Tafuta

2025.11.29 Ziara ya Kitume huko Turkiye - Saini ya Tamko la Pamoja katika Jumba la Upatriaki. 2025.11.29 Ziara ya Kitume huko Turkiye - Saini ya Tamko la Pamoja katika Jumba la Upatriaki.  (@Vatican Media)

Papa Leo na Patriaki Bartholomew:Tisitumie jina la Mungu kuhalalisha vita

Papa Leo na Patriaki wa Kiekumeni wa walitia saini 'Tamko la Pamoja' huko Phanar,Istanbul,wakithibitisha kujitolea kwa umoja wa Kikristo na tarehe ya pamoja ya Pasaka.Wametoa wito wa kumalizika mara moja janga la vita huku wakishangazwa na hali ya sasa ya kimataifa.Walizindua ujumbe wa matumaini:Mungu hawaachi wanadamu na kamwe tusitumie jina la Mungu kuhalalisha vita na vurugu.

Angella Rwezaula  - Vatican.

Mrithi wa Mtume  Petro, Baba Mtakatifu Leo XIV na Mrithi wa Mtume Andrew, Patriaki wa Kiekumeni Bartholomew I, walikusanyika pamoja Novemba 28 kwenye sehemu ya kupumzikia ya Iznik kando ya ziwa kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 1700 ya Mtaguso wa Kwanza wa Kiukemeni. Lakini pia Jumamosi tarehe 29 Novemba 2025, kwa ajili ya majadiliano ya meza ya mduara na viongozi wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo katika Kanisa la Mor Ephrem; pamoja tena alasiri, katika Kanisa la Upatriaki la Mtakatifu George kwa ajili ya sala(Doxology), iliyosikia na nyimbo na litania katika lugha mbalimbali na iliyojaa harufu ya uvumba na mishumaa ikiwaka.

Wakati wa kutia saini tamko la pamoja
Wakati wa kutia saini tamko la pamoja   (@Vatican Media)

Hatimaye, mara baada ya sala hiyo  kwa pamoja huko Phanar, katika kiti cha Upatriaki wa Kiekumeni wa Constantinopoli, waliweza kutia saini kwa Tamko la Pamoja. Tamko hili linaongozwa na kifungu cha zaburi kisemacho: "Mshukuruni Bwana, kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele,"(Zb 106(105):1).Ifuatayo ni tamka kamili: Katika usiku wa kuamkia siku kuu ya Mtakatifu Andrea, Mtume wa Kwanza, kaka wa Mtume Petro na msimamizi wa Upatriaki wa Kiekumeni, sisi, Papa Leo XIV na Patriaki Bartholomew wa Kiekumeni, tunamshukuru Mungu kwa dhati, Baba yetu mwenye huruma, kwa zawadi ya mkutano huu wa kidugu. Kwa kufuata mfano wa watangulizi wetu wa heshima, na kwa kutii mapenzi ya Bwana wetu Yesu Kristo, tunaendelea kutembea kwa azma thabiti katika njia ya mazungumzo, katika upendo na kweli (taz. Ef 4:15), kuelekea urejesho kamili unaotarajiwa wa ushirika kati ya Makanisa yetu dada.

Papa Leone XIV e il Patriarca ecumenico di Costantinopoli con la Dichiarazione congiunta appena firmata.

Papa Leo XIV na Patriaki wa Kiekumeni wakiwa wameshika Tamko la Pamoja baada ya saini(@Vatican Media)

Tukifahamu kwamba umoja wa Kikristo si tu matokeo ya juhudi za kibinadamu, bali ni zawadi inayotoka juu, tunawaalika washiriki wote wa Makanisa yetu - mapadre, watawa, watu waliowekwa wakfu, na waamini walei - kwa bidii kutafuta utimilifu wa sala ambayo Yesu Kristo alimwambia Baba: “Wote wawe na umoja, kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako... ili ulimwengu upate kuamini” (Yh 17:21).

Ukumbusho wa kumbukumbu ya miaka 1700 ya Mtaguso wa Kwanza la Kiekumeni wa Nicea, ulioadhimishwa usiku wa mkutano wetu, ilikuwa wakati wa ajabu wa neema. Mtaguso wa Nicea uliofanyika mwaka 325 BK ulikuwa tukio la umoja. Hata hivyo, kusudi la kuadhimisha tukio hili, si tu kukumbuka umuhimu wa kihistoria wa Mtaguso, bali ni kututia moyo tuwe wazi kwa Roho Mtakatifu yuleyule aliyezungumza kupitia Nicea, tunapopambana na changamoto nyingi za wakati wetu.

