Papa Leo XIV,Sala Malaika wa Bwana:Tuwe kama mtoza ushuru kwa kukiri makosa yetu kwa Mungu
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu leo XIV mara baada ya Ibada ya misa Takatifu kwa ajili ya Jubilei ya timu ya Sinodi na vikundi shirikishi, katika Kanisa Kuu la Mtakatifu petro mjini Vatican, Dominika tarehe 26 Oktoba 2025, alikwenda katika dirisha la Jumba la Kitume kwa ajili ya sala ya Malaika wa Bwana. Akiwageukia waamini na mahujaji waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, kwa kudadavua Injiili ya Siku Papa alisema: “Injili ya leo inatupatia watu wawili, Farisayo na mtoza ushuru, wakiomba Hekaluni (Lk 18:9-14).
Papa alisema kuwa “wa kwanza anajivunia orodha ndefu ya sifa. Anafanya kazi nyingi njema, na kwa sababu hiyo anajiona bora kuliko wengine, ambao anawahukumu kwa dharau. Anasimama akiwa ameinua kichwa chake juu. Mtazamo wake ni wa kiburi waziwazi: unaashiria utunzaji kamili wa Sheria, ndiyo, lakini hauna upendo, unaojumuisha "kutoa" na "kupokea," madeni na mikopo, bila huruma.” Kwa upande wa Mtoza ushuru pia anaomba, lakini kwa njia tofauti sana. Ana mengi ya kupata kwa msamaha: yeye ni mtoza ushuru katika malipo ya Milki ya Kirumi, na kazi yake iko chini ya mkataba unaomruhusu kubashiri mapato kwa gharama ya watu wenzake. Hata hivyo, mwishoni mwa mfano, Yesu anatuambia kwamba yeye, kati ya hao wawili, ndiye anayerudi nyumbani "amehesabiwa haki," yaani, amesamehewa na kupyaishwa na kukutana kwake na Mungu.
Je ni kwa nini? Papa anauliza na kujibu: Kwanza kabisa, mtoza ushuru ana ujasiri na unyenyekevu wa kujionesha mbele za Mungu. Hajifungi katika ulimwengu wake mwenyewe, hajiachilii maovu aliyoyafanya. Anaondoka mahali ambapo anaogopwa, salama, na kulindwa na nguvu anayotumia juu ya wengine. Anakuja Hekaluni peke yake, bila mlinzi, hata kwa gharama ya kukabiliwa na sura kali na hukumu kali, na anasimama mbele za Bwana, nyuma, akiwa ameinamisha kichwa chake, akisema maneno machache: "Ee Mungu, unirehemu mimi mwenye dhambi" (rej. 13). Kwa hivyo Yesu anatupatia ujumbe wenye nguvu: si kwa kuonesha sifa zako kwamba mtu huokolewa, wala kwa kuficha makosa yake, bali kwa kujionesha kwa uaminifu, kama sisi tulivyo, mbele za Mungu, mbele yake mwenyewe, na mbele ya wengine, kwa kuomba msamaha na kujikabidhi kwa neema ya Bwana.”
Akitoa maoni yake kuhusu kipindi hiki, Papa ameongeza kusema “Mtakatifu Agostino anamlinganisha Farisayo na mtu mgonjwa ambaye, kwa aibu na kiburi, huficha majeraha yake kwa daktari, na mtoza ushuru na mwingine ambaye, kwa unyenyekevu na hekima, huweka wazi majeraha yake mbele ya daktari, hata yakiwa mabaya kiasi gani, akiomba msaada. Na anahitimisha: "Haishangazi [...] ikiwa mtoza ushuru huyo, ambaye hakuwa na aibu kuonesha upande wake dhaifu, akarudi [...] amepona" (Mahubiri 351,1).
Papa kwa njia hiyo ametoa ushauri kwamba hasa sisi sote “tufanye vivyo hivyo. Tusiogope kukiri makosa yetu, kuyaweka wazi, kuchukua jukumu kwa ajili yake na kuyakabidhi kwa rehema ya Mungu. Hivyo, Ufalme Wake utaweza kukua, ndani yetu na karibu nasi, Ufalme ambao si wa wenye kiburi, bali wa wanyenyekevu, na ambao hupandwa, katika sala na maishani, kupitia uaminifu, msamaha, na shukrani. Tumwombe Maria, mfano wa utakatifu, atusaidie kukua katika fadhila hizi.
