Papa,Mtandao Katoliki wa Misaada:kuwa wakala wa matumaini kwa watu wengi wanaokaribia Kanisa
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leone XIV, aliandika Ujumbe unaonesha tarehe 4 Oktoba 2025 na kutumwa katika fursa ya Mkutano 115 wa Mwaka, wa Mtandao wa Kikatoliki wa kutoka Msaada huko Marekani, ambao unafanyika huko Mtakatifu Juan, Porto Rico, kwa kuwaona washiriki takribani 600. Mtandao huo ambao mwaka 2024 ulisaidia watu wapatao milioni moja walio katika matatizo, ulianzishwa kunako 1910 na unajumuisha mashirika huru 168 yaliyojitolea kutoa chakula, malazi, matibabu, usaidizi wa kisheria na ishara zingine nyingi za fadhili.
Shauku na matarajio ya mambo mema yajayo
Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu anaadika kuwa: “Nilifurahishwa kujua kuhusu Mkutano wa 115 wa Mwaka wa Mtandao wa Misaada ya Kikatoliki wa Marekani unaofanyika San Juan, Puerto Rico, na ninatoa salamu za na heri kwa wale wote wanaoshiriki. Mmekusanyika pamoja Kanisa linapoadhimisha Mwaka wa Jubilei unaozingatia fadhila ya matumaini, ambayo mtangulizi wangu alifafanua kama “shauku na matarajio ya mambo mema yajayo, licha ya kutojua kwetu ni nini kitakuja wakati ujao” (Barua ya kutangaza Mwaka Mtakatifu 2025, 1).”
Kusaidi mambo msingi:chakula,malazi na usaidizi kisheria
Kupitia mashirika yako 168 ya Misaada ya Majimbo Katoliki, Papa aliongeza kuwa wanakuwa "wakala wa matumaini" kwa mamilioni ya watu wanaokaribia Kanisa nchini Marekani wakitafuta huruma na utunzaji. Wengi wa wale unaowahudumia ni miongoni mwa walio hatarini zaidi, wakiwemo wahamiaji na wakimbizi. Kwa vile hawawezi kutegemea rasilimali zao wenyewe na kutegemea Mungu na wema wa wengine, kwa njia nyingi huduma yao hufanya usimamizi wa Bwana kuwa thabiti kwao. Kupitia kutoa chakula, malazi, matibabu, usaidizi wa kisheria, na ishara nyingine nyingi za fadhili, Mashirika ya Misaada ya Kikatoliki Marekani yote yanaonesha kile ambacho Papa Francisko mara nyingi alirejea kuwa “mtindo” wa Mungu wa ukaribu, huruma, na upole.
Maskini na wahamiaji wanakumbana na changamoto
Papa leo alisisitiza kuwa ingawa wale walioathiriwa na umaskini na uhamiaji wa kulazimishwa wanakumbana na changamoto ngumu, “tusisahau kwamba wanaweza pia kuwa mashuhuda wa kutumaini si tu kupitia imani yao katika usaidizi wa kimungu, bali pia kwa uthabiti wao wa kushinda vizuizi vingi katika safari zao.” Papa alisema kwamba kwa namna ya pekee, wahamiaji na wakimbizi wa Kikatoliki wamekuwa wamisionari wa matumaini katika mataifa mengi, yakiwemo yako wewe mwenyewe, kwa kuleta imani changamfu na ibada zinazopendwa na watu wengi ambazo mara nyingi huwatia nguvu tena maparokia wanaowakaribisha (taz. Ujumbe kwa Siku ya 111 ya Wahamiaji na Wakimbizi). Inaweza kusemwa kwamba kwa kuwasaidia watu waliohamishwa kupata makazi yao mapya katika nchi yao, wao pia wanafanya kazi kama wajenzi wa daraja kati ya mataifa, tamaduni na watu.
Kristo aendelee kuwasindikiza na kuwapa furaha na amani
Kwa hiyo Papa amewatia moyo, basi, kuendelea kusaidia jumuiya zinazowapokea hawa kaka na dada wapya waliowasili kuwa mashuhuda hai wa matumaini, wakitambua kwamba wana utu wa ndani wa kibinadamu na wanaalikwa kushiriki kikamilifu katika maisha ya jumuiya. Papa alitoa shukrani zake za dhati kwa yote ambayo wao wale wanaofanya kazi na mitandao yao wanafanya kila siku ili kutekeleza kwa vitendo maonyo ya Bwana ya kumwona na kumtumikia katika maskini, wenye njaa, wasio na makazi, na watu katika aina yoyote ya uhitaji (taz. Mt 25:31-46). Kristo aendelee kuwasindikiza na kuwapa furaha na amani yake. Kwa hisia hizo Papa aliukabidhi Mkutano wa Mwaka kwa maombezi ya Maria, Mama wa Kanisa, na kwa hiari yake alitoa Baraka zake za Kitume kwa wote katika Mtandao wa Kikatoliki wa kutoka Misaada wa Marekani kama ahadi ya neema tele za mbinguni.
Asante sana kusoma makala hii. Kama unataka kubaki na sasisho, tunakualika kujiandikisha hapa ili kupata habari za kila siku: cliccando qui
