Ujumbe wa Baba Mtakatifu Kwa Maadhimisho ya Dominika ya 99 ya Umisionari Ulimwenguni
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Dar Es Salaam, Tanzania
Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake anasema, katika Dominika hii kila mwaka, Kanisa zima linaungana katika kusali kuombea Wamisionari na matunda ya kazi yao ya kitume wanayoifanya kwa nguvu na majitoleo makubwa ulimwenguni kote. Anaeleza uzoefu wake akiwa Padre na baadaye Askofu Mmisionari huko Peru katika Amerika ya Kusini, jinsi sala na matendo ya huruma yanayofanyika katika Dominika hii yanavyochangia kuleta mabadiliko makubwa katika kazi ya Uinjilishaji. Sala na michango mbalimbali imechangia kwa kiasi kikubwa katika programu mbalimbali za Katekesi, Ujenzi wa Makanisa na huduma za kijamii kama vile, Elimu, Afya, majanga ya asili na misaada kwa maskini. Hivyo anaomba Parokia Katoliki Ulimwenguni kote kushiriki kwa hali na mali katika kazi hii ya Umisionari, kumpeleka Kristo tumaini letu kati ya watu, tukitambua kuwa kila mbatizwa ni Mmisionari wa Matumaini.Ndugu wapendwa! Kwa Maadhimisho ya Dominika ya 99 ya Kimisionari Ulimwenguni katika Mwaka wa Jubilei ya 2025, ujumbe mkuu ni matumaini (taz. Bull Spes Non Confundit, 1), nimechagua kauli mbiu: "Wamisionari wa Matumaini kwa Watu Wote." Inawakumbusha Wakristo binafsi na Kanisa zima, jumuiya ya wabatizwa, juu ya wito wetu wa msingi wa kuwa, katika nyayo za Kristo, wajumbe na wajenzi wa matumaini. Ninatumaini kwamba itakuwa kwa kila mtu wakati wa neema pamoja na Mungu mwaminifu ambaye ametuzaa upya katika Kristo mfufuka “kwa tumaini lililo hai” (rej. 1 Pet 1:3-4). Hapa, ningependa kutaja baadhi ya vipengele vinavyohusika vya utambulisho wetu wa Kikristo wa kimisionari, ili tuweze kujiachia kuongozwa na Roho wa Mungu na kuwaka kwa bidii takatifu kwa ajili ya msimu mpya wa uinjilishaji katika Kanisa, ambao unatumwa kufufua matumaini katika ulimwengu ambao vivuli vya giza vinatanda (taz. Fratelli Tutti, 9-55).
Katika nyayo za Kristo tumaini letu: Kuadhimisha Jubilei ya kwanza ya Kawaida ya Milenia ya Tatu baada ya ile ya Mwaka Mtakatifu wa 2000, tunamkazia Kristo macho yetu, kitovu cha historia, "ambaye ni yeye yule jana na leo na hata milele" (Ebr 13:8). Katika sinagogi la Nazareti, Yesu alitangaza kwamba Maandiko yalitimizwa katika “leo” ya uwapo wake katika historia. Hivyo alidhihirisha kwamba yeye ndiye aliyetumwa na Baba kwa mpako wa Roho Mtakatifu kutangaza Habari Njema ya Ufalme wa Mungu na kuzindua “mwaka wa Bwana uliokubaliwa” kwa ajili ya wanadamu wote” (rej. Lk 4:16-21). Katika “leo” hii ya fumbo, itakayodumu hadi mwisho wa dunia, Kristo ndiye utimilifu wa wokovu kwa wote, na kwa namna ya pekee kwa wale ambao tumaini lao pekee ni Mungu. Katika maisha yake hapa duniani, “alizunguka huko na huko, akitenda mema na kuponya wote” kutoka kwa waovu na yule Mwovu (rej. Mdo 10:38), akirudisha tumaini kwa Mungu kwa wahitaji na watu. Alipitia udhaifu wetu wote wa kibinadamu, isipokuwa ule wa dhambi, hata nyakati zile ngumu ambazo zingeweza kusababisha kukata tamaa, kama vile katika uchungu katika bustani ya Gethsemane na Msalabani. Yesu alitoa kila kitu kwa Mungu Baba, kwa utiifu akitumaini mpango wake wa kuokoa wanadamu, mpango wa amani kwa ajili ya wakati ujao uliojaa tumaini (rej. Yer 29:11). Kwa njia hii, akawa Mmisionari wa kimungu wa matumaini, kielelezo kikuu cha wale wote katika karne zote ambao wanatekeleza utume wao wenyewe waliopewa na Mungu, hata katikati ya majaribu makali.
