Tafuta

2025.11.21 Papa Leo akutana na Vijana wa Marekani, kwa njia ya kidijitali. 2025.11.21 Papa Leo akutana na Vijana wa Marekani, kwa njia ya kidijitali.  (@Vatican Media)

Papa:Ulimwengu unahitaji wamisionari,kushiriki nuru na furaha ya Yesu!

"Ni wakati wa kuota ndoto kubwa.Ninyi ndiyo Uwepo wa Kanisa,"yalikuwa ni maneno ya nguvu ya Papa Leo XIV akikutana na vijana 16,000 washiriki wa Mkutano wa Kitaifa wa Vijana Wakatoliki waliokusanyika katika Uwanja wa Lucas Oil huko Indianapolis.Katika kuunganishwa kwa njia ya video,aliwageukia vijana waliomuuliza maswali muhimu ya maisha yao na kuwapa ushauri.Teknolojia mpya iwasaidie katika njia ya kukua na kuwa waangalifu kuhusu maisha ya kijuu juu,bali wakuze urafiki na Yesu.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Wakati ujao ni sasa, ni wakati wa mdundo, pumzi inayotualika kuota ndoto kubwa. Upepo wa vijana huvuma kwa nguvu na kutusukuma zaidi ya faraja na upekee. Unatuita tuanze safari kuelekea ukuu  uliozaliwa na ukarimu, upendo, na urafiki. Ni safari bila hofu ya kubadilisha upeo wa mtazamo, kwa sababu macho yetu yanapoongozwa na mahusiano ya kweli, mwisho unaweza kuwa "furaha na uhuru tu. Ni harakati ambayo haioneshi bendera, kwa sababu imani haiwezi kuzuiliwa ndani ya makundi ya kisiasa. Na hivi ndivyo tunavyokua: kwa kufuata uzuri, kwa kuelekea wakati ujao kwa teknolojia mpya ambazo hazidhoofishi safari, bali zinasindikizana.

Mkutano wa vijana na Papa kidijitali
Mkutano wa vijana na Papa kidijitali   (@Vatican Media)

Haya yote  na mengine mengi yamo kwenye majibu ya Baba Mtakatifu Leo XIV kupitia kiungo cha video Ijumaa, alasiri, tarehe 21 Novemb 2025 aliposhiriki Mkutano wa Kitaifa wa Vijana Wakatoliki (NCYC) katika jiji la Indianapolis nchini Marekani,  wapatao 16,000. Ukiongozwa na Katie Prejan McGrady, tukio hilo lilishuhudia Wakatoliki sita vijana  wakimuuliza na kumwomba Papa kushirikisha mawazo yake kuhusu mada kuanzia Sakramenti, afya ya akili, Akili  Unde (AI) na mustakabali wa Kanisa kwa ujumla. Kwa njia hiyo katika  hotuba yake ya ufunguzi, Papa Leo aliwasifu vijana wa Marekani kwa kuchukua muda wa kukutana pamoja ana kwa ana, na kuwatia moyo kuwa wanachama hai wa jumuiya zao za parokia. Mkutano huo uliwapatia  nafasi ya kuhudhuria Misa, kusali kabla ya Sakramenti Takatifu, na kupokea Sakramenti ya Upatanisho, na Papa alisema shughuli hizi ni fursa halisi za kukutana na Yesu.

Katika Sakramenti

Swali la kwanza aliloulizwa Papa kuhusu kukubali huruma ya Mungu tunapotenda dhambi au kuwakatisha tamaa wengine. Papa Leo XIV alikiri kwamba kila mtu anapambana na kuomba huruma ya Mungu na kukubali kwamba kweli anatusamehe katika Kuungama. "Dhambi haina neno la mwisho.  Wakati wowote tunapoomba huruma ya Mungu, Yeye hutusamehe. Papa Francisko alisema kwamba Mungu hachoki kusamehe, bali ni sisi tunaochoka kuomba!" Papa Leo aliongeza kusema,  “Moyo wa Mungu ni tofauti na wetu, kwani Yeye hachoki kutafuta kondoo waliopotea.” Papa aliwaalika vijana kukutana na Kristo katika Sakramenti ya Upatanisho, wakitubu dhambi zao waziwazi na kukaribisha msamaha wa Yesu katika msamaha wa kuhani.

Mkutano wa vijana kidijitali
Mkutano wa vijana kidijitali

Mapambana na mfadhaiko na masuala ya afya ya akili

Papa alijibu swali kuhusu mapambano ya afya ya akili, kama vile kuhisi huzuni au kuzidiwa. Aliwaalika kila mtu kujifungulia uhusiano wa kina na Yesu, kukabidhi matatizo yao kwake katika sala. "Katika ukimya, tunaweza kuzungumza kwa uaminifu kuhusu yaliyo mioyoni mwetu. Wakati wa ibada ya Ekaristi, unaweza kumtazama Yesu katika Sakramenti Takatifu na kujua kwamba anakutazama kwa upendo." Papa aliongeza kuwa vijana wanapaswa pia “kupata watu wazima wanaowaamini, ili Mungu aweze kuzungumza nao kupitia wengine, kama vile wazazi, walimu, makuhani, na wahudumu wa vijana.”

