Tafuta

2025.10.10 Wawakilishi wa Mfuko wa Kanisa Hitaji. 2025.10.10 Wawakilishi wa Mfuko wa Kanisa Hitaji.  (@VATICAN MEDIA)

Papa Leo XIV kwa Shirika la Kanisa Hitaji:Kiungo kimoja kikiumia,vyote huumia pamoja

Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba kwa Mfuko wa Kipapa wa Kanisa Hitaji,Oktoba 10,alisisitiza kujitolea kwake kusaidia Wakristo walio wachache katika nchi kama vile Jamhuri ya Afrika ya Kati,Burkina Faso,Msumbiji na Peru,nchi yake ya umisionari kabla ya kuja Roma.”Ulimwengu wetu unaendelea kushuhudia uadui na jeuri inayoongezeka dhidi ya wale walio na imani tofauti,wakiwemo Wakristo wengi.”

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV tarehe 10 Oktoba 2025 amekutana na wajumbe wa Mfuko wa Kipapa wa  Kanisa Hitaji, mjini Vatican ambapo Papa alionesha furaha yake kuwasalimu  waliokusanyika Roma wakati wa Jubilei hii ya Matumaini. Ziara yao imekuja wakati muafaka, kwa kuwa ulimwengu wetu unaendelea kushuhudia uadui na jeuri inayoongezeka dhidi ya wale walio na imani tofauti, wakiwemo Wakristo wengi.  Kinyume chake, utume wao unatangaza kwamba, kama familia moja katika Kristo, hatuwaachi kaka na dada zetu wanaoteswa. Badala yake, tunawakumbuka, tunasimama pamoja nao, na tunajitahidi kupata uhuru wao waliopewa na Mungu. Maneno ya Mtakatifu Paulo yanatukumbusha: “Kiungo kimoja kikiumia, vyote huumia pamoja” (1Kor 12:26).

Wawakilishi wa Mfuko wa Kanisa Hitaji
Wawakilishi wa Mfuko wa Kanisa Hitaji   (@VATICAN MEDIA)

Baba Mtakatifu Leo aliendelea kusema kuwa “maneno haya yanajirudia katika mioyo yetu leo, kwa maana mateso ya mshiriki yeyote wa Mwili wa Kristo yanashirikishwa na Kanisa zima. Na ndiyo ukweli huo ambao Papa amesema kuwa  mbele yao anawahutubia. Kila mwanadamu amebeba ndani ya moyo wake hamu kubwa ya ukweli, maana, na ushirika na wengine na Mungu. Shauku hii inainuka kutoka katika kina cha utu wetu. Kwa sababu hii, haki ya uhuru wa kidini si ya hiari bali ni muhimu.  Ukiwa na mizizi katika adhama ya mwanadamu, aliyeumbwa kwa mfano wa Mungu na aliyejaliwa uwezo wa kufikiri na uhuru wa kuchagua, uhuru wa kidini huruhusu watu binafsi na jumuiya kutafuta ukweli, kuuishi kwa uhuru, na kuutolea ushuhuda waziwazi.

Kwa hiyo ni msingi wa jamii yoyote ya uadilifu, Papa alisisitiza kuwa  “kwa kuwa hulinda nafasi ya kimaadili ambamo dhamiri inaweza kuundwa na kutumiwa. Kwa hiyo, uhuru wa kidini si haki ya kisheria au pendeleo tunalopewa na serikali; ni hali ya msingi inayofanya upatanisho wa kweli uwezekane.  Uhuru huu unaponyimwa, mwanadamu ananyimwa uwezo wa kuitikia kwa uhuru wito wa ukweli.  Kinachofuata ni mtawanyiko wa polepole wa vifungo vya kimaadili na kiroho vinavyodumisha jamii; uaminifu hutoa nafasi ya woga, mashaka huchukua nafasi ya mazungumzo, na uonevu huzaa jeuri. Hakika, kama mtangulizi wake Papa Francisko alivyo bainisha, Papa Leo XIV alisema "hakuwezi kuwa na amani bila uhuru wa dini, uhuru wa mawazo, uhuru wa kujieleza na heshima kwa maoni ya wengine" (Papa Francisko, Urbi Et Orbi, 20 Aprili 2025). Kwa sababu hiyo, Kanisa Katoliki daima limetetea uhuru wa kidini kwa watu wote. Mtaguso wa Pili wa Vatican, katika Hati ya Dignitatis Humanae, yaani “Hadhi ya Binadamu” ulitangaza kwamba haki hii lazima itambuliwe katika maisha ya kisheria na kitaasisi ya kila taifa (taz. 7 Desemba 1965, 4).

