Papa akutana na waigizaji:msiogope kukabiliana na majeraha ya Ulimwengu
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Sinema ni lugha ya amani, haipaswi kuogopa kukabiliana na majeraha ya dunia. Mwaliko wa sanaa ya saba ya kusimulia vurugu, upweke, na vita vilivyosahaulika. Daima inabaki kuwa mahali pa kukutana na nyumbani kwa wale wanaotafuta maana. Na Taasisi ziunge mkono sinema, zilizo hatarini leo. Sinema ni sanaa changa, yenye ndoto, na isiyotulia, ingawa sasa ina umri wa karne moja. Haya na mengine yamo kwenye Hotuba ya Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa kukutana na wakurugenzi, waigizaji na watengenezaji filamu zaidi ya 160 katika Ukumbi wa Clementine mjini Vatican, Jumamosi tarehe 15 Novemba 2025.
Papa Leo XIV katika hotuba yake kama kawaida alianza na Ishala ya msalaba na kuwayakia amani, huku akiwasalimia na kuwakaribisha wote. Sinema ni sanaa changa, yenye ndoto, na isiyotulia, ingawa sasa ina umri wa karne moja. Kwa sasa inaadhimisha miaka 130, ikihesabu onesho la kwanza la hadharani, lililofanywa na ndugu wa Lumière mnamo tarehe 28 Desemba 1895, huko Paris. Hapo awali, sinema ilionekana kama mchezo wa mwanga na vivuli, uliokusudiwa kuburudisha na kuvutia. Lakini mapema, matokeo yake ya kuona ilifunua ukweli wa ndani zaidi, na kuwa usemi wa hamu ya kutafakari na kuelewa maisha, kusimulia ukuu na udhaifu wake, kutafsiri hamu yake ya kutokuwa na mwisho.
Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu kwa furaha, maliwasalimu na kwa shukrani kuwapongeza kile ambacho sinema inachowakilisha: sanaa maarufu kwa maana bora zaidi, iliyozaliwa kwa kila mtu na kuzungumza na kila mtu. Ni vizuri kutambua kwamba, wakati taa ya kiini macho ya sinema inapowaka, katika giza, Mtazamo wa roho huwashwa kwa wakati mmoja, kwa sababu sinema inajua jinsi ya kuchanganya kile kinachoonekana kama burudani tu na simulizi la matukio ya kiroho ya mwanadamu. Mojawapo ya michango muhimu zaidi ya sinema ni ile hasa ya kumsaidia mtazamaji kurudi kwenye nafsi yake, kutazama kwa macho mapya ugumu wa uzoefu wake mwenyewe, kuona ulimwengu kana kwamba ni kwa mara ya kwanza, na kugundua tena, katika zoezi hili, sehemu ya tumaini hilo ambalo bila hilo uwepo wetu hautatimizwa. Papa aliongeza: “Inanifariji kufikiria kwamba sinema si tu picha zinazotembea: ni kujiweka katika harakati ya matumaini!
Kuingia kwenye ukumbi wa sinema ni kama kuvuka kizingiti. Katika giza na ukimya, jicho hupata mwelekeo wake tena, moyo hujiruhusu kufikiwa, akili hufunguka kwa kile ambacho hakikuwahi kufikiria. Kiukweli, wanajua kwamba sanaa yao inahitaji umakini. Kwa kazi zao, Papa alisisitiza tena kwamba wanashirikiana na wale wanaotafuta wepesi, lakini pia na wale walio na wasiwasi mioyoni mwao, kutafuta maana, haki, na uzuri. Leo hii, tunaishi na skrini za kidijitali zikiwa zimewashwa kila wakati. Mtiririko wa habari ni wa kudumu. Lakini sinema ni zaidi ya skrini rahisi: ni njia panda ya matamanio, kumbukumbu, na maswali. Ni utafutaji nyeti ambapo mwanga hupenya giza na maneno hukutana na ukimya. Katika njama inayoendelea, macho huelimishwa, mawazo hupanuka, na hata maumivu yanaweza kupata maana.”
Sinema zikabiliwa na mmomonyoko unaotia wasiwasi:wito kwa serikali
Taasisi za kiutamaduni kama vile sinema na kumbi za tamthiliya ni mioyo inayodunda ya jamii zetu, ikichangia katika ubinadamu wao. Ikiwa jiji liko hai, pia ni kutokana na nafasi zake za kiutamaduni: lazima tuishi ndani yake, tujenge uhusiano, siku baada ya siku. Lakini sinema zinakabiliwa na mmomonyoko unaotia wasiwasi unaowaondoa katika miji na vitongoji. Na kuna wengi wanaosema kwamba sanaa ya sinema na uzoefu wa sinema ziko hatarini. Papa alitoa wito kwamba “Ninazisihi taasisi zisikate tamaa na kushirikiana ili kuthibitisha thamani ya kijamii na kiutamaduni ya shughuli hii.”
Mantiki ya (algorithimu), yaani mifumo ya kimashine huelekea kurudia kile "kinachofanya kazi," lakini sanaa hufunguka kwa kile kinachowezekana. Sio kila kitu lazima kiwe cha haraka au kinachotabirika: teteeni upolepole wakati unahitajika, ukimya wakati unapozungumza, tofauti wakati unapochochea. Uzuri si kutoroka tu, bali zaidi ya yote ni maombi. Sinema, inapokuwa halisi, haitulizi tu: ina changamoto. Inauliza maswali yanayokaa ndani yetu na, wakati mwingine, hata machozi ambayo hatukujua tunahitaji kuelezea.
