Papa Leo XIV,Instanbul:Wito wa maono ya kiinjili,kwa kuangaziwa na Roho Mtakatifu!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV tarehe 28 Novemba 2025 akiwa katika Ziara yake ya Kwanza ya Kitume kimataifa, ameshiriki muda wa maombi katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu huko Istanbul, na waamini wapatao 800, ambapo Maaskofu, Mapadre, mashemasi, watawa wa kike na waliowekwa wakfu, na wahudumu wa kichungaji walikuwa wamekusanyika ndani ya Kanisa Kuu hilo Umati wa watu ulijipanga mitaani kumsalimu Baba Mtakatifu, ambaye alifika akiwa amevaa mozzetta nyekundu. Hasa, kulikuwa kuna vijana, makuhani, watoto na kundi kubwa la mapadre kutoka Harakati la Neokatekumenali wakiwa katika hija ambao walipeleka jiwe la msingi la parokia mpya ambayo itajengwa huko Dallas, katika kitongoji cha wahamiaji, na kuwekwa Mlinzi msimamizi Mtakatifu Agostino.
Baba Mtakatifu Leo XIV akianza hotuba yake alionesha furaha kubwa kwake kuwa nao. “Ninamshukuru Bwana kwamba katika Ziara yangu ya kwanza ya Kitume amenipa neema ya kutembelea "nchi hii takatifu" ambayo ni Türkiye, mahali ambapo histroia ya watu wa Israeli inakutana na kuzaliwa kwa Ukristo, ambapo Agano la Kale na Jipya hukumbatia na ambapo kurasa za Mitaguso mingi ziliandikwa. Imani inayotuunganisha ina mizizi mirefu. Kwa kutii wito wa Mungu, Baba Yetu Ibrahimu aliondoka Uru wa Wakaldayo na kisha, kutoka eneo la Harrani kusini mwa Türkiye ya leo hii, aliondoka kwenda Nchi ya Ahadi (taz. Mw 12:1). Katika utimilifu wa wakati, baada ya kifo na ufufuko wa Yesu, wanafunzi wake pia walikuja Anatolia. Katika Antiokia, ambayo askofu wake alikuwa Mtakatifu Ignatius, waliitwa "Wakristo" kwa mara ya kwanza (taz. Mdo 11:26). Kutoka mji huo, Mtakatifu Paulo alianza baadhi ya safari zake za kitume zilizosababisha kuanzishwa kwa jumuiya nyingi. Vile vile ilikuwa Efeso kwenye ufukwe wa Anatolia, ambapo, kulingana na baadhi ya vyanzo vya kale, Yohane Mfuasi Mpendwa na Mwinjili aliishi na kufa (taz. Mtakatifu Irenaeus, Adversus Haereses, III, 3, 4; Eusebius wa Kaisaria, Historia ya Kanisa, V, 24, 3).
Zaidi ya hayo, tunakumbuka kwa pongezi historia kubwa ya Byzantine, msukumo wa kimisionari wa Kanisa la Constantinople na kuenea kwa Ukristo katika eneo lote. Hata leo hii huko Türkiye kuna jumuiya nyingi za Wakristo wa Mashariki - Waarmenia, Washami na Wakaldayo - pamoja na zile za Kilatini. Upatriaki wa Kiekumeni unabaki kuwa sehemu ya marejeo kwa waamini wake wa Kigiriki na kwa wale wa Makanisa mengine ya Kiorthodox. Papa Leo alisema kuwa Jumuiya zao ziliibuka kutoka katika utajiri wa historia hii ndefu, na wao wanaitwa leo hii kulea mbegu ya imani tuliyopewa na Ibrahimu, Mitume na Mababa. Historia iliyowatangulia si kitu cha kukumbukwa tu na kisha kuheshimiwa kama historia tukufu huku tukitazama kwa kujiamini jinsia mbavyo Kanisa Katoliki limekuwa dogo kiidadi. “Kinyume chake, tunaalikwa kuchukua maono ya kiinjili, tukiwa tumeangaziwa na Roho Mtakatifu.…..