Papa alishiriki na vijana wadogo mkutano
Papa alishiriki na vijana wadogo mkutano   (@Vatican Media)

Papa Leo pia aliwaalika waombee "zawadi ya marafiki wa kweli, ambao wanatusukuma kumtafuta Yesu wakati maisha yanapochanganyikiwa au magumu. Vijana wengi husema, 'Hakuna anayenielewa.' Lakini wazo hilo linaweza kukutenga. Linapokuja, jaribu kusema, 'Bwana, unanielewa vizuri kuliko ninavyojielewa,' na uamini kwamba atakuongoza."

Imani na teknolojia

Akijibu swali kuhusu athari za teknolojia kwenye imani, Papa Leo XIV alisisitiza umuhimu wa zana za kisasa kuwaunganisha watu walio mbali  kwa maelfu kilomita. "Teknolojia inaweza kutusaidia kufanya mambo mengi na hata kutusaidia kuishi imani yetu ya Kikristo. Pia inatupatia zana za ajabu za maombi, kusoma Biblia, na kujifunza zaidi kuhusu tunachoamini. Wakati huo huo, Papa alibainisha kuwa teknolojia haiwezi kuchukua nafasi ya mahusiano halisi, ya ana kwa ana na ushiriki katika Ekaristi, akiwaalika vijana Wakatoliki kuwa na nia ya muda wao wa kutazama na kuhakikisha kwamba teknolojia inahudumia maisha yao, si kinyume chake.

Maswali ya vijana
Maswali ya vijana   (@Vatican Media)

Akili Unde, alisema Papa Leo, imekuwa sifa muhimu ya nyakati zetu, akibainisha kuwa usalama si tu kuhusu kudhibiti maendeleo ya mifumo ya AI bali pia kuhusu kuwawezesha watu kufanya maamuzi yenye afya kupitia elimu na uwajibikaji binafsi. Kila zana inapaswa kusaidia safari yetu ya imani na maendeleo ya kiakili, si kuizuia, alisema. "Kuweni waangalifu kwamba matumizi yenu ya AI hayazuii ukuaji wenu wa kweli wa kibinadamu. Itumieni kwa njia ambayo, ikiwa itatoweka kesho, bado mtajua jinsi ya kufikiria, kuunda, na kutenda peke yenu. Kumbukeni: AI haiwezi kuchukua nafasi ya zawadi ya kipekee mliyo nayo kwa ulimwengu, " Papa alitoa taadhari. Na hata hivyo aliwapa mfano wa kuigwa kwa Mtakatifu Carlo Acutis katika kutumia mitandao ya kijamii. Na vile vile Sura ya Giorgio Frassati.

Papa azungumza na vijana wakatoliki wa Marekani 21 Novemba 2025

Mustakabali wa Kanisa

Baba Mtakatifu Leo alijibu pia swali kuhusu mustakabali wa Kanisa, akikumbuka ahadi ya Yesu kwa Petro kwamba "milango ya kuzimu haitalishinda Kanisa." Kanisa hujiandaa kwa ajili ya mustakabali kwa kubaki "mwaminifu kwa kile Yesu anachotuomba leo," alisema, huku  akikumbuka kwamba Roho Mtakatifu ameongoza Kanisa kupitia milenia mbili za masuala na changamoto. Vijana, sio  mustakabali wa Kanisa tu,  bali pia ni wakati wake wa sasa, na aliwasihi wajihusishe kwa kuhudhuria Misa ya Dominika na kujiunga na shughuli za vijana ambapo imani yao inaweza kukua. "Ikiwa unahisi kuwa Bwana anaweza kukuita kwa jambo maalum, zungumza na Padre  wako wa parokia au kiongozi mwingine anayeaminika," Papa aliwashauri na kusema tena "Wanaweza kukusaidia kutambua kile ambacho Mungu anaomba."

Marafiki wa Kristo, wamisionari wa Injili

Hatimaye, Papa Leo XIV alielezea matumaini yake kwa mustakabali wa vijana katika Kanisa, akiwaalika kusaidia kuliunda katika miaka ijayo. Kujibu hamu yao ya ujana ya kufanya jambo lenye maana, Papa aliwasihi Wakatoliki vijana hao kutoa muda na vipaji vyao kwa ukarimu ili kulijenga Kanisa. "Kwa undani zaidi, tunatamani ukweli, uzuri, na wema kwa sababu tuliumbwa kwa ajili hiyo,” alisema. “Na hazina hii tunayotafuta ina jina yaani: Yesu, anayetaka kupatikana na wewe.”

Papa akizungumza na vijana
Papa akizungumza na vijana   (@Vatican Media)

“Vijana wameitwa kuwa marafiki wa Kristo na wapatanishi, wanaojenga madaraja badala ya kuta, wanaothamini mazungumzo na umoja badala ya mgawanyiko. Kuweni makini msitumie makundi ya kisiasa kuzungumza kuhusu imani,” alisema. “Kanisa si la chama chochote cha siasa. Badala yake, linasaidia kuunda dhamiri yenu ili muweze kufikiri na kutenda kwa hekima na upendo.” Kwa kumalizia, Papa Leo aliwaalika vijana hao Wakatoliki wa Marekani kusikiliza wito wa Mungu katika maisha yao na kutambua wito wao, iwe ni kwa ndoa, ukuhani, au maisha ya kitawa. Ni kwa sababu gani kubwa zaidi unayoweza kujitolea maisha yako kuliko Injili?” aliuliza swali hili akiwaachia kila mmoja ajiulize. “Ulimwengu unahitaji wamisionari. Unawahitaji kushiriki nuru na furaha mliyoipata kutoka katika Yesu.”

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here

21 Novemba 2025, 18:23