Tafuta

Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 28 Mwaka C wa Kanisa: Rudi kwa imani na unyenyekevu kumshukuru Mungu kwa wema na ukarimu wake. Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 28 Mwaka C wa Kanisa: Rudi kwa imani na unyenyekevu kumshukuru Mungu kwa wema na ukarimu wake.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Tafakari Dominika ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa: Neema na Baraka Si Haki! Moyo wa Shukrani

Dominika ya leo inatukumbusha kurudi, kumwambia Mungu asante. Inatukumbusha pia kutochukulia baraka hizi za Mungu kama haki yetu, bali ni ukarimu tu wa Mungu, anayetupa bila hata mastahili yetu. Rudi, kwa imani na unyenyekevu mkubwa, mwambie Mungu asante. Tumwombe Mungu msamaha mara zote tulizosahau kumshukuru inavyostahili, kwa baraka nyingi anazotujalia kila siku ya maisha yetu. Falsafa ya neno Asante ni kuomba tena neema na baraka!

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya 28 ya mwaka C wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatukumbusha, “kurudi na kumshukuru Mungu” kwani Mwenyezi Mungu kwa nyakati mbalimbali na kwa namna nyingi, ametubariki katika mengi. Tumesali mara nyingi, kwa ajili ya mahitaji yetu mbalimbali, mahitaji ya kiroho na kimwili. Kuna nyakati hata tumeweka ahadi kwa Mungu kwamba, Mungu ukinijibu katika hili nitakutumikia kwa moyo wangu wote, Mungu wangu ukiniponya katika hili sitakusahau kamwe, Mungu wangu ukiniinua katika hili sitawasahau wengine, Mungu wangu ukiniwezesha katika hili sitaacha kukushukuru. Huwa kila mmoja wetu anasema hivi au amewahi kusema hivi kwa wakati wake. Anapotubariki tunasahau kurudi na kumshukuru, anapotuponya tunasahau kumrudishia Mungu sifa na utukufu. Swali analotuuliza Kristo katika dominika hii ni kwamba, “Hawakutakaswa wale kumi? Wale kenda wa wepi? Je, hawakuonekana waliorudi kumpa Mungu utukufu ila mgeni huyu?” Kumbe, Dominika ya leo inatukumbusha kurudi, kumwambia Mungu asante. Inatukumbusha pia kutochukulia baraka hizi za Mungu kama haki yetu, bali ni ukarimu tu wa Mungu, anayetupa bila hata mastahili yetu. Rudi, kwa imani na unyenyekevu mkubwa, mwambie Mungu asante. Tumwombe Mungu msamaha mara zote tulizosahau kumshukuru inavyostahili, kwa baraka nyingi anazotujalia kila siku ya maisha yetu.

Papa Francisko akiwashukuru madaktari na wauguzi waliomhudumia
Papa Francisko akiwashukuru madaktari na wauguzi waliomhudumia   (ANSA)

Somo la Kwanza: Ni kitabu cha 2 Fal 5:14-17. Somo la kwanza ni kutoka Kitabu cha Pili cha Wafalme. Somo hili linaeleza tukio la uponywaji wa Naamani chini ya Nabii Elisha. Naamani tunaambiwa alikuwa ni Jemedari wa jeshi la mfalme wa Shamu na hivyo hakuwa Mwisraeli. Naamani alipatwa na ugonjwa mbaya sana wa ukoma. Aliposikia habari juu ya Mungu wa Israeli anaamua kufunga safari hadi kwa Nabii Elisha. Nabii Elisha anamwamuru akaoge mara saba katika mto Yordani naye akapona. Baada ya uponywaji huu, Naamani alirudi kumshukuru Mungu. Anakiri kwamba Mungu wa Israeli ana wema na nguvu za kipekee kuliko miungu ya nchi yake. Kwa hiyo alitaka kumshukuru Mungu kwa kumjengea madhabahu kwa kutumia udongo wa nchi ya Israeli. Imani yake imemponya, na anaona hitaji la kurudi kumwambia Mungu asante. Zaburi ya 98:1-4: Katika Zaburi hii ya 98:1-4, Mzaburi anatualika kumshukuru Mungu, kwa uaminifu, kwa matendo yake makuu ya ajabu katika maisha yetu. Anakiri nguvu na uweza wa Mungu anayedhihirisha Matendo yake makuu kwetu katika nyakati mbalimbali. Anakiri wokovu, matendo hayo makuu yanatoka kwa Mungu pekee, si kwa nguvu za kibinadamu.  Anatualika kumshukuru daima Mungu wetu.

