila kushirikishwa, changamoto na mwaliko kwa waamini kumwilisha ndani mwao Heri za Mlimani kwa wale wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria katika utenzi wake wa “Magnificat” ili kuwaonjesha huruma na upendo, maskini na wakoma wanaosukumiziwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Ulimwengu una kiu ya haki na amani
Ulimwengu una kiu ya haki na amani   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini, kama Bikira Maria kufuata njia ya Kristo Yesu ambayo inawaongoza kukutana na kila binadamu, hasa maskini, waliojeruhiwa na wadhambi, ili kuwashirikisha watu wa Mungu upole wa Mungu; njia yake ya “Kuwa Mama” na hivyo kuonekana katika Kanisa. Unyenyekevu na upole ni fadhila za wanyonge na wenye nguvu wanaoridhika na hali yao kwa sababu Mwenye nguvu amewatendea makuu: “amewashusha wenye nguvu kutoka viti vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu. Wenye njaa amewashibisha mema, matajiri amewaondoa mikono mitupu. Lk 1: 52-53. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, “Kila tunampomtazama Bikira Maria, tunakuja kuamini kwa mara nyingine katika asili ya kimapinduzi ya upendo na upole. Katika yeye tunaona kwamba unyenyekevu na upole si fadhila za walio wanyonge bali ni za wale walio na nguvu wanaohitaji kuwatendea wengine vibaya ili wajihisi kuwa wa maana wao wenyewe. Kwa kumtaamuli Bikira Maria, tunatambua kwamba yeye aliyemsifu Mungu kwa “kuwashusha wenye nguvu kutoka kwenye viti vyao vya enzi” na kuwarudisha matajiri mikono mitupu” (Lk 1:52-53) ni yeye pia anayetia joto la kinyumbani katika harakati zetu za kutafuta haki.” Evangelii gaudium, 288.

Watu wa Mungu wana kiu ya haki na amani
Watu wa Mungu wana kiu ya haki na amani   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, Ulimwengu mamboleo una kiu ya haki na amani, changamoto na mwaliko wa kuhakikisha kwamba, waamini wanaendelea kuisimamisha Tasaufi ya Kikristo na Ibada katika maeneo mbalimbali yaliyobarikiwa na Mwenyezi Mungu, ambayo yamesaidia kuleta mabadiliko katika uso wa dunia. Waamini waendelee kutumia nguvu hizi kupyaisha uso wa dunia na kuendelea kuleta mabadiliko. Maadhimisho ya Jubilei yanatoa wito wa toba na wongofu wa ndani, urejeshaji, tafakari na ukombozi. Bikira Maria, tumaini la waamini aendelee kuwaongoza kwa Kristo Yesu, Bwana na Msulubiwa, kwani ndani mwake kuna wokovu wote. Mwishoni mwa Ibada ya Misa Takatifu Mahujaji wa Tasaufi ya Bikira Maria walijiweka wakfu chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria na hatimaye, kusali Sala ya Malaika wa Bwana.

Tasaufi ya Bikira Maria
12 Oktoba 2025, 15:09