Papa Leo XIV:Ni hamu yangu kuwatangazia watu wote wa Ulaya: 'Yesu Kristo ndiye Tumaini letu
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV alikutana Alhamisi tarehe 6 Novemba 2025 na Wajumbe wa Kamati ya Pamoja ya Baraza la Mabaraza ya Maaskofu Ulaya, (CCEE),Baraza la Makanisa Ulimwenguni(WCC)na Wawakilishi wa Makanisa ya Kikristo ya Ulaya(CEC),Mkutano huo na Papa umekuja siku moja baada ya wawakilishi wa Makanisa ya Kikristo barani Ulaya kusaini Charta Oecumenica mpya, yaani Hati mpya ya Kiekumene ambayo inafanya kazi kama msingi wa ushirikiano wa kiekumeni wa Ulaya, katika Abasia ya Visima vitatu huko Roma (Tre Fontane).
Katika hotuba yake, Papa alisema hati iliyosasishwa ambayo ilisainiwa miaka 25 baada ya Mkataba wa kwanza wa Kiekumeni, inalenga kushughulikia safari ya kiekumeni inayobadilika kila mara ya Wakristo barani Ulaya, huku ikijibu wasiwasi wa kisasa katika kutangaza Injili. Alibainisha kuwa Ulaya imeona vizazi vipya vikizaliwa na watu wanawasili kutoka nchi za mbali ambao huleta "historia na misemo mbalimbali ya kiutamaduni."
Ingawa kuna dalili chanya na za kutia moyo za ukuaji katika baadhi ya maeneo ya Ulaya, wakati huo huo jumuiya nyingi za Kikristo zinajihisi kuwa chache zaidi. Papa Leo kwa hiyo aliwahimiza Makanisa ya Ulaya kusikiliza sauti na historia mpya, ili Wakristo wajifunze kukuza vyema mazungumzo na udugu katikati ya kelele za vurugu na vita. Katika hali hizi zote, neema, huruma, na amani ya Bwana ni muhimu sana, kwani msaada wa kimungu pekee ndio utakaotuonyesha njia ya kushawishi zaidi ya kumtangaza Kristo katika mazingira haya yenye changamoto kubwa."
Papa alithibitisha kwamba Mungu huzungumza na kupitia watu wake watakatifu, na akaiita Charta Oecumenica kuwa ushuhuda wa utayari wa Makanisa barani Ulaya kutazama historia yetu kupitia macho ya Kristo. Roho Mtakatifu, atawaruhusu Wakristo wa Ulaya kugundua maeneo ambayo wamefanikiwa kutangaza Injili pamoja, pamoja na nyakati ambazo wameshindwa. Charta, yaani Hati hiyo haipendekezi mbinu tu, lakini pia inasisitiza wasaidizi kwa safari na njia zinazowezekana za kusonga mbele. Kwa kufanya hivyo, hebu tuendelee kuwa wazi kwa misukumo na mshangao wa Roho Mtakatifu!
Baba Mtakatifu Leo XIV aliunganisha safari ya kiekumene ya Kanisa Katoliki na safari yake ya kisinodi, akibainisha kwamba Hati hiyo (Charta Oecumenica) inaakisi safari ya Kikristo barani Ulaya ya kusikilizana na kutambua pamoja njia bora za kuhubiri Injili. "Mojawapo ya mafanikio muhimu ya mchakato wa kurekebisha Hati hiyo imekuwa uwezo wa kuchukua mtazamo wa pamoja kuhusu changamoto za kisasa na kuandaa vipaumbele kwa mustakabali wa bara, huku tukidumisha imani thabiti katika umuhimu usio na mwisho wa Injili," alisema.
Kwa kuhitimisha Papa Leo XIV alikumbuka ziara yake ijayo kwenye eneo ambalo Mtaguso wa Nicea Ulifanyika kunako mwaka 325, ambapo atasali na viongozi wa jumuiya zingine za Kikristo. "Pia ni hamu yangu, katika Mwaka huu wa Jubilei," alihitimisha kuwatangazia watu wote wa Ulaya kwamba 'Yesu Kristo ndiye Tumaini letu,' kwani Yeye ndiye njia tunayopaswa kufuata, na mwisho wa safari yetu ya kiroho."
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku: Just click here