Ukoma ni ugonjwa mbaya sana katika maisha ya mwanadamu
Ukoma ni ugonjwa mbaya sana katika maisha ya mwanadamu   (2025 Getty Images)

Somo la Injili: Ni Injili ya Lk. 17:11-19: Katika somo la Injili Takatifu tumesikia muujiza wa kuponywa kwa wakoma kumi. Tisa kati ya hawa walikua ni Wayahudi na mmoja alikua ni Msamaria, mtu wa mataifa. Tukumbuke kuwa ugonjwa wa ukoma ulikua ni ugonjwa mbaya, wa kuogofya, ugonjwa wa fedheha na aibu ambapo wale wote ambao walioupata walihesabika kuwa najisi na hivyo walipaswa kutengwa kabisa na jamii ili wasiwaambukize wengine (Kut 19:6). Yesu alipowasikia aliwahurumia na akawaambia wakajioneshe kwa Makuhani na walipokuwa wanaenda wakatakasika wote kumi.  Kati ya wakoma wale kumi walioponywa, ni mmoja tu, yule Msamaria anayekumbuka kurudi na kumwambia Mungu asante. Simulizi hili linafanana na lile tulilosikia katika somo la kwanza kwamba, anayerudi kutoa shukrani kwa Mungu baada ya kuponywa ukoma wake kati ya wale kumi sio Myahudi bali ni Msamaria, mtu wa mataifa. Wale Wayahudi walifikiri ni haki yao, walifikiri walistahili kwa kuwa wao ni taifa teule, hawakuona haja ya kushukuru. Ndugu zangu katika Masomo haya mawili tuna mafundisho matano ya kujifunza. Kwanza: Kutambua kuwa mimi ni mkoma. Naamani, licha ya kuwa alikuwa mtu mkubwa, mwenye heshima na mamlaka alitambua kuwa alikua ni mkoma. Anatambua kuwa alipungukiwa kitu kikubwa na alihitaji uponyaji (2 Fal 5:1-2), ujemedari wake haukufaa kitu, nguvu zake hazikufaa kitu, mamlaka yake haikufaa kitu, anakua mpole, anatambua udhaifu ulio ndani mwake. Hali kadhalika na wale wakoma kumi walitambua kuwa walikua wakoma na walihitaji rehema kutoka kwa Yesu ndio maana walipomwona Yesu walipaza sauti zao kumwomba awaponye (Lk 17:13-14). Wanasahau tofauti zao zote, wanaelekeza nguvu zao kumwita Kristo ili awaponye, awatoe katika fedheha ile.

Hawakutakaswa wale kenda?
Hawakutakaswa wale kenda?   (2025 Getty Images)