Tunawashukuru sana viongozi na wajumbe wote wa Makanisa mengine na jumuiya za kikanisa ambao walikuwa tayari kushiriki katika tukio hili. Mbali na kutambua vikwazo vinavyozuia kurejeshwa kwa ushirika kamili miongoni mwa Wakristo wote,  vikwazo ambavyo tunatafuta kushughulikia kupitia njia ya mazungumzo ya kitaalimungu,  lazima pia tutambue kwamba kinachotuunganisha pamoja ni imani inayooneshwa katika kanuni ya imani ya Nicea.

La cerimonia

Kuelekea katika maadhimisho (@Vatican Media)

Hii ni imani inayookoa katika nafsi ya Mwana wa Mungu, Mungu kweli kutoka kwa Mungu kweli, Mwenye umungu mmoja na Baba, ambaye kwa ajili yetu na wokovu wetu alitwaa mwili na akakaa kati yetu, alisulubiwa, akafa na kuzikwa, akafufuka siku ya tatu, akapaa mbinguni, na atakuja tena kuwahukumu walio hai na wafu. Kupitia kuja kwa Mwana wa Mungu, tunaingizwa katika fumbo la Utatu Mtakatifu  wa Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu  na tunaalikwa kuwa, ndani na kupitia utu wa Kristo, watoto wa Baba na warithi pamoja na Kristo kwa neema ya Roho Mtakatifu. Tukiwa tumejaliwa ungamo hili la pamoja, tunaweza kukabiliana na changamoto zetu za pamoja katika kutoa ushuhuda wa imani iliyooneshwa huko Nicea kwa heshima ya pande zote, na kufanya kazi pamoja kuelekea suluhisho halisi kwa matumaini ya kweli.

Tunaamini kwamba ukumbusho wa kumbukumbu hii muhimu unaweza kuhamasisha hatua mpya na za ujasiri kwenye njia ya kuelekea umoja. Miongoni mwa maamuzi yake, Mtaguso wa Kwanza wa  Nicea pia ulitoa vigezo vya kubaini tarehe ya Pasaka, ambayo ni ya kawaida kwa Wakristo wote. Tunashukuru kwa maongozi ya Mungu kwamba mwaka huu ulimwengu wote wa Kikristo ulisherehekea Pasaka siku hiyo hiyo. Ni hamu yetu ya pamoja kuendelea na mchakato wa kuchunguza suluhisho linalowezekana la kusherehekea pamoja Siku ya Sikukuu kila mwaka. Tunatumaini na kuomba kwamba Wakristo wote, “kwa hekima yote na ufahamu wa kiroho” (Kol 1:9), watajitoa katika mchakato wa kufikia sherehe ya pamoja ya ufufuko mtukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Papa katika sala
Papa katika sala   (@Vatican Media)

Mwaka huu pia tunaadhimisha kumbukumbu ya miaka 60 ya Tamko la Pamoja (kuhusu makanisa yasiyo ya kikiristo)la kihistoria la watangulizi wetu watukufu, Papa Paulo VI na Patriaki wa Kiekumeni Athenagoras, ambalo lilizima ubadilishanaji wa kutengwa kwa 1054. Tunamshukuru Mungu kwamba ishara hii ya kinabii ilisababisha Makanisa yetu kufuata "kwa roho ya uaminifu, heshima na upendo wa pande zote mazungumzo ambayo, kwa msaada wa Mungu, yatasababisha kuishi pamoja tena, kwa ajili ya mema zaidi ya roho na ujio wa ufalme wa Mungu, katika ushirika kamili wa imani, mwafaka wa kidugu na maisha ya kisakramenti ambayo yalikuwepo kati yao wakati wa miaka elfu ya kwanza ya maisha ya Kanisa" (Tamko la Pamoja la Papa Paulo VI na Patriaki wa Kiekumeni Athenagoras, 7 Desemba 1965).

