Papa Leo XIV kwa Walinzi wa Uswiss:Kuweni wamisionari wa matumaini katika watu!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV akikutana na Kikosi cha Walinzi wa Kipapa wa Uswiss katika Ukumbi wa Clementina katika Jumba la Kitume mjini Vatican, Ijumaa tarehe 3 Oktoba 2025 aliwapongeza kwa huduma yao ya kujitoa kwa bidii bila kuchoka. Lakini pia Papa aliwaeleza kwamba” Peke yenu, humwezi kujitambua kikamilifu. Mnahitaji kila mmoja kujifunza, kuendelea, kutumika katika ulimwengu unaozidi kujaribiwa na migawanyiko na kutengwa. Ukarimu, uaminifu, mshikamano, na kuheshimiana ni nguzo ambazo juu yake inawezekana kujenga maisha yenye maelewano.” Mkutano huu wa Papa na Kikosi cha Ulinzi wake ni katika fursa ya kuapishwa kwa watumishi wapya ishirini na saba kati ya miamoja therathini na tano. Papa akianza hotuba yake alisema “ninatoa salamu zangu kwa wote na kuwakaribisha katika Jumba la Kitume. Tangu hatua za kwanza za Upapa wangu, walinzi wapendwa wa Uswiss, nimeweza kutegemea huduma yenu ya uaminifu, ambayo mnaitekeleza kwa kujitolea na bidii kubwa.”
Papa alitoa shukrani kwamba “Ninachukua fursa hii ya sherehe za kiutamaduni wa kuapishwa kutoa shukrani zangu za dhati kwa kujitoa na kujitolea kwenu. Mrithi wa Petro anaweza kutimiza utume wake katika huduma kwa Kanisa na ulimwengu kwa uhakika kwamba mnaangalia usalama wake.” Akifafanua sehemu wanakotoka alisema “Wapendwa, mnatoka katika maeneo mbalimbali ya Uswiss, yenye tamaduni, lugha na desturi zenu. Hata hivyo, mmeitwa kuunda mwili wa umoja, kuunda vifungo vyenye nguvu na vyema vya urafiki kati yenu. Peke yenu, humwezi kujitambua kikamilifu. Mnahitaji kila mmoja kujifunza, kuendelea, kutumika katika ulimwengu unaozidi kujaribiwa na migawanyiko na kutengwa. Ukarimu, uaminifu, mshikamano, na kuheshimiana ni nguzo ambazo juu yake inawezekana kujenga maisha yenye maelewano.”
Kila mmoja wetu anaweza kuwa kielelezo kwa wengine kwa maneno na mwenendo wetu, kwa upendo na imani (rej. 1 Tim 4:12). Na mnaweza kuwa ujumbe wa umoja kwa Curia nzima ya Romana. Papa aliongeza kusema kuwa Mji wa Roma, pamoja na hazina na utajiri wake, unawapatia safari isiyosahaulika katika historia, si ya sanaa tu, bali pia na juu ya imani yote ya Kikristo, kuanzia na mashahidi wa kwanza waliomfuata Kristo, wakati mwingine hadi kufikia hatua ya kutoa maisha yao. Kwa njia hiyo Papa aliomba watumie fursa hiyo kukuza maisha yao ya ndani, katikati ya msisimko wa jamii yetu, kuimarisha uhusiano wao na Bwana, kama Mtakatifu Agostino alivyopendekeza: "Usitoke nje yako mwenyewe, rudi kwako mwenyewe; ukweli hukaa ndani ya mtu wa ndani" (De vera religione, 39).
Kwa kiapo hicho, Papa aliwaelekea vijana hao wapya kwamba wanaingia katika hatua mpya ya kuwepo kwao. Na hivyo aliwatia moyo kuishi utume huo kwa usadikisho, wakijiweka katika shule ya Kristo mnyenyekevu na mtiifu. Wengi wao watarudi nyumbani baada ya kutoa huduma nzuri na ya uaminifu kwa Kiti Kitakatifu. Na njia iliyojaa fursa itafunguka. Wengine wataendelea na masomo yao, wengine wataingia kwenye ulimwengu wa kazi. Labda wengine watakuwa wamekuza wito wa ukuhani. Huenda wengine wakadhamiria kugundua ulimwengu kabla ya kufanya maamuzi mahususi. Hata uamuzi wao wowote, Papa amewashauri wakumbuke kwamba uzoefu wao katika Curia Romana, utawasaidia kukabiliana na mabadiliko kwa uhakika na mtazamo wa ulimwengu mzima wa kuwa Mkristo.
Changamoto zinazokabili kizazi chao ni nyingi sana. Ni pamoja na masuala ya mazingira, mabadiliko ya kiuchumi, mivutano ya kijamii, mapinduzi ya kidijitali, akili unde na mambo mengine changamano ambayo yanahitaji utambuzi na hisia ya kuwajibika. Kukaa kwao Roma kutawasaidia kukuza na kukomaa katika nyanja hizi za maisha ya kijamii pia. Zaidi ya yote, Baba Mtakatifu aliwasihi wabaki waaminifu kwa Injili na tunu msingi za imani yao ya Kikristo, ambayo inawafanya wabatizwe na kusadikishwa juu ya chaguzi zao. Katika Mwaka huu Mtakatifu, na wao kwa ushuhuda wao rahisi, wawe wamisionari wa matumaini kwa watu unaokutana nao. Mwali wa matumaini uwaangazie maisha yao na kuwapa ujasiri wa kuthubutu na kuchangia pamoja katika ustaarabu wa upendo.
Papa hatimaye aliwaomba wawe na uhakika wa maombi yake kwa ajili yao. Akiwakabidhi kwa utunzaji wa uzazi wa Bikira Maria na ulinzi wa watakatifu walezi wao Martin na Sebastian, amewapatia Baraka yake ya Kitume kwao, familia yao, na marafiki wanaoshiriki katika sherehe yao. Aliwapatia heri tena na kuwashukuru.
Asante sana kusoma makala hii, ikiwa unakata kubaki na masasisho zaidi, tunakualika kujiandikisha hapa: Just click here