Ndugu wapendwa, hatua ya kwanza ya kupokea uponyaji kutoka kwa Mungu ni kutambua kuwa mimi ni dhaifu, mimi ni mkoma. Kutambua kuwa nimepungukiwa kitu ndani mwangu. Naamani alitambua fedheha iliyokuwa inakwenda kumpata kutokana na ugonjwa ule mbaya wa ukoma. Alijitahidi kuficha, na kutafuta suluhisho kwa mali na uwezo aliokuwa nao lakini hakufanikiwa kupona. Anatambua, licha ya kwamba alikua na vyote, bado alihitaji Mkono wa Mungu. Ndugu mpendwa, tunaweza kuwaza ukoma kwa maana ya ugonjwa, lakini kila mmoja wetu ana kitu kikubwa anakosa, ana madhaifu yake mbalimbali ambayo kimsingi yanamrudisha nyuma katika kupiga hatua fulani, katika maendeleo yetu ya kimwili na kiroho. Yaweza kuwa; Ukoma wa kutokuwajibika: Mara kadhaa ninashindwa kuwajibika vyema vile ninavyopaswa katika nafasi yangu, katika familia, katika jamii na katika Kanisa. Huenda nimeshindwa kutimiza malengo mbalimbali niliyojiwekea kwa sababu ya udhaifu wangu wa kutokuwajibika vile inipasavyo. Huu ni ukoma wangu, huenda unanimaliza taratibu katika kufikia pale Mungu alitaka nifike, katika kuifikisha familia yangu pale Mungu alitaka niifikishe, katika kulifikisha taifa letu pale Mungu alitaka tulifikishe. Ninasali na kumwomba Mungu atende kitu lakini mimi siwajibiki vile ninavyopaswa. Ninapotambua, udhaifu huu na kuufanyia kazi ni hatua ya kwanza ya uponyaji.

Hatua ya kwanza ya uponyaji ni kutambua udhaifu wako!
Hatua ya kwanza ya uponyaji ni kutambua udhaifu wako!   (2025 Getty Images)

Ukoma wa kukata tamaa na kuwakatisha tamaa wengine: Huenda katika maisha yangu nimekua mtu wa kukata tamaa, kupoteza kabisa matumaini kwamba kesho yangu yaweza kuwa njema. Nashindwa kupiga hatua kwa kuwa sioni tumaini la kesho. Kukata tamaa kunafifisha mpango wa Mungu ndani mwangu. Lakini kuna wakati pia nimekuwa mtu wa kuwakatisha wengine tamaa tu, katika mapambano yao na katika jitihada zao. Matokeo yake tunawarudisha wengine nyuma na kuwapoteza kabisa katika matumaini na imani yao. Huu ni ukoma kwa kuwa unafifisha ndoto zangu za wengine kufika pale Mungu alikusudia wafike. Huenda neno langu moja la kutia moyo lingemtoa mtu kutoka hatua moja kwenda nyingine, huenda neno langu moja limeua kabisa ndoto za watu wengine. Ukoma wa wivu, vinyongo na visasi, Mara kwa mara nimekuwa mtu mwenye wivu, kuona uchungu juu ya baraka za Mungu kwa wengine. Kuona uchungu pale Mungu anapowainua na kuwabariki wengine kuliko mimi. Nimekuwa mtu wa vinyongo ninayetamani kulipiza kisasi kwa wale ambao nyakati fulani waliniumiza, walionikwaza, walionitendea mabaya. Huenda ninasali kwa ajili ya mabaya na maanguko yao. Tunapofungia moyoni mwetu vinyongo, wivu, chuki, hasira na roho ya kulipiza visasi, tunakufa ndani kwa ndani kama vile ukoma unavyokula taratibu kiungo kimoja baada ya kingine. Tunajivika mbawa nzito zinazotuzuia kuruka kuziendea baraka za Mungu. Jifunze kuachilia, jifunze kuruhusu yapite. Acha moyo wako ukiwa na afya.

Kuna ukoma wa kupenda anasa na starehe
Kuna ukoma wa kupenda anasa na starehe   (AFP or licensors)