Kupitia wanafunzi wake, waliotumwa kwa watu wote na kuandamana naye kwa namna ya fumbo, Bwana Yesu anaendelea na huduma yake ya matumaini kwa wanadamu. Bado anawainamia wale wote walio maskini, wanaoteseka, waliokata tamaa na walioonewa, na kuwamwagia “kwenye majeraha yao mafuta ya faraja na divai ya matumaini” (Utangulizi “Yesu Msamaria Mwema”.) Kwa utii kwa Bwana na Mwalimu wake, na katika roho ile ile ya huduma, Kanisa, jumuiya ya wanafunzi wamisionari wa Kristo, linaendeleza utume huo, likitoa maisha yake kwa ajili ya wote katikati ya mataifa. Huku likikabiliwa na mateso, dhiki na matatizo, pamoja na kutokamilika na kushindwa kwake kutokana na udhaifu wa washiriki wake, Kanisa daima linasukumwa na upendo wa Kristo kudumu, katika muungano naye, katika safari yake ya umisionari na kusikia, kama yeye na pamoja naye, kilio cha wanadamu wanaoteseka na, kwa hakika, kuugua kwa kila kiumbe kinachongojea utimilifu wa ukombozi. Hili ndilo Kanisa ambalo Bwana daima na milele analiita kufuata nyayo zake: “si Kanisa linalosimama, bali ni Kanisa la kimisionari linalotembea na Bwana wake katika mitaa ya ulimwengu” (Homilia katika Misa ya Kuhitimisha Mkutano Mkuu wa Kawaida wa Sinodi ya Maaskofu, 27 Oktoba 2024). Na sisi pia tujisikie kuvutiwa kushika njia tukizifuata nyayo za Bwana Yesu ili tuwe, pamoja naye na ndani yake, ishara na wajumbe wa matumaini kwa wote, katika kila mahali na hali ambayo Mungu ametujalia kuishi. Na wote waliobatizwa, wakiwa wanafunzi wamisionari wa Kristo, wafanye tumaini lake ling’ae katika kila pembe ya dunia!
Wakristo, wabebaji na wajenzi wa matumaini kati ya watu wote: Katika kumfuasa Kristo Bwana, Wakristo wanaalikwa kukabidhi Habari Njema kwa kushiriki hali halisi za maisha ya wale wanaokutana nao, na hivyo kuwa wabebaji na wajenzi wa matumaini. Hakika, "furaha na matumaini, huzuni na uchungu wa watu wa wakati wetu, hasa wale ambao ni maskini au wanaoteseka, ni furaha na matumaini, huzuni na uchungu wa wafuasi wa Kristo pia. Hakuna kitu chochote ambacho ni cha kibinadamu kweli kinachoshindwa kupata mwangwi ndani ya mioyo yao" (Gaudium et spes 1). Tamko hili adhimu la Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican linalodhihirisha hisia na mtindo wa Jumuiya za Kikristo katika kila zama, linaendelea kuwatia moyo washiriki wao na kuwasaidia kuambatana na ndugu zao duniani. Hapa ninawafikiria miongoni mwenu hasa wale ambao ni wamisionari kwa watu wa Mataifa (Ad gentes). Kufuatia wito wa Bwana, mmeenda kwa mataifa mengine ili kuudhihirisha upendo wa Mungu katika Kristo. Kwa hili, ninawashukuru kwa moyo wote! Maisha yenu ni mwitikio wa wazi kwa agizo la Kristo mfufuka, ambaye aliwatuma wanafunzi wake kuinjilisha mataifa yote (rej. Mt 28:18-20). Kwa njia hii, ninyi ni ishara za wito wa kiulimwengu wa waliobatizwa kuwa, kwa uwezo wa Roho na juhudi za kila siku, wamisionari kati ya watu wote na mashahidi wa tumaini kuu tulilopewa na Bwana Yesu.