Tunapotazama kwa macho ya Mungu, tunagundua kwamba amechagua njia ya udogo, akishuka katikati yetu. Hii ndiyo njia ya Bwana, ambayo sote tumeitwa kuishuhudia. Manabii wanatangaza ahadi ya Mungu kwa kuzungumzia chipukizi dogo litakalochipuka (taz. Isaya 11:1). Yesu anawasifu wadogo wanaomtumainia (taz. Mk 10:13–16). Anafundisha kwamba ufalme wa Mungu haujilazimishi kwa maonesho ya nguvu (taz. Luka 17:20–21), bali hukua kama mbegu ndogo zaidi kuliko zote zilizopandwa ardhini (taz. Mk 4:31). Mantiki hii ya udogo ni nguvu ya kweli ya Kanisa. Haiko katika rasilimali zake au miundo yake, wala matunda ya utume wake hayategemei idadi, nguvu za kiuchumi au ushawishi wa kijamii. Badala yake Kanisa linaishi kwa nuru ya Mwanakondoo; likiwa limekusanyika kumzunguka, linatumwa ulimwenguni kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Katika utume huu, anaitwa kila mara kuamini ahadi ya Bwana: “Msiogope, enyi kundi dogo, kwa maana ni radhi ya Baba yenu kuwapa ufalme” (Lk 12:32). Tukumbuke pia maneno ya Papa Francisko aliyesema, “Jumuiya ya Kikristo ambayo waamini, mapadre na maaskofu hawafuati njia ya udogo haina mustakabali…
Ufalme wa Mungu huchipuka katika vitu vidogo, daima katika vile vidogo” (Mahbiri huko Mtakatifu Marta, 3 Desemba 2019). Kanisa huko Türkiye ni jumuiya ndogo, lakini yenye matunda kama mbegu na chachu ya ufalme. Kwa hivyo Papa aliwahimiza kukuza mtazamo wa kiroho wa tumaini la uhakika, lenye mizizi katika imani na katika muungano na Mungu. Kuna haja ya kushuhudia Injili kwa furaha na kutazama wakati ujao kwa matumaini. Baadhi ya ishara zenye matumaini tayari zipo wazi. Kwa hivyo, tumwombe Bwana neema ya kuzitambua na kuzilea. "Labda kuna ishara zingine ambazo tunaweza kuhitaji kuzionesha kwa ubunifu kupitia uvumilivu katika imani na katika ushuhuda. Miongoni mwa ishara nzuri na zenye kuahidi zaidi, Papa alingozea " ninawafikiria vijana wengi wanaogonga milango ya Kanisa Katoliki wakiwa na maswali na wasiwasi wao. Katika suala hili, ninawasihi muendelee na kazi nzuri ya uchungaji mnayofanya." Pia Papa Leo XIV aliwahimiza kusikiliza, kusindikizana vijana, kutoa kipaumbele maalum kwa maeneo ambayo Kanisa huko Türkiye limeitwa kutumikia: mazungumzo ya kiekumene na ya kidini, kusambaza imani kwa wakazi wa eneo hilo, na huduma ya kichungaji kwa wakimbizi na wahamiaji.
Kipengele hiki cha mwisho Papa Leo alisema "kinastahili kutafakariwa kwa njia ya pekee. Uwepo mkubwa wa wahamiaji na wakimbizi katika nchi hii unaipatia Kanisa changamoto ya kuwakaribisha na kuwahudumia baadhi ya walio katika mazingira magumu zaidi. Wakati huo huo, Kanisa hili lenyewe linaundwa kwa kiasi kikubwa na wageni, na wengi wenu, mapadfre, watawa wa kike na kiume na mnatoka nchi zingine. Hili linahitaji kujitolea maalum kwa utamaduni ili lugha, mila na utamaduni wa Türkiye ziwe zaidi na zaidi kuwa zenu. Zaidi ya hayo, mawasiliano ya Injili hupitia utamaduni huo kila wakati." Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu Leo alipenda pia kukumbusha kwamba ilikuwa katika nchi yao hiyo ambapo Mitaguso nane ya kwanza ya Kiekumeni ilifanyika. Mwaka huu unaashiria kumbukumbu ya miaka 1700 ya Mtaguso wa Kwanza la Nicea, "hatua muhimu katika historia ya Kanisa lakini pia ya ubinadamu kwa ujumla" (Francisko, Hotuba kwa Tume ya Kitaalimungu ya Kimataifa, 28 Novemba 2024). Tukio hili linaloendelea kutupatia changamoto kadhaa ambazo Papa Leo alipenda kuzitaja:
La kwanza ni umuhimu wa kuelewa kiini cha imani na kuwa Mkristo. Karibu na Imani, Kanisa huko Nicea liligundua upya umoja wake (taz. Bull Spes Non Confundit, 17). Imani si kanuni ya mafundisho tu; ni mwaliko wa kutafuta - katikati ya hisia tofauti, mambo ya kiroho na tamaduni - umoja na kiini muhimu cha imani ya Kikristo inayozingatia Kristo na Mapokeo ya Kanisa. Nicea bado inatuuliza: Yesu ni nani kwetu? Kimsingi inamaanisha nini kuwa Mkristo? Imani, ikikubaliwa kwa kauli moja pamoja, inakuwa kigezo cha utambuzi, dira, kitovu ambacho imani na matendo yetu lazima yazunguke. Katika kuzungumza kuhusu uhusiano kati ya imani na matendo, ningependa kuyashukuru mashirika ya kimataifa kwa msaada wao kwa shughuli za hisani za Kanisa, hasa kwa msaada uliotolewa kwa waathiriwa kufuatia tetemeko la ardhi mwaka wa 2023. Hapo Papa alitaja Caritas Internationalis na Kirche.