Ukoma wa anasa na starehe za dunia: Mwenyezi Mungu anatubariki katika mengi, lakini starehe, anasa zinatuangusha. Huenda mara nyingi nimetumia vibaya baraka za Mungu, kwa anasa, ulevi, starehe, na hivi vyote vinanikwamisha kutimiza kusudio la Mungu katika maisha yangu na kwa ajili ya wengine kupitia mimi. Sikumbuki familia, sikumbuki mipango ya maendeleo, sikumbuki kuweka akiba, sikumbuki kusaidia wengine. Huu ni ukoma. Yesu niguse leo, nitumie vyema baraka unazonijalia. Ukoma wa uzembe Uregevu wa moyo: Mara kadhaa nimekua mzito katika mambo ya kiroho, kutokupokea Sakramenti, kutoshiriki mambo ya Kanisa, kutosoma na kutafakari Neno la Mungu, kukosa muda wa kusali na kukaa na Yesu. Haya yote yamenitenga mbali na Mungu na nimeshindwa kujenga urafiki wa karibu naye. Umbali wangu na Mungu. Mara kadhaa nimekua mtu wa kuahirisha sana mambo, nitafanya kesho. Kuungama, nitaungama kesho, kufunga ndoa, tutafunga kesho, kuhudhuria ibada za misa, nitakwenda kesho. Huu ni ugonjwa wa kufikiri kwamba, bado nina muda mwingi na kusahau kuwa muda ni sasa, na wokovu ni leo hii. Ukoma wa Lawama: Huenda katika maisha yangu nimekuwa mtu wa kulalamika na kulaumu mara nyingi zaidi kuliko kushukuru. Kulaumu ni ishara ya ukosefu wa shukrani kwa Mungu, kushindwa kukaa na kutafakari na kuona ni wapi Mungu amenitoa hata sasa, ni mema mangapi Mungu amenitendea bila hata mastahili yangu. Tunaposhukuru tunaomba tena na tutapokea tena. Tunapolaumu na kulalamika tu tunapoteza baraka za Mungu, hata kwa yale machache aliyotubariki.

Kuna ukoma wa uchoyo na ubinafsi
Kuna ukoma wa uchoyo na ubinafsi

Ukoma wa uchoyo: Mungu alinibariki kwa mambo mengi, kwa vipaji na karama mbalimbali, biashara nzuri, ajira nzuri, amani na utulivu katika ndoa, katika mahusiano au katika familia yako, upendo na furaha nk. Katika hayo yote, tuwe baraka pia kwa wengine. Tutumie baraka za Mungu kuwainua wengine, kuwasadia maskini, kuwagusa wengine majeraha yao, kuwaponya wengine katika shida zao. Ninaposhikila baraka za Mungu ilihali alinipa hayo yote ili niwe njia ya kuwafikishia wengine, huo ni ugonjwa mbaya. Pili: Kumwendea mtu sahihi ili tupate uponyaji wa kweli. Naamani alipotambua kuwa alikua ni mkoma, hakuwaza kwenda kwa waganga wa kienyeji, hakuwaza kwenda kwa manabii wa uwongo waliokuwa wengi wakati ule wala kwa watenda miujiza waliojiinua bali, baada ya kuambiwa habari juu ya mtu wa Mungu aliyekuwepo Samaria, yeye hakusita kumwendea ili apate uponyaji (2 Fal 5:3-4). Hali kadhalika wakoma hawa kumi wanafahamu mtu sahihi ambaye angeweza kuwaponya na wanamwita Yesu ili awarehemu (Lk 17:13-14. Ndugu wapendwa, huenda tunasumbuka sana na vilema, madhaifu na changamoto mbalimbali tunazopitia katika maisha yetu ya kila siku. Ni dhahiri kwamba kuna mambo mengi na magumu tunakutana nayo, ya kutisha, ya kukatisha tamaa na ya kuumiza. Je, tunafunga safari kwenda wapi? Katika hayo yote ni wazi pia katika hali yetu ya kibinadamu kuna nyakati tunatafuta majibu ya gharama kubwa. Tunadharau nguvu ya sala, nguvu ya imani ndogo hata kama punji ya haradali iliyo ndani mwetu. Tunatafuta majibu ya haraka na kusahau kwamba Mungu anajibu sala zetu kwa wakati wake. Ndugu zangu, suluhisho sahihi la changamoto zetu tutalipata iwapo tu tutakua tayari kumwendea mtu sahihi na huyu si mwingine ni Bwana wetu Yesu Kristo. Yesu amezaliwa katikati yetu ili kutuletea uponyaji wa kweli wa madhaifu na changamoto zetu mbalimbali ambazo tunakutana nazo. Naamani alitambua kuwa Mungu wa Israeli ana nguvu na uweza. Hali kadhalika wakoma kumi walitambua nguvu ya Kristo. Uponyaji huu wa Naamani na wakoma kumi unatukumbusha kuwa, Mungu ana uwezo na nguvu ya kuyabadili yote na kuwa mapya kabisa, ana uwezo wa kubadili huzuni zetu kuwa furaha kubwa, ana uwezo wa kubadili unyonge wetu kuwa ujasiri na nguvu, ana uwezo wa kubadili maanguko yetu kuwa hatua kuelekea ushindi mkubwa, ana uwezo wa kubadili kabisa historia yetu.