Mwaka wa Jubileo Kanisa linaalika kutembea kwa matumaini
Baba Mtakatifu Leo kadhalika aliendelea kusema kuwa “Katika Mwaka huu wa Jubilei, Kanisa linapotualika kusafiri kuelekea matumaini, uwepo wao kutoka mataifa mengi na zaidi ya yote, kazi yao ya kila siku ya kisanii ni ishara zinazong'aa. Kwa sababu wao pia, kama wengine wengi wanaokfika Roma kutoka kila sehemu ya dunia, wanasafiri kama mahujaji wa mawazo, watafutaji wa maana, wasimulizi wa matumaini, wajumbe wa ubinadamu. Njia wanayosafiri haipimwi kwa kilomita bali kwa picha, maneno, hisia, kumbukumbu za pamoja, na matamanio ya pamoja. Ni hija katika fumbo la uzoefu wa kibinadamu ambayo wanapita kwa mtazamo unaopenya, wenye uwezo wa kutambua uzuri hata katika mikunjo ya maumivu, tumaini ndani ya misiba ya vurugu na vita. Kanisa linawaangalia kwa heshima wao wanaofanya kazi kwa mwanga na wakati, kwa nyuso na mandhari, kwa maneno na ukimya.
Papa katika hotuba yake, alisema Papa Mtakatifu Paulo VI aliwaambia: "Kama ninyi ni marafiki wa sanaa ya kweli, ninyi ni marafiki zetu," akikumbuka kwamba "ulimwengu huu tunaoishi unahitaji uzuri ili kuepuka kuzama katika kukata tamaa" (Ujumbe kwa Wasanii Mwishoni mwa Mtaguso wa Pili wa Vatican tarehe 8 Desemba 1965). “Natamani kufufua urafiki huo, kwa sababu sinema ni maabara ya matumaini, mahali ambapo mwanadamu anaweza tena kujiangalia yeye mwenyewe na hatima yake mwenyewe.” Labda tunahitaji kusikiliza tena maneno ya mwanzilishi wa sanaa ya saba, David W. Griffith. Alisema: “Kile ambacho filamu ya kisasa haina ni uzuri, uzuri wa upepo unaosonga kwenye miti.” Tunawezaje kutofikiria, tukimsikiliza Griffith akizungumzia upepo kwenye miti, kuhusu kifungu hicho kutoka Injili ya Yohana: "Upepo huvuma unakotaka, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda: ndivyo ilivyo kwa kila mtu aliyezaliwa kwa Roho" (3:8). Kwa hiyp Papa aliwahimiza akisema " Wapendwa mabwana wa kale na wapya, fanyeni filamu kuwa sanaa ya Roho." Enzi yetu inahitaji mashuda wa matumaini, uzuri na ukweli
“Enzi yetu inahitaji mashuhuda wa matumaini, uzuri, na ukweli: Ninyi pamoja na kazi yenu ya kisanii, mnaweza kuwa wao. Kurejesha uhalisia wa picha ili kulinda na kukuza heshima ya binadamu kunategemea nguvu ya filamu nzuri na waumbaji wake na wahusika wakuu. Msiogope kukabiliana na majeraha ya ulimwengu. Ukatili, umaskini, uhamisho, upweke, madawa ya kulevya, vita vilivyosahaulika ni majeraha ambayo yanahitaji kuonekana na kusimuliwa. Sinema kubwa haitumii maumivu: inaambatana nayo, inayachunguza. Wakurugenzi wote wakubwa wamefanya hivyo. Kutoa sauti kwa hisia tata, zinazopingana, na wakati mwingine zisizojulikana zinazokaa mioyoni mwa wanadamu ni kitendo cha upendo. Sanaa haipaswi kukimbia fumbo la udhaifu: lazima iisikilize, lazima iweze kusimama mbele yake. Filamu, bila kuwa ya kufundisha, ina ndani yake yenyewe, katika aina zake za kisanii, uwezo wa kuelimisha macho. Kwa kumalizia, kutengeneza filamu ni juhudi ya jamii, kazi ya kwaya ambayo hakuna mtu anayejitosheleza.
Kila mtu anajua na anathamini ustadi wa mkurugenzi na ustadi wa waigizaji, lakini filamu isingewezekana bila kujitolea kimya kimya kwa mamia ya wataalamu wengine: Wasaidizi, wakimbiaji, mameneja wa mali, mafundi umeme, mafundi sauti, vifaa, wasanii wa vipodozi, watengeneza nywele, wabunifu wa mavazi, mameneja wa maeneo, wakurugenzi wa waigizaji, wakurugenzi wa upigaji picha na muziki, waandishi wa filamu, wahariri, mafundi wa matokeo, wazalishaji… Ni Matumaini ya Papa kwamba hakiweza kumwacha yeyote nje lakini kuna wengi sana! Kila sauti, kila ishara, kila ujuzi huchangia kazi ambayo inaweza kuwepo kwa ujumla. Katika enzi ya kujiona kulikokithiri na kukinzana, wao wanatuonesha jinsi ya kutengeneza filamu nzuri kunahitaji kushirikisha vipaji vya kila mtu. Lakini kila mtu anaweza kuacha karama yake ya kipekee iangaze kutokana na vipawa na sifa za wale wanaofanya kazi pamoja naye, katika mazingira ya ushirikiano na udugu. Sinema yao ibaki kuwa mahali pa kukutania kila wakati, nyumbani kwa wale wanaotafuta maana, lugha ya amani. Isipoteze kamwe uwezo wake wa kushangaza, ikiendelea kutuonesha hata kipande kimoja cha fumbo la Mungu. Papa alihitimisha kwa kuwaobea Baraka ya Bwana, kazi yao, na wapendwa wao. Nna kwamba awasindikize kila wakati kwenye hija yao ya ubunifu, ili wawe mafundi wa matumaini.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here