Wawakilishi wa Mfuko wa Kanisa Hitaji
Wawakilishi wa Mfuko wa Kanisa Hitaji   (@VATICAN MEDIA)

Utetezi wa uhuru wa kidini, basi, hauwezi kubaki kuwa wa kufikirika; ni lazima uiishi, ulindwe na kukuzwa katika maisha ya kila siku ya watu binafsi na jamii. Kutokana na imani hii kwamba shirika lao lilizaliwa, lilianzishwa mwaka 1947 ili kukabiliana na mateso makubwa yaliyosalia baada ya vita, utume wake tangu mwanzo umekuwa ni kuhimiza msamaha na upatanisho, na kulisindikiza na kutoa sauti kwa Kanisa popote linapohitaji, popote linapotishiwa, popote linapoteseka. Kwa zaidi ya miaka ishirini na mitano, Uhuru wao wa Kidini katika Ripoti ya Dunia imekuwa chombo chenye nguvu cha kuongeza ufahamu. Ripoti hii inafanya zaidi ya kutoa habari; inatoa ushuhuda, inatoa sauti kwa wasio na sauti, na kufichua mateso ya wengi yaliyofichika. Kujitolea kwao pia kunaenea katika kuunga mkono utume wa Kanisa  ulimwenguni  kote kwa kufikia jumuiya ambazo mara nyingi zimetengwa, zilizotengwa au chini ya shinikizo. Popote ambapo Msaada kwa Kanisa Hitaji hujenga upya Kanisa, kutegemeza watawa, au kutoa kituo cha radio au gari, wanaimarisha maisha ya Kanisa, pamoja na muundo wa kiroho na maadili wa jamii. Na kama alivyo na uhakika wanafahamu, shirika lao limesaidia misheni nyingi nchini Peru, pamoja na Jimbo la Chiclayo, mhali ambapo  "nilipata fursa ya kuhudumu. "                                                   

Usaidizi wao vivyo hivyo huwasaidia Wakristo, hata walio wachache na walio katika mazingira magumu, kuwa “wapatanishi” (Mt 5:9) katika nchi zao. Katika nchi kama vile Jamhuri ya Afrika ya Kati, Burkina Faso na Msumbiji, Kanisa mahalia, mara nyingi likidumishwa na usaidizi wao na kuwa ishara hai ya maelewano ya kijamii na udugu, likiwaonesha majirani zao kwamba ulimwengu tofauti unawezekana (taz. Malaika wa Bwana 3 Agosti 2025). Papa Leo XIV aliwashukuru kila mmoja wao  kwa kazi hiyo ya mshikamano. "Msichoke kutenda mema (taz. Gal 6:9), kwa maana utumishi wenu huzaa matunda katika maisha yasiyohesabika na kumtukuza Baba yetu aliye mbinguni." Kwa kuhitimisha, Papa aliwaombea na wote wanaowahudumia,  faraja ya Roho Mtakatifu.  Bikira Maria, Mama wa Matumaini, akae karibu nao na wote wanaoteseka. Kwa mapenzi mazito,  na alitoa Baraka yake ya Kitume kama ahadi ya neema na amani katika Yesu Kristo Bwana wetu.

Papa na Kanisa Hitaji

Asante sana kusoma makala hii. Kama unataka kubaki na sasisho, tunakualika kujiandikisha hapa ili kupata habari za kila siku: cliccando qui

10 Oktoba 2025, 12:29