Tafuta

Ujumbe wa Papa Leo XIV kwa vijana:muwa wajenzi wa madaraja katika ulimwengu unaoangaziwa na mgawanyiko

Papa Leo XIV alituma ujumbe wa video kwa vijana waliokusanyika katika Kanisa Kuu la Košice nchini Slovakia na kuwatia moyo kuleta nuru ya Kristo kwa familia zao,shule, sehemu za kazi na zaidi.

Vatican News

Yesu anawaita kuwa mashahidi wa ushirika, wajenzi wa madaraja na wapandaji wa uaminifu katika Ulimwengu ambao mara nyingi huwakisiwa na mgawanyiko na mashaka.” Haya ni maneno ya kutia moyo ambayo Baba Mtakatifu  Leo XIV aliwahutubia vijana waliokusanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Elizabeth huko Košice, Slovakia, katika ujumbe kwa njia ya video uliotolewa Jumamosi, tarehe 8  Novemba 2025.

"Msiogope basi, kuonesha kwamba ninyi ni Wakristo, kuishi Injili kwa shauku, na kushiriki furaha inayotokana na kukutana na Bwana," aliendelea.

Mkusanyiko huo uliandaliwa na Jimbo Kuu la Košice kusherehekea Jubilei ya Vijana. Ulijumuisha Misa iliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo na Rais wa Baraza la Maaskofu wa Slovakia, Bernard Bober, na Balozi wa Vatican nchini, Askofu Mkuu Nicola Girasoli. Tukio hilo pia lilijumuisha tamasha ambalo lilishuhudia maonyesho ya kikundi cha Wakatoliki wa Slovakia, Godzone, na DJ wa Kireno, Padre Guilherme Peixhoto, aliyecheza katika Siku ya Vijana Duniani 2023 huko Lisbon.

Katika ujumbe wake Papa aliwakumbusha vijana kwamba "hawako peke yao kamwe, kama watoto tunapendwa, tunasamehewa na kutiwa moyo na Mungu kila wakati," huku akinukuu ujumbe wake kwa ajili ya  Siku ya 40 ya Vijana - ambayo itaadhimishwa katika majimbo  ulimwenguni kote hivi karibuni mnamo Novemba 23.

Pelekeni furaha kwa familia zenu, shule, mahali pa kazi

Papa Leo XIV aliwasihi vijana kuwapelekea wengine ufahamu huu kwani kiukweli ni "uhakika huu unaowafanya wawe huru, unaowainua juu ya kutojali, na kuwachochea kupenda kwa moyo ulio wazi na mkarimu."

"Kuweni mashahidi wa furaha hii!" alisisitiza, huku akiwaalika vijana kupeleka "nuru ya Kristo" kwa "familia zao, shule, vyuo vikuu, mahali pa kazi na jamii." "Kwa njia hii, uso wa ujana wa Kanisa utaendelea kung'aa katika moyo wa Ulaya ya Kati, ambapo imani ya mababu zenu inabaki hata leo hii kuwa chanzo cha maisha mapya," aliongeza.

Papa wa Roma kadhalika alisisitiza kwamba Kanisa Kuu la Košice ni "moyo unaodunda wa imani na matumaini" na kwamba kukusanyika kwa vijana ni "ishara inayoonekana ya udugu na amani inayoingizwa mioyoni mwetu kupitia urafiki na Kristo." Papa alihitimisha ujumbe wake kwa njia ya video kwa kutoa Baraka yake ya Kitume kwa washiriki wote na kuwakabidhi kwa Bikira Maria.

Vijana Slovakia

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here

09 Novemba 2025, 14:41