Papa Leo XIV akutana na Patriaki wa Kanisa la Ashuru:Mazungumzo yetu yaharakishe siku iliyobarikiwa
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu leo XIV alikutana Patriaki wa Kanisa la Ashuru ya Mashariki Mar Awa III na wajumbe wa Tume ya pamoja kwa ajili ya mazungumzo katika ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Asiria - Ashuru ya Mashariki, Jumatatu tarehe 27 Oktoba 2025 mjini Vatican. Papa Leo XIV alianza hotuba yake alisema: “Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo iwe nanyi”(Efe 1:2). Kwa maneno haya ya Mtakatifu Paulo, ninakukaribisha, Mkuu, kama ndugu mpendwa katika Kristo, na ninatoa shukrani zangu tena kwa uwepo wako katika uzinduzi wa upapa wangu.
Pia natoa salamu zangu za dhati kwa wajumbe wa Tume ya Pamoja ya Majadiliano ya Kitaalimungu kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Ashuru la Mashariki. Ziara hizi za pamoja za Wakatoliki-Upatriaki wa Kanisa la Ashuru la Mashariki na wajumbe wa Tume zinawakilisha desturi nzuri iliyoanzishwa katika miaka ya hivi karibuni. Zinashuhudia ukweli kwamba mkutano wa kidugu na mazungumzo ya kitaalimungu ni vipengele vya pamoja katika njia ya umoja. "Majadiliano ya ukweli" ni usemi wa upendo ambao tayari unaunganisha Makanisa yetu, huku "majadiliano ya upendo" lazima pia yaeleweke kitaalimungu.
Ziara yake ya mwisho, mwaka wa 2024, iliadhimisha miaka thelathini ya mazungumzo rasmi kati ya Makanisa yetu. Maendeleo yaliyopatikana katika miaka hii ni muhimu, baada ya kufuata kwa uaminifu agizo na mbinu zilizowekwa na watangulizi wetu. Kama ilivyoelezwa katika Tamko la Pamoja la Mtakatifu Yohane Paulo II na Patriaki Mar Dinkha IV la 1994: "Ili kuwa kamili na kamili, ushirika unamaanisha umoja kuhusu maudhui ya imani, sakramenti, (communicatio in sacris) na katiba ya Kanisa."
Utatu huu ulitoa mfumo wa awamu zilizofuata za mazungumzo yetu ya kitaalimungu. Baada ya kufikia makubaliano kuhusu imani ya Kikristo, na hivyo kutatua utata wa miaka 1,500, mazungumzo yetu yaliendelea na utambuzi wa pamoja wa sakramenti, na kuruhusu mawasiliano fulani katika sakramenti kati ya Makanisa yetu. Papa alitoa shukrani zake za dhati kwa kila mmoja wao, wataalimungu wa Tume ya Pamoja, kwa michango yao muhimu na juhudi za pamoja, ambazo bila hizo makubaliano haya ya mafundisho na ya kichungaji yasingewezekana.
Kuhusu katiba ya Kanisa—mada ambayo kwa sasa ni kitovu cha mazungumzo—changamoto kuu iko katika kuendeleza kwa pamoja mfumo wa ushirika kamili, ulioongozwa na milenia ya kwanza, huku tukijibu kwa makini changamoto za sasa. Papa Leo XIV alisema kama watangulizi wake walivyosisitiza mara kwa mara, mfumo kama huo haupaswi kusababisha kunyonya au kutawala; badala yake, lazima uhimize ubadilishanaji wa zawadi kati ya Makanisa yetu, yaliyopokelewa kutoka kwa Roho Mtakatifu kwa ajili ya ujenzi wa Mwili wa Kristo (taz. Efe 4:12).” Papa ameonesha jinsi anavyosubiri kwa hamu matunda ya mazungumzo yao ya kitaalimungu ya yanayoendelea kuhusu ombi hili, yaliyofanywa "dhahiri pamoja," kama Papa Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alivyotamani sana katika Waraka wake wa Ut Unum Sint ili tuwe wamoja (n 95).
Katika safari hii kuelekea ushirika kamili, sinodi inajionesha kama njia yenye matumaini ya kusonga mbele. Wakati wa ziara yake mwaka 2022, ambapo Papa Francisko alibuni usemi uliojumuishwa baadaye katika Hati ya Mwisho ya Sinodi ya hivi karibuni kuhusu Sinodi ya Kanisa Katoliki; Ninanukuu: "Njia ya sinodi, ambayo Kanisa Katoliki linaifuata, ni na lazima iwe ya kiekumeni, kama vile njia ya kiekumeni ilivyo sinodi" (Kwa Kanisa la Sinodi: Ushirika, Ushiriki, na utume, n. 23). Katika roho ya Sinodi hiyo, ni matumaini ya dhati ya Papa kwamba maadhimisho ya miaka 1700 ya Mtaguso wa Nicea yatatuongoza "kutekeleza aina za sinodi miongoni mwa Wakristo wa tamaduni zote" na kututia moyo kwa "mazoea mapya ya sinodi ya kiekumeni" (, n. 138-139).
Papa Leo kwa njia hiyo alisisitiza kwamba: “Tunaweza kuendelea na hija hii tukiimarishwa na maombi ya watakatifu wote wa Makanisa yetu, hasa Mtakatifu Isaka wa Ninawi, ambaye jina lake liliongezwa kwenye Kitabu cha Mashahidi wa Kirumi mwaka jana! Kupitia maombezi yao, Wakristo wa Mashariki ya Kati watoe ushuhuda mwaminifu kwa Kristo aliyefufuka, na mazungumzo yetu yaharakishe kufika kwa siku iliyobarikiwa tutakaposherehekea pamoja katika altare moja, tukishiriki Mwili na Damu moja ya Mwokozi wetu, "ili ulimwengu upate kuamini" (Yh 17:21). Kwa kuhitimisha Baba Mtakatifu alisema “ Kwa pamoja katika maombi na Mwokozi wetu, sasa ninawaalika tusali Sala ya Bwana pamoja nami. Baba yetu…”
Asante kwa kusoma makala haya. Ikiwa unataka kuendelea kupata taarifa mpya, tunakualika ujiandikishe kwa jarida letu kwa kubofya hapa: Just click here.