Falsafa ya Neno Asante ni kuomba tena!
Falsafa ya Neno Asante ni kuomba tena!   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Tatu: Ili tupokee uponyaji tunahitaji, Imani, Unyenyekevu na utii kwa Neno la Mungu. Katika simulizi la uponyaji wa Naamani, tumeona namna alivyotii maagizo aliyopewa na Nabii Elisha. Hayakuwa maagizo magumu, ni maagizo ya kawaida, rahisi kabisa ambayo hata Naamani mwenyewe alitaka kuyapuuza. Anapofuata maagizo kadiri ya Neno la Elisha ambalo kimsingi ni Neno la Mungu, Naamani anatakasika, anapona kabisa ukoma wake (2 Fal 5:14-15). Wakoma kumi hali kadhalika waliambiwa na Yesu waende kujionesha kwa makuhani na walipokua njiani wakatakasika (Lk 17:14). Katika matukio haya mawili, hawakudaiwa chochote, hawakudaiwa fedha wala dhahabu, hawakupewa sharti lolote gumu, walihitaji imani, utii na unyenyekevu. Ndugu wapendwa, ikiwa tunataka kupata uponyaji wa kweli hatuna budi kuwa na imani ambayo kimsingi inaambatana na utii na unyenyekevu. Yesu anawaagiza wakoma kwenda kujionesha kwa makuhani na wakiwa njiani wanaponywa. Hali kadhalika Eliya anamwagiza Naamani kwenda kujichovya katika Yordani, akiisha kufanya hivyo anatakasika. Maagizo haya ni kipimo cha utii, unyenyekevu wao ili kupata uponyaji. Ndugu mpendwa Kristo Yesu anazungumza nasi kwa namna za kawaida kabisa. Anatubariki kwa namna mbalimbali hata ambazo hatuwezi kufahamu. Wakati mwingine Mungu amebeba baraka zako kupitia watu wa kawaida kabisa ambao huwezi hata kutarajia. Amebeba baraka zako kupitia watu wadogo, huenda maskini tu hata wasio na umuhimu. Mungu anaweza kubeba baraka zako kupitia mtu ambaye umekataa kabisa kumsamehe, umemfungia vioo. Naamani hakutarajia kama binti yule mdogo angeweza kumwelekeza kumwendea Mtu wa Mungu. Nabii Elisha hali kadhalika hakutambulika sana katika nyumba ya mfalme, hakua mtu mkubwa. Kristo Yesu anakuja kwetu katika hali hiyo hiyo, hali ya udogo na unyenyekevu, akitutaka nasi pia tumpokee katika hali hiyo hiyo ya unyenyekevu na utii mkubwa. Maagizo yake si magumu, anatuambia yeye nira yake ni laini na mzigo wake ni mwepesi. Tuwe wanyenyekevu, kwa imani tutembee katika Neno la Kristo, naye atatupa uponyaji wa kweli. Naamani alitembea katika Neno la Elisha, wakoma walitembea katika Neno la Kristo nao wakapata uponyaji. Mungu anafanya kazi kwa wale walio wanyofu wa moyo na watii. Mungu akufungue moyo na akili yako, ukawe mtii kwa Neno lake, ili ukapate uponyaji. Nyenyekea, tii ili ukutane na muujiza wa Mungu. Mlango una kufuli si kwa lengo la kutufungia nje, bali ili tuwe na funguo sahihi na tuweze kuufungua. Funguo sahihi ya kufungua baraka za Mungu kwetu ni imani, utii na unyeyekevu. Matokeo yake ni baraka na uzima.

Uponyaji unakita mizizi yake katika:Imani, Unyenyekevu na Utii
Uponyaji unakita mizizi yake katika:Imani, Unyenyekevu na Utii   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Nne: Kuwa mtu wa shukrani kwa mema mengi anayokutendea Mungu. Naamani baada ya kupokea uponyaji kutoka kwa Mungu anarudi na kumwambia Mungu asante. Anatambua ya kuwa si kwa nguvu wala uwezo wake, wala si kwa mastahili yake anapokea uponyaji bali Mungu ndiye aliyetenda hayo kupitia kwa mtumishi wake Elisha. Anarudi na kumwambia Mungu, asante (2Fal 5:15-16). Anakiri kwamba hakuna Mungu ila Mungu wa Israeli. Anakiri kuwa uponyaji wake si matokeo ya ujanja ujanja na nguvu zake bali ni Mungu. Mkoma mmoja Msamaria kati ya wakoma kumi hali kadhalika ndiye aliyerudi kumpa Mungu sifa na utukufu lakini wengine tisa walidhani ili kua ni haki yao na kwamba walistahili, walikosa moyo wa shukrani kwa Yesu (Lk 17:17-18). Ndugu wapendwa, kila mmoja akitazama kwa kina tangu Januari mpaka sasa anaona ana kila sababu ya kumwambia Mungu, asante. Tunapomwambia Mungu asante tunatambua na kukiri kwamba vyote tulivyo navyo vimetoka kwake, sio matokeo ya nguvu zetu na juhudi zetu, bali ni Mungu tu. Mara kadhaa tumekuwa tukisali na kuomba kwa ajili ya nia zetu mbalimbali. Mara nyingine tunaweka mpaka ahadi kwa Mungu kwamba, Mungu ukinibariki katika katika nia yangu hii, sitaacha kamwe kukushukuru. Ukinibariki nikipata hii kazi, sitaacha kukutolewa sadaka ya shukrani. Ukiniponya katika maradhi haya, Mungu wangu sitakuacha kamwe. Ukiwabariki watoto wangu, Mungu nitakutukuza milele. Ukinitoa katika mtihani huu mgumu Mungu wangu nitakushukuru milele na milele. Shida na changamoto zinatukumbusha kuwa Mungu ana nafasi, Mungu ana nguvu. Lakini Mungu anapotutendea huenda tunasahau. Anakuuliza leo, upo wapi? Haukutakaswa nawe pia? Je, hukuonekana kumpa Mungu utukufu na shukrani? Rudi, mwambie Mungu ninatimiza ahadi yangu kwako. Ulinipa afya mwezi mzima huu, nakushukuru, nakurudishia sifa, shukrani na utukufu, nipe afya tena kwa mwezi ujao. Hivyo hivyo kwa mambo mengine yote, yawe mazuri yawe mabaya, shukuru Mungu.  Mara nyingi tunakumbushwa wajibu wetu huu wa kurudi na kumshukuru Mungu. Mara ngapi nimekua mgumu kutoa zaka, kumshukuru Mungu kwa baraka zake kwa mwezi mzima, mpaka nikumbushwe kwa semina na msisitizo mkubwa? Zaka inatoka kwa masharti makubwa, wakati wema wa Mungu amenipa bure kabisa. Rudi, mwambie Mungu nimekuja kusema asante. Ninaomba endelea kunibariki tena. Endelea kufungua milango ya baraka kwa ajili yangu na familia yangu. Kristo atatubariki zaidi.

