Tafuta

2025.11.26 Papa alikutana na Tume ya Taalimungu Kimataifa. 2025.11.26 Papa alikutana na Tume ya Taalimungu Kimataifa.  (@Vatican Media)

Papa Leo XIV kwa Tume ya Kimataifa ya Taalimungu:Maisha yalingane na Injili

Papa Leo XIV alihimiza Tume ya Kitaalimungu kutafakari mafunzo yao kwa sayansi zingine,ili watu waweze kuelewa vyema jinsi ya kukabiliana na changamoto zinazokabili Kanisa na ubinadamu."Taalimungu lazima ichunguze vipengele vyote vya sayansi ya binadamu."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV alikutana Jumatano tarehe 26 Novemba 2025 na wajumbe wa Tume ya Kimataifa ya Taalimungu  katika fursa ya  mkutano wao wa jumla Jijini Roma. Katika hotuba yake, Papa aliwashukuru kwa huduma yao kwa Kanisa kama sehemu ya Tume, ambayo Papa Mtakatifu Paulo VI aliiunda mwaka 1969 ili kuongoza ufufuo wa Kitaalimungu wa Kanisa baada ya Mtaguso wa Pili wa Vatican. Alitoa shukrani kwa hati yao ya hivi karibuni inayochunguza maadhimisho ya miaka 1,700 ya Mtaguso wa Kwanza wa Kiekumeni wa Nicea, akiuita "maandishi yenye mamlaka" ambayo iliandaa njia kwa Ziara yake ya Kitume kwenda Türkiye, ambapo atatembelea eneo la Mtaguso ulikofanyikia.

Kutambua mambo mapya katika familia ya binadamu

Papa Leo XIV aliwahimiza wataalimungu  kuendelea na dhamira yao ya kutambua mambo mapya yanayoashiria njia ya familia ya binadamu na Kanisa. Haya ni mambo halisi ambayo yanatupatia changamoto kubwa kama watu wa Mungu, ili tuweze kutangaza kwa uaminifu wa ubunifu Habari Njema iliyotolewa kwa Ulimwengu 'mara moja kwa wote' na Mungu Baba yetu kupitia Bwana Yesu Kristo," alisema Papa Leo. Tume ya Kimataifa ya Kitaalimungu ina  jukumu la kutoa maarifa, mbinu za kifasihi kwa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na Maaskofu wote, dhamira aliyosema inasaidia kujenga Mwili wa Kristo. Papa aliwasihi wataalimungu  kutumia "uzito muhimu wa mbinu ya taalimungu na vipengele vitatu vya ziada vya tafakari ya Taalimungu.

Ukatoliki na imani yetu vitajirishwe

Kwa njia hiyo aliwaalika  kutafakari kila wakati ukatoliki wa imani yetu, ili waweze kutajirishwa na uzoefu mwingi wa kiutamaduni wa Makanisa mahalia ulimwenguni kote. Papa pia alisisitiza umuhimu wa kufanya kazi pamoja katika taaluma za kitaalimungu, ambazo husaidia kila moja kuelezea dhana za kitaalimungu kwa ufanisi na kwa uhalisia kwa lengo la uinjilishaji wa watu wa tamaduni zote. Kisha akaelekeza mifano na tafakari za Walimu wakuu waa Kanisa, akiwemo Mtakatifu Agostino, Mtakatifu Bonaventure, Mtakatifu Thomas Aquinas, Mtakatifu Therese wa Lisieux, na Mtakatifu John Henry Newman. "Ndani yao," alisema, utafiti wa kitaalimungu ulihusishwa kila wakati na sala na uzoefu wa kiroho, masharti muhimu ya kukuza uelewa wa Ufunuo, ambao hauwezi kupunguzwa kuwa ufafanuzi juu kanuni ya imani."

Maisha yalingane na Injili

Ni maisha tu yanayolingana na Injili ambayo yanaweza kufanya ushuhuda wetu kwa Kristo na utume wa Kanisa kuwa wa kuaminika kwa wale tunaotumwa kwao.  "Kama scientia fidei ("sayansi ya imani"), taalimungu ina jukumu la kutafakari, na kisha kutafakari na kueneza nuru ya kudumu na ya mabadiliko ya Kristo katika mwendo unaobadilika wa historia yetu." Papa Leo XIV alikumbuka wasiwasi wa Hayati Papa Benedikto XVI kuhusu "ugawaji mkubwa wa maarifa" na kufungwa kwa sayansi ya binadamu kwa metafizikia. Mgawanyiko huu wa maarifa, unazuia sayansi yenyewe na hata maendeleo ya watu. "Kama ambavyo hakuna kitivo ambacho imani haichoki, vivyo hivyo hakuna sayansi ambayo taalimungu  inaweza kupuuza. Kupitia utafiti kamili, kwa hivyo wanaitwa kutoa mchango wao wa thamani katika utambuzi na utatuzi wa changamoto zinazokabili Kanisa na ubinadamu kwa ujumla.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here

26 Novemba 2025, 11:36