Changamoto ya pili ni uharaka wa kugundua tena katika Kristo uso wa Mungu Baba. Nicea inathibitisha umungu wa Yesu na usawa wake na Baba. Katika Yesu, tunapata uso wa kweli wa Mungu na neno lake la uhakika kuhusu ubinadamu na historia. Ukweli huu unapinga mawazo yetu wenyewe kuhusu Mungu kila wakati yanapokuwa hayaendani na kile ambacho Yesu amefunua. Inatualika kwenye utambuzi unaoendelea kuhusu aina zetu za imani, sala, maisha ya kichungaji na kiroho. Lakini pia kuna changamoto nyingine, ambayo tunaweza kuiita "Uarian mpya," iliyopo katika utamaduni wa leo hii na wakati mwingine hata miongoni mwa waamini. Hili hutokea wakati Yesu anapongezwa kwa kiwango cha kibinadamu tu, labda hata kwa heshima ya kidini, lakini haonekani kweli kama Mungu aliye hai na wa kweli kati yetu. Umungu wake, ubwana wake juu ya historia, umefunikwa na kivuli, na amepunguzwa hadi kuwa mtu mkuu wa kihistoria, mwalimu mwenye busara, au nabii aliyepigania haki, lakini hakuna zaidi. Nicea inatukumbusha kwamba Yesu Kristo si mfano wa wakati uliopita; yeye ni Mwana wa Mungu aliyepo kati yetu, akiongoza historia kuelekea wakati ujao ulioahidiwa na Mungu.
Hatimaye, changamoto ya tatu ni upatanisho wa imani na maendeleo ya mafundisho. Katika muktadha tata wa kiutamaduni, Kanuni ya Imani ya Nicaea ilionesha kiini cha imani kupitia aina za kifalsafa na kiutamaduni za wakati wake. Lakini miongo michache tu baadaye, katika Mtaguso wa Kwanza la Constantinople, tunaona kwamba iliimarishwa zaidi na kupanuliwa. Shukrani kwa maendeleo haya ya mafundisho, kulitokea uundaji mpya, kanuni ya Imani ya Nicaea na Constantinopoli ambayo tunasali pamoja katika liturujia zetu za Dominika. Hapa pia tunajifunza fundisho muhimu kwamba: imani ya Kikristo lazima ielezwe kila wakati katika lugha na aina za utamaduni tunamoishi, kama vile Mababa walivyofanya huko Nicaea na katika Mabaraza mengine. Wakati huo huo, ni lazima tutofautishe kiini cha imani kutoka kwa fomula za kihistoria zinazoielezea — fomula ambazo huwa za sehemu na za muda na zinaweza kubadilika kadri mafundisho yanavyoeleweka kwa undani zaidi.
Papa Leo alisisitiza kwamba tukumbuke kwamba Mwalimu mpya wa Kanisa, Mtakatifu John Henry Newman, alisisitiza juu ya maendeleo ya mafundisho ya Kikristo, kwa sababu mafundisho si wazo la kufikirika, lisilobadilika, bali yanaonyesha fumbo la Kristo. Kwa hivyo, maendeleo yake ni muhimu, sawa na yale ya uhalisia ulio hai, yakionesha polepole na kuelezea kikamilifu moyo muhimu wa imani. Papa Leo kabla ya kuhitimisha hotuba yake alipenda kumkumbuka mtu mpendwa sana kwao Mtakatifu Yohane XXIII, ambaye aliwapenda na kuwatumikia watu wa nchi hyoi. Aliandika, "Ninapenda kurudia kile ninachohisi moyoni mwangu: Naipenda nchi hii na wakazi wake."
Papa aliongeza kusema kuwa alipokuwa akiwatazama kutoka dirishani mwa nyumba ya kijesuit wavuvi waliokuwa na shughuli nyingi na mitumbwi na nyavu zao kwenye Bosporus, aliendelea: “Maono yananigusa. Usiku uliopita, yapata saa saba asubuhi, mvua ilikuwa ikinyesha, lakini wavuvi walikuwa pale, bila woga katika kazi yao ngumu… Kwa njia hiyo "Kuwaiga wavuvi wa Bosporus wakifanya kazi mchana na usiku na taa zao ikiwa zimewashwa, kila mmoja kwenye mtumbwi wake ndogo, wakifuata maelekezo ya viongozi wao wa kiroho, huu ni wajibu wetu mzito na mtakatifu.” Ni matumaini ya Papa kwamba watasukumwa na shauku hiyo hiyo, ili kudumisha furaha ya imani, na kuendelea kufanya kazi kama wavuvi jasiri katika mtumbwi wa Bwana. Maria Mtakatifu sana Theotokos Mama wa Mungu , awambee na awatunze.
