Tafuta

Papa Leo XIV Wosia wa Kitume "Dilexi te" Yaani "Nimekupenda" Kuhusu Upendo kwa Maskini. Ufu 3:9. Umezinduliwa rasmi tarehe 9 Oktoba 2025. Papa Leo XIV Wosia wa Kitume "Dilexi te" Yaani "Nimekupenda" Kuhusu Upendo kwa Maskini. Ufu 3:9. Umezinduliwa rasmi tarehe 9 Oktoba 2025. 

Papa Leo XIV Wosia wa Kitume Dilexi Te: Nimekupenda: Kuhusu Upendo Kwa Maskini

Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Leo XIV “Dilexi te” Yaani “Nimekupenda” Kuhusu Upendo kwa Maskini. Ufu 3:9 uliotiwa mkwaju, tarehe 4 Oktoba 2025 katika kumbukumbu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, umezinduliwa rasmi tarehe 9 Oktoba 2025, kama sehemu ya mwendelezo wa Waraka wa Kitume ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko “Dilexit nos” yaani “Alitupenda” Waraka wa Kitume juu ya upendo wa kibinadamu na wa Kimungu wa Moyo Mtakatifu wa Yesu Kristo.”

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Leo XIV “Dilexi te” Yaani “Nimekupenda” Kuhusu Upendo kwa Maskini. Ufu 3:9 uliotiwa mkwaju, tarehe 4 Oktoba 2025 katika kumbukumbu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, umezinduliwa rasmi tarehe 9 Oktoba 2025, kama sehemu ya mwendelezo wa Waraka wa Kitume ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko “Dilexit nos” yaani “Alitupenda” Waraka wa Kitume juu ya upendo wa kibinadamu na wa Kimungu wa Moyo Mtakatifu wa Yesu Kristo.” Kristo Yesu aliwapenda waja wake upeo na kuwataka kutambua kuwa, hakuna jambo lolote linaloweza kuwatenga na upendo wake, kiasi kwamba aliwaita rafiki zake. Kristo Yesu anapenda kuwapatia waja wake upendo na urafiki na kwamba, “alitupenda sisi kwanza. Rej. 1Yn 4:10. Na kwa sababu ya Kristo Yesu “Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi.” 1Yn 4:16. Papa Leo XIV anakazia upendo wa Kanisa kwa maskini, kama njia ya utakatifu inayowawezesha waamini kumtambua Kristo Yesu kati ya maskini na wanaoteseka, kiini cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, ambao watakatifu wengi walitamani kuuiga. Wosia huu wa kitume, umegawanyika katika: Sura tano: Sura ya Kwanza inafafanua kuhusu maneno muhimu yaliyotumika katika Wosia huu: Sura ya Pili ni Upendeleo wa Mungu kwa maskini. Sura ya Tatu ni Kanisa kwa ajili ya maskini. Sura ya Nne inaonesha Mwendelezo wa Historia katika huduma kwa maskini. Sura ya Tano ni kuhusu Changamoto endelevu.

Papa Leo XIV Wosia Dilexi te-nimekupenda kuhusu upendo kwa maskini
Papa Leo XIV Wosia Dilexi te-nimekupenda kuhusu upendo kwa maskini   (@Vatican Media)

Sura ya Kwanza inafafanua kuhusu maneno muhimu yaliyotumika katika Wosia huu. Upendo kwa Kristo Yesu na upendo kwa maskini ni chanda na pete na kwamba, hii ni historia inayoendelea kukumbukwa kama alivyofanya yule mwanamke aliyemmiminia Yesu marhamu kule Bethania, akimwandaa Kristo Yesu kwa kifo chake na kwamba hii ndiyo njia muafaka ya kukutana na Yesu kwa njia ya maskini na kwamba, maskini wanaendelea kuzungumza na watu wa Mungu hata leo hii. Mtakatifu Francisko wa Assis alijisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini, akawa ni chanzo cha mabadiliko katika historia mamboleo na kwamba, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wakachukua huduma kwa maskini kuwa ni sehemu ya tasaufi ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na kwamba, upendeleo kwa maskini ni kiini cha upyaisho wa Kanisa na jamii katika ujumla wake, changamoto na mwaliko kwa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini. Kuna mifumo mbalimbali ya umaskini: maskini wanaokosa mahitaji msingi; maskini wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya kijamii; maskini wa kiutu, kimaadili na kitamaduni; watu dhaifu na maskini wanaonyimwa haki, uhuru na fursa na kwamba, ndio maana Umoja Mataifa katika Malengo ya Maendeleo Endelevu Ifikapo Mwaka 2030 umeelekeza kutokomeza umaskini wa aina zote kila mahali. Kwa hakika kiwango cha umaskini kinaendelea kuongezeka maradufu. Kuna itikadi ya maamuzi mbele inayodharirisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni changamoto kwa waamini kurejea tena katika Maandiko Matakatifu na kwamba, huduma kwa maskini ni kiini cha Habari Njema.