Upeo wa tumaini hili unapita mambo yapitayo ya ulimwengu huu na kufungua njia kwa kweli za kimungu ambazo tunashiriki hata sasa. Kwa hakika, kama Mtakatifu Paulo VI alivyoona, wokovu katika Kristo, ambao Kanisa hutoa kwa wote kama zawadi ya huruma ya Mungu, sio tu "wa ndani, unaokidhi mahitaji ya kimwili au hata ya kiroho... umeshikwa kabisa na tamaa, matumaini, masuala na mapambano ya kidunia. Badala yake, unavuka mipaka hiyo yote ili kufikia utimilifu katika ushirika na mmoja aliye Mkuu, ambaye ni Mungu. Ni ukombozi ambao ni wa upeo wa juu sana na wa milele, ambao hakika una mwanzo wake katika maisha haya, lakini hutimilizwa katika umilele” (Evangelii nuntiandi, 27.) Kwa kuchochewa na tumaini hili kuu, jumuiya za Kikristo zinaweza kuwa vielelezo vya ubinadamu mpya katika ulimwengu ambao, katika maeneo "yaliyoendelea" zaidi, huonesha dalili hatarishi za mahangaiko makubwa ya mwanadamu: hisia iliyoenea ya kuchanganyikiwa, upweke na kutojali mahitaji ya wazee, na kusita kufanya jitihada za kuwasaidia jirani zetu wenye mahitaji. Katika mataifa yaliyoendelea zaidi kiteknolojia, "ukaribu" unatoweka: sote tumeunganishwa, lakini hatuhusiani. Kuzingatia sana ufanisi na kushikamana na vitu vya kidunia na matamanio vinatufanya tuwe wabinafsi na kushindwa kuwa wakarimu kwa wengine. Injili, iliyogusa maisha ya jumuiya, inaweza kuturudisha katika ubinadamu mzima, wenye afya na uliokombolewa.
Kwa sababu hii, kwa mara nyingine tena ninamualika kila mmoja wetu kutekeleza kazi zilizotajwa katika “Bolla - Bull of Indiction of the Jubilee” (Na. 7-15), tukiwa makini hasa kwa walio maskini na dhaifu zaidi, wagonjwa, wazee na wale waliotengwa na jamii inayothamini zaidi mali na utumiaji. Na kufanya hivyo kwa "mtindo" wa Mungu: kwa ukaribu, rehema na huruma, kukuza uhusiano binafsi na kaka na dada zetu katika hali zao halisi (taz. Evangelii gaudium, 127-128). Mara nyingi wao ndio wanaotufundisha jinsi ya kuishi katika matumaini. Kupitia mawasiliano binafsi, tutaeneza pia upendo wa moyo wa Bwana wenye huruma. Tutatambua kwamba “moyo wa Kristo... ndio kiini hasa cha utangazaji wa awali wa Injili” (Dilexit nos, 32). Kwa kuchota kutoka katika chanzo hiki, tunaweza kutoa kwa urahisi tumaini tulilopokea kutoka kwa Mungu (rej. 1 Pet 1:21) na kuwaletea wengine faraja ile ile ambayo tumefarijiwa nayo na Mungu (taz. 2Kor 1:3-4). Katika moyo wa kibinadamu na wa kimungu wa Yesu, Mungu anataka kuzungumza na moyo wa kila mwanamume na mwanamke, akituvuta sote kwa upendo wake. “Tumetumwa kuendeleza utume huu: kuwa ishara za moyo wa Kristo na upendo wa Baba, tukikumbatia dunia nzima” (Hotuba kwa Washiriki wa Mkutano Mkuu wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari, 3 Juni 2023).
Kuhuisha utume wa matumaini: Wakikabiliwa na uharaka wa utume wa matumaini leo, wanafunzi wa Kristo wanaitwa kwanza kugundua jinsi ya kuwa "wataalamu" wa matumaini na warejeshaji wa ubinadamu ambao mara nyingi hukengeushwa na hauna furaha. Kwa ajili hiyo, tunahitaji kuhuishwa katika hali ya kiroho ya Pasaka inayopatikana katika kila adhimisho la Ekaristi na hasa katika Siku Tatu Kuu za Pasaka, kitovu na kilele cha mwaka wa liturujia. Tumebatizwa katika kifo cha ukombozi na ufufuko wa Kristo, katika Pasaka ya Bwana ambayo inaashiria majira ya kuchipua ya milele ya historia. Kwa hiyo, sisi ni "watu wa majira ya kuchipua", tukiwa tumejawa na matumaini kwa ajili ya wote, kwa kuwa katika Kristo "tunaamini na kufahamu kwamba kifo na chuki sio neno la mwisho" linalotamkwa juu ya uwepo wa mwanadamu (taz. Katekesi, 23 Agosti 2017). Kutokana na mafumbo ya Pasaka, yanayotolewa katika maadhimisho ya liturujia na katika sakramenti, daima tunachota nguvu za Roho Mtakatifu ili kufanya kazi kwa bidii, ari na subira katika nyanja pana ya uinjilishaji duniani. “Kristo, aliyefufuka na kutukuzwa, ndiye chemchemi ya tumaini letu, na hatatunyima msaada tunaohitaji ili kutekeleza utume ambao ametukabidhi” (Evangelii Gaudium, 275). Ndani yake, tunaishi na kutoa ushuhuda wa tumaini hilo takatifu ambalo ni "zawadi kutoka kwa Mungu na kazi kwa Wakristo" (Hope is a Light in the Night, Vatican City 2024, 7).
