Papa,wanahija wa Latvia:Kutumaini si kupata jibu ni kumfuata Kristo kwa karibu
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV alikutana Jumatatu tarehe 24 Novemba 2025 na ujumbe wa mahujaji Wakristo kutoka Latvia, katika fursa ya miaka mia moja tangu walipofanya hija rasmi ya kwanza kutoka nchini humo hadi Roma. Miongoni mwao alikuwa Bi Evika Siliņa, ambaye ni Waziri Mkuu wa Latvia tangu 2023 na ambaye alikutana na Baba Mtakatifu katika Jumba la Kitume, ukifuatiwa Mkutano na Sekretarieti ya Vatican.
Katika hotuba yake, Papa Leo alisema, nchi hiyo ambayo inapakana na Urusi na imeathiriwa sana na vita vinavyoendelea nchini Ukraine leo hii inakabiliwa pia na nyakati ngumu. Katika hali kama hizo, ni muhimu kwetu kumgeukia Mungu na kuimarishwa kwa neema Yake. Papa alitoa shukrani zake kwa kuimarika kwa uhusiano kati ya Vatican na Latvia katika miaka michache iliyopita, na akamshukuru Waziri Mkuu wa Latvia Evika Siliņa kwa uwepo wake katika mkutano huo.
Katika hotuba yake kwa kikundi hicho, Papa alisema kwamba watakatifu waliozikwa mjini Roma wote wameonesha kwamba tumaini halikatishi tamaa, licha ya kutokuwa na uhakika wa hali zao na changamoto walizokabiliana nazo. Alisisitiza tena kwamba matumaini haimaanishi kuwa na majibu yote, bali ni suala la kumtumaini Mungu na kumfuata Kristo kwa karibu zaidi.
“Ingawa mgogoro wa sasa katika eneo lenu unaweza kukumbusha nyakati hizo zenye misukosuko, ni muhimu kwetu sote kumgeukia Mungu na kuimarishwa na neema yake tunapokabiliwa na dhiki kama hizo.” Hakika, ukosefu wa usalama na hali ngumu vimeiathiri historia ya nchi hiyo, alisema Papa Leo XIV. Mtangulizi wake, Papa Francisko, alikumbusha hilo alipotembelea Latvia mwaka 2018, katika maadhimisho ya miaka mia moja ya uhuru wake.
Papa Leo pia alitoa mawazo machache kuhusu umuhimu wa hija ambayo kundi hilo kutoka Latvia lilikuwa limeanza. Safari kama hizo, alipendekeza, ziwaondoe kwenye utaratibu na kelele za maisha ya kila siku na kuwapatia nafasi na ukimya wa kusikia sauti ya Mungu kwa uwazi zaidi. Kwa hivyo Papa aliwaalika mahujaji wa Latvia kutumia vyema muda wao jijini Roma, ili iweze kuimarisha imani yao na kuwapatia amani ambayo ulimwengu hauwezi kutoa:
“Kwa hivyo, ninawatia moyo mtumie fursa hii kuomba na kujifungulia neema ya Mungu, ili iweze kuwaimarisha imani yenu na kuwapatia amani ambayo ulimwengu hauwezi kutoa.”
Alihitimisha kwa baraka yake. Hija ya hii kutola Latvia ilijumuisha wajumbe wapatao 200,ambao walifika katika muktadha wa mwaka mtakatifu wa Jubilei wa 2025, ambao mada yake ni “Mahujaji wa Matumaini.”
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku, bofya hapa tu: Just click here