Ibada ya Misa Takatifu, Siku ya Maskini Ulimwenguni
Ibada ya Misa Takatifu, Siku ya Maskini Ulimwenguni

Sura ya Pili ni Upendeleo wa Mungu kwa Maskini. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo na amejifunua kwa walimwengu kwa njia ya Mtoto mchanga aliyelazwa katika hori ya kulia wanyama. Upendeleo wa Mungu kwa maskini ni kielelezo cha huruma ya Mungu kwa maskini na binadamu dhaifu anayesubiri kufunguliwa kwa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, udugu wa kibinadamu na mshikamano na kwamba maskini wanayo nafasi ya pekee katika moyo wa Mungu, mwaliko kwa Mama Kanisa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaonyanyaswa na kudhulumiwa. Kimsingi, historia nzima ya ukombozi inasimikwa katika uwepo wa maskini kama inavyojionesha kwenye historia ya Fumbo la Umwilisho, katika maisha. Ni Masiha maskini na kwa ajili ya maskini, aliyetumwa na Baba yake wa mbinguni kuwatangazia maskini Habari Njema. Katika Agano la Kale, umaskini ulifungamanishwa na dhambi binafsi, lakini Kristo Yesu katika Agano Jipya anaonesha kwamba, maskini wana nafasi ya pekee miongoni mwa watu wa Mungu. Kimsingi, huruma kwa maskini imeoneshwa kwa kina katika Maandiko Matakatifu na kwamba, Mungu ni upendo ndiyo maana Mama Kanisa anakazia matendo ya huruma: kiroho na kimwili na kama Kristo Yesu anavyobainisha kwenye Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu na kwamba, hiki ni kielelezo cha imani tendaji kama Mwinjili Luka anavyosimulia katika Kitabu cha Matendo ya Mitume. Upendo kwa maskini ni ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo, mwaliko kwa waamini kuiga mfano huu mzuri, utakao zaa utajiri mkubwa.

Upendeleo wa Mungu kwa maskini
Upendeleo wa Mungu kwa maskini   (@VATICAN MEDIA)

Sura ya Tatu ni Kanisa kwa ajili ya maskini. Hayati Baba Mtakatifu Francisko alitamani sana kuona Kanisa maskini na kwa ajili ya maskini; Kanisa linalojisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini: “Diakonia”, kielelezo cha ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu, kiasi hata cha kuyamimina maisha, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Stefano, Shuhuda wa imani na huduma ya upendo kwa maskini. Mtakatifu Laurenti, Shemasi, aliyewaonesha maskini kuwa ni hazina na utajiri wa Kanisa. Ni kosa la jinai kwa watu kujitajirisha kutokana na umaskini wa watu. Katika maisha na utume wao, Mababa wa Kanisa daima wamekazia huduma ya upendo kwa maskini, kwa kuwatambua kwamba, wao ni sehemu hai ya Fumbo la Mwili wa Kristo. Daima Kanisa limejipambanua kuwa ni Mama wa maskini, mahali pa ukarimu na haki. Tangu mwanzo, Kanisa lilijikita katika kutoa huduma makini kwa jamii, kama kielelezo cha imani tendaji, kwani imani bila matendo hiyo imekufa. Rej. Yak 2:17. Waamini wajibidiishe kukutana na Kristo Yesu kati ya maskini wanaosimama mlangoni mwa Kanisa na kwamba, Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya upendo na haki, viwasukume waamini kuipenda Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na hivyo kuwa makini kwa maskini. Upendo ni kielelezo cha Ibada ya kweli na huduma kwa maskini na ndiyo maana ya haki jamii na kwamba huduma kwa maskini ni kuwarejeshea maskini haki yao na kwa Mtakatifu Augustino, maskini ni Sakramenti ya uwapo wa Kristo Yesu na kuwa upendo na ukarimu kwa maskini ni chemchemi ya baraka na neema kutoka kwa Mungu. Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani unaofumbata huduma kwa maskini. Kanisa katika maisha na utume wake, halina budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, ili kweli Kanisa liwe ni maskini kwa ajili ya maskini, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kanisa halina budi kujibidiisha kutoa huduma kwa wagonjwa, ili kugusa mateso na mahangaiko ya Fumbo la Mwili wa Kristo Yesu.

Kanisa limewekeza sana katika huduma kwa wagongwa na maskini
Kanisa limewekeza sana katika huduma kwa wagongwa na maskini   (ANSA)

Huu ndio mfano na ushuhuda kutoka kwa Mtakatifu Yohane wa Mungu, Muasisi wa Shirika la Wakamilliani, Wahudumu wa Wagonjwa, waliomwilisha ndani mwao huduma kwa wagonjwa, kama ilivyo kwa Kristo Yesu, Mganga mkuu. Mama Kanisa ameendelea kutoa huduma kwa wagonjwa na maskini; waraibu wa pombe na dawa za kulevya na majeruhi vitani. Huduma kwa wagonjwa imekuwa ikitolewa kwenye nyumba za wamonaki kama kielelezo cha maisha, utume na tasaufi yao. Mtakatifu Benedikto, Abate anasema, maisha ya kijumuiya ni shule ya upendo na kwamba, ukarimu kwa wageni na mahujaji ni sehemu ya utambulisho wao. Tangu mwanzo, Monasteri zimekuwa ni kitovu cha malezi na majiundo ya kitamaduni na maisha ya kiroho kwa maskini. Maisha ya kimonaki yakawa ni mtindo wa utakatifu na chachu ya mabadiliko kijamii. Haya ni maisha yanayosimikwa katika sala na huduma; ukimya na ibada na kwamba, hapa ni mahali ambapo mtu hujifunza kuhudumia kwa ufanisi zaidi. Kanisa pia limekuwa likiwahudumia wafungwa magerezani na kwamba, uhuru wa wafungwa ni kielelezo cha upendo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Rej. 1Kor 6:20. Leo hii kuna mifumo mipya ya utumwa mamboleo: Biashara haramu ya binadamu na viungo vyake mambo ambayo yanafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa: katika kazi za suluba, ukahaba, biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na uhalifu wa magenge; uhamiaji wa shuruti matendo yote haya ni uhalifu dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, wote hawa wanahitaji kukombolewa na kwamba, uhuru wa kweli ni ushuhuda wa historia ya upendo inayojali na kumkomboa mwanadamu kutoka katika mifumo yote ya utumwa. Rej. Gal 5:1. Mtakatifu Francisko wa Assisi na watakatifu wengine ni mashuhuda wa Ufukara wa Kiinjili, uliowawezesha kukumbatia na kuambata: ufukara na unyenyekevu; kujenga na kudumisha udugu wa Kiinjili; mshikamano wa udugu wa upendo na hivyo yote haya kuwa ni chachu ya utakatifu. Maskini ni kielelezo cha mahujaji, wanyenyekevu na udugu wa Kikanisa, kielelezo cha utambulisho wao wa kweli na kwamba, utakatifu unapata chimbuko lake kutoka katika moyo wa unyenyekevu.

Kanisa limewekeza sana katika sekta ya elimu
Kanisa limewekeza sana katika sekta ya elimu

Mama Kanisa amekuwa mstari wa mbele kutoa elimu kwa maskini inayomkomboa mwanadamu na kumrejeshea tena utu, heshima na haki zake msingi. Ni elimu inayomuunda mtu na kwamba, kwa Kanisa, elimu ni tendo la haki na imani, kwa kufuata mfano wa Kristo Yesu, Mwalimu mkuu aliyewafundisha watu kweli za Kimungu na Kibinadamu. Kanisa limeendelea kuwafundisha watoto wa Mungu kuhusu ukweli na upendo, mwanzo wa kuibuka kwa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, yaliyojipambanua katika sekta ya elimu na kwamba, elimu ilikuwa ni kielelezo cha huduma katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Kumbe, huduma ya elimu ilikwenda sanjari na mchakato wa uinjilishaji, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya mtu mzima: kiroho na kimwili, kwa kusaidia kujenga dhamiri nyofu, kwa kuwapatia nyenzo za kuleta mabadiliko katika maisha, kwa kuwaimarishia utu na tunu msingi za maisha. Mama Kanisa kwa kuunganisha imani na tamaduni akawa anapandikiza mbegu za Ulimwengu ujao, kwa kuheshimu sura ya Mungu ndani mwao, tayari kujenga jamii iliyo bora zaidi.

Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa wakimbizi
Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa wakimbizi   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha. Tangu mwanzo wa maisha na utume wake, Kanisa limekuwa mstari mbele kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji na watakatifu Yohane Baptist Scalabrini na Mtakatifu Frances Xavier Cabrini wamejipambanua katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji kiasi cha Papa Pio XII kumtangaza kuwa ni Msimamizi na Mwombezi wa Wakimbizi na Wahamiaji, wakati wa Maadhimisho wa Mwaka Mtakatifu 1950. Huduma hii bado inaendelezwa na Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis pamoja na Taasisi mbalimbali za Misaada. Mama Kanisa amekuwa pia mstari wa mbele kwa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kama ilivyokuwa kwa Mama Theresa wa Calcutta, mfano wa huduma kwa maskini wanaopaswa: kuheshimiwa, kuthaminiwa, kupendwa na kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki zao msingi zinalindwa, kuendelezwa na kudumishwa. Huduma kwa maskini ni njia ya kukutana na Kristo Yesu anayepaswa kupendwa na kuabudiwa na ndiyo maana Kanisa linapaswa kuwa na upendeleo wa pekee kwa maskini. Katika historia kumekuwepo na viongozi waliojipambanua kwa huduma kwa maskini, wakasimama kidete kupambana na mifumo inayozalisha umaskini; ukosefu wa usawa, ukosefu wa fursa za kazi na ajira, ardhi na makazi pamoja na ukosefu wa haki msingi za kazi, daima wakawa mstari wa mbele katika ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Hii ni changamoto kwa wanasiasa na wataalamu kusikiliza na kujibu kilio cha maskini, kuwasaidia maskini kupambania utu, heshima, ili kuwa na uhakika wa leo na kesho iliyo bora zaidi. Hii ni changamoto kwa taasisi mbalimbali za Kanisa kuendeleza mapambano hayo.

Kanisa ni chombo cha ujenzi wa amani na mshikamano
Kanisa ni chombo cha ujenzi wa amani na mshikamano   (ANSA)

Sura ya Nne inaonesha Mwendelezo wa Historia katika huduma kwa maskini. Kanuni maadili na utu wema ni kiini cha Mafundisho Jamii ya Kanisa, chombo cha ujenzi wa amani na majadiliano ili kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu sanjari na ujenzi wa udugu wa kibinadamu ulimwenguni. Ni mwongozo rasmi wa Kanisa Katoliki kuhusu siasa, uchumi, jamii, na masuala ya dini, yakilenga kutetea utu, haki msingi za binadamu, ustawi wa jamii, maendeleo fungamani, na mshikamano. Yanachota msukumo kutoka Maandiko Matakatifu, Mapokeo ya Kanisa, na akili, yakiweka kipaumbele cha kwanza kuwa ni kuunda dunia yenye haki, amani, ukweli, upendo, uhuru, na utunzaji bora wa mazingira kwa ustawi wa wote. Ni mafundisho yenye amana na utajiri mkubwa kuhusu huduma kwa maskini, kama ambavyo wanakazia Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na kutiliwa mkazo na “Magisterium ya Kanisa” yaani “Mamlaka fundishi ya Kanisa. Papa Leo XIV anabainisha miundo mbinu ya dhambi inayowatumbukiza watu wengi katika umaskini na ukosefu wa usawa kama kielelezo cha umaskini jamii: Uchumi wa kiimla; Ukosefu wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu na hivyo kupelekea ukosefu wa haki msingi za binadamu; utu na heshima ya binadamu, changamoto ni ujenzi wa Ufalme wa Mungu, wongofu wa maisha ya kiroho; upendo kwa Mungu na jirani. Maskini wanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, ili hata maskini wawe ni wakala wa uinjilishaji mpya; kwa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki zao msingi. Waraka wa Mkutano wa Aparecida uliofanyika nchini Brazil kunako mwaka 2007 ulikazia upendeleo na uinjilishaji kwa maskini, ili hata maskini wawe ni wadau wa uinjilishaji, watambuliwe na kuheshimiwa utu, haki zao msingi na mchango wao katika ustawi na maendeleo ya Kanisa na kwamba, upendo wa kweli unawasukuma watu wa Mungu kuhudumia.