Wakati huo huo, tunawahimiza wale ambao bado wanasita kwa aina yoyote ya mazungumzo, kusikiliza kile ambacho Roho anawaambia Makanisa (taz. Uf 2:29), ambaye katika hali ya sasa ya kihistoria anatuhimiza kuwasilisha kwa ulimwengu ushuhuda mpya wa amani, upatanisho na umoja. Tukiwa tumetambua umuhimu wa mazungumzo, tunaelezea uungaji mkono wetu unaoendelea kwa kazi ya Tume ya Pamoja ya Kimataifa ya Majadiliano ya Kitaalimungu kati ya Kanisa Katoliki la Roma na Kanisa la Kiorthodox, ambalo katika awamu yake ya sasa linachunguza masuala ambayo kihistoria yamekuwa yakichukuliwa kuwa ya mgawanyiko. Pamoja na jukumu lisiloweza kubadilishwa ambalo mazungumzo ya kitaalimungu huchukua katika mchakato wa upatanisho kati ya Makanisa yetu, pia tunapongeza vipengele vingine muhimu vya mchakato huu, ikiwa ni pamoja na mawasiliano ya kidugu, sala, na kazi ya pamoja katika maeneo yote ambapo ushirikiano tayari unawezekana. Tunawasihi sana waamini wote wa Makanisa yetu, na hasa mapadre  na wataalimungu, kukumbatia kwa furaha matunda ambayo yamepatikana hadi sasa, na kufanya kazi kwa ajili ya ongezeko lao linaloendelea. Lengo la umoja wa Kikristo linajumuisha lengo la kuchangia kwa njia ya msingi na inayotoa uhai kwa amani miongoni mwa watu wote.

Patriaki akimpatia zawaidi
Patriaki akimpatia zawaidi   (@Vatican Media)

Kwa pamoja tunapaza sauti zetu kwa bidii katika kuomba zawadi ya Mungu ya amani juu ya ulimwengu wetu. Cha kusikitisha, katika maeneo mengi ya ulimwengu wetu, migogoro na vurugu vinaendelea kuharibu maisha ya wengi. Tunawaomba wale walio na majukumu ya kiraia na kisiasa kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba janga la vita linakoma mara moja, na tunawaomba watu wote wenye mapenzi mema waunge mkono ombi letu. Kwa namna ya pekee tunakataa matumizi yoyote ya dini na jina la Mungu kuhalalisha vurugu. Tunaamini kwamba mazungumzo halisi kati ya dini, mbali na kuwa chanzo cha mchanganyiko na mkanganyiko, ni muhimu kwa kuwepo kwa pamoja kwa watu wa mila na tamaduni tofauti.

Papa akipatiwa zawadi
Papa akipatiwa zawadi   (@Vatican Media)

Tukizingatia maadhimisho ya miaka 60 ya tamko la Nostra Aetate, tunawahimiza wanaume na wanawake wote wenye mapenzi mema kufanya kazi pamoja ili kujenga ulimwengu wa haki na usaidizi zaidi, na kutunza kazi ya uumbaji, ambao tumekabidhiwa na Mungu. Ni kwa njia hiyo  tu familia ya binadamu inaweza kushinda kutojali, tamaa ya kutawaliwa, uchoyo wa faida na chuki dhidi ya wageni. Ingawa tuna wasiwasi mkubwa na hali ya sasa ya kimataifa, hatupotezi tumaini. Mungu hatawaacha wanadamu. Baba alimtuma Mwanawe Mzaliwa Pekee kutuokoa, na Mwana wa Mungu, Bwana wetu Yesu Kristo, alitupa Roho Mtakatifu, ili atufanye washiriki katika maisha yake ya kimungu, akihifadhi na kulinda utakatifu wa mwanadamu. Kwa Roho Mtakatifu tunajua na tunapata uzoefu kwamba Mungu yuko pamoja nasi. Kwa sababu hiyo, katika maombi yetu tunamkabidhi Mungu kila mwanadamu, hasa wale wanaohitaji, wale wanaopitia njaa, upweke au ugonjwa. Tunawaombea kila mwanafamilia ya wanadamu neema na baraka ili "mioyo yao ifarijiwe, wakiunganishwa pamoja katika upendo, ili wapate utajiri wote wa ufahamu uliohakikishwa na ujuzi wa siri ya Mungu," ambaye ni Bwana wetu Yesu Kristo (Kol 2:2).

Imetiwa saini huko Phanar, tarehe 29 Novemba 2025.

Papa akitazama zwadi
Papa akitazama zwadi   (@Vatican Media)

Asante kwa kusoma makala haya. Ukitaka kuendelea kupata taarifa mpya, tafadhali jiandikishe kwa jarida letu: cliccando qui

29 Novemba 2025, 16:28