Wamisionari wa matumaini ni wanaume na wanawake wa sala, kwani “mtu anayetumaini ni mtu anayesali”, kwa maneno ya Mtumishi wa Mungu Kardinali François-Xavier Van Thuan, ambaye yeye mwenyewe alidumishwa katika matumaini katika kipindi kirefu cha kifungo chake kutokana na nguvu alizopata kutokana na sala aminifu na Ekaristi (taz. The Road of Hope, Boston, 2001, 96301). Tusisahau kwamba sala ni shughuli ya msingi ya kimisionari na wakati huo huo "nguvu ya kwanza ya matumaini" (Katekesi, 20 Mei 2020). Kwa hiyo tufanye upya utume wa matumaini, tukianzia na sala, hasa sala iliyojisimika katika neno la Mungu na hasa Zaburi, ule wimbo mkuu wa sala ambao mtunzi wake ni Roho Mtakatifu (taz. Katekesi, 19 Juni 2024). Zaburi hutufundisha kuwa na matumaini katikati ya dhiki, kutambua ishara za tumaini lililo karibu nasi, na kuwa na hamu ya mara kwa mara ya "kimisionari" kwamba Mungu atukuzwe na watu wote (taz. Zab 41:12; 67:4). Kwa kusali, tunatunza hai cheche ya tumaini inayowashwa na Mungu ndani yetu, ili iweze kuwa moto mkubwa, unaomuangazia na kumpa joto kila mtu anayetuzunguka, pia kwa vitendo na ishara zile thabiti ambazo sala yenyewe huchochea.
Kuhitimisha, uinjilishaji daima ni mchakato wa kijumuiya, kama vile tumaini lenyewe la Kikristo (taz. Benedict XVI, Spe salvi, 14). Mchakato huo hauishii kwa utangazaji wa awali wa Injili na Ubatizo, bali unaendelea na ujenzi wa jumuiya za Kikristo kwa kuandamana na kila mmoja wa wabatizwa katika njia ya Injili. Katika jamii ya kisasa, ushirika katika Kanisa kamwe haupatikani mara moja tu na ikatosha. Ndiyo maana shughuli ya kimisionari ya kukabidhi na kuchagiza imani iliyokomaa katika Kristo ni “mfano wa shughuli zote za Kanisa” (Evangelii gaudium, 15), kazi inayohitaji ushirika wa sala na matendo. Hapa ningesisitiza kwa mara nyingine tena umuhimu wa muondoko wa kisinodi wa kimisionari wa Kanisa, pamoja na huduma inayotolewa na Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari katika kukuza wajibu wa kimisionari wa waliobatizwa na kusaidia Makanisa Mapya Mahalia. Ninawasihi ninyi nyote, watoto, vijana, watu wazima na wazee, kushiriki kikamilifu katika utume wa pamoja wa uinjilishaji wa Kanisa kwa ushuhuda wenu wa maisha na sala, kwa sadaka zenu na kwa ukarimu wenu. Asanteni kwa hili! Wapendwa dada na kaka, tumrudie Maria, Mama wa Yesu Kristo tumaini letu. Kwake tunamkabidhi sala zetu kwa ajili ya Jubilei hii na kwa miaka ijayo: "Mwanga wa tumaini la Kikristo na umuangazie kila mwanamume na mwanamke, kama ujumbe wa upendo wa Mungu unaoelekezwa kwa wote! Kanisa na litoe ushuhuda wa uaminifu kwa ujumbe huu katika kila sehemu ya dunia!" (Bull Spes Non Confundit, 6).
Roma, Mtakatifu Yohane Laterano, 25 Januari 2025, Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume.
FRANCISKO.