Kanisa linasukumwa kwa upendo kuhudumia
Kanisa linasukumwa kwa upendo kuhudumia   (@Vatican Media)

Sura ya Tano ni kuhusu Changamoto endelevu. Upendo kwa maskini ni kito cha thamani katika historia ya Mungu kwa mwanadamu na kwamba, maisha ya maskini yana nafasi ya pekee katika hija ya watu wa Mungu na kwamba, Mama Kanisa anahimizwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, kama kielelezo cha upyaisho wa maisha na utume wake. Huduma ya Kanisa kwa maskini ni tofauti sana na huduma inayotolewa na Mashirika ya Kimataifa. Huu ni mwaliko kwa Kanisa anasema Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwa Kanisa kutafakari Injili ya Msamaria mwema ndiye mtu pekee aliyethubutu kumwonea huruma, akamkaribia na kumfunga jeraha zake, akazitia mafuta na divai. Lakini ikumbukwe kwamba, Wasamaria ni watu waliokuwa wanadharaulika sana. Rej. 2 Fal 17. Msamaria mwema aliweza kusimama na kushuka kwa sababu aliguswa na utu, akawa tayari kumsaidia na kumhudumia yule mtu aliyekuwa amejeruhiwa, akampeleka kwenye nyumba ya kutunza wageni na kuahidi kumgharimia zaidi kwa kutambua kwamba, huyu alikuwa ni mtu aliyehitaji huduma yake na wala si mzigo wa kuegeshwa pale kwenye nyumba ya wageni!

Huduma ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi
Huduma ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, hii ni changamoto kwa waamini kusitisha safari zao kwa muda, ili kuwahudumia jirani wanaohitaji huruma na upendo. Kristo Yesu amejisadaka na kuwaonea huruma na upendo waja wake na kwa njia hii, atawawezesha waamini kuwa wenye upendo na huruma. Wataweza kukua na kuongezeka katika utu na hivyo kuboresha mahusiano na mafungamano yao yanayorutubishwa kwa huruma na upendo. Waamini wamwombe Kristo Yesu ili awakirimie neema ya kuwa na huruma na upendo kama alivyo Kristo Yesu mwenyewe na hii ndiyo maana ya kuwa ni Mkristo! Yaani Mfuasi wa Kristo Yesu, hali ambayo inapaswa kujionesha pia katika Jumuiya za Kikristo na kwamba, kila mwamini anaitwa na kutumwa kuwa ni Msamaria mwema. Umaskini ni changamoto mamboleo na kwamba, maskini ni shule ya unyenyekevu, haki na huruma yenye upendo na kwamba, maskini ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo Yesu. Kanisa kwa asili linaonesha mshikamano na maskini ambao ni kiini, amana na utajiri wa Kanisa. Huduma kwa maskini kiroho na kimwili ni sehemu ya Mafundisho Jamii ya Kanisa na kielelezo cha ushiriki wa Kanisa katika kazi ya uumbaji na ni sehemu ya baraka na neema kutoka kwa Mungu kama inavyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu. Rej. Mit 22:9; Lk 12:33. Msaada kwa maskini hauna budi kutolewa kwa Kwa akili, bidii na uwajibikaji wa kijamii kama kielelezo cha kugusa Madonda Matakatifu ya Yesu. Kwa asili upendo wa Kikristo ni wa kinabii, hutenda miujiza na kamwe hauna ukomo. Upendo ni mtazamo katika maisha na njia ya kuishi. Kanisa halina ukomo katika upendo, halina maadui, bali linapaswa kuwapenda watu, hili ndilo Kanisa linalohitajika kwa sasa katika Ulimwengu mamboleo. Yesu anasema: “Dilexi te” Yaani “Nimekupenda.” Ufu 3:9.

Papa Leo XIV Dilexi Te
09 Oktoba 2025, 14:32