Waamini wawe ni mashuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu
Waamini wawe ni mashuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu   (@Vatican Media)

Tano: Tuwalete wengine kwa Kristo ili wapate uponyaji. Katika somo la kwanza tumesikia huyu mtumwa mmoja kijana mwanamke kutoka Israeli aliyekuwa akimhudumia mkewe Naamani anamsaidia Naamani kupelekwa kwa Elisha ili apate uponyaji. Anasema, “Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule Nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake” (2 Fal 5:3-4). Anamsaidia Naamani kuendea uponyaji. Ndugu wapendwa, maisha yetu ya kila siku wapo wengi kati yetu ambao wamesaidia wengine kutambua udhaifu wao na kuendea tiba sahihi ya kiroho na kimwili. Wapo walioona wenzao wakikata tamaa, katika familia, katika kazi, katika wito na wakasema kama huyu mtumwa kwamba, “Laiti mume wangu, au mke wangu, au watoto wangu, au jirani zangu, au padre mwenzangu, au mtawa mwenzangu, au mwanajumuiya mwenzetu, angekuwa pamoja na yule Nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake” Tumewasaidiaje wenzetu kuendea uponyaji? Au nimemwagizia kwenda kwa Mitume na manabii, kwenda kwa waganga wa kienyeji ilihali najua kabisa tiba ya kweli ipo kwa Yesu? Je, nimewashauri na kuwashawishi watu mara ngapi katika mwaka huu kwenda kukanyaga mafuta na kunywa maji ya upako badala ya kuwaleta kwa Yesu Ekaristi? Tumwombe Yesu atupe nguvu ya kuwaleta wenzetu kwa Yesu ili wapate uponyaji sahihi. Baraka za Mungu zinatolewa bure kabisa, Nabii Eliya anatuthibitishia hilo kwa kukataa kupokea fedha kutoka kwa Naamani. Ametupa neema na baraka zake zote bure ili zitufae kuupata uzima wa milele.

Uvumilivu katika mateso, mahangaiko na madhulumu
Uvumilivu katika mateso, mahangaiko na madhulumu

Somo la Pili: Ni Waraka wa Mtume Paulo kwa Timotheo 2:8-13: Katika somo hili la pili, Mtume Paulo anatufundisha mambo makubwa matatu. Jambo la kwanza, Tushukuru katika hali zote. Yeye anamshukuru Mungu sio kwa mafanikio tu, bali anamshukuru Mungu hata kwa changamoto alizokutana nazo katika kazi yake ya Injili. Kumbe, nyakati za mateso zipo, ndio gharama ya ufuasi wetu, lakini katika hayo yote tumtazame Kristo. Jambo la pili: anatukumbusha nguvu ya Neno la Mungu, kwamba mambo mengine yaweza kufungwa lakini Neno la Mungu lina nguvu, halifungwi na mtu, halifungwi na hali, halifungwi na nyakati. Tuwe watii kwa Neno hilo kwa kuwa linatunenea daima baraka, halirudi bure iwapo tunalitii na kuwa wanyenyekevu katika kulisikiliza na kuliishi. Jambo la mwisho, Paulo anampa matumaini Timotheo kwamba, awe mvumilivu kwa kuwa mateso na changamoto haziwezi kuondoa lengo na dhumuni la Mungu la ukombozi juu yetu.  Hitimisho: Dominika ya Ishirini na Nane ya Mwaka C wa Kanisa inatukumbusha kurudi, kumwambia Mungu asante. Inatukumbusha pia kutochukulia baraka hizi za Mungu kama haki yetu, bali ni ukarimu tu wa Mungu, anayetupa bila hata mastahili yetu. Rudi, kwa Imani na unyenyekevu mkubwa, mwambie Mungu asante. Tumwombe Mungu msamaha mara zote tulizosahau kumshukuru inavyostahili, kwa baraka nyingi anazotujalia kila siku ya maisha yetu.

Tafakari D28
11 Oktoba 2025, 08:13