Tafuta

Papa Leo XIV: Mpango wa Utulivu Mashariki ya Kati 2025: Amani Na Utulivu

Baba Mtakatifu Leo XIV amegusia pia makubaliano ya “Mpango wa Utulivu Mashariki ya Kati 2025” yanayopania pamoja na mambo mengine kumaliza mapigano ya miaka miwili kati ya Israeli na Jeshi la Hamas ambayo yamepelekea mgogoro mkubwa wa kibinadamu Ukanda wa Mashariki ya Kati. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya amani na kwamba, Mama Kanisa daima yuko karibu na wanaoteseka na majamha ya vita!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV, Dominika tarehe 12 Oktoba 2025 katika mahubiri yake kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Tasaufi ya Bikira Maria, amekazia kwamba, Tasaufi ya Bikira Maria inarutubisha imani ya Wakristo kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu; Neno la Mungu ni hai, tena lina nguvu, na lina ukali kuliko upanga! Tasaufi ya Bikira Maria ni kwa ajili ya huduma ya Injili, amana na utajiri unaobubujika kutoka katika furaha ya utenzi wa Magnificat; ni tasaufi inayofuata nyayo za Yesu; Ulimwengu una kiu ya haki na amani na kwamba, Yesu ni kiini cha wokovu wa watu wote. Jubilei ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, upyaisho wa maisha ya kiroho sanjari na ukombozi. Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, aliwapongeza mahujaji waliohudhuria Jubilei ya Tasaufi ya Bikira Maria, wakiwa wameungana na Bikira Maria kusali kwenye “Chumba cha Juu.” Hili ni kundi lenye Ibada kwa Bikira Maria na kwamba, wanapaswa kuhakikisha kwamba, tasaufi yao inapata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa.

Maadhimisho ya Jubilei ya Tasaufi ya Bikira Maria
Maadhimisho ya Jubilei ya Tasaufi ya Bikira Maria   (@VATICAN MEDIA)

Baba Mtakatifu Leo XIV amegusia pia makubaliano ya “Mpango wa Utulivu Mashariki ya Kati 2025” yanayopania pamoja na mambo mengine kumaliza mapigano ya miaka miwili kati ya Israeli na Jeshi la Hamas ambayo yamepelekea mgogoro mkubwa wa kibinadamu Ukanda wa Mashariki ya Kati. Wachunguzi wa mambo wanasema, hatua hii ni mwanzo wa ujenzi wa enzi mpya ya amani, utulivu na usalama huko Mashariki ya Kati. Jeshi la Hamas linatakiwa kuwaachia huru mateka wote wa Israeli walioko mikononi mwao kama sehemu ya kwanza ya utekelezaji wa makubaliano hayo. Kwa upande wake, Serikali ya Israeli imekubali kuwaachia mateka wa kivita na wafungwa wa Kipalestina. Lengo ni kuanzisha mazingira rafiki ya kudumu kisiasa yanayolenga kupatikana kwa suluhu ya kudumu. Misaada ya kibinadamu imeanza kuwasili Ukanda wa Gaza. Kwa hakika amani ya kweli kamwe haiwezi kupatikana kwa ncha ya upanga, bali ni kwa njia ya mazungumzo yanayosimikwa katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana sanjari na kujenga matumaini mapya kwa vijana wa kizazi kipya.

Siku ya Kuwakumbuka na Kuwaombea watu waliopata ajali kazini Italia
Siku ya Kuwakumbuka na Kuwaombea watu waliopata ajali kazini Italia   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, mapigano ya miaka miwili kati ya Israeli na Palestina yameacha machungu kati ya wananchui huko Ukanda wa Gaza. Mama Kanisa yuko karibu na wale wote wanaoteseka na kwamba, hata katika giza na usiku mnene, Kristo Yesu bado anasema, “Dilexi te” Yaani “Nimekupenda.” Ufu 3:9. Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya amani, mwaliko kwa waamini kumwomba ili aweze kuganga na kuponya madonda yote, ambayo kwa sasa yanayoonekana kushindikana, ili hatimaye, kuweza kugundua ndugu na marafiki, ambao watu wanaweza kuangaliana machoni, kusameheana na hatimaye, kuweza kutoa matumaini na upatanisho. Baba Mtakatifu Leo XIV amesikitishwa na mashambulizi ya kivita yaliyofanyika hivi karibuni nchini Ukraine na kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Baba Mtakatifu Leo XIV anaungana na wale wote wanaoteseka, watu wanaoendelea kuishi katika hofu na majanga. Baba Mtakatifu anawaalika tena wahusika kusitisha vita na kuanza kujielekeza kwenye majadiliano katika ukweli na uwazi, tayari kujenga na kudumisha amani. Anasema yuko karibu sana na watu wa Mungu nchini Perù ambao wako katika kipindi cha mpito wa kisiasa, ili waendelee kujikita katika njia ya upatanisho, majadiliano na ujenzi wa umoja na ushirikiano wa Kitaifa. Mwishoni wa tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, amewakumbusha watu wa Mungu nchini Italia tarehe 12 Oktoba ya kila mwaka, Serikali ya Italia inawakumbuka na kuwaombea waliofariki na kuathirika katika ajali kazini na kwamba, anawaombea wote ili kuhakikisha kwamba usalama unaimarishwa sehemu za kazi.

Ukanda wa Gaza
13 Oktoba 2025, 14:41